Serikali: Ripoti ya kesi za ukatili kwa watoto, Ubakaji 5,899, mimba 1,677, ulawiti 1,114

JanguKamaJangu

JF-Expert Member
Feb 7, 2022
2,308
5,460
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Uratibu wa Bunge, George Simbachawene amesema kesi za ukatili dhidi ya watoto zilizoripotiwa mwaka 2021 jumla ni 11,499.

Waziri Simbachawene amesema takwimu za Jeshi la Polisi zinaonesha kuwa kuanzia Januari hadi Desemba, 2021 kulikuwa na idadi hiyo ya kesi ambapo matukio makubwa ni ubakaji 5,899, mimba 1,677 na ulawiti ni 1,114.

Amesema vyombo vyote vya ulinzi vinapaswa kushughulikia kwa haraka na kutolea uamuzi mashauri yote yanayohusu mimba kwa watoto, ubakaji pamoja na ulawiti.

“Pia wazazi wote ambao watabainika kumaliza wenyewe kwa wenyewe mashauri yanayohusu ukatili dhidi ya watoto kama vile ubakaji, ulawiti na mimba wachukuliwe hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine,” alisisitiza Simbachawene.

Vilevile, alisema moja ya sababu zinazochangia ongezeko la watoto wa mitaani ni migogoro katika familia inayosababisha ndoa kuvunjika na watoto kukosa malezi ya wazazi.

"Baadhi ya familia zinaishi bila upendo hali inayosababisha kutengana kwa wazazi na kusababisha ongezeko la watoto mitaani katika miji mbalimbali Nchini, lakini serikali inaendelea kufanya jitihada za kumaliza hali hii ikiwamo ujenzi wa makao ya kulelea watoto nchini,” alisema Simbachawene.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, alisema serikali inatambua na inathamini familia kama chanzo cha nguvu kazi ya taifa.

“Hivyo katika kuimarisha uwezo wa familia kutimiza majukumu yake, serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, imekuwa ikitekeleza afua mbalimbali za kuwezesha familia kuishi kwa amani na upendo,” alisema Dk. Gwajima.

Alisema baadhi ya afua hizo ni kutoa elimu ya malezi chanya kwa wataalamu wa halmashauri 7,445 wakiwamo maofisa Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Maofisa Lishe na walimu.

“Aidha, wataalamu hawa kwa kipindi cha Julai 2020 hadi Juni 2021 walifanikiwa kutoa mafunzo na wazazi na walezi vinara (Champion) 110,805 ambao wamepewa jukumu la kuendeleza elimu ya malezi kwa wenzao katika mikoa 26 ya Tanzania Bara.

Alisema Tanzania inaungana na nchi nyingine duniani katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Familia inayofanyika kila mwaka Mei 15.

Maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika kimkoa na mikoa yote 26 inafanya maadhimisho hayo kwa utaratibu ambao wanaona unafaa kulingana na mazingira yao.



Source: IPP Media
 
Back
Top Bottom