SEHEMU YA 71...
Vijana wa David waliogopa, walimfahamu bosi wao, hakuwa mtu wa mchezo, aliposema kwamba alihitaji kitu fulani, haraka sana alitaka kupata majibu ya kitu hicho. Alichukia kufanyiwa uhuni wa kuibiwa laptop yake na pesa zake, alikasirika, hakutaka kuona mwizi huyo akiendelea kuishi, alichokitaka ni kumuua kama malipo kwa kile alichokuwa amekifanya.
Vijana wakaingia mitaani, kwa kuwa Ibrahim alikuwa akijulikana sana kama muokota chupa, hata walipoanza kumtafuta hakukuwa na ugumu wowote ule, ilikuwa ni kumuulizia kijana aliyekuwa akiokota chupa na hivyo kuonyeshewa mahali alipokuwa akiishi.
“Ni mtoto wa mitaani?” aliuliza Jumanne, mmoja wa wanaume waliotumwa na David.
“Ndiyo!”
“Anauza chupa wapi?”
“Ilala Mabondeni!”
“Twende!”
Hawakutaka kubaki mahali hapo, ilikuwa ni lazima waende kumtafuta, waliamini kwamba kama kweli alikuwa ameelekea huko ilikuwa ni lazima wampate. Njiani walikuwa wakizungumza, walimuona mkuu wao alivyokuwa na hasira, siku hiyo hasira zake zilikuwa tofauti na siku nyingine, alivimba, aliwaka, alichokuwa akikihitaji ni vitu vyake tu.
Jumanne na mwenzake, Fred wakafika mpaka Ilala Mabondeni, hapo, kulikuwa na sehemu iliyokuwa na milima mikubwa ya chupa, wakawafuata vijana fulani waliokuwa mahali hapo na kuwauliza kuhusu Ibrahim, kijana aliyekuwa akiokota chupa maeneo ya Posta.
“Huko Posta hawaruhusu watu kwenda kuokota, sasa iweje huyo aende huko?” aliuliza kijana aliyekuwa mahali hapo.
“Hatujui, ila alikwenda huko. Unamjua?” aliuliza Jumanne.
“Hapana! Wapo wengi sana, au labda mngenionyeshea picha zake,” alisema kijana huyo.
Hawakutaka kumficha, waliona kwamba huyo ndiye angekuwa msaada wao mkubwa. Wakamwambia kilichokuwa kimetokea, jinsi kijana huyo alivyotumia nafasi ya kuokota chupa na kuwaibia kiasi kikubwa cha pesa.
“Huyo atakuwa Ibra!” alisema kijana huyo.
“Kwa nini?”
“Alikuja hapa na kusema kwamba haokoti tena chupa! Maisha yake yanakwenda kuwa ya kitajiri,” alisema kijana huyo.
“Tutampata wapi?”
“Nendeni Ilala Bungoni, kule kulipokuwa na Chuo cha DSJ, kuna nyumba ina rangi ya Bluu, hapo kuna watoto wengi wa mitaani, yupo hapohapo,” alisema kijana huyo.
Itaendelea.