SoC01 Simanzi: Kumbukumbu za wafu na mapitio ya vita kubwa ya wakati huu

Stories of Change - 2021 Competition

clinician

JF-Expert Member
Mar 5, 2014
1,622
3,479
Siku za hivi karibuni moyo wangu umegubikwa na simanzi nzito. Simanzi inayoletwa na kumbukumbu za zamani zenye kuhuzunisha sana. Kumbukumbu za wapendwa wangu waliotangulia mbele ya haki. Kumbukumbu za mambo yote tuliyofanya pamoja ambayo yalifanya maisha kuwa na maana. Kumbukumbu hizi zimepelekea nikumbuke safari za mara kwa mara za marehemu mama angu kwenda kijijini kuzika wajomba,shangazi,mama wa wadogo na ndugu wengine wengi.

Kumbukumbu hizi zinaenda mbali kwenye kichwa changu na kutua kwenye tafakari ya minong'ono niliyokuwa nikisikia. Minong'ono iliyoanza kama sauti za chini chini zilizoongezeka kidogo kidogo hata kuwa wimbo mkuu wa Taifa. Minong,ono iliyodai kwamba wapendwa wangu na watu wengineo wengi waliokuwa wakitutoka sehemu mbalimbali nchini, walikuwa waathirika wa Upungufu wa kinga mwilini,yaani Ukimwi. Janga lilioonekana kuwa jipya katika nchi yetu kipindi hiko. Kumbukumbu zangu zikaenda kwenye vita changa tuliyokuwa nayo kipindi kile katika jamii yetu.Vita ya jasho,machozi na damu. Vita dhidi ya adui mpya mkali tusiyemjua vizuri, Ukimwi. Adui aliyeikumba nchi yetu miaka michache baada ya ile vita mbaya ya msituni katika mkoa wa Kagera. Adui aliyegunduliwa kwa mara ya kwanza kwenya jamii yetu mwaka 1984 katika hospitali ya misheni ya Ndolage iliyopo wilayani Muleba Mkoani Kagera. Adui aliyezusha minong'ono ile yenye kuleta hofu na taharuki kubwa.

Katika tafakari yangu ya vita dhidi ya janga la Ukimwi,vita vilivyoanza miaka 37 iliyopita nimeguswa sana na juhudi za makusudi zilizofanywa na serikali,wafadhili,taasisi za kidini na mashirika yasiyo ya kiserikali tangu kipindi hiko hadi sasa. Elimu kuhusu Ukimwi imekuwa ikitolewa kupitia vyombo mbalimbali vya habari,mashuleni,vyuoni,majukwaa ya dini na kupitia kazi mbalimbali za sanaa. Uanzishwaji wa Tume yenye mamlaka ya kuratibu mapambano dhidi ya janga la Ukimwi na uanzishwaji wa huduma za kupima virusi vya Ukimwi na kupatikana dawa za kurefusha maisha (ARV) bila malipo ni hatua kubwa kwenye vita hii.

Licha ya juhudi zote hizo takwimu za madhira yatokanayo na janga la Ukimwi katika nchi yetu bado ni za kuogofya sana. Katika chapisho la mwezi December mwaka 2018 la Wizara ya afya,maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto lililopewa jina la TANZANIA HIV IMPACT SURVEY au kwa kifupi THIS (A population-based HIV impact assesment 2016-2017) linaonesha kuwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwa mwaka kwa watu wenye umri wa miaka 15 na kuendelea ni 0.24%, ikiwa na maana ya kesi mpya 24 za maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwa kila watu 10,000 kwa mwaka. Pia takwimu zinatuonesha kwamba hali ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi katika jamii (prevalance) miongoni mwa watu wenye umri wa zaidi ya miaka 15 ni 4.9% huku kesi nyingi zaidi zikiripotiwa kwa wanawake kuliko wanaume,vijana wakiwa ni waathiriwa wakuu.Inakadiriwa kwamba hadi kufikia mwaka 2016 watu millioni 1.4 walikuwa wakiishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi nchini Tanzania. Takwimu hizo zinatisha zaidi kwa kueleza kwamba katika kila nyumba kumi nchini,nyumba moja ina angalau mtu mmoja anayeishi na Virusi vya Ukimwi.

Takwimu hizo zinatufundisha kwamba vita dhidi ya janga la Ukimwi katika nchi yetu bado changa sana,zinatushinikiza uendelezwaji na utiliwaji mkazo wa njia madhubuti za awali za mapambano dhidi ya janga la Ukimwi na uanzishwaji wa mapambano mapya ya kimkakati dhidi ya janga la Ukimwi.

Kufahamu madhira yatokanayo na janga la Ukimwi katika jamii yetu yakupasa kuangalia kwa mapana nini ugonjwa huo umefanya katika jamii,kama takwimu zinavyotuonesha. Lakini ili kujua nini kifanyike na kuweka malengo ya kimkakati ya kupambana na janga la Ukimwi yatupasa kurudi katika jamii zetu na kuangazia kiini haswa cha tatizo hili kinachofanya vita dhidi ya janga la Ukimwi kuonekana bado changa licha ya juhudi za miaka nenda rudi.

Vyanzo mbalimbali vya habari,mahubiri ya kwenye nyumba za ibada,tafiti za kisayansi na mijadala rasmi na isiyo rasmi katika ngazi zote za kijamii zinaonesha kuna changamoto katika mienendo yetu ya kimaisha inayofanya juhudi za mapambano dhidi ya Ukimwi zionekane kutofaa kitu.

Kwenye jamii zetu bado kuna kundi kubwa la watu wana wapenzi zaidi ya mmoja. Ndoa za mitala,uchumba,urafiki na mahusiano mengine ya kimapenzi yanayohusisha kushiriki kingono na wapenzi zaidi ya mmoja imeendelea kuwa chachu ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Matumizi hafifu ya kondomu nayo inatajwa kama chanzo kingine kinachochochea kasi ya kuenea kwa Virusi vya Ukimwi. Miongoni mwa wanaotumia kondomu bado kuna kundi lisilofahamu matumizi yaliyo sahihi ya kondomu hizo.

Tatizo la vijana kuanza kufanya mapenzi katika umri mdogo nalo linazidi kushamiri hali inayopelekea wasijue njia sahihi za kujilinda na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi,magonjwa mengine ya zinaa na mimba za utotoni. Kwa mujibu wa shirika la umoja wa mataifa linaloshughulika na idadi ya watu duniani ( UNFPA ) katika Tanzania wasichana 4 kati ya 10 wanaolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.

Tafiti za kisayansi zinaonesha kwamba wanaume wasiofanyiwa tohara wapo kwenye hatari zaidi ya kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwa sababu ni rahisi zaidi kwa ngozi ya mbele ya uume usiotahiriwa kupata michubuko. Nchini Tanzania miongoni mwa wanaume wenye umri wa miaka 15 na kuendelea asilimia 49.7% tu ndio waliopata tohara ya kitabibu kulingana na chapisho la THIS 2016-2017. Katika ripoti hiyo hiyo 27.9% ya wanaume wenye umri tajwa walipata tohara isiyo ya kitabibu hali inayowaweka kwenye hatari ya kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi. Tohara ya wanawake nayo inamchango mkubwa katika kuenea kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Umaskini na ukosefu wa ajira bado ni tatizo kubwa katika jamii yetu hali inayosababisha wimbi kubwa la vijana wa kike kwa wakiume kujiingiza katika biashara ya ukahaba. Kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano kumesababisha kushamiri kwa biashara ya ukahaba kwa kutoa jukwaa linalotumiwa na watoa huduma hiyo kuwafikia wateja wao kwa urahisi zaidi.

Ni mengi tunaweza kuzungumza kuhusiana na janga la Ukimwi,lakini lengo la barua hii ni kuleta muamsho katika jamii wa hali mbaya ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi iliyopo na kuhamasisha mabadiliko ya tabia za mtu mmoja mmoja pamoja na kuchochea maboresho ya mikakati iliyopo sasa ya mapambano dhidi ya janga hili. Mabadiliko makubwa katika jamii zetu yanaanzia kwetu wana jamii wenyewe.

Mabadiliko yanaanzia kwa wanajamii kutambua uwepo wa janga la Ukimwi na kisha kufuata njia madhubuti za kujikinga na janga hilo kwa kuacha kabisa tabia zote hatarishi nilizoangazia hapo juu.

Natoa rai kwa serikali, mashirika ya kidini na asasi za kiraia kuendelea kutoa elimu yenye lengo la kuamsha mawazo chanya yatakayobadili upepo wa vita dhidi ya janga la Ukimwi kwenda kwenye ueleko wa kumaliza tatizo hili.

Vyombo vya kutoa huduma kwa waathirika wa Virusi vya Ukimwi viongeze mikakati ya kuwatambua wagonjwa walio na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na kuwaingiza katika mpango wa huduma za waathirika kwani kwa ripoti ya THIS 2016-2017 ni silimia 60.6 pekee ya watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi wanafahamu hali yao ya maambukizi.

Serikali kama chombo kikuu cha maamuzi isimamie kwa ukamilifu sheria zinazopinga mambo yote yanayopelekea kuongezeka kwa kasi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi,mfano ndoa za utotoni na tohara za wanawake.

Serikali iangalie tatizo la ukosefu wa ajira na kufanya juhudi thabiti katika kupunguza umaskini nchini ili kupunguza kushamiri kwa biashara ya ukahaba.

Ombwe la utayari wa mapambano dhidi ya janga la Ukimwi katika jamii yetu bado ni kubwa. Ni matumaini yangu mapitio haya ya hali ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwenye nchi yetu yataamsha kiu ya mapambano zaidi kwa kila mwanajamii wa taifa hili. Mategemeo yangu makubwa ni kwamba serikali na vyombo vyote vinavyohusika na mapambano dhidi ya janga la Ukimwi vitaangalia namna bora za kuboresha juhudi za mapambano. Ni matamanio yangu makubwa kuona kama taifa sote tukiwa na kiu hii ya kumtokomeza kabisa adui huyu mbaya. Adui anayeendelea kuua idadi kubwa ya wapendwa wetu na kulididimiza zaidi taifa letu kwenye umaskini. Adui huyu aliyeikumba nchi yetu miaka michache baada ya ile vita mbaya ya msituni katika mkoa wa Kagera hastahili kutusumbua sasa . Uwezo wa kumpiga tunao,nia ya kumpiga tunayo na sababu za kumpiga tunazo. Tufunge vibwebwe, tunyanyue silaha zetu, tayari kumkabili.
 
Karibuni kusoma andiko langu,kama utavutiwa na andiko hili naomba uniunge mkono kwa kunipigia kura.Asante
 
Mshahara wa dhambi ni Mauti. Ukimwi unatokana na Uzinzi na uasherati yakiondoka hayo utaondoka. Mapambano ya kweli ni kujichunga kwa kusubir wakati sahihi wa kuanza Mapenzi unaoa. The Rest utavuna unachopanda
 
Back
Top Bottom