Sehemu ya 16
“Mmeshanipata, muacheni Annabel aondoke,” alisema Ethan.
“Haondoki mtu hapa!”
“Sasa mnataka mumpeleke Marekani akafanye nini? Hili ni suala langu na nyie, yeye hausiki na chochote kile,” alisema Ethan huku akianza kuingiwa na hasira.
“Usijali, hatofika Marekani, tutamtupa baharini, ngoja tufike kina kirefu, tukimwacha, atatoa siri na hivyo kukamatwa,” alisema Thorn.
Walichokifanya ni kumchukua Ethan na kisha kumpeleka katika chumba kile alichofungwa Annabel, alipoingizwa, hakumuona Annabel kutokana na giza nene lililokuwemo mule ndani. Giza lile tu, kwake likaonekana kuwa mateso makubwa, hakujua Annabel alikuwa wapi, alichokifanya ni kuanza kumuita.
“Annabel...” alimuita msichana huyo huku akiwasha simu yake, hata kabla msichana huyo hajaitikia, Ethan alishtukia akipigwa kibao kimoja kizito mpaka simu kumdondoka, alikuwa Annabel.
“Kwa nini umenifanyia hivi?’ aliuliza Annabel huku akimshika fulana Ethan.
“Nisikilize kwanza mp....” alisema lakini hata kabla hajamaliza sentensi yake, akashtukia akipigwa kibao kingine.
“Kwa nini? Kwa nini?” aliuliza msichana huyo, alionekana kuwa na hasira mno.
“Mpenzi! Naomba unisamehe.”
“Wewe ni nani?”
“Ethan.”
“Nakuuliza wewe ni nani?”
“Annabel subiri, punguza hasira, tutazungumza mengi,” alisema Ethan.
“Niambie kwanza, wewe ni nani na hawa ni wakina nani?’ aliuliza Annabel.
Ethan hakuzungumza kitu, alibaki kimya huku akimwangalia msichana huyo kwa msaada wa mwanga wa simu yake, ni kweli alijiona kufanya kosa kubwa, kitendo cha kumficha msichana huyo kwamba alikuwa nani na wale watu walikuwa wakina nani kilimuumiza sana.
Annabel alilia na kulia, Ethan akamsogela na kisha kumkumbatia, alikuwa msichana wake, aliyemthamini, msichana aliyekuwa na nguvu kubwa katika maisha yake, hakutaka kumuona akilia, kitendo cha kububujikwa na machozi mashavuni mwake kilimuumiza mno.
“Nisamehe mpenzi,” alisema Ethan huku akiwa amemkumbatia.
“We..we ni n..an..i..?” aliuliza Annabel kwa sauti ya kilio kilichojaa kwikwi.
“Kuna mengi ya kuzungumza ila amini kwamba umeubadilisha moyo wangu Annabel,” alisema Ethan huku akiwa amemkumbatia msichana huyo.
“Niambie wewe ni nani.”
“Mimi ni muuaji mstaafu.”
“Umemuua nani?”
“Nimeua watu wengi kabla ya kukutana na wewe ambaye umeyabadilisha maisha yangu,” alijibu Ethan kwa sauti ndogo.
“Naomba usinidanganye.”
“Siwezi kukudanganya, mimi ni muuaji,” alisema Ethan.
Hapo ndipo Ethan alipoanza kumsimulia Annabel historia fupi ya maisha yake namna alivyokuwa akifanya kazi kwa mzee Sanchez mpaka alipoacha baada ya mzee huyo kufariki na hatimaye kuhamia kwa bwana Cook ambaye aliamua kuachana naye mara baada ya kukutana na msichana huyo mrembo.
Hakutaka kumficha kitu chochote, aliona kwamba huo ndiyo ulikuwa muda wa kumwambia ukweli juu ya kila kitu alichokuwa amekifanya, vitu vilivyomfanya kuwa mahali hapo kipindi hicho.
Annabel alilia sana, alimlalamikia mno kwa kumwingiza katika matatizo, lakini katika yote hayo, aligundua kwamba kama kutokea, tayari mambo yote hayo yalikuwa yametokea na kilichobaki ni kupanga nini cha kufanya baada ya hapo.
Akamsamehe kwa kila kitu, walichokubaliana ilikuwa ni lazima watoroke, hawakutaka kufika Marekani, Ethan alimfahamu bwana Cook, alikuwa mtu mwenye roho mbaya ambaye kwenye mambo ya biashara hakuonekana kuwa na mchezo hata kidogo.
“Sitaki kufika Marekani, ikitokea ikawa hivyo, ni lazima tutauawa,” alisema Ethan huku akimshika Annabel.
“Kwa hiyo tufanye nini?”
“Ni lazima tutoroke.”
“Tutaweza?”
Yote niachie mimi, hatufiki Marekani salama, kama kutuua, bora watuue ila si kufika mikononi mwa bwana Cook,” alisema Ethan, muda huo tayari meli ikang’oa nanga na safari ya kuelekea nchini Marekani kuanza kwa kupitia Afrika Kusini.
*****
Mpango uliokuwepo ni wa kutoroka ndani ya meli ile, hawakujua ni jinsi gani wangetoroka lakini kitu pekee walichokijua ni kwamba hawakutakiwa kufika nchini Marekani.
Unyevuunyevu wa ndani ya chumba kile uliwaweka kwenye wakati mgumu, hakukuwa na mtu aliyekaa chini, walibaki wakiwa wamesimama na kila miguu ilipochoka, walikuwa wakichuchumaa tu.
Bahari ilitulia, walisikia upepo ukipiga kwa nje huku kelele ya injini ikisikika chumbani mule walipokuwa.
Hawakuwa wakijua Kaskazini ulikuwa upande gani, Magharibi wala pande nyingine za dunia.
Ndani ya meli hiyo, Thorn na wenzake walikuwa na furaha mno, hawakutegemea kama wangefanikiwa kumpata Ethan ambaye kwao alionekana kuwa lulu zaidi ya madini yoyote yale.
Walichokifanya ni kusherehekea tu, walitoa mizinga ya pombe kali na kuanza kunywa, walipongezana na kugongesheana glasi zao, kila kitu kilichokuwa kikiendelea ilikuwa ni shangwe tele.
“Hatimaye tumefanikiwa, ni lazima tutapiga hela sana tukifika,” alisema Thorn kwa sauti ya kilevi.
“Ndiyo hivyo! Kwanza tukifika Afrika Kusini tumtupe baharini yule mwanamke,” alisema Bruno.
“Sawasawa. Hakuna tatizo, hatakiwi kufika Marekani kabisa,” alisema Stephan huku akionekana kuwa mwenye furaha tele.
Hiyo ndiyo ilikuwa mipango yao, Annabel hakutakiwa kufika nchini Marekani, iwe isiwe ilikuwa ni lazima kutupwa baharini na sehemu ambayo walikuwa wameipanga ilikuwa ni Afrika Kusini, sehemu ambapo bahari mbili za Indi na Atlantiki zilipokuwa zikikutana.
Mtu ambaye alikuwa akihitajika alikuwa Ethan tu na si mwingine, kila walipokuwa wakisherehekea walikumbuka kile walichotaka kukifanya. Baada ya siku mbili, huku wakiingia na kutoka ndani ya chumba kile kwa ajili ya kuwapa chakula, wakafika nchini Malawi ambapo hawakutaka kusimama, waliunganisha na kuanza kuitafuta Msumbiji.
“Tukifika Afrika Kusini, kitu cha kwanza ni kununua pombe,” alishauri Bruno.
“Hakuna tatizo, tena pale kuna pombe nyingi, zenye ulevi wa hali ya juu, hakuna tatizo,” alisema Thorn huku kila mmoja akionekana kuwa na furaha.
Upande wa pili Ethan hakutaka kutulia, alikuwa akihangaika huku na kule, kazi kubwa aliyokuwa nayo ni kutafuta njia ya kuweza kutoka ndani ya chumba kile kilichoonekana kuwa na mateso makali.
Kulikuwa na maboksi mengi, hawakuelewa yalikuwa ni maboksi ya nini, waliachana nayo, waliyasogeza huku na kule na mishemishe za kutafuta jia ya kutokea kuendelea. Waliangalia kila sehemu ili kuona kama wangeweza kuona tundu au kitu chochote kile na waweze kujitoa lakini hawakuambulia kitu.
Kuna kipindi walikata tamaa, wakaona kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima kufika nchini Marekani. Ethan akaonekana kuchoka, hakujua ni kipi kingine alitakiwa kufanya kwani chumba kilionekana kutimia.
Meli ilizidi kusonga mbele, kila baada ya masaa sita, mmoja wa Wazungu wale aliingia ndani na kisha kuwapatia chakula na kuondoka zake.
Wakati mwingine kitu alichokuwa akikifikiria Ethan ni kupambana na yeyote ambaye angewaletea chakula na hatimaye kuondoka melini humo, ila swali kubwa lililomjia kichwani, wangetorokaje na wakati walikuwa katikati ya bahari?
“Haya maboksi yana nini?” aliuliza Annabel.