RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 60
“Uko wapi?”. Sauti ya yule mtu upande wa pili ikaniuliza kwa mashaka kidogo.
“Jardin Public kama tulivyokubaliana”. Nikaongea kwa kujiamini kisha kitambo kifupi cha ukimya kikafuatia na wakati ule upande wa pili wa ile simu kwa mbali nikasikia mazungumzo mafupi katika lugha ya Kirundi ambayo sikuyaelewa. Hatimaye ile sauti ikarejea tena hewani.
“Wewe ni Luteni?”. Ile sauti ikaniuliza kwa mashaka.
“Luteni kanali Luade Ngouma, nimeshafika Jardin Public, wewe uko wapi?”. Nikamuuliza yule mtu kwa kujiamini na wakati nikiendelea na yale maongezi kwenye ile simu mara nikaliona gari fulani likiingia kwenye barabara ya mzunguko wa ile bustani huku likitembea taratibu kiasi cha mtu yeyote mtembea kwa miguu kuweza kulipita pasipo jitihada kubwa. Dereva wa lile gari alikuwa amewasha taa za mbele zenye mwanga dhaifu au dimlight. Nikaendelea kulitazama lile gari kwa makini huku damu ikianza kunichemka mwilini.
“Tazama gari ndogo inayoingia kwenye mzunguko wa barabara ya hiyo bustani. Mimi nipo ndani ya hili gari”. Ile sauti ikazidi kusisitiza.
“Ndiyo nimeliona”. Nikaongea kwa hakika huku nikiendelea kulitazama lile gari namna lilivyokuwa likitembea taratibu kwenye barabara ya mzunguko wa ile bustani.
Ilikuwa gari ndogo aina ya Volkswagen Comb nyeupe, vioo vya ile gari vilikuwa vimewekwa tinted nyeusi hivyo sikuweza kuwaona watu waliokuwa mle ndani kwa urahisi.
“Ifuate hii gari hadi kwenye kona ndogo ya kuchepukia barabara ya Avenue Janvier. Tafadhali harakisha Luteni kabla mambo hayajaharibika zaidi”. Ile sauti ikasisitiza.
“Mko wangapi ndani hiyo gari?”. Nikauliza
“Tupo wawili, mimi na dereva”
“Tunaelekea wapi?”. Nikauliza kwa udadisi.
“Com on!, punguza maswali mengi Luteni. Laiti ungeijua hatari iliyopo mbele yetu usingepoteza muda hata sekunde”
“Kwa hatua tuliyofikia ni muhimu kufahamu kila kinachoendelea”. Nikaongea katika namna ya ushawishi huku kwa tahadhari nikitoka kwenye ile bustani na kuanza kulifuata lile gari kwenye mzunguko wa ile barabara huku mkono wangu wa kushoto ukiwa tayari umezama kwenye mfuko wa koti langu kuikamata vyema bastola yangu.
“Nakupa dakika tatu Luteni kama hutofika tutaondoka kwani hili eneo si salama”. Ile sauti ya upande wa pili kwenye simu ikasisitiza huku mzungumzaji akionekana kuwa ni mtu mwenye mashaka.
“Punguza dakika moja ya muda wako nitakuwa tayari nimefika hapo”. Nikaongea kwa msisitizo na kujiamini kisha nikakata ile simu na kuizima nikiitia mfukoni.
Muda mfupi uliofuata nikawa nimetoka kwenye ile bustani ya Jardin Public na kuingia kwenye ule mzunguko wa barabara, nikitembea kando kando ya ile barabara kwa tahadhari ya hali ya juu.
Kona ndogo ya barabara ya Avenue Janvier ilikuwa upande wa kushoto wa mashariki mwa ile bustani. Hivyo nikaona kuwa ingekuwa vyema endapo ningeshika uelekeo ambao ungenipelekea nitokezee nyuma ya lile gari na siyo mbele ambapo muonekano wangu pasina shaka yoyote ungeweza kuwatia mashaka wale watu waliokuwa ndani ya lile gari kuwa sikuwa Luteni Kanali Luade Ngouma waliokuwa wakimtarajia.
Mara moja nikageuka kutazama nyuma yangu, sikumuona mtu yeyote akinifuatilia na hali ile ikanitia faraja kuwa bado nilikuwa salama. Hata hivyo nilikuwa makini sana na mjongeo wa hatua zangu huku nikiyatembeza macho yangu kutazama huku na kule.
Hatimaye nikaiona ile gari Volkswagen Comb ikiwa imeegesha kwenye kona ndogo ya barabara ya Avenue Janvier, mwisho wa ule mzunguko wa bustani. Moyo wangu ulikuwa ukienda mbio isivyo kawaida huku kijasho chepesi kikianza kunitoka maungoni. Kwa tahadhari ya hali ya juu nikaendelea kutembea nikilifuata lile gari pale lilipokuwa limeegesha na kwa kweli moyo wangu ulikuwa umepoteza utulivu kabisa. Mishipa yangu mwilini ilikuwa ikisukuma damu katika presha ya hali ya juu, mikono yangu ilikuwa ikitetemeka na hatua zangu miguuni sasa zilianza kupwaya. Nilifahamu kuwa nilikuwa nikiikaribia hatari ambayo ingeweza kuugharimu uhai wangu lakini kamwe sikuwa tayari kurudi nyuma kwani wakati huu kila tukio mbele yangu lilikuwa na taarifa muhimu za kuelekea kukamilisha uchunguzi wangu.
Kupitia yale maongezi kwenye simu nilikuwa nimeanza kuhisi kuwa kulikuwa na jambo hatari na la siri lililokuwa limefichika baina ya Luteni Kanali Luade Ngouma na watu waliokuwa kwenye lile gari mbele yangu. Hatimaye nikalifikia lile gari na kupitia giza nene lililokuwa eneo lile nikafahamu fika kuwa isingekuwa rahisi kwa wale watu waliokuwa ndani ya lile gari kuweza kunishtukia kwa haraka kuwa sikuwa Luteni Kanali Luade Ngouma waliyekuwa wakimtarajia.
Nilipolifikia lile gari nikashika kitasa cha mlango wa nyuma na kujaribu kuufungua ule mlango huku tayari nikiwa nimeichomoa bastola yangu kutoka kwenye mfuko wa koti na kuikamata vyema mkononi. Mlango wa nyuma wa lile gari haukufunguka kwa urahisi kama nilivyotarajia na hapo hofu dhidi ya kushtukiwa hila yangu ikaanza kuniingia. Vioo vyeusi vya lile gari havikuniwezesha kuona mle ndani hivyo nikauacha ule mlango na kusogea dirishani kwa dereva na kuanza kugonga. Hata hivyo dereva wa lile gari hakufungua mlango wala kushusha kioo. Sekunde chache zikapita nikiwa nimesimama pale mlangoni kama sanamu na wakati nikiwa mbioni kukata tamaa mara dereva wa lile gari akawasha taa za mbele za gari. Kufuatia tukio lile nikahisi wale watu ndani ya lile gari walikuwa katika mkakati wa kutaka kujiridhisha kuwa nilikuwa Luteni Kanali Luade Ngouma na si vinginevyo. Taratibu nikaanza kuhisi jambo la hatari.
Loh! ule mwanga wa taa za mbele za lile gari ukanisaidia walau kuona kwa shida idadi ya watu waliokuwa ndani ya lile gari. Mzungumzaji kwenye ile simu alikuwa sahihi. Mle ndani kulikuwa na watu wawili tu na wote walikuwa wameketi sehemu ya mbele ya lile gari na ghafla wakati nikiendelea kutafakari mara nikaona kioo cha dirishani cha ule mlango wa dereva kikishushwa taratibu kisha nikaisikia vizuri ile sauti ya kike iliyokuwa ikizungumza na mimi kwa njia ya simu. Loh! moyo wangu ukalipuka hata hivyo nikajitahidi kuumeza mshtuko wangu.
“Fungua mlango wa nyuma uingie Luteni, tunatakiwa kuondoka haraka eneo hili”. Yule mwanamke alikuwa ameketi kando ya dereva na aliongea kwa kujiamini pasipo kugeuka na kunitazama dirishani. Sauti yake ikafufua vizuri kumbukumbu zangu akilini na hapo moyo wangu ukashtuka. Yule mwanamke alikwa Amanda kwani sauti yake nilikuwa nikiikumbuka vyema. Kwa kweli sikuwa nimetarajia kabisa kuwa yule mwanamke niliyekuwa nikuzungumza naye kwenye simu angekuwa yeye. Kukutana kwa mara nyingine na mwanaharamu yule kwangu ilikuwa ni zaidi ya bahati niliyokuwa nikiisubiri katika maisha yangu.
Bila kupoteza muda nikasogea nyuma na kufungua mlango, mara hii mlango ule ulifunguka bila pingamizi na hapo nikaingia mle ndani kama zombi. Amanda na yule dereva wakageuka nyuma haraka kunitazama, nikagundua kuwa wasingeweza kunitambua kwa urahisi kwa vile kichwani nilikuwa nimejifunika kofia ya koti langu la mvua. Hatimaye wakanipigia saluti za kijeshi na tukio lile likanipelekea nijisikie kuuvaa vizuri uhusika wa Luteni Kanali Luade Ngouma. Nikazijibu salamu zile za kijeshi kwa weledi wa hali ya juu bila kuzungumza neno lolote na kwa kuwa kule nyuma nilikuwa nimeketi peke yangu hali ile ikanipa faraja. Bastola yangu nikaikamata vyema mkononi. Amanda alipogeuka kutazama mbele akamwambia yule dereva aendeshe gari ili tuondoke eneo lile na hapo safari ikaanza.
“Mambo yameharibika Luteni. Tunahitaji kutoroka nchi hii haraka iwezekanavyo”. Amanda akavunja ukimya.
“Una maanisha nini?”. Nikamuuliza Amanda kwa udadisi huku taratibu nikiiruhusu risasi moja kuingia kwenye chemba ya bastola yangu mkononi sambamba na kikohozi cha kujifanyisha. Amanda akageuka tena nyuma kunitazama na namna ya utazamaji wake ukanitia shaka. Lakini kwa kuwa nilikuwa nimejifunika kofia ya koti langu ingelimchukua muda mrefu kunitambua. Sikuoneshwa wasiwasi wowote hivyo hatimaye Amanda akageuka tena kutazama kule mbele na kuendelea kuongea.
“Baadhi ya wenzetu wametusaliti kwa kuvujisha siri za mipamgo yetu ya mapinduzi ya kijeshi kwa wanajeshi watiifu kwa serikali. Taarifa zinaonesha miongoni mwa makomredi wetu wapo waliokamatwa na wengine kuuwawa kinyama”
“Nani aliyekupasha habari hizo?”. Nikauliza kwa shauku.
“Watu wetu tuliowapandikiza kwenye vitengo vya usalama”. Amanda akaongea huku akiitazama saa yake ya mkononi.
“Tunatoroka kuelekea wapi?”. Yule dereva akauliza kwa shauku.
“Nchi yoyote tutakapokubaliwa kupata hati ya ukimbizi wa kisiasa”. Amanda akafafanua huku akigeuka na kumtazama yule dereva.
“Vipi kuhusu mgao wa pesa?”. Wasiwasi ukiwa mbioni kumvaa yule dereva nikamsikia akiuliza kwa sauti iliyopwaya.
“Huu siyo wakati wa kufikiria pesa. Tunachotakiwa sasa ni kutafuta namna ya kutoroka kwanza kabla hatujakamatwa”. Amanda akasisitiza hata hivyo maneno yale hayakuonekana kumuingia vizuri yule dereva.
“Tunahitaji kwanza pesa. Bila pesa hatuwezi kuvuka mipaka ya nchi hii. Tutakamatwa kama panya kwenye tenga na baada ya hapo tutateswa kinyama kabla ya kupigwa risasi za kichwa. Loh! laiti ningelijua nisingejiingiza kwenye mpango huu…”. Yule dereva hakumaliza kuongea akakatishwa na mguso wa mdomo wa bastola ya Amanda kichwani mwake.
“Acha kulalamika wewe muoga”. Amanda akamfokea yule dereva.
“Pesa ziko wapi?”. Nikauliza kwa udadisi na hivyo kuuzima mjadala baina ya Amanda na yule dereva.
“Maelezo niliyapata kuhusu sehemu ilipofichwa fedha ni ya uongo. Nimejaribu kupeleleza sehemu hiyo bila mafanikio”. Amanda akajitetea.
“Maelekezo hayo uliyapata wapi?”. Nikauliza.
“Niliyapata kutoka kwa mmoja wa watu wetu wa benki lakini mtu huyo kwa sasa ni marehemu”. Maelezo ya Amanda yakanipelekea nilikumbuke vizuri lile tukio la kwenye kile chumba Amanda alipomuua yule mwanaume baada ya kumalizia kufanya naye mapenzi. Sasa nilianza kupata picha juu ya nini kilichokuwa kikiendelea. Amanda na wenziwe walikuwa wakitarajia kupata kiasi fulani cha fedha pengine kwa ajili ya kufanikisha jaribio lile la mapinduzi ya kijeshi huku yule mtu aliyeuwawa na Amanda kwenye ile nyumba akiwa ndiye kiungo muhimu katika ufanikishaji wa upatikanaji wa fedha hizo. Huku yule mtu aliyeuwawa akiwa ameahidiwa nafasi ya kuwa gavana wa benki kuu ya Burundi mara baada ya mapinduzi hayo kufanikiwa.
Nikaanza kuwaza kiasi cha pesa ambacho kingeweza kugawanywa kwa watu muhimu katika mapinduzi yale. Kwa vyovyote kilitakiwa kiwe kiasi kikubwa cha pesa za kuhamasisha, pesa ambayo kwa vyovyote ingekuwa ya magendo. Maelezo ya Amanda pia yakanipelekea niikumbuke vizuri ile bahasha ndogo niliyoichukua chini ya godoro kule chumbani kwenye ile nyumba. Nikakumbuka kuwa ndani ya ile bahasha kulikuwa na ramani ndogo isiyoeleweka. Mara moja nilipokumbuka vile akili yangu ikachangamka kwani kupitia ile ramani ningeweza kuyafikia maficho ya fedha hizo na hakuna mtu mwingine ambaye angeifahamu vizuri siri ile.
“Ni lazima tufikirie namna ya kufanikisha kutoroka kwetu kwani kwa sasa suala la kupata fedha tuliyokuwa tukiitarajia halipo tena”. Amanda akaendelea kujitetea kisha akaingiza mkono mfukoni na kuchukua bahasha ndogo ya kaki. Nilipoitazama ile bahasha haraka nikaikumbuka kuwa ilikuwa ni ile bahasha ambayo Amanda aliichukua chumbani kwenye ile nyumba baada ya kumuua yule mwanaume kitandani.
Amanda alipoifungua ile bahasha akatoa karatasi fulani kutoka kwenye ile bahasha na kwa kuwa kulikuwa na giza akataka kuwasha taa iliyokuwa kwenye paa ya lile gari ili sote tuweze kuona kilichokuwa kwenye ile karatasi. Haraka nikashtuka kuwa ile taa endapo ingewashwa ingeweza kunifichua hivyo nikawahi kutumbukiza mkono mfukoni kuchukua kurunzi yangu kisha nikaiwasha na kumulika kwenye ile karatasi.
Tukiwa tumezama katika kuichunguza ile karatasi ndiyo lilipotokea tukio ambalo kamwe sikulitarajia katika fikra zangu. Ghafla tukasikia mshindo mkubwa uzioelezeka masikioni, kisha nikasikia sauti fulani zisizoeleweka kama za watu wanaopiga mayowe ndani ya kisima kirefu kisichokuwa na maji. Kelele kama za mazimwi katika masimulizi ya kale, na hapo nikajihisi kama niliyerushwa kwa wepesi wa hali ya juu kwa nguvu isiyoelezeka kutokea nyuma yangu. Kisha kichwa changu kikapigwa na dhoruba kali wakati niliposikia kelele za mpasuko mbaya masikioni mwangu. Kichwa changu kikavamiwa na ulevi mkali nisioujua chanzo chake, wingu zito jeusi likatanda kwenye mboni za macho yangu kisha maumivu makali yakaanza kusambaa mwilini kama niliyepigwa shoti ya umeme mkubwa.
Mara nikajiona nikididimia taratibu kwenye shimo refu lenye kiza kinene na jitihada zangu za kujinasua hazikuweza kufua dafu. Nikataka kupiga yowe ili niombe msaada lakini mdomo wangu ulinisaliti. Hatimaye taratibu nikafumba macho yangu, fahamu zangu zikitekwa na kupelekwa katika sayari nyingine na hapo sikuweza tena kufahamu kinachoendelea.
_____
Niliyafumbua macho yangu taratibu kisha pasipo kufanya mjongeo wowote masikio yangu nikayatega vyema nikijaribu kusikiliza sauti ya kitu chochote mle ndani. Sikusikia sauti yoyote, lile eneo lilikuwa na utulivu wa kupita kiasi. Nikajiuliza hapa ni wapi?, jibu sikulipata lakini maumivu makali yaliyosambaa haraka mwilini mwangu yakazirejesha kumbukumbu zangu.
Mara ya mwisho nikakumbuka kuwa nilikuwa kwenye gari Volkswagen Comb na mle ndani ya gari tulikuwa watatu, yaani mimi, Amanda na kijana mwingine dereva ambaye sikuweza kulifahamu jina lake. Tulikuwa tukielekea wapi?. Hapana sikufahamu tulipokuwa tukielekea, labda Amanda na yule kijana dereva wangeweza kulijibu swali lile kwa usahihi. Nikakumbuka kuwa tulikuwa kwenye mpango wa kutoroka, niseme walikuwa kwenye mpango wa kutoroka mahaini wale baada ya jaribio la mapinduzi ya kijeshi chini Burundi kugonga mwamba.
Walikuwa wamepanga kutorokea wapi vile?. Oh!, ndiyo Amanda alisema kuwa wangetorokea kwenye nchi yoyote ambayo wangeweza kupata hati ya ukimbizi wa kisiasa. Kha! Amanda atoroke?, kwanini anitoroke kirahisi wakati ana majibu mengi ya maswali yangu?. Kwanini anitoroke bila kulipa gharama ya ufedhuli alionifanyia?. Halafu nikakumbuka kuwa wasingeweza kutoroka kwa kuwa hawakuwa na fedha za kufanikisha kutoroka kwao.
Sasa tabasamu jepesi likachanua usoni mwangu pale nilipoikumbuka ile bahasha yenye mchoro kamili wa pesa ilipofichwa. Bahasha ambayo niliichukua kutoka kwenye ile nyuma ya yule mwanaume aliyeuwawa kwa kupigwa risasi na Amanda.
Tabasamu langu halikufika mbali, nikaliyeyusha taratibu kama kipande cha siagi kwenye kikaango cha moto kwani mishipa ya kichwa changu ilikuwa ni kama imeshtuka na hivyo kusambaza maumivu makali mwilini. Hata hivyo furaha ile haikutoweka, sasa nikataka niupeleke mkono wangu kwenye mfuko wa siri wa kipenyo cha koti langu kuipapasa ile bahasha. Loh! sikufanikiwa kwani kicheko cha mtu aliyekuwa pembeni yangu kikanishtua na hapo taratibu nikageuka kutazama upande wa kulia.
Niliona kitanda cha hospitali na juu ya kitanda kile alikuwa amelala mtu mmoja ambaye kamwe sikumfahamu. Taswira ya mtu yule hakika ilinitisha, alikuwa mtu mrefu sana na mweusi ti, alikuwa amevaa bukta nyeupe lakini bukta ile ilikuwa imelowa damu chapachapa, majeraha yaliyokuwa mwilini hayakufaa kutazamwa mara mbili, ni kama alikuwa amchomwa na kukatwa na kitu chenye ncha kali kama kisu, bikari au bisbisi. Mikono na miguu yake ilikuwa imefungwa kwa nyaya ngumu zilizopelekea mvilio wa damu sehemu zile. Kichwani alikuwa na majeraha mabichi sana yaliyovuja damu kwa muda refu na damu ile kuganda. Jicho lake moja lilikuwa limeng’olewa, sikio lake moja limekatwa na kutupwa kusikojulikana na mdomo wake ulikuwa umechanika hovyo kama sikio la mmasai. Loh! sikuwahi kumuona mtu aliyesulubiwa kinyama namna ile na hata alipocheka alionekana kama anayelia. Maumivu makali yalikuwa yamepita mwilini mwake na kiwango kile cha maumivu kilimfanya aonekane kama punguani kidogo, nati chache za kushikilia akili yake huwenda zilikuwa zimeanza kulegea.
“Unataka kufanya nini wewe?”. Yule mtu akaniuliza.
“Nataka kukaa”. Nikaongea huku nikitabasamu na hapo yule mtu akaendelea kucheka, kicheko chake kilipokoma akaniambia.
“Sasa utakaa vipi wakati umefungwa mikono na miguu?. Hii siyo sehemu ya starehe komredi”
“Kwani hapa ni wapi?”. Nikamuuliza yule mtu kwa shauku huku nikayafumbua vizuri macho yangu kutazama huku na kule na kwa kufanya vile nikamuelewa vizuri yule mtu aliyekuwa kando yangu akinisemesha. Mikono na miguu yangu vilikuwa vimefungwa na zaidi ya nguo yangu ya ndani sikuwa na nguo nyingine ya kunisitiri mwilini.
Nilikuwa nimelala juu ya kitanda chakavu cha hospitali chenye godoro chakavu la foronya ya mpira. Hatukuwa watu wawili tu mle ndani, tulikuwa zaidi ya watu ishirini na sita. Watu wale walikuwa wamefungwa kama mimi huku baadhi yao wakiwa watundikiwa dripu. Hali ya afya za watu wale zilikuwa mbaya sana. Baadhi walikuwa wamefunikwa kwa mashuka yaliyolowa damu ya muda mrefu na hivyo kuvunda. Wengine walikuwa uchi wa mnyama hawajafunikwa chochote na majaraha yao mwilini yalitisha mno kuyatazama. Wote walikuwa wamelala mle ndani isipokuwa mimi na yule jirani yangu ambaye nilipozinduka nilimkuta akiwa macho.
“Tupo sehemu ya mangojeo kabla ya kupelekwa kwenye chumba cha mahojiano”. Yule mtu akaniambia huku akiendelea kutabasamu kama mwehu na hapo nikahisi akili yake ilikuwa mbioni kufyatuka kutokana na kupitia mateso makali.
“Mahojiano ya nini?”. Nikamuuliza yule mtu kwa mshangao huku nikiendelea kukisahili vizuri kile chumba kikubwa. Kulikuwa na mlango mkubwa wa chuma upande wa kushoto hata hivyo mlango ule ulikuwa umefungwa. Upande wa kulia ukutani kulikuwa na matundu madogo mawili ambayo yasingeweza kuruhusu hata mkono wa binadamu kupenya na kupelekea hewa ya mle ndani iwe nzito mno. Kulikuwa na taa mbili za tubelight kwenye dari ya kile chumba zilizokuwa zikiangaza mle ndani na kupitia mwanga wa zile taa nikaweza kubaini kuwa ule ulikuwa usiku wa manane.
“Mahojiano ya kawaida tu, mfano wewe ni nani, umeoa au hujaolewa, unatokea wapi, kazi yako ni ipi na unafanya nini hapa Burundi”. Yule mtu akaendelea kunifafanulia na nilipomtazama nikagundua kuwa akili yake haikuwa sawa kabisa na wala hakuonekana kujuta kuwa mle ndani. Hata hivyo nikaendelea kuyatafakari maelezo yake kwa utulivu huku nikivuta picha. Loh! jasho likaanza kunitoka baada ya kugundua kuwa nilikuwa nimekamatwa na kuwekwa kizuizini, jasusi aliyeko kwenye tundu la kifo. Hofu ikaniingia na hapo nikageuka na kumuuliza yule mtu.
“Nimefikaje fikaje hapa?”
“Leo ni siku yako ya sita humu ndani. Ulipoletwa siku ile nikajua tayari umekufa kumbe una roho ngumu kama ya paka. Daktari akikuona atakusifu kwa kuzinduka mapema. Mimi ananilaumu sana kwa kutolala usiku kucha, mimi huwa namcheka tu”. Yule mtu akaendelea kuongea huku akitabasamu.
“Daktari yupi?”
“Daktari wa humu ndani”. Maelezo ya yule mtu yakanipeleke nimtazame kwa kutafakari kabla ya kumuuliza.
“Nililetwa peke yangu humu ndani?”. Nikamuuliza yule mtu kwa udadisi huku taswira ya Amanda ikijengeka kwa hasira kichwani mwangu.
“Uliletwa na mwenzako mmoja, wakadhani kuwa ni mzima kumbe keshajifia zamani”
“Wa kike au wa kiume?”
“Wa kiume, alilazwa kitanda kile kwa siku moja asubuhi kulipopambazuka wakashtukia kuwa tayari amekufa, wakamtoa na kumpeleka wanakokujua”.
“Una hakika kuwa alikuwa wa kiume?”. Nikamuuliza.
“Unaelekea unapenda sana wanawake wewe,eti eh?”. Yule mtu akaniambia huku akicheka na hapo nikatabasamu.
“Tuliletwa na nani humu ndani?”
“Mliletwa na wanajeshi nane wenye roho mbaya kama shetani”. Maelezo ya yule mtu yakanipelekea nitabasamu kidogo huku nikianza kuvuta picha ya hatari iliyoko mbele yangu. Yule mtu akaendelea.
“Nasikia waliwaokota kwenye ajali mbaya ya gari mkiwa hamjitambui”
“Nani aliyekwambia?”
“Niliwasikia wale wanajeshi waliowaleta humu ndani wakizungumza”
Mara moja kupitia maongezi ya yule mtu nikalikumbuka lile tukio la mwisho ambalo sikuwa nimelielewa kabisa. Tukio lililonipelekea kupoteza fahamu zangu na hapo ndiyo nikatambua kuwa tulikuwa tumepata ajali mbaya baada ya watu wote kwenye lile gari kuzama katika kuichunguza ile karatasi ya Amanda.
“Wewe ni nani?”. Nikamuuliza yule mtu nikijaribu kumpeleleza.
“Kepteni Amadou Coulibary Sidibe”. Yule mtu akajitambulisha huku akionekana kufurahishwa na jina lake, na hapo nikageuka na kumtazama vizuri. Jina lake lingefaa kufananishwa na majina ya watu wa nchi za Afrika magharibi, nchi kama Senegal, Burkinafaso, Gambia, Mali au Ivory coast.
“Unatokea nchi gani?”. Nikamuuliza yule mtu huku nikianza kufurahishwa na urafiki wetu.
“Natokea Mali”. Yule mtu akanijibu kwa kujiamini.
“Nchi ya Mali?”
“Ndiyo, natokea kaskazini mwa nchi ya Mali katika jimbo la Azawad. Umewahi kulisikia?”. Yule mtu akaniuliza mara hii akiacha kutabasamu na kunitazama kwa uyakinifu. Tukatazamana kwa sekunde chache huku akili yangu ikifanya kazi na kwa kufanya vile nikaikumbuka vizuri nchi ya Mali hususani jimbo lililoko upande wa kaskazini mwa nchi hiyo liitwalo Azawad. Ni katika jimbo hilo la Azawad ndiyo lilipochipukia kundi hatari la waasi wa Tuareg mapema mwaka 2012. Kundi hilo hatari la waasi likipigana kufa na kupona kuing’oa mdarakani serikali ya rais Amadou Toumani Toure. Lengo la kundi hilo likiwa ni kujipatia uhuru wake binafsi kama nchi nyingine za Afrika na kuliongoza jimbo la Azawad chini ya chama cha MNLA-Mouvement national de liberation de lʾAzawad kinachoongozwa na Bilal Ag Acherif.
“Mbali na kulisikia pia nalifahamu vizuri”. Nikamwambia yule mtu huku nikianza kuvutiwa na wasifu wake. Kisha ukimya kidogo ukapita nikiuma meno yangu baada ya maumivu makali kupita kichwani mwangu. Maumivu yale yalipopungua nikamuuliza yule mtu.
“Wewe ni mwanajeshi wa Tuareg?”
“Ndiyo wala hujakosea, nimefurahi umeniita vizuri sana komredi. Mwanajeshi wa Tuareg siyo muasi wa Tuareg kama vyombo vya habari vya magharibi vinavyojitosa kuunadi ubaya wetu. Sisi ni watu wema kabisa tunapigania uhuru wetu”
“Imekuwaje ukafika humu ndani?”. Nikamuuliza yule mtu kwa udadisi na hapo akasita kidogo.
“Tumekuja kusaidia mapinduzi ya kijeshi hapa Burundi”
“Mmekuja…?, wewe na nani?”
“Wenzangu, baadhi wametoroka na wengine ndiyo sisi humu ndani tuliokamatwa”. Nikamtazama yule na mara moja nikamuelewa vizuri. Alikuwa askari wa kukodiwa, yeye na wenzake.
“Nyinyi ni mamluki?”
“Tumekuja tu kusaidia mapinduzi ya kijeshi ya wenzetu wapenda haki kama sisi”. Yule mtu akijitetea.
“Mlikuwa wangapi?”......ITAENDELEA