NITAKUPATA TU
SEHEMU YA 073
Walikuwa watu sita wenye silaha nzito. Watu ambao waliingia pale katika namna ambayo hata Teddy mwenyewe alijiuliza. Ukimya ulitawala kanakwamba hapakuwa na watu walioingia hapo sebuleni. Mkononi alikamatia bastola yake aina ya semi automatic pistol huku sehemu fulani ndani ya mavazi yake kukiwa na Sig-sauer p20 nayo ikiwa imetulia ikisubiri kuifanyakazi hiyo. Ukimya, kwa nini ukimya wakati watu wameingia hapa muda mfupi uliopita? Tena watu sita wenye silaha nzito? Huu ukimya ni wa nini? Wameenda wapi watu hawa? Ni maswali aliyojiuliza Teddy huku mikono yake ikiwa tayari. Sekunde, dakika na sasa ilikuwa inafika dakika ya tatu, babo ukimya, bado hapakusikika chochote kutoka sebuleni. Hata nyayo hazikusikika. Sehemu ilikuwa kimya, ukimya ambao ulimaanisha hakuna kitu chochote. Teddy hakutaka kuamini hilo. Bado aliuamini muda, bado aliitambua Subira kama kitu muhimu sana kwenye eneo kama hilo. Semi Automatic pistol Bado haikuondoka mkononi. Bado kidole hakikutoka sehemu ya kufyatulia Risasi. Macho yake yakaanza kulizoea giza lilikilokuwa limeanza kutanda kwenye nyumba ile. Kuanza kuingia kwa giza kukampa uwezo wa kuona kilichokuwa kikiendelea. Kwani ni wakati giza likiingia akahisi kuisikia michakato ya hatua za watu. Michakato ya miguu ikitembea katika aina ya kunyata. Akajiweka tayari, akajiweka akikabiliana na watu waliokuwa wakisogea. Punde akakiona kivuli mtu, mtu ambaye mavazi yake yalifanana kabisa na giza lililopo mle ndani. Mdomo wa bastola ukainuka na kutizama kule kilipo kivuli. Muda mfupi alikuwa akimuona mtu akipita akiwa kimya kabisa. Hakusubiri ainue mguu wa pili. Semi automatic pistol ikakohoa. Ikatoa cheche na kumwaga njugu. Ulikuwa mlio mfano wa chafya ama kuvunjwa kijiti. Risasi ilikuwa imepenya kooni kwa mtu yule. Hakuweza kuongea wala kupiga kelele. Akaporomoka chini akiwa amelishika koo lake. Teddy katulia Tena na kuhama Upande mwingine, akasimama pembeni mwa mlango. Macho yake yalikuwa mbele, macho yake yalikuwa yakitizama mlangoni. Lakini safari hii ukimya ulirejea Tena. Hapakusikika chochote tena. Hata zile hatua za watu zikakoma na nyumba nzima ikawa kimya. Ni wakati huo akiwa ametulia akausikia mngurumo wa gari nje nyumba hiyo. Mngurumo ambao uliishia getini kuonyesha kuwa gari ilikuwa imesimama nje ya geti la nyumba hiyo. Mara akalisikia geti likifunguliwa kisha mngurumo wa gari ukasikika tena. Safari hii gari hii ilikuwa ikiingia ndani ya uzio wa nyumba hii. Teddy akajiuliza huyu ni nani?kabla hajapata jibu. Akausikia mlango wa ndani ukifunguliwa. Kisha michakato ya miguu ya watu ikasikika kusogea. Bado Semi Automatic ilikuwa mkononi akisubiri kutoa hukumu nyingine. Miguu hii sasa ilikuwa ikiukaribia mlango wa chumba alichokuwa ametulia. Miguu ikasikika tena safari hii ikiwa katika usawa wa chumba kile. Lakini cha ajabu hakumuona mtu, hakumuona akipita na hata kivuli chake hakukiona. Huyu ni nani? Mbona kama mzimu? Lilikuwa swali ambalo halikudumu sana akauhisi ukelele wa sauti ya mtu ukitokea mbele kidogo ya pale alipojibanza. Hakuliacha hilo limpite, hakuliacha liondoke na hata kwenda hivi hivi. Akajitoa taratibu, alitaka kwenda kuona na hata kumuangalia huyu mtu. Alitaka kushuhudia na kuona huyu mtu alikuwa nani na kwanini ameingia pasipokuwa na wasiwasi. Bastola mkononi huku macho yakipambana na Giza ndani ya nyumba ile, Teddy alinyata kwa umakini mkubwa mpaka nje ya chumba kile. Licha ya kunyata na kutokea hapo, lakini hakuona chochote zaidi ya ukimya kwa mara nyingine. Hata yule mtu aliyekuwa akipiga ukelele hakusikika tena. Nyumba ikarudi kwenye kimya tena. Hilo halikumbabaisha jasusi huyu wa kike. Bado aliyatembeza macho yake, macho yaliyozoea giza. Hazikupita sekunde tano, akaisikia kelele tena ikitokea juu. Hii ilikuwa sauti ya mtu wa makamo. Mtu ambaye alionyesha kuwa na umri mkubwa. Safari hii sauti ya mtu huyu ilikuwa ikitoka kwa maumivu ya kipigo ama kubanwa na kitu. Alikuwa akilia kama mtoto huku akisema hajui kitu huku akiwataka wauaji wakamuone Baba Askofu Ibrahim Lexandre Rengima. Kutajwa kwa jina la baba Askofu katika mateso ya mtu huyu anayelia kukamfumbua tena kutoka kwenye giza. Alitambua mtu huyo anayepiga kelele ndiye mtu aliyetumwa kuja kumuona na kumuokoa. Lakini kama ni hivyo kwa nini Masimba alimtuma kwenda nyumbani kwa Askofu kumuondoa mtu? Mtu mwenyewe ni nani na kama ni Baba Askofu kwa nini nimemkuta akiwa amejeruhiwa? Ina maaba kulikuwa na mtu mwingine zaidi ya Askofu na mtu huyu anayepiga kelele? Yalikuwa maswali mfululizo, maswali yaliyopita kichwani kwa Teddy. Maswali ambayo hayakuwa na majibu kwa wakati ule wakati sauti ya mteswaji ikizidi kutamalaki.
Akauona upuuzi kuendelea kujiuliza, upuuzi ambao ungemfanya akose kile ambacho alitakiwa kukipata. Akaliacha eneo hilo sasa akielekea sehemu hiyo. Kila alipozidi kusogea ndipo hapo sauti zilipozidi kutanda katika masikio. Akiwa amebakisha hatua kazaa kufika sehemu husika, akawa anakisikia kile ambacho kilikuwa kikitamkwa kutoka ndani. Kikitamkwa na Mteswaji kujibu maswali ya Mtesaji. "Tunaitaka bahasha uliopewa na baba Askofu. La sivyo nitakuua sasa hivi." Aliisikia sauti hiyo ambayo ilipenya mpaka ndani ya moyo wake. Sauti ambayo aliijua. Ilikuwa sauti Ya Ben. Sauti ya mtu katili kuwahi kumuona.
"Sina bahasha yoyote, kama mnaniua niueni tu." Ilisikika sauti hii. Sauti ya mtu aliyetayari kufa sababu ya bahasha ambayo ilikuwa mikononi kwake. Akauona ulikuwa muda wa kufanya kitu, muda wa kufanya kile ambacho kingemuokoa mtu huyu. Ulikuwa wakati wa kumuua Ben. Akatoka hapo sasa akikifuata kile chumba. Lakini kabla ya hapo alitaka kuitafuta swichi ya kuwashia taa. Alitaka kuitumia mbinu hiyo kujua watu hawa wako wapi. Akaendelea kupapasa huku na huko kutafuta anachokitafuta. Baada ya kutafuta sana akaiona swichi hiyo. Huku bastola ikiwa tayari akaifyatua Swichi. Nyumba yote ikawa nyeupe. Watu wanne waliojificha pale ukumbini wakashtushwa na kuduwaa kwa sekunde. Ni wakati wa mduao huo, semi automatic ikakohoa na kumwaga risasi. Watu watatu waliku wamepaa angani kwa Risasi na hata walipokuja kufika chini walikuwa marehemu. Hilo halikutegemewa na watu waliokuwepo hapo ndani. Milio ya risasi ikalindima kutoka kwa wakora hawa waliokuwa wakifyatua risasi hovyo bila kujua hatari mbele yao. Teddy bado alikuwa ametulia, bado alikuwa akiwatizama wakora wale walivyokuwa wamehamanika. Alitamani hata kucheka, alitamani hata kuwaita. Lakini muda huo akamuona mtu akitokea katika aina iburudishayo moyoni na hata machoni. Mtu huyu alikuwa akiyupa kwa wepesi wa karatasi, wepesi wa sisiminzi na hata wepesi wa ubua. Alitoka hapa akienda pale katika namna ambayo ilivutia sana. Alikuwa masimba huku mikono yake yote ikiwa na bastola. Mkono wa kushoto alikuwa na Bastola aina ya PPQ (polizei pistole quick defense) iliyotengenezwa Nchini Italy na mkono wa kulia alikamatia bastola aina ya Springfield XD ambayo hii ilitengenezwa katika nchi ya Marekani. Alitia raha kumtizama na hata kumuangalia, Teddy akapandwa na Mzuka, mzuka wa Kushambulia. Wakati mara ya kwanza alikuwa atumia Bastola moja, Safari hii akaichomoa bastola yake nyingine. Bastola iliyotengenezwa nchini Brazil. Wakati kulia kulia alikuwa na semi automatic, kushoto alikuwa na SIg -sauer p320. Masimba alikuwa akishambulia kutoka mbele, teddy naye alikuwa akimlinda masimba kwa mbele. Ilikuwa burudani katika aini yenye kutoa raha. Kila risasi ilipelekwa sehemu husika, kila ilipotumwa, risasi ilikwenda hapo. Hakufika wala kuchukua Dakika. Zilikuwa sekunde thelathini tu. Kila mkora alikuwa yupo chini akivuja damu.. alikuwa marehemu huku matundu ya Risasi yakionekana Kifuani. Wakatizamana katika macho ya upendo, macho ya kujali na hata kuaminiana. Macho yao yalikuwa yakiongea mapenzi. Hawakujali walikuwa sehemu gani, midomo yao ikakutana katika namna fulani uburishayo nafsi. Lakini hawakufika katika lengo lao, lengo la kuburudika zaidi. Kwani macho ya masimba yakamuona mtu. Mtu ambaye alikuwa ameuinua mdomo wa bunduki yake aina ya combart shotgun akiwa lenga wao. Akiwa lenga pale waliposimama. Hakuwahi kufanya alichotaka kukifanya. Alifanya kile ambacho akukitarajia. Risasi mbili zikatoka mahali apo.. moja ikatua begani kwa Ben na nyingine katikati ya paji la uso. Ben ajayumba na Bunduki yake mkononi na kwenda kujimwaga chini. Alijibwaga tayari akiwa maiti. Wakati huo ndio kwanza Teddy alikuwa akigeuka. Akigeuka kuangalia kile ambacho kilitendwa na kufanywa. Ben alikuwa chini kichwa kikiwa kama chapati. Risasi ilikuwa imefumua kichwa cha ben. Teddy hakulitegemea na hata kuliwaza. Aliporudisha macho Usoni kwa Masimba akakutana na tabasamu. Tabasamu lililomfanya Teddy ajilaze kifuani kwake. Kifua ambacho kilikuwa maalum kwa sababu yake. Ikawa hiyo.
KESHO