[05-28, 13:44] Ibrahim Masimba: NITAKUPATA TU
SEHEMU YA 070
Akatua chini mfano wa ubua. Akatoka hapo akitembea na tumbo mpaka nyuma ya kibanda ambacho kimejengwa kwa ndani. Akatulia hapo kwa muda akitizama kama atamuona mtu yoyote yule. Mtu ambaye atatokea ama yule ambaye atahisi uwepo wake. Hapakuwa na mtu na hapakuwa na dalili yoyote ya uwepo wa mtu. Akasogea tena na tena akiitafuta njia ya kuingilia kwa ndani. Wakati anakaribia kuufikia mlango, akausikia mngurumo wa gari ukitokea kwa nje, kisha akalisikia lango likifunguliwa kisha ule mngurumo wa gari ukaendelea kusikika. Sekunde mbili baadae akahisi gari ikisimama. Hapo akatambua kuwa Suresh ndiye aliyekuwa ameingia hapo. Akaufuata mlango na kukinyonga kitasa. Mlango ukafunguka, akaingia ndani kwa mwendo wa Taratibu, mwendo ambao haukusikika hata kwa mtu ambaye yuko mbele kwa umbali wa hatua mbili. Wakati akiifikia sehemu fulani ndani ya jumba hilo akaisikia sauti yenye lafudhi ya kihindi kutokea nje. Hapo akajua kuwa huyo lazima atakuwa ni suresh. Akaendelea kusubiri, ndani ya sekunde akauhisi mlango ukifunguliwa kisha kusikia hatua za mtu zikitembea. Kwa kuwa kulikuwa na giza Masimba Hakujua mtu huyu alikuwa nani. Akaendelea kutulia akimngojea apite. Manukato mazuri puani na hatua za taratibu zilitosha kumfahamisha masimba na kumueleza kuwa mtu huyu alikuwa ni mwanamke. Mtu huyu alikuwa ni mwanadada. Wakati akiliona hilo mwanamke yule alikuwa amefika usawa wa pale mahali aliposimama. Masimba akamuacha apite kwanza kisha akaanza kumfuatilia nyuma nyuma. Bado hatua zake zilikuwa zile Zile ambazo hazikusikika. Lakini kwa nini jumba lote hili limejengwa huku na lipo giZa? Ni swali alilojiuliza wakati mwanamke yule akiufungua mlango wa chumba kilicho mbele yao. Kabla mlango haujajifunga masimba akawahi na kujitumbukiza. Hata hapa walipoingia bado kiza kiliwapokea, licha ya ukimya huo lakini pia sehemu hii iliuonekana kama stoo ama chumba kinachotumiwa kwa shughuli ambayo haikutakiwa kuonekana. Mabox sambamba na mifuko mikubwa ambayo ilionekana kujazwa vitu ilikuwa imehifadhiwa vizuri sana. Macho yake bado yalikuwa yakimtizama mtu yule. Kumtizama mwanamke yule. Kumtizama katika utimamu wa kiakili na kimwili. Mikono yake ilikuwa tayari kuichomoa bastola na kumuulia mbali, lakini hakutaka kufanya hivyo kwa kuwa alitaka kujua kule aliko suresh na wapi anapoelekea mwanamke huyu. Wakaipita ile sehemu na kutokea sehemu nyingine. Bado giza liliendelea kutawala katika jengo hilo. Mbele kidogo akauona ukuta, ukuta ambao ulikuwa ukionyesha ulikuw mwisho wa ile safari yao. Mwisho kwa kuwa haapa kuonyesha kama mbele kuna mlango uliokuwa ukiendelea. Lakini uelekeo wa mwanamke huyu ulionyesha uwepo wa kitu fulani. Akaona ulikuwa muda wa kumuwahi. Muda wa kumzuia kusogea ama kusonga mbele. Ilikuwa sekunde tu iliyotosha kuufanya mdomo wa bastola kumtekenya mwanamke yule ubavuni. "Tulia dada na usijaribu kufanya chochote.. " aliongea masimba huku mdomo wa bastola akizidi kuugandamiza.
"Wewe nani kwani? Na utanataka nini? Umeingiaje humu ndani?." Aliuliza mwanamke maswali mfululizo akionyesha kutetemeka. "Sio shughuli yako kujua nimeingiaje, ilaunapaswa kujua kile ninachokitaka. Sasa ninachokitaka ni roho ya Suresh. Na nataka unisaidie kumpata. Ukikaidi hata wewe roho yako nitaiweka katika orodha ya roho zile ambazo zimepangwa kupelekwa kuzimu. Naomba uongoze ulipokuwa unakwenda bila kufungua mdomo wako, la sivyo hutaliona Jua la kesho." Alinguruma masimba huku akiendelea kuugandamiza mdomo wa bastola mgongoni kwa binti. "Kaka mbona unanionea? Mbona suresh simfahamu na sijui unachoongea.!!.." aliongea binti akionyesha kutokujua kitu. "Binti usinilazimishe nikuue. Usinilazimishe niufumbe mdomo wako kwa risasi. Unafanya ninachotaka hufanyi? Alisema Masimba huku akimuangalia msichana. "Fanya kwa kuwa unaongea kitu nisicho... uwiiii nakufa... " hakuimaliza kauli yake, risasi kutoka kwenye bastola ya masimba yenye kiwambo cha kuzuia mlio ikapenya kwenye paja lake la mguu wa kushoto. Binti akalalama kwa maumivu. Hakujua kama Masimba alikiwa hatanii. "Naona sasa umekipata kile ambacho ulikuwa ukikihitaji. Naomba ufanye kama nilivyokwambia, nataka unionyesha alipo Suresh kabla sijakumaliza." Alisema Masimba huku sasa akimuonyesha Ishara ya kumtaka abonyeze kitufe kimoja kati ya vitatu vilivyopo ukutani. Msichana huyu akigugumia kwa maumivu akabonyeza kitufe, punde ukuta ukajifungua na kuacha uwazi kama mlango. Masimba akamtaka aongoze kuingia ndani. Binti hakuwa mbishi tena. Akaongoza ndani huku akigugumia kwa maumivu. Muda wote bastola ilikuwa mkononi tena mgongoni kwa mwanamke huyu. Walipopita kwenye ule uwazi binti akabonyeza vitufe kwa ndani sehemu ikajifunga tena wote wakajikuta ndani ya chumba kizuri na kilichopambwa sana. Kilionekana kuwa ni chumba cha kulala.
"Msubiri suresh atakuja hapa muda mfupi.." aliongea yule msichana huku akimuangalia Masimba Usoni. Macho yake yakurembua yalikuwa usoni kwa masimba. Ingawa macho yalikuwa usoni kwa Masimba, lakini mkono wake ulikuwa ukishuka taratibu sehemu ambapo palihifadhiwa bastola. Lakini hakujua kuwa macho ya masimba yalishamuona zamani, yalishamuona wakati mkono ukielekea sehemu hiyo. Mkono wa mwanamke yule haukufika hapo, haukufika sehemu husika. Risasi mbili zilitosha kuumaliza uhai wa binti huyu. Akajilaza taratibu kitandani akiwa maiti. Baada ya kugundua ameshakufa akamuweka vizuri na kumfunika na shuka, kisha yeye akatulia pembeni ili kumsubiri suresh akiwa katika giza lile lile. Aliona ulikuwa ni mpango bora na kurahisisha kazi kuanza na watu hawa ambao walikuwa kama matawi katika biashara hii.
[05-28, 13:44] Ibrahim Masimba: Ulikuwa ni mpango mzuri kuanza na watu hawa. Ulikuwa mpango mzuri wa kulimaliza hili suala katika aina kama hii. Jimmy na Suresh ndio chanzo cha kuharibika kwa watoto wengi. Vijana wengi walitopea katika utumiaji wa madawa ya kulevya kutokana na hawa watu wawili wakishirikiana na viongozi wa serikali. Ni aibu kuwaacha wakiendelea kuishi wakati huku mtaani vijana wengi walikuwa wameharibika na kuharibikiwa. Alioona hukumu sahihi ya Watu hawa ni Risasi, risasi ya kichwa ndio hukumu sahihi kwa watu hawa. Leo hii alikuwa chumbani kwa suresh akimsubiri huku pembeni yake kukiwa na maiti ya mwanamke ambaye alionyesha kuwa ni kimada wa Suresh. Alikuwa ametulia vilevile na giza bastola yake ya Kirusi Revolver colt 48 ilikuwa mkononi ikisubiri kuitoa roho ya suresh na kuisafirisha. Alitaka kuipeleka kuzimu, alitaka kuipeleka ikakutane na watu wote waliouawa na waliokufa kutokana na Matumizi ya Madawa ya Kulevya. Akaivuta subira katika aina ya kutokukata tamaa. Punde ukuta ule ukajifungua kisha akaonekana mwanaume wa kihindi akiingia taratibu. Baada ya kuingia mtu huyu akabonyeza vitufe mlangoni na ukuta ule kujifunga tena. Baada ya kufanya hivyo akatembea kwa madaha mpaka iliposwichi ya kuwashia Taa katika Chumba kile. Akaupeleka mkono na kuwasha.. nusura azimie kwa mshtuko baada ya kumuona Masimba akiwa ametulia pembeni huku Bastola yake ikiwa anamtizama yeye. "Karibu sana Mr Suresh.. Pia nisamehe kwa kukuingilia kwa Njia hii. Sikuwa na budi isipokuwa kufanya hivi." Aliongea Masimba akitizamana na Suresh katika aina fulani iliyompendeza machoni kwake. Masimba akainuka na kusimama Bastola Ikiwa mkononi bado. "Suresh leo nimeamua kuja mwenyewe kukuuliza machache ambayo nadhani utanijibu pasipo kuleta purukushani." Aliongea Masimba sasa akisogea karibu kabisa na Suresh. Suresh bado hakuinua mdomo wala macho kutizama. Alikuwa muoga kupindukia, alikuwa akitetemeka na hata midomo kukutana. "Suresh sasa naomba kaa pale ujibu maswali yangu. Naomba ujibu nitakavyo usije ukaniacha nikakupoteza kama huyo malaya wako." Bado aliongea Masimba huku akimuonyesha Suresh sehemu sahihi ya kukaa. Suresh bila kubisha akaongoza mfano wa kondoo. Akajibweteka chini akionyesha kuwaza kitu. Kitu ambacho hakujua ni vipi angeweza kukipata. Mwili wa mwanamke uliolala ukiwa hauna uhai ulimtisha na kumtia Hofu. Sasa alikuwa akikiangalia kifo mbele ya macho yake. Kifo ambacho alipenda kukitenda kwa watu wengine. Leo Ilikuwa zamu yake, leo ilikuwa zamu ya kifo chake. Akainua macho kumtizama masimba na hata kuuangalia unbali sahihi. Umbali kutoka alipo masimba na hata kutaka kujaribu kumvamia. Bado macho ya Masimba yalimuangalia kwa umakini na upole. Bado macho ya Masimba yalikuwa yametulia usoni kwake. Hakupepesa na hata kuangalia sehemu Tofauti. Alimtizama akikisoma kilicho katika akili yake. "Mbona ananitizama hivi? Mbona haonyeshi kuogopa? Yalikuwa maswali yaliogonga kichwani kwa Suresh. Akaamua kutulia na kuitafuta mbinu nyingine. "Suresh nahitaji kujua ukimuondoa Hayati waziri mkuu, ni nani mwingine yupo nyuma ya biashara hii mnayoifanya? Akauliza masimba kwa sauti tulivu. Suresh akakaa kimya kana kwamba hakuwa amelisikia swali hilo. "Suresh naongea na wewe, nani yupo nyuma ya hii biashara? Akauliza tena Masimba. Lakini bado Suresh hakutaka kujibu. Bado suresh alikuwa kimya. "Suresh usitake nitumie nguvu katika hili utajuta.." alilisisitiza Masimba. "Sijui unachozungumzia Ndio maana sina majibu ya maswali yako. Pia huwezi kuvamia nyumba za watu na kuua watu hovyo. Hata kama wewe ni mpelelezi hatuendi hivyo." Akajibu Suresh kwa sauti yenye kejeli ndani yake. "Suresh naomba unijibu maswali yangu. Narudia tena sitaki kutumia nguvu.. tambua ukinilazimisha na nikatumia utaumia." Narudia mara ya mwisho, ni nani yupo nyuma ya Biashara Yenu ukimtoa Waziri mkuu.? Akarudia tena.
"Sijui unachozungumzia na sielewi unachosema. Kama unaona una hofu na mimi nipeleke kwenye vyombo vya dora." Akajibu Suresh kwa kejeli tena.
"Sawa nimekuelewa. Lakini nikwambie kuwa sitakupeleka kwenye chombo chochote cha dora, bali nitakusafirisha kukupeleka Kuzimu. Sasa pokea hiyo kwanza." Aliongea Masimba huku bastola ikikohoa na risasi kwenda kupenya kwenye mkono wa kushoto... "haapana haapaana utanionea bure mimi sijui chochote." Aliongea Suresh huku akihamanika. Muda ule ule akakurupuka na kutaka kwenda kumvaa Masimba. Hakuujua Wepesi wa Masimba. Hakuujua wepesi wa mtu huyu. Kwani muda ule ule akajikuta akipokelewa na mateke matatu mfululizo. Mateke yaliyomrudisha chini na kumuacha akitweta. "Inuka upambane, wewe si mwanaume? Inuka tena nikumalizie." Aliongea masimba huku akimuangalia Suresh aliyekuwa akitweta pale chini. "Sasa naomba unijibu kabla sijakipasua kichwa chako kwa risasi. Huwa nawachukia sana watu wa aina yako. Mmeniharibu mamilioni ya vijana kwa uroho wenu wa pesa. Sasa niambie nani yupo nyuma yenu." Alifoka masimba. "Unajisumbua na kupoteza muda wako. Niue tu maana hutapata chochote kutoka kwangu." Aliongea Suresh huku akionyesha hana masihara. Haikupita sekunde Suresh alionekana kuilaza Shingo Yake pembeni huku mapovu meupe ya kimtoka mdomoni. Kilikuwa kitu ambacho hakikutarajiwa kabisa. Suresh alikuwa amejiua kwa kumeza vidonge fulani ambavyo hutumiwa Sana na majasusi wengi duniani kuepusha kutoa siri hasa pale unapobanwa. Suresh aliamua kuifuata njia hiyo. Alikuwa amekufa bila kutoa siri ama kitu chochote ambacho kingeweza kumsaidia masimba.