SoC03 Serikali Iwalinde Wafanyabiashara na Wajasiriamali Wadogo Nchini Tanzania

Stories of Change - 2023 Competition

Tukuza hospitality

JF-Expert Member
Jul 30, 2022
242
615
Utangulizi
Baadhi ya wafanyabiashara wakubwa, nikimaanisha wale waliofikia kiwango cha kumiliki makampuni makubwa na/au viwanda vikubwa, wana tabia ya kuwameza wafanyabiashara wadogowadogo, kwa namna mbalimbali. Kwa mfano, kampuni ina kiwanda cha kuchakata ngano, na inauza ngano iliyokobolewa na kusagwa kwenye maduka ya jumla na ya rejareja. Watumiaji wakubwa wa bidhaa hii ni Mama Lishe na Baba Lishe ambao wanaitumia kutengeneza chapati na maandazi kwa ajili ya kuuzia wateja wao. Kitu ambacho hakiniingii akilini ni pale mwenye kiwanda hiki naye anatengeneza chapati na maandazi na kuuzia soko lilelile la Mama/Baba Lishe. Kwa mfano huu, itafikia mahali huyu mfanyabiashara ndogondogo atashindwa kufanya biashara, na kumwachia huyu mfanyabishara mkubwa kufanya biashara zote, yaani kubwa na ndogondogo!

Kielelezo Na. 1: Biashara Ndogondogo (Chapati na Maandazi)
Biashara za Mama Lishe.png

Chanzo: Google. Mama Lishe Tanzania

Biashara Ndogondogo Zinatambuliwa na Umoja wa Mataifa

Kwa mujibu wa Jarida la Umoja wa Mataifa (Juni 30, 2017), Biashara ndogondogo na zile za wastani zinatambuliwa na Umoja wa Mataifa, ndio maana Juni 27 kila mwaka ni siku ya kimataifa ya biashara ndogondogo na zile za wastani. Siku hii ambayo imeadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2017, baada ya kupitishwa na Azimio la Baraza Kuu ya Umoja wa Mataifa, inalenga kuhimiza umuhimu wa sekta ya biashara ndogondogo na zile za wastani katika kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu (“Sustainable Development Goals [SDGs]”).

Jarida hili linaendelea kusema, biashara hizi hutoa fursa za ajira kwa takriban watu milioni 250 na ni uti wa mgongo wa uchumi katika mataifa mengi kote ulimwenguni, huku zikitoa mchango muhimu katika nchi zinazoendelea. Biashara hizi zinatajwa kuwa muhimu katika ajira na fursa za kujipatia kipato, na ni muarobaini katika kukabiliana na umaskini na kuchagiza maendeleo, hasa lengo namba nane la Malengo ya Maendeleo Endelevu (“SDGs”), ambalo ni Kazi ya Staha na Ukuaji wa Uchumi (“Decent Work and Economic Growth”).

Jarida linaendelea kuripoti kwamba, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, biashara ndogondogo na za wastani, rasmi na zisizo rasmi zinajumuisha asilimia 90 ya biashara zote na kwa wastani huajiri asilimia kati ya 60-70 ya jamii, huku zikichangia asilimia 50 katika pato la ndani la taifa (“Gross Domestic Product - GDP”).

Tanzania ni moja kati ya nchi zenye fursa ya kuwa na wafanyabiashara na/au wajasiriamali wengi, tena vijana, ambapo kwa mtizamo wangu haijaweza kutumiwa vizuri kuleta tija ya kiuchumi nchini.

Kielelezo Na. 2: Wafanyabiashara Wadogowadogo Jijini Dar es Salaam
Wafanyabiashara Ndogondogo Dar II.png

Chanzo: Google. Wafanyabiashara wadogo

Wafanyabiashara wadogo nchini Tanzania ni wengi sana, na wapo vijijini na mijini. Ni ukweli kwamba, kilimo ni sehemu ya ajira kwa Watanzania zaidi ya asilimia 60, Wakulima wengi, pamoja na shughuli zao za kilimo, pia wanafanya biashara ndogondogo, mfano, mtu ana shamba la mahindi, maharage, migomba, kahawa, mifugo, nk. lakini wakati huo huo anamiliki na kuendesha duka, mgahawa, genge la bidhaa za nyumbani, au ana meza ya kuuza bidhaa mbalimbali sokoni, na kadhalika.

Kwa muktadha huu, unaweza kuona jinsi gani wafanyabiashara au wajasiriamali wadogo walivyo wengi na muhimu kwa jamii. Hoja hii inaungwa mkono na Gazeti la Mwananchi (Machi 16, 2021), ambapo mwandishi anasema, “Wafanyabiashara hawa wamekuwa chachu ya ajira kwa wenzao ambao wamekuwa wakiishi bila kazi. Mbali ya kuwaajiri na kuwalipa kulingana na kipato chao, vilevile wafanyakazi hao hujifunza mbinu na maarifa ya kuanzisha shughuli za ujasiriamali”.

Tukianzia vijijini, kila kijiji, kuna maduka ya bidhaa mbalimbali kwa matumizi ya nyumbani kwa wakazi wa kijiji husika; kina soko au masoko kwa ajili ya kuuza na kununua bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mazao wanayozalisha wakulima kijijini. Zote hizi ni biashara ndogondogo na zinafanywa na wafanyabiashara wadogo, ambazo ni muhimu kwa Maisha ya kila siku ya jamii.

Kwa mjini, wafanyabiashara wengi wadogo, hawana kazi nyingine zaidi ya biashara; kwa hiyo wanategemea biashara zao kwa karibu mahitaji yao yote. Biashara zinazofanyika mjini, ni za maduka, migahawa, magenge ya vyakula, masoko kwa ajili bidhaa mbalimbali, biashara za kutembea au za mkononi (maarufu kama “umachinga”).

Wafanyabiasahara (hasa wadogo) wanategemewa sana na jamii kwa Maisha ya kila siku, iwe ni vijijini au mijini. Mfano mdogo, jijini Dar es Salaam, katikati ya mwezi Mei mwaka huu (2023) wafanyabiashara (wengi wakiwa ni wale wadogowadogo) waligoma kwa siku mbili wakilalamikia Mamlaka ya Mapato Tanzania kuhusu utaratibu wa utozaji kodi. Watu wengi sana waliathirika na mgomo huo, kwani walishindwa kupata bidhaa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na/au ya biashara/ujasiriamali. Bahati nzuri, wale wafanyabiashara wa masokoni hawakuwa sehemu ya mgomo huu; vinginevyo hali ingekuwa mbaya zaidi. Bila shaka, serikali ilikosa mapato makubwa, kufuatia biashara nyingi kufungwa kwa muda huo mfupi!

Na huu ndio msingi wangu wa kuisihi serikali kuwalinda hawa wafanyabiashara na/au wajasiriamali wadogo kwa faida ya pande zote, yaani wananchi na serikali yenyewe.

Wafanyabiashara/Wajasiriamali Wadogo Walindwe katika Maeneo Matatu
Kwa kuwa Biashara ndogondogo huajiri zaidi ya asilimia 60 ya watu wote, na huchangia zaidi ya asilimia 50 ya pato la ndani, napendekeza walindwe katika maeneo haya:
  • Masoko yaboreshwe na kuwa ya kisasa. Serikali kupitia halmshauri zake za wilaya/miji/manispaa/majiji itenge bajeti ya kutosha kujenga na/au kukarabati masoko ili yakidhi mahitaji ya wafanyabiashara husika. Masoko mengi, hayaridhishi na hayavutii baadhi ya wafanyabiashara kufanyia huko biashara zao. Ndio maana, kwenye miji mikubwa kama Dar es Salaam, wafanyabiashara wengi wapo mitaani, na hata kufikia hatua ya kufunga baadhi ya barabara.
  • Watambuliwe kisheria na kuwezeshwa kujiunga na mifuko ya jamii ikiwa ni pamoja na bima ya afya. Hii ni muhimu sana, itawafanya wajione wenye thamani sawa na wale watumishi wenye ajira rasmi.
  • Kuwe na Sera na/au sheria maalumu itakayolinda biashara zao zisimezwe au kutolewa sokoni na wafanyabiashaa wakubwa. Hapa naamanisha, wafanyabiashara wakubwa wasipate mwanya wa kuwadidimiza wafanyabiashara wadogowadogo, kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutengeneza na kuuza bidhaa ambazo zinakwenda kushindana na zile wanazozalisha wafanyabiashara wadogowadogo kwa kutumia malighafi wanazonunua kwao (Wafanyabiashara wakubwa). Hii itaondoa mgongano wa maslahi kati yao (Wafanyabiashara wakubwa na wale wadogo).
Marejeo
Jarida la Umoja wa Mataifa (Juni 30, 2017), Biashara ndogondogo na mchango wake katika fursa za ajira

Mwananchi (Machi 16, 2021), Mjasiriamali: Umuhimu wa wafanyabiashara wadogo kwa Taifa
 
Wafanyabiashara wakubwa hutegemea sana wafanyabiashara wadogo na wa kati, na vivyohivyo wafanyabiashara wadogo na wa kati hutegemea sana wafanyabiashara wakubwa; hivyo hawa wanategemeana. Kumbe kila kundi lina nafasi yake katika kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi.
 
Serikali inahitaji kuweka sera nzuri na bajeti kidogo kuwezesha wafanyabiashara ndogondogo, na kutarajia makubwa zaidi.
 
Back
Top Bottom