Serikali yasisitiza matumizi ya Tehama taasisi za umma

Suley2019

JF-Expert Member
Oct 7, 2019
1,817
4,566
Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), imetoa wito kwa taasisi za umma nchini kujiunga na mfumo wa ubadilishanaji wa taarifa serikalini (GovESB) ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.

Wito huo umetolewa jana Jumamosi Agosti 6, 2023 na Meneja Mawasiliano wa e-Ga, Subiria Kaswaga wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonyesho ya wiki ya wakulima jijini Mbeya, akisema taasisi hizo zitaweza kuwasiliana na kubadilishana taarifa kidijitali kupitia mfumo huo.

Kaswaga amebainisha faida za mfumo huo kuwa ni kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika taasisi za umma, kuokoa muda, gharama za uendeshaji wa taasisi pamoja na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa wakati.

“Mfumo wa GovESB ni jitihada za mamlaka za kuhakikisha mifumo ya Tehama katika taasisi za umma inazungumza na kubadilishana taarifa ili kupunguza urudufu wa mifumo serikalini.

"Kwa sasa taasisi mbalimbali za umma zimeunganisha mifumo yake na GovESB lakini zingine bado. Nitoe wito kwa taasisi hizo kujiunga na mfumo huu," amesema Kaswaga.

Amesema, Mamlaka imedhamiria kuhakikisha mwananchi anapata huduma zote za Serikali kidijitali mahali alipo na kuongeza kuwa ili kufikia malengo hayo wanashirikiana na taasisi mbalimbali za umma kwa kutengeneza mifumo ya kisekta itakayosaidia utendaji kazi.

Naye, Ofisa Tehama wa e-GA, Caesar Mwambani amesema mamlaka hiyo kwa kushirikiana Ofisi ya Rais, (Utumishi wa Umma na Utawala Bora), imetengeneza Mfumo wa e-Mrejesho unaowezesha wananchi kuwasiliana na Serikali kidijitali.

Amefafanua kuwa mfumo huo unawezesha wananchi kuwasilisha maoni, changamoto, pongezi au malalamiko kwenda katika taasisi yoyote ya umma na kisha kufuatilia utekelezaji wake kwa njia ya kidijitali.

“Mfumo huu unamrahisishia mwananchi kuwasiliana na serikali kidijitali na hivyo kumpunguzia gharama za kusafiri kwenda katika taasisi husika ili kuwasilisha kero yake na badala yake anaweza kuwasiliana na taasisi hiyo kupitia mfumo wa e-Mrejesho popote alipo,” amesema.
 
Back
Top Bottom