SEHEMU ya 15...
Hilo ndilo alilolifanya Sarafina, hakutaka kuchelewa, akampigia simu David na kumwambia lengo lake la kutaka kutoa mimba hiyo hivyo alihitaji kiasi fulani cha pesa. David hakutaka kuchelewa, hapohapo, tena kwa haraka sana akamtumia kiasi cha shilingi laki mbili.
“Kaitoe haraka sana,” aliandika ujumbe mfupi.
“Sawa mpenzi!” aliitikia Sarafina na kumpanga Catherine kwamba siku inayofuata ilikuwa ni ya kwenda kwenye zahanati ya uchochoroni kwa ajili ya kutoa mimba.
**** Moyo wa Richard haukuwa na nafuu, ulitawaliwa na majonzi tele, alikosa furaha ambayo alitegemea kwamba angeipata. Alihuzunika mno kwa sababu alikataliwa na msichana aliyekuwa akimpenda kwa moyo wote.
Hakuacha kumfikiria, kila alipolala usiku, taswira ya msichana huyo ilimjia ndotoni. Wakati mwingine alitamani kumwambia kwamba alikuwa mtoto wa bilionea mkubwa lakini aliogopa kufanya hivyo.
Kila siku ilikuwa ni ya mateso tele, alipokwenda chuo na kumuona Sarafina akiwa na wakina David, moyo wake ulimuuma kupita kawaida. Alitamani kuwafuata wanaume hao na kuwaambia wamuachie msichana aliyekuwa akimpenda kwa moyo wa dhati lakini hilo halikuwezekana kabisa.
Siku ziliendelea kukatika, baada ya miezi kadhaa, akamuona Sarafina akianza kubadilika. Hakuonekana kuwa na furaha kama kipindi cha nyuma, hakuonekana kuwa na ukaribu na David kama ilivyokuwa.
Hilo halikumsumbua, aligundua kwamba mwanaume huyo alimchezea msichana huyo na hivyo kuamua kuachana naye. Hiyo ilionekana kuwa nafasi yake na kumfuata lakini alihofia. Kama Sarafina alimkataa kipindi cha nyuma, alikuwa amebadilika nini? Ilikuwa ni lazima kumkataa kwa mara nyingine tena.
Akaachana naye, akaendelea na mambo yake lakini kila alipomuona, moyo wake haukuacha kuuma kwani alitamani kumuona akiwa na furaha siku zote, furaha isiyomuhusisha mwanaume yeyote yule zaidi yake.
Baada ya kupita miezi mitatu, akashtuka kumuona msichana huyo akiwa amenenepa na kugundua kwamba alikuwa na mimba. Huo ndiyo ulikuwa msumari mkubwa kuliko yote moyoni mwake. Aliumia kwani kwa jinsi alivyompenda Sarafina hakutegemea kumuona akiwa na mimba ya mwanaume mwingine.
Je, nini kitaendelea?