Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,478
- 39,996
Ubepari ule wa asili kabisa una matokeo mengi mazuri na mabaya; nitawaacha wengine wayazungumzie mazuri lakini lakini itoshe miye kusema tu kuwa mojawapo ya matokeo mabaya ya ubepari ni mgongano kati ya waajiri na wafanyakazi. Wafanyakazi chini ya mfumo wa kibepari hujikuta mara zote katika mgongano na mazungumzo na waajiri kwa sababu mfumo wa ubepari hauwezi kamwe kuwatuliza wafanyakazi na kuwahakikishia maisha bora na usalama wa kazi zao.
Ni lazima tuelewe kwanini mgogoro unanukia kati ya wafanyakazi na serikali pamoja na waajiri wengine; mgogoro ambao matokeo yake yatakuwa ni mgomo wa kitaifa. Hatuwezi kuuelewa mgogoro huu au mingine itakayotokea huko mbeleni bila kuelewa japo kwa kiasi tu mfumo wa ubepari ulivyo na kwanini mfumo ndio unatengeneza hali zinazosababisha migongano hii ya waajiri na wafanyakazi.
Mojawapo ya makosa makubwa ambayo kama taifa tumeyafanya baada ya kuamua kuacha kujenga nchi kwa mfumo wa ujamaa tuliotaka kuujenga ni kujaribu kujenga nchi bila kuanisha mfumo tunaotaka kujenga nchi hiyo. Wanasiasa wetu waliopokea jukumu la kutuongoza kuelekea kwenye mabadiliko ya kiuchumi waliamua kufanya hivyo kwa kubunia na kukisia bila kuanisha itikadi na nadharia za kutuongoza huko tunakotaka kwenda. Matokeo yake waliupokea ubepari bila kuuhoji, kuukosoa, kuuchambua wala kuufafanua kwa wananchi.
Makala ifuatayo ni ngumu kidogo.. ni mifupa zaidi na inaweza kuonekana ni ya kichochezi... soma kwa risk yako mwenyewe!