NITAKUPATA TU
SEHEMU YA 021
Hawakujua kwamba nyuma yao alikuwepo teddy, tena akiwa na bastola mbili mikononi, vidole viwili vikiwa tayari kwenye trigger kuruhusu risasi. Alikuwa akizihesabu sekunde, hakutaka kufanya kwa haraka sana kukifanya kile alichotaka kukifanya. Sekunde ya kwanza ilipita wakati kidole bado kikiwa kwenye kitufe cha kuruhusu risasi. Hata sekunde ya pili ikapita patupu pasipo kitendo chochote. Lakini sekunde ya tatu haikupita na kwenda bure, bastola ikakohoa mara tatu mfululizo, risasi zikatua na kupenya pale zilipoagizwa, watu watatu walikuwa chini wakivuja damu katika kuonyesha hawakuwa hai. Kilikuwa kitendo mujarabu machoni kwa Teddy, kitendi kilicho mfanya atabasamu. Aliipenda damu, alipenda kuiona ikitoka mwilini kwa mtu na aliihusudu zaidi pale yeye awapo chanzo cha kutoka kwa hiyo damu. Hakutoka pale kwa haraka, bado aliendelea kutizama pale alipoangukia Jimmy. Bado alitaka kuitumbukiza Risasi katika kichwa cha mtu huyu. Licha ya kuangalia sana lakini hakuonekana, hakumuona Jimmy na kibaya zaidi hakumuona Masimba na hatq mmoja kati ya wale watatu walioingia. Sebule ilikuwa kimya, ukimya wa kuonyesha hapakuwa na mtu. Hilo likamfanya auvute muda, hilo likayafanya macho yake yawe makini kwa kila kitu. Bastola mbili bado zilitangulia mbele. Lakini ukimya nao bado uliendelea kutamalaki. Sasa alikuwa ameamua kujitokeza, kujitokeza kuangalia zaidi na zaidi, ikiwezekana aondoke kabisa. Lakini wazo hilo likapingwa na hisia zake, bado hapakuwa na usalama wa yeye kujitokeza. Akaangaza macho yake pembeni kama ataona chochote cha kumsaidia, akakiona kisadolini kidogo ambacho kilionekana kama kimejaa maji. Akainama na kukichukua, baada ya hapo akajaribu kukitupa upande mwingine kama angeweza kugundua chochote, lakini haikuwa hivyo... Bado ukimya uliendelea kuwepo. Hilo likampa uhakika kwamba hapakuwa na watu eneo lile. Akaipiga hatua ya kwanza na ya pili, alipotaka kupiga hatua ya tatu akasikia yowe likitokea nyuma yake. Yowee lililofuatana na mgugumio wa maumivu kutoka kwa mtu. Hakutaka kugeuka kuangalia, kugeuka kwake nyuma kungesaidia kupigwa Risasi iwapo angekuwepo mtu wa kufanya hivyo. Alichokifany yeye ni kuchupa na kuangukia pembeni. Akatulia akiangaza huku na huko. Bado ukimya ulichukua nafasi yake. Hapakuonekana kama kuna tukio kutokana na ukimya. Hapakuonyesha kuwepo kwa mtu. Nani amelifanya tukio lililopita muda mfupi? Masimba! Ndiye mtu pekee wa kulifanya hili, lakini amekalia wapi? Mbona Jimmy haonekani, nani amepigwa risasi nyuma yangu? Amepigwa na Masimba au na mtu gani? Kabla hajalipata jibu bastola ikagota tena kwa mara ya pili kisogoni. Tofauti ya huyu na yule wa mwanzo, huyu hakuongea kitu. Aliendelea kuikandamiza bastola kisogoni. Kabla hajakaa sawa, akashikwa na kugeuzwa kwa nyuma.
Hapo akajikuta akitizamana uso kwa uso na Masimba, Bastola yake ilikuwa bado kichwani kwa teddy. Macho yake yalikuwa yamebadilika kupindukia. Sura yake haikuonyesha utani, sura yake haikuwa na masihara. Teddy akatulia akimuangalia masimba, alitulia akihofu na kuwa na mashaka na mabadiliko yale. Macho ya Masimba hayakuonyesha ule utani. Macho ya masimba yalimaanisha kitu kingine. Akakiona kidole cha Masimba kikishuka kwenye kitufe cha kuruhusu risasi. Akauona uso wa Masimba ukiendelea kubadilika. Hakuonyesha masihara, hakuonyeshq utani, macho yake yalisomeka kifo na sura yake aliongelea mauti. Teddy bado alitulia, bado alikuwa akiiomba toba. Alitulia kuruhusu chochote, haikuwa hivyo wala vile, bali ilikuwa hivi. Bastola ilishushwa kisha bila kuambiwa chochote akamuona masimba akiondoka. Akiondoka huku akiachwa yeye akiwa amesimama. Hakubaki hapo, alikuwa nyuma akimfuata Masimba. Alikuwa nyuma akimfuata mpenzi wake. Hakuwa na wazo tena la kukumbuka uwepo wa Jimmy.
*********
Chumba kilikuwa kimya, kila mmoja alikuwa kimya akimtizama mwenzake kwa utofauti. Wakati teddy akimtizama masimba kwa staili ya nisamehe, masimba alikuwa akimtizama kwa staili ya nautaka ukweli. Uso wake haukuwa na tabasamu, mishipa ya hasira bado ilichukua sehemu kubwa usoni. Sura ya Asteria, Godfrey Maboba sambamba na familia yake, bado zilikuwa usoni mwake. Kumuangalia teddy kulifuatana na kumbukumbu ya mtoto aliyelala mbele ya macho yake akiwa na matundu mawili ya Risasi. Mtoto ambaye hakuwa na hatia, mtoto ambaye hakujua chochote kile aliuawa kwa risasi. Chanzo kikiwa teddy. Ni teddy huyu huyu aliyetaka kumuua kule kigamboni. Kufikia hapo akaanza kutembea kusogea pale aliposimama teddy. Teddy bado hakusogea wala hakurudi nyuma. Alisimama pale pale akimuangalia masimba usoni.
"Kwa nini Umemuua Asteria na familia yake?" Lilikuwa swali, swali ambalo halikutarajiwa na teddy. Sio kutarajiwa kwa kuwa alidhani masimba anajua. Lilikuwa swali ambalo lilimshtua na kumgutusha kupita kiasi. Ni kweli alipewa amri ya kumuua Asteria, lakini hakumuua yeye kwa kuwa alimfahamu Asteria tokea wapo wote Ifakara. Alimfahamu asteria kwa undani zaidi, na hata familia yake aliijua. Ingawa alipokea kweli amri lakini asingeweza kumuua asteria na hata dada yake. "Sikumuua Asteria wala familia ya dada yake. Ni kweli amri ya kuua nilipewa, lakini kabla sijatekeleza hilo wakatumwa watu wengine wakaua ili nionekane mimi ndio nimefanya. Kuhusu familia ya dada yake sikuhusika na chochote kwa kuwa tukio lililotokea mjimwema Kigamboni lilinichanganya baada ya kugundua kuwa gari yetu ndio imelipuliwa na wewe ukiwemo ndani yake. Hilo likanifanya nirudi tena kigamboni kuangalia uwezekano wa kuuona mwili wako lakini sikuuona. Hapo nikatambua kuwa hukuwepo ndipo niliporudi nyumbani kukusubiri. Teddy alimueleza Masimba kila kitu kilichotokea, hata kuvamiwa na walinzi binafsi wa taasisi nyeti. Hakuacha kuongelea usaliti na kukubali kuwa alikuwa tayari kusaliti.
"Nani Yupo nyuma ya mpango wenu wa kutorosha madawa kutoka kwenye mikono ya usalama? Aliuliza Masimva.
"Jimmy Lambert!" Akajibu Teddy
"Ukimtoa Jimmy?
"Yupo mtu mwingine mkubwa sana, lakini mtu huyo anajulikana na watu wawili tu." Akajibu teddy.
"Nani na nani wanamjua?
"Jimmy na suresh. Akajibu teddy
Lilikuwa jibu ambalo halikutegemewa na masimba. Akamuangalia teddy zaidi na zaidi, akihitaji ahakikishiwe kama jibu hilo lina ukweli. Bado teddy alimjibu pasipo na wasiwasi. Alimhakikishia kwamba Suresh alikuwa mmoja kati ya watu wanaomfahamu mmoja ya vigogo waliokuwa nyuma ya mpango huo. Akamuangalia Tena, kisha kwa sauti tofauti akamuuliza. "Unajua kuwa nilikamatwa na kupelekwa makao makuu kabla sijahamishiwa katika nyumba moja ya siri inayomilikiwa na usalama wa TAIFA?
"Mwanzo sikujua, lakini nilipowaona walinzi wale nikajua hili suala limepelekwa mamlaka nyingine. Nilijua utakuwa umeharibu ama njama za kukushurutisha uonyesha ulipo mzigo wa madawa zinaendelea." Akajibu Teddy.
"Upo tayari kuwa na mimi au bado unaitaka pesa?
AKAULIZA MASIMBA HUKU AKIMUANGALIA TEDDY USONI.