~!~Sambusa ni tamu bwana~!~

~!~Sambusa ni tamu bwana~!~

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Joined
Mar 10, 2006
Posts
34,092
Reaction score
43,265
Nipeni kiti nikae, nikae na niteteme,
Ndugu msinishangae, nililonalo niseme,
Ya chakula cha ukae, maneno yangu nipime,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za kitanzania!

Nilialikwa na Rozi, Fatuma naye Amina,
Nikawa kama balozi, mlaji mwenye amana,
Hawakupika mbaazi, bali sambusa kwa sana,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania!

Ilikuwa tafrija, ya vyakula vya nyumbani,
Chakula kimoja moja, kikajapangwa mezani,
Mtori sinia moja, na pilau mdalasini
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania.

Pembeni wali wa nazi, na nyama ya binzari,
Bakuli ya maandazi, yaliyopikwa vizuri,
Sikuifanya ajizi, wa kijiji sina shari,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za kitanzania!

Vyote hivyo sikutaka, nilichotaka sambusa,
Kuleni mnavyotaka, wadada niliwaasa,
Mkila mlivyopika, niachieni sambusa,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania!

Ndipo nikala za Rozi, sambusa zilivoiva,
Nilikula kama chizi, kama ninakula mbeva,
Nikatafuna kwa pozi, utadhani mi dereva,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za kitanzania!

Ndipo kaleta Fatuma, sambusa kanigawia,
Ulimi nikajiuma, utamu kuniingia,
Nikakumbuka Dodoma, Sambusa zake Sofia,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania!

Ndipo akaja Amina, sambusa kunipatia,
Funga kazi kiaina, jinsi kanipakulia,
Nikala tena na tena, manusura kuzimia,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania!

Kama hujala sambusa, hasa za Kitanzania,
Hujui unachokosa, utamu wauachia,
Jaribu hata Mombasa, bure watakupikia,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania.

Si fumbo nililosema, msianze kuwazia,
Wajanja mkalalama, kusema nawafumbia,
Yote niliyoyasema, ni sambusa nasifia,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania

Kaditamati natama, beti haziendi tena,
Kapiga simu Rehema, mwaliko katoa jana,
Juma lijalo kasema, ni kwake kwenda jichana,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania!


Na M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)
 
Mzee shukrani naona umenchokoza acha nipumzike kidogo nitarudi
 
Heshima na taadhima, uwanjani naingia,
jama simameni wima, la mgambo limelia,
walio kwenye mlima, mabondeni nao pia,
Sambusa mie siili, ni heri kula muhogo.

Sambusa iwe ya moto, utamu sikilizii
hata majira ya joto, sambusa siililii,
ya baridi au moto, sambusa sing'ang'anii,
Sambusa mie siili, ni heri kula muhogo.

Sijui utamu wake, sambusa waisifia,
yenye mapishi ya kike, ya Rozi ama Sofia,
Fatuma naye apike, na warembo wa dunia,
sambusa mie siili, ni heri kula muhogo.

Sambusa nina aleji, Mwanakijiji ifaidi,
afadhali ninywe uji, panapo siku ya idi,
iwe kutoka Rifiji, ama kule Bariadi,
sambusa mie siili, ni heri kula muhogo.

Niulize ni kwa nini, sambusa siitamani,
ina huo walakini, wa toka enzi jamani,
hata uweke na nini, mimi niko alejini,
sambusa mie siili, ni heri kula muhogo.


Muhogo nautamani, mie kwetu kijijini,
sambusa mi asilani, ni ya nyinyi wa mjini,
muhogo wa dizaini, sambusa mie ya nini,
sambusa kula mwenyewe, hata ile ilo chacha.
 
mama weee..

Mama nakupa elimu, ya vyakula vya nyumbani,
Miogo ni kazi ngumu, mpaka uichimbe chini,
Sambusa yajaza hamu, miogo siitamani,
Jaribu kula sambusa, mihogo hutatamani!

Namfahamu Saida, apenda vyote viwili,
Miogo ni kama ada, hata yenye pilipili,
Na sambusa bila shida, anazila mbilimbili,
Jaribu kula sambusa, mihogo hutatamani
 
nami ninene yakwangu, yanayotoka moyoni
wa kijiji na mamangu, halo nawasalimuni
hakika hili la kwangu, nalinena kwa yakini
siitamani sambusa, wala muhogo wa shamba

mie napenda matunda, yanayotoka mtini
yale hayawezi vunda, mimi nawaambieni
Adamu aliyapenda, akakiuka yamini
siitamani sambusa, wala muhugo wa shamba

kwa chai ya asubuhi, vyakula vikasheheni
jamani ninawasihi, matunda jitengeeni
kula papai la bahi, au pera la handeni
siitamani sambusa,wala muhogo wa shamba

matunda ya mchanyato, rafiki utamuwini
hasa yale ya Lushoto, yalimwayo milimani
hamtapata majuto, wapendwa yajaribuni
siitamani sambusa, wala muhogo wa shamba

sambusa kichefuchefu, wapikavyo siamini
wanaweka nyama mfu, iliyokufa kundini
miye hiyo yanikifu, kwanini waitamani?
siitamani sambusa, wala muhogo wa shamba

kuna mihogo michungu, yachonyota kama nini
hata upike kwa chungu, magadi uweke ndani
hautaila mwanangu, utawashwa mdomoni
siitamani sambusa, wala muhogo wa shamba

kaditama wa tamati, nimefika kituoni
unidunde kwa manati, au konzi la kichwani
mimi hapo hunipati, sitiwi majaribuni
ni heri nile mabungo, nijilambe mdomoni.
 
Mzee mwanakijiji, asante kwa ushauri,
sambusa wanazifoji, wanatia na shayiri,
sitaki mie kuhoji, ulosema mhariri,
nitajilia muhogo, huhitaji spais.

mihogo yachimbwa chini, asili yenye ashki,
sambusa ninaihini, abadan siitaki,
yasagwa nyama buchani, iliyokuwa mabaki,
nitajilia muhogo, huhitaji spais.


Sambusa na bakteria, ni kama chanda na pete,
spaisi ukatia, na vipande vya mkate,
sambusa kufaidia, shuruti uipakate,
nitajilia muhogo, huhitaji spais.


Nachelea na magonjwa , ya sambusa ilo lala,
jee nayo utainywa, juisiye si jaala,
mwenzangu we utawashwa, uitupe kwa jalala,
sambusa niya wabwanga, asilani sithubutu.
 
SAMBUSA NI KITU GANI KITAMU NI KITUMBUA

Ntakupa hata kigoda,Ili haya utambue
Utamezea na soda,Ila lazima ujue
Hujakutana na Rhoda,Akakupa uchague
Sambusa ni kitu gani,Kitamu ni kitumbua

Sambusa imekauka,Ina mafuta ya choyo
Wakati mwingine yanuka,Haipozi hata moyo
Yakutaka kukuruka,Ili weze tuza moyo
Sambusa ni kitu gani,Kitamu ni kitumbua

Kitumbua cha mafuta,Utamuwe siulize
Hata huwezi pauka,Utang'ara nikwambie
Kipata sichopasuka,shida zako zitatue
Sambusa ni kitu gani kitamu ni kitumbua

Kitumbua kama nesi,Chaponesha njaa yako
Wala usile upesi,Utakabwa koo lako
Kuna vile vya wadosi,Vyeupe viso ukoko
Sambusa ni kitu gani,Kitamu ni kitumbua

Kwa sambusa wajiuma,Je ukila kitumbua
Muulize hata Juma,Cha Halima chasumbua
Kina ladha iso noma,Kama jipu watumbua
Sambusa ni kitu gani Kitamu ni kitumbua

Chaliwa na sebuleni,Waweza kula chumbani
Ukipata siwe soni,Usifunge yako mboni
Alikula kaka Boni,Kaka ake dada Moni
Sambusa ni kitu gani,kitamu ni kitumbua

Sambusa nyingi mekula,Hakuna ilovutia
Nikila kwanza nalala,usingizi wanijia
Kwanza ina kilo dala,Dukani siwezi jia
Sambusa ni kitu gani,Kitamu ni kitumbua

Alinipa Fauzia,Kitumbua lichopikia
Kwa kuwa ni wangu dia,Hata sikukiringia
Wakijiji nakusia,Mwombe mina takugea
Sambusa ni kitu gani,Kitamu ni kitumbua

Kalamu yangu nashusha,sambusa kuikandia
Kwanza menikumbusha,Si kitu cha kusifia
Kitmbua chanirusha,Mwili akili pia
Sambusa ni kitu gani,Kitamu ni kitumbua
 
Mundu... mambo mazito hayo... shukrani!!!!

Mwanakiji umeyachokoza hizo shukrani zito kwa mistari.
Very interesting and impressing watu wana vipaji bwana, nakumbuka malenga wetu sijui bado hii programm ipo? maana vijiredio vimekuwa vingi mpaka tunashindwa nini tusikilize
 
Kumbe fani ya maelnga bado inadumu. Nimepata faraja kubwa mno kusoma beti za wahusika. Hongereni.
 
LOL.Leo nimefaidi kweli utamu wa sambusa, kitumbua na mhogo!
Hongereni sana malenga wetu. Ntafurahi zaidi kama mtiririko huu utaendelea.
 
Sambusa nasasambua,
Nakula na kucheua,
Vingine sitochukua,
Hizi nimezichagua.

Nakula nikirarua,
Nyamanyama nanyafua,
Utamu najing'atua,
Nikila ninachenua!

Kamwe sili kitumbua,
Mizizi sitochukua,
Sambusa zanikwatua,
Nang'ata kama halua!

Matunda yanichefua,
Ya miti yenye maua,
Mbegu zinanisumbua,
Mdomoni kuchambua!

Sambusa nimechagua,
Natafuna kama muwa,
Vidole vikichambua,
Ulimi ukirambua!

Hakika nimegundua,
Baada ya kuchungua,
Jaribuni mtajua,
Nanyi mtajishaua!

Onjeni mtatambua,
Sambusa mtakwapua,
Nanyi mtazinyakua,
Mkipewa mwachukua!

Nililosema mwajua,
utamue mwaujua
kuleni kama washua,
Sambusa nasasambua!
 
Nipeni kiti nikae, nikae na niteteme,
Ndugu msinishangae, nililonalo niseme,
Ya chakula cha ukae, maneno yangu nipime, Ya leo kali ya ulanzi au mnazi
Sambusa ni tamu bwana, hasa za kitanzania!

Nilialikwa na Rozi, Fatuma naye Amina,
Nikawa kama balozi, mlaji mwenye amana,
Hawakupika mbaazi, bali sambusa kwa sana,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania!

Ilikuwa tafrija, ya vyakula vya nyumbani,
Chakula kimoja moja, kikajapangwa mezani,
Mtori sinia moja, na pilau mdalasini
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania.

Pembeni wali wa nazi, na nyama ya binzari,
Bakuli ya maandazi, yaliyopikwa vizuri,
Sikuifanya ajizi, wa kijiji sina shari,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za kitanzania!

Vyote hivyo sikutaka, nilichotaka sambusa,
Kuleni mnavyotaka, wadada niliwaasa,
Mkila mlivyopika, niachieni sambusa,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania!

Ndipo nikala za Rozi, sambusa zilivoiva,
Nilikula kama chizi, kama ninakula mbeva,
Nikatafuna kwa pozi, utadhani mi dereva,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za kitanzania!

Ndipo kaleta Fatuma, sambusa kanigawia,
Ulimi nikajiuma, utamu kuniingia,
Nikakumbuka Dodoma, Sambusa zake Sofia,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania!

Ndipo akaja Amina, sambusa kunipatia,
Funga kazi kiaina, jinsi kanipakulia,
Nikala tena na tena, manusura kuzimia,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania!

Kama hujala sambusa, hasa za Kitanzania,
Hujui unachokosa, utamu wauachia,
Jaribu hata Mombasa, bure watakupikia,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania
Si fumbo nililosema, msianze kuwazia,
Wajanja mkalalama, kusema nawafumbia,
Yote niliyoyasema, ni sambusa nasifia,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania

Kaditamati natama, beti haziendi tena,
Kapiga simu Rehema, mwaliko katoa jana,
Juma lijalo kasema, ni kwake kwenda jichana,
Sambusa ni tamu bwana, hasa za Kitanzania!


Na M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)
Ya leo ni kali mnazi au ulanzi lakini itanoga zaidi kama itanywewa na wisky.Bravooo
 
Heko tena Mzee Mwanakijiji!!! We ni zaidi hadi sasa!
Tunasubiri majibu kwa hamu!
 
mwanakijiji mzee,
watoto unilelee,
sambusa uwamegee,
mimi nakukatalia

nawe mama yangu wee,
una muhogo pekee,
wanangu siwatengee,
bibi watakulilia

amani kwa mambo wee!
eti washerehekee,
kitumbua bei chee,
si levo ya kwangu mie

tunda langu kwa wazee
wajilia kwa ushee,
hata uwaongezee,
nyumbani watachukua

tafakarini mazee,
hadithi muirejee,
nyumbani kwangu mjee
matunda niwapatie.
 
Kidete nimesimama
Kamwe sitashika tama
Kwa sambusa ilo nyama
Huwezi kunisakama

Kitumbua hamu yangu
Ila sio cha kizungu
Cheusi chenye ukungu
Chanipunguzia gundu

Kipike pishi la pwani
Au hata la ziwani
Kiweke mdalasini
Hutoacha kutamani

Mundu unalo tunda
Visheti au bumunda?
Ukinipa nitasunda
Kitumbua bado nyanda

Kitumbua chavutia
Kwa sharubati na bia
Laini kwa kujilia
Kinauzwa shingi mia

Sambusa si kitu kamwe
Ladha yake dome dome
Sura yake dume dume
Nakufanya upogome
 
Maharage

Sambusa na vitumbua, ni kwa ajili ya chai,
Onja na utatambua, vyote havina uhai,
Muhogo nao hauna, zile ladha anuai,
Maharage ya chumvi, kwa utamu tajilamba!
 
Back
Top Bottom