Riwaya: Nitakupata tu

Riwaya: Nitakupata tu

NITAKUPATA TU

SEHEMU YA 023

******
Muziki ulikuwa ukisikika kwa mbali ukitokea ndani ya nyumba moja kubwa maeneo ya mbezi beach. Taa nyekundu zilikuwa zikiwaka kuonyesha kuwa ulikuwa usiku thabiti, usiku wa mahaba na usiku wa mapenzi. Mwanamke alikuwa katika vazi jepesi la kulalia ambalo hili lilimuonyesha mpaka nguo yake ya ndani aliovaa. Mkononi alikuwa na glass ya mvinyo mwekundu huku pembeni yake kukiwa na bastola. Muda wote alikuwa akiitizama saa ya ukutani kanakwamba ndio kwanza alikuwa akiitizama. Kila baada ya sekunde alikuwa akiitizama saa yake ya ukutani. Akaonyesha kukerwa na kitu, muda mfupi alinyanyuka na kuliendea pazia la dirishani. Alipolifikia akalifunua kisha akaanza kutupa macho yake nje akiangalia uzuri wa jiji la dar es salaam. Alisimama hapo kwa muda wa dakika kama mbili akitizama nje. Alionekana akimsubiri mtu, mtu ambaye alikuwa mpenzi wake ama hawara. Lakini bado muda ulizidi kwenda bila kumuona huyo mtu. Akiwa ameanza kukata tamaa akaliona gari nyeusi ikisogea taratibu ikielekea uelekeo wa kwake. Moyo wake ukachanua kwa tabasamu safi. Bado aliuvuta muda akiitizama gari ile ikiendelea kusogea. Punde mkono wake wa kulia ukapanda mpaka juu ya titi lake lake la kushoto. Akaishika chuchu na kuanza kuichezea polepole. Mara akaisikia honi ikitokea kwa nje. Akashuka taratibu kwa mwendo wake wa mapozi. Mtoto wa kipare alitembea kama analazimishwa. Alikuwa mwamvita Rajabu. Alikuwa hapo kwa minajili ya kuuburudisha mwili wake. Akaufungua mlango akaelekea huko kulifungua geti. Ni wakati akilifungua geti akashangazwa na kitu ambacho alikiona. "DAMU" Ndio neno pekee kumtoka mdomoni kwake. Kwenye mlango wa gari la mtu wake ilionekana damu ikichuruzika. Damu ikitoka ndani ya gari na kudondokea sakafuni. Hakulitegemea wala kulitarajia. Hilo likamfanya aduwae kwa sekunde kadhaaa akishindwa kufanya maamuzi. Hakuliwaza hilo, mwili wake uliwaza mapenzi, moyo wake ulihitaji kuburudishwa, lakini mbona damu tena? Hilo likamuondoa katika mawazo. Punde bastola yake ilikuwa mkononi akijivuta kuelekea garini. Macho yakizunguka mfano wa bundi alizidi kusogea. Akaufikia mlango kisha kuushika. Kwa kasi ya umeme akaufungua mlango...
"Mamaaaa" kwa mara ya kwanza Mwamvita akapiga yowe huku mwili wake ukimtetemeka. Mbele ya macho yake alikuwa akiiutizama mwili wa mpenzi wake ukiwa ukiwa umelalia usukani wa gari huku kichwa kikiwa hakitamaniki kutokana na kufumiliwa kwa Risasi. Akashikwa na woga, akaogopa na kutaka kurudi nyuma. Lakini akajipa utulivu, kukimbia haikuwa suluhu ya hiki kinachotokea. Alitakiwa kulijua tatizo, alitakiwa kujua nani ambaye amefanya mauaji haya. Akaendelea kuuangalia mwili wa mpenzi wake, damu ilikuwa ikiendelea kuvuja. Akaizunguka gari akiutafuta kila upande. Hakumuona mtu, ingawa hakumuona lakini akakiona kitu ambacho kilimpa hisia tofauti. Hii ilikuwa magazine ya risasi. Kwa nini magazine? Na kwa nini iko hapa? Ina maana hakuuawa hapa? Kama hakuuawa hapa, nani alikuja na hii gari hapa? Haya yalikuwa maswali, maswali ambayo bado hakupata jibu. Wakati akiendelea kujiuliza, mara akaiona gari nyingine ikija na uelekeo ule. Uelekeo wa nyumbani kwake. Akarudi na kujitupa uvunguni mwa gari. Ujaji wa gari ili ulimshtua sana. Akatulia pale uvunguni akiangaza macho kuelekea kule mbele. Bastola ilikuwa mkononi mdomo ukiitizama gari ile. Kidole kilikuwa tayari kwa kuiruhusu risasi akaamua kuivuta subira. Gari ile ikaendelea kusogea na kusogea. Hakuendelea tena baada ya kufika hatua sita, gari ikasimama kisha taa kuzimwa. Ukimya wa ajabu ukatokea. Hakushuka MTU kutoka kwenye gari na hapakuwa na dalili yoyote ya kushuka kwa MTU. Hata yeye akatulia akitaka kukiona kile kitakachotokea. Baada ya ukimya wa dakika mbili akauona mlango wa gari ukifunguliwa. Punde akashuka MTU ambaye alimtambua. MTU ambaye alimjua. Licha ya kumtambua lakini hakujitokeza. Bado hakuamini MTU na bado hakutaka kumuamini. MTU aliyeshuka alikuwa Jimmy . Hata pale alipoanza kusogea pale kwenye gari bado Mwamvita hakujitokeza. Bado alivumilia kuuona mwisho. Jimmy alikuwa amesogea na sasa alikuwa ameikaribia gari, macho yake yakakiona kitu mfano wa maji yakichuruzika kutoka ndani ya gari. Hakuwa mgeni wa maji Yale, na hakuwa mwepesi wakuamini kwamba yalikuwa maji. "Damu" ndio neno lililogonga kichwani. Wakati huo huo mkono wake ukashuka kiunoni na kuchomoa bastola yake. Akaendelea kusogea kwa hatua za mashaka. Akaufikia mlango ambao ulikuwa wazi. Macho yake yakatua juu ya mwili wa binadamu uliofumuliwa kichwa kwa risasi, akahisi baridi ikimuingia, baridi ya woga na fadhaa. Aliogopa na kuogopa. Hakuwahi kukiona kifo cha aina ile. Ni hapo alipokumbuka kuwa Mwamvita alikuwa ndani ama naye atakuwa ameshauawa. Akaliendea geti na kujaribu kulisukuma. Geti likamtii. Akaingia ndani sasa akiwa ameuvaa ujasiri. Hakuwa muoga tena. Akaanza kuzikwea ngazi kuingia ndani kabisa ya jengo. "Jimmy nipo huku." Ilikuwa sauti iliomfanya Jimmy ageuke kwa kasi ya umeme huku bastola mkononi. Hata alipomuona Aliyemuita hakuishusha bastola. Alikuwa akimuangalia Mwamvita kwa mashaka. Mashaka yakutokumuamini kwa kile alichokiona nje. Hakuwahi kuona Unyama wa aina ile. Kwa Mara ya kwanza akauona Umuhimu wa kuongeza watu. Hakuwahi kufikiria hilo.

*********
Alikuwa akiishi kama mwizi kama sio kibaka. Muda wote alikuwa akibadilika kama kinyonga. Mtaani alikuwa akitafutwa na wana usalama wa kila aina. Kila hoteli ilipandikizwa watu maalum wa kuchunguza kila aingiaye na atokae. Anayekuja kula na hata wale waliokuwa na mambo yao binafsi. Kila mmoja alikuwa akiangaliwa kwa umakini sana. Wana usalama walikuwa wakimtafuta masimba kila kona ya mtaa na hata mji. Wakati huku Dar yakiendelea hivi, Masimba alikuwa nje kidogo ya jiji LA dar es salaam. Hakuwa huko kwa sababu ya kuogopa purukushani za maafisa usalama wanao msaka. Bali alikuwa nyumbani kwa Mama wa Marehemu Asteria kupata kile ambacho alitaka kupewa kabla ya kifo cha mwanawe na hata mwanawe wa pili. Alitelemka kwenye daladala kama abiria wa kawaida. Kichwani alijifunika kwa kofia aina ya cowboy. Chini alivaa suruali sambamba na raba ambazo zilisababisha aonekane kama kijana mtanashati pale kijijini. Baada ya kushuka hapo akaingia sehemu yenye huduma ya vyakula. Akatafuta sehemu nzuri na kutulia kisha kuagiza chakula. Baada ya chakula kuletwa, akaanza kula taratibu huku macho yake yakiangaza huku na huko kuona kama alikuwa akifuatiliwa ama lah!
 
Ibra tuendelee kaka Yan hii story yako ina arosto aisee usikawie sana
 
NITAKUPATA TU

SEHEMU YA 024

Macho yake yalikuwa yakimtizama kila atokae na hata aingiae. Muda wote alikuwa akimshuku kila mtu ambaye angeingia na kusimama pasipo kufanya kitu. Alijua kinachoendelea Jijini ni kutafutwa kwake katika namna ya kipekee. Alitambua kujiokoa kutoka kuzimu ni kitu ambacho mkurugenzi na majasusi wote wasingekubali. Hakuna mtu alieingizwa ndani ya chumba kile na kutoka akiwa hai. Lakini kwake yeye aliweza na kuthubutu. Hilo ndio lingekuwa chanzo cha kutafutwa kwake. Na sio kutafutwa tu bali kupotezwa kabisa katika uso wa dunia hii. Maelezo kutoka kwa Teddy juu ya kinachoendelea kilimsisimua sana mwili wake. Watu wenye suti sambamba na waliovalia mavazi ya kawaida walikuwa wakipishana kumtafuta katikati ya jiji. Hata wale wa kike waliokuwa wakitembeza mboga za majano walikuwa wakimtafuta yeye. Nyumba yao haikukosa kuangaliwa kila wakati, wasichana wachafu wenye mabeseni yenye mboga za majani walipita kila wakati. Yote hiyo ilikuwa ni kutafutwa kwake. Hakuihofu taarifa hiyo kutoka kwa teddy, hakuiogopa kwa kuwa alikuwa ameizoea purukushani, alishazoea mapigano na hata kusumbuana na wana usalama. Aliutazama ujumbe ule kutoka kwa teddy kwa makini, aliporidhika akairudisha simu mahala pake. Akaendelea kula huku sasa akiiwaza kazi iliyo mbele yake. Kazi ambayo mwanzo haikuwa ngumu, kazi ambayo aliichukulia kama kazi ya kawaida. Lakini sasa ilikuwa ngumu baada ya kuingilia na Idara ya usalama wa taifa. Kitendo cha mkurugenzi kumkalipia kilionyesha ni kiasi gani mkurugenzi amekubali kudanganywa. Hakuamini na hakutaka kuamini kama Jasusi mwandamizi kama yeye anaweza kudanganywa kwa hila kisha kukubali. Hata alipowaza nani alipanga kile kilivhotokea hakuweza kugundua. Kuuawa kwa Godfrey Maboba na familia yake, kisha kukutwa na kikosi maalum cha kupambana na ujangili wa kutisha, ni mpango ambap ulipangwa na kutengenezwa na watu wanaomfahamu. Nani alimuona wakati anakwenda nyumbani kwa dada wa Marehemu Asteria. Hilo likampa picha kuwa mtu anayeogopewa na Teddy inawezekana ndio mpangaji wa haya matukio. Ndio huyu aliyemshawishi hata DG wa TISS akubali kukitenda kile ambacho hakuwaza kama kitatendwa na Mtu mwenye mafunzo yote kama yeye. Ni nani huyu anayeogopewa? Ni nani huyu mwenye nguvu kuliko Idara ya Usalama wa taifa? Ina maana hata kile kitengo chenye watu watano kimeshindwa kumgundua huyu mtu? Nina huyu? Yalikuwa maswali yaliyomtia hamu, hamu ya kumuona na kumjua huyo mtu. Alitaka kuonana naye uso kwa uso ama kumtafuta na kuhojiana naye kupitia mawasiliano. Hakuwahi kumuogopa mtu na hakuwahi kuogopa kabisa. Aliyawaza hayo akiendelea kula taratibu. Mara moja moja hakuacha kuangalia nje. Baada ya kumaliza kula sasa alikuwa tayari kwenda kwa mama wa marehemu Asteria. Akainuka kama kawaida huku macho yake yakimuongoza kwa kila hatua. Akakiacha kimgahawa kile na kuchepuka mpaka upande wa pili wa barabara. Ingawa alikuwa mgeni katika maeneo yale ya mkuranga, lakini alikuwa na maelezo yote ya kumfikisha nyumbani kwa mama Asteria. Alitembea kama mtu wa kawaida, wakati akiikaribia nyumba ile akamuona mtu akitoka ndani. Mtu ambaye alimshangaza na kumsisimua, mtu ambaye hakuamini kama angemuona pale. Alikuwa Teddy akitoka ndani ya Nyumba ya Mama wa Marehemu Asteria. Hilo likamstaajabisha, likamshangaza na kumduwaza. Teddy amefikaje huku, teddy amekuja kufanya nini huku? Yupo na nani? Wakati akijiuliza hilo, akamuona mtu mwingine ambaye alizifanya kengele za hatari kulia kichwani mwake. Huyu alikuwa Mwamvita, huyu alikuwa yule mwanamke aliyehusika na mlipuko kule kigamboni. Kwa Mara ya pili teddy alikuwa ameasi. Teddy alikuwa ameamua kurufi kundini kwake. Alikuwa ameikubali pesa na sio taifa lake. Kumbe wakati anatoa taarifa kuhusu wanausalama kuiweka chini ya uangalizi alikuwa akiipumbaza akili yake. Kumbe alikuwa yupo katika mipango ya kufika huku. Akauona usalama wa Mama Asteria kuwa mdogo.

Hakuweza kukurupuka, bado aliwatizama hasa akimuangalia Teddy. Alimuangalia kwa muda wote huku mishipa ya hasira ikajitokeza. Akawaona wakishuka ma kujipakia ndani ya gari kisha kuondolewa kwa kasi. Bado masimba aliduwaa, akili yake ilimtuma kuwahi pale, lakini bado kuna kitu alikihofu. Wakati bado anashindwa kitu cha kuamua, akamuona mama wa Asteria akitoka akiwa sambamba na kitoto kingine kidogo cha kike. Masimba akajitokeza sasa akielekea pale. Hatua ya kwanza kupiga akahisi kitu, kitu ambacho hakukijua. Hatua ya pili akahisi kitu kingine ambacho hata hiki hakukijua. Hatua ya tatu akagundua kuwa alikuwa akitizamwa na mtu kutoka sehemu fulani. Akaendelea kutembea akiziamini hisia zake, hisia ambazo hazikuwahi kumdanganya. Sasa akaikaribia nyumba ile, zilikuwa ni hatua tano kutoka ilipo nyumba. Kengele za hatari zikagonga tena. Safari zikiambana na uhatari wenyewe. Mama alikuwa akitabasamu, alikuwa akimuangalia masimba. Mkono alikuwa ameshikilia simu kubwa, simu ambayo kwa macho ya Masimba haikuwa simu, haikuwa simu ya aina yoyote bali ilikuwa rimoti, akili za masimba zikafanya kazi kwa haraka sana.. akaanza kukimbia huku akimuomba mama yule aitupe ile rimoti. Kabla hajamfikia akashuhudia mama yule akibonyeza kitu. Kilikuwa kitendo cha sekunde tatu Masimba kuruka hewani na kutua pembeni kabisa ya barabara. Mlipuko mkubwa ukasikika. Moto mkubwa ulikuwa angani huku jumba la mama wa Asteria likiwaka moto. Kilikuwa kishindo kilichotingisha mji wote wa mkuranga. Masimba alikuwa akikimbia kwenye moto kwenda kumuokoa yule mama. Hakuujali moto, hakujali kelele za watu ambao walikuwa wakipiga kelele. Alikimbia na kuingia katikati ya moto. Baada ya kuingia akaanza kutafuta. Alitafuta kwa shida kutokana na hewa nzito. Wakati anataka kukata tamaa akasikia sauti ya mtu akilia. Akaangalia hapo kwa tabu, akamuona Mama wa Asteria akiungua huku akimngika mjuu wake asiungue. Haikuwa picha nzuri kuitizama. Alisogea haraka na kumshika yule bibi. Akataka kumuinua lakini yule mama akamzui. Hata macho yake yalikuwa yakionyesha kukata tamaa.

"Naku....faaa mwa mwa.. nangu.. nao..mba muokoe huyu ni..nia.che mimi nife." Aliongea mama kwa uchungu huku machozi yakimtoka. Masimba hakuchelewa akamuangalia mama kwa sekunde. Akamuachia mkono huku akilia kwa uchungu. Akamchukua mtoto na kuanza kutoka naye. Hakutoka kupitia alipoingilia bali alitokea kwa upande wa nyuma. Mtoto alikuwa begani. Akafanikiwa kuuvunja mlango wa nyuma. Akatoka sambamba na mtoto yule. Akakimbia naye mpaka sehemu ambayo kulikuwa na watu wengi akasimama kisha kuomba maji. Hayakuwa maji ya kunywa, mwili wa mtoto ulikuwa na moto. Akamuweka mtoto chini ili apewe huduma ya kwanza. Lakini kumuweka tu chini akagundua mtoto alikuwa ameshakufa. Ameshakufa sambamba na bibi yake. Masimba hakuamini, hakuamini kama yule mtoto amefariki. Akaendelea kumtingisha kwa nguvu huku akilia. Lakini halikuubadilisha ukweli. Mtoto yule alikuwa ameshakufa. Masimba akamuangalia kanakwamba haamini kama yule mtoto amekufa. Teddy alikuwa amemrudisha tena kwenye maumivu. Akasimama huku watu wakimshangaa. Akarudi kwenye utimama wake. Ilikuwa ni lazima arudi kwenye utimamu wake. Kila kitu kilikuwa kigumu kwake. Alikuwa teddy pekee aliyeijua safari yake ya kwenda mkuranga. Ni yeye aliyejua kwamba anakwenda kuonana na mama wa Asteria. Kwahiyo hapa alijua teddy ndiye amehusika na kitendo kile cha kinyama
 
NITAKUPATA TU

SEHEMU YA 025

Teddy pekee ndiye aliyekuwa akiifahamu safari yake. Safari ya kwenda kuongea na Mama wa Asteria. Lakini ni Teddy huyu huyu ambaye alimuona akiwa sambamba na mwamvita. Teddy ambaye alimueleza kuwa hakuwa tena kule. Teddy ambaye alimuamini na kuamini maneno yake. Lakini leo hii teddy alikuwa ameamua kuimaliza familia ya Asteria. Mama yake alikuwa akiendelea kuteketea na moto, huku mtoto mdogo wa kike akiwa amelala mbele yake akiwa hana uhai tena. Hilo likamuuma sana? Licha ya kuumia lakini hakutakiwa kuwa pale. Ulikuwa muda wa kuondoka na kupotea kabisa. Hakujali macho yaliokuwa yakimtizama, hakujali vilio na ving'ora vya polisi.. aliondoka akiwa amechanganyikiwa, aliondoka akiwa na Hasira na teddy, alitamani kupiga Risasi katika kichwa chake. Alianza na Asteria akafuatia Mwamvua, kisha dada yake na familia yake akiwemo Mumewe, Mr Godfrey Maboba. Sasa ameamua kuwamaliza wote. Kuna siri gani hapa nyuma? Ina maana ni mzigo tu wa madawa ndio sababu ya vifo vyote vile? Hapo akahisi kitu kingine, alihisu kuna kitu kingine nyuma ya mauaji haya. Alihisi hivyo na aliamini hivyo. Akaamua sasa kumfungia kazi Teddy, alitaka kwenda kumuonyesha kuwa yeye ni mtu mwingine katika medani ile. Kama mzigo wa madawa ameshauchukua kipi kinampa hofu teddy? Kwa nini aendelee kuua? Hakuweza kujibu hilo swali bali akasonya na kutukana tusi zito. Baada ya kutembea sana akajikuta akitokea sehemu yenye kituo cha daladala, bila kujali macho ya watu, akajipakia ndani ya costa moja na safari ya kurudu dar ikaanza. Muda wote wa safari alikuwa amekiinamisha kichwa chake kwenye siti akiliwaza tukio lililotokea punde. Sauti ya mama wa Asteria ilikuwa ikijirudia kila wakati. Tukio zima liliendelea kumtesa. Akatamani afike Dar akamuone Teddy. Alikuwa tayari ameapa kwenda kuitumbukiza Risasi Kichwani kwa Teddy. Ni wakati akiliwaza hilo akausikia Ujumbe ukiingia kwenye simu yake. Akataka kupuuza, alitaka kutoitazama simu, lakini akaisikia sauti ikimwambia "wewe ni mpelelezi unayetafutwa usipuuze kitu."!!! Akaitii sauti ile. Muda mfupi vidole vyake vilikuwa na kazi ya kuifungua Meseji.

"Uko salama, nasikia kuna nyumba imelipuliwa huko!!!? Ulisomeka Ujumbe ulionekana kutumwa na Teddy. Hilo pia hakuliacha lipite hivi hivi. Teddy alikuwa akimchezea akili yake, teddy alikuwa akimuona mjinga. Lakini kingine kilichomfurahisha ni kule kugundua kuwa teddy hakuwa amemuona wakati akitoka ndani. Hilo likampa uhuweni wa kumfikia pasipo rabsha yoyote. Teddy alikuwa ameingiwa na tamaa, ni yeye na mwamvita waliotoka ndani ya nyumba ya mama wa Asteria. Lakini muda huu anamtumia Ujumbe kuhusu kilichotokea, alikuwa akiipima akili ya masimba. Hakuona sababu ya kumjibu, akaitizama simu kwa muda kisha kuirudisha mfukoni. Alimchukia teddy na bado alitamani kufika Dar es salaam akutane nae.

*******
Alishuka maeneo ya mbagala saa moja na nusu usiku. Baada ya kushuka hapo akaona ilikuwa muhimu kumpigia teddy kutaka kujua wapi alipo. Akatafuta sehemu yenye utulivu akaipiga simu ya teddy, lakini cha ajabu haikuwa hewani. Akajaribu tena na Tena lakini bado hali ikawa ni hivyo. Simu ya teddy haikuwa ikipatikana. Akakiona kitu ambacho alikihisi hapo mwanzo. Teddy alikuwa amemchezea akili yake, inawezekana alimuona kule ndio maana akamtumia ule ujumbe. Sasa kutokupatikana kwa teddy kilikuwa ni kitu kingine cha kushangaza. Akaona haukuwa muda wa kuendelea kubaki mbagala. Ilikuwa ni lazima arudi kinondoni kwa usiku ule. Lakini kabla hajaamua kurudi lazima awasiliane na rafiki zake ambao wapo katika nafasi nyeti nchini. Wa kwanza kumpigia alikuwa Dee Plus, huyu alikuwa mmoja kati ya vijana wake. Aliongea naye mawili matatu. Baada ya hapo akarudi tena kituo cha daladala. Hapo akachukua usafiri wa kuelekea huko.

********
"Masimba anaelekea mkuranga kwa mama wa Asteria. Hakikisheni anazuia au mama anafutwa katika uso huu wa Dunia." Ilikuwa sauti ya teddy akiongea na mwamvita. Simu hiyo alipiga baada ya kikao kizito kati yake na washirika wenzake kufanyika na kufanikiwa kumrudisha teddy kundini. Ni simu hiyo ambayo iliwalazimu teddy na mwamvita kuelekea mkuranga. Ni simu hiyo iliyotumika kumtumia ujumbe masimba kwamba alikuwa akisakwa na wanausalama. Ujumbe ule kwenda kwa masimba ulitumwa na teddy wakati huo wakiwa mkuranga. Aliutuma mahususi ili kumfanya masimba achelewe kurudi Jijini, ili watu wao waendelee na utafutaji wa mzigo wao ambao uliibiwa. Licha ya watu waliotumwa kuipekua nyumba ya masimba nje ndani na ndani nje. Hawakuweza kupata chochote. Hawakuweza kuupata mzigo wao, mzigo ambao ndio chanzo cha mauaji na uasi uliofanywa na Teddy. Lakini kingine ambacho kiliwashangaza Jimmy na washirika wake, nikule kuambiwa hata masimba hawakumuona kule mkuranga. Ni taarifa hiyo ambayo bado ili wachanganya na kuwafanya kila mmoja awaze lake.. ndipo hapo amri ilipotoka kwamba wategeshe bomu ndani ya nyumba ya mama wa Asteria na kabla ya hapo walipewa amri ya kumsubiri masimba hapo. Muda ulivyokuwa ukisonga na kutokuonekana kwa masimba ndipo maamuzi ya kilichotokea mkuranga yakafanyika. Hawamuona masimba wakati akisogea pale, hawakumuona kwa kuwa walikuwa katika uharaka wa kuondoka. Na hicho ndicho walichokosea.

**********

Simu ya teddy bado haikupatikana licha ya kuipiga mara kwa mara. Bado hakikuwa kitu cha kawaida kwake, teddy amtumie meseji lakini ndani ya muda huu alikuwa hapatikani. Haikuwa kawaida kwake, haikuwa kawaida kwa kuwa alimfahamu teddy. Wakati akiwaza hilo akausikia mlio wa simu yake kuonyesha kwamba alikuwa akipigiwa. Ikaichomoa simu, akatupa macho Juu ya kioo, akakutana na namba mpya. Akaitizama ile simu kwa muda bila kuipokea mpaka ilipokatika. Hakuwa na utaratibu wa kupokea namba ngeni katika kazi yake hii ya hatari. Baada ya ile simu kuita na kukata bila kuipokea, akapata hisia za kuingalia namba ile vizuri, alitaka kumjua mmiliki na alitaka kujua inapigwa kutoka wapi. Muda mfupi alikuwa akiongea na simu Nyingine hewani. Baada ya kukata akatulia akisubiri kupata maelekezo kutoka kwa mtu wake. Haikupita muda muda mrefu simu yake ikaita tena. Alikuwa ni yule mtu wake. Akaipokea na kuongea kwa dakika kama moja hivi kabla ya kuikata simu. Mwili wake ulisisimkwa na kushikwa na ubaridi. Namba mpya iliompigia ilipigwa kutokea katikati ya jiji la dar es salaam maeneo ya posta. Ilikuwa taarifa aliyoitegemea kqbisa. Alijua simu hiyo ilitoka kwenye moja ya majengo yanayomilikiwa na Idara ya Usalama Wa Nchi. Hilo likamfanya aamue kuelekea huko, alitaka kwenda kumjua mwenye namba ile. Hakuwa na sababu ya kuogopa wakati alikuwa akisakwa. Baada ya daladala aliopanda kufika maeneo ya uhasibu alishuka, kisha akachukua usafiri wa pikipiki mpaka maeneo ya posta. Alishuka na kulipa ujira kisha kuongoza kuelekea pale ambapo alipakusudia. Alitembea kwa uangalifu mpaka maeneo ya bandarini nje ya kituo cha mabasi yaendayo kasi. Kulikuwa na umbali mfupi sana kutoka kwenye jengo binafsi linalotumiwa na usalama wa taifa. Jengo ambao lilikuwa likitizamana na Makao makuu ya Mamlaka ya mapato Tanzania. Vilevile ulikuwa umbali mfupi na kilipo kituo kikuu cha polisi Dar es salaam (Central police) baada ya kusimama hapo kwa muda akiangalia hili na lile, akaichomoa simu yake, kisha akaitafuta ile namba harafu akaipiga akiwa mkononi pasipo kuipeleka sikioni. Baada ya kuita tu, akaikata kisha akaondoka pale kwa haraka mpaka pale kituo cha posta ya Zamani. Akatulia pale huku macho yake yakitizama kule alipotoka. Haikupita hata sekunde thelathini, akawaona watu wanne ambao hawakuonyesha kama wako pamoja wakipishana huku na huko. Hakuwa mgeni na majasusi, aliwajua na kuwatambua hata kama wamejibadilisha kwa kiasi gani.
 
Asante.vipi unataka bando? Kazi unayofanya I really appreciate
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom