Riwaya: Nitakupata tu

[20/05 3:44 PM] Ibrahim Masimba: NITAKUPATA TU

SEHEMU YA 064

Bastola ilikuwa juu ya meza tayari kumuondoa mbunge wa kigamboni. Hakutaka kutumia muda mwingi kumfikia. Alichokitaka ni kumuua na kumuondoa katika uso wa hii dunia. Aliendelea kuutafuta usawa wa kuifanya kazi yake. Wakati huo wote mhudumu bado hakuwa amefika kuulizia oda. Hiyo ilikuwa ni bahati kwake. Muda mfupi alikuwa ameupata usawa, usawa wa kuweza kuiruhusu risasi kuingia mwilini kwa mbunge yule. Akaupeleka mkono wake ndani ya Gazeti. Mkono ukaishika bastola na kidole kikashuka chini ya kitufe cha kufyatulia Risasi. Sekunde ya pili risasi ilikuwa imeshatoka ikielekea ilipotumwa. Punde kichwa cha mbunge yule kikafumuka huku mwenyewe akitupwa nyuma na kwenda kujibamiza ukutani. Hakuweza kuinua mguu tena. Alikuwa tayari ameshakufa. Purukushani na mayowe ya watu yakamuondoa masimba pale alipokuwa amekaa na kujichanganya na watu waliokuwa wakikimbia hovyo huku wakipiga kelele. Alitoka mtaa wa magengeni akitembea mpaka Kituo maarufu kiitwacho Tungi stendi. Kufika hapo akaongoza mpaka alipotokea barabara iendayo kisiwani. Hapo akasimama akiangalia watu walivyokuwa wakimiminika kuelekea kule alipolifanya tukio la kumuua Mbunge wa Kigamboni. Hakutaka kusubiri wala kushangaa watu waliokuwa wakikimbizana. Alisimamisha Bajaji ambayo ilimpeleka mpaka feri, hapo akavuka mpaka upande wa pili. Hapo akachukua bodaboda ambayo ilimpeleka mpaka masaki. Nia yake ilikuwa ni kwenda kuwaangalia watoto wake. Ingawa Aliamini Teddy asingeweza kufanya kile kitu, lakini alitaka kuhakikisha watoto wanabaki kwenye usalama. Alishuka kwenye pikipiki na kuanza kutembea kwa miguu akielekea nyumbani Kwa Chief. Moyo wake ulikuwa umechafuka sana. Moyo wake ulikuwa umegeuka mithili ya mnyama. Alitamani angempata mwanMke yule. Alitamani kumpata aliyemuua vicky ili aongee naye mawili matatu. Risasi tano aliziweka kwa sababu ya kuuondoa uhai wa Mwanamke huyo. Hakuamini wala kukubali kushindwa, siku zote aliamini hakuzaliwa kwa sababu ya kushindwa. Aliamini kushinda siku zote. Kifo cha Asteria P Paulo sambamba na familia yake. Kifo cha mama yake sambamba na Dee Plus hata kama alimuua Mwamvita lakini aliamini bado alikuwa akidaiwa Damu. Damu ya watu waliouawa pasipo na hatia. Ni wapi angemuona Jimmy ili wahojiane kwa risasi? Ni wapi angemuona Suresh ili ampe tiketi yake? Hilo ndilo pekee ambalo alikuwa akilihitaji kwa aina na njia yoyote.

******

Vilio vilikuwa vimetawala eneo lote la nyumba ile katika mitaa maarufu ya Toangoma. Nyimbo za kusifu na kuabudu zilikuwa zikisikika sehemu yote na kuwafanya waombolezaji nao kufuatia. Mama wa marehemu aitwaye Nina mndeme alikuwa ameshikwa huku na huku wakati wakuuga mwili wa mtoto wake. Hakuwa na nguvu ya kutembea.. Teddy alikuwa pembeni akiwa amesimama akibubujikwa na machozi. Hakuwa akiamini kama ndio kweli alikuwa akimuaga mdogo wake. Alilitizama tukio lile kama mtu anayeangalia kitu asichokiamini. Akasogea kuelekea lilipo jeneza la mwili wa mdogo wake. Akamuangalia Vicky aliyekuwa ametulia. Vicky aliyekuwa hapumui tena.
[20/05 3:44 PM] Ibrahim Masimba: Machozi yakashuka mfano wa maji. Mfano wa maji yaliokuwa yakitiririka kutoka kwenye chem chem. Akakishika kichwa cha mdogo wake na kukiangalia katika muda ule. Hakuwa akiamini kama ndio alikuwa akimuaga vicky. Akalibusu paji lake la Uso. Punde akamuona mtoto wa marehemu aitwaye Cleapatra akitembea akisogea pale. Alikuwa mtoto mdogo ambaye bad0 alimhitaji mama yake. Lakini ukaidi na ubishi wa Masimba ukasababisha Vicky aondoke na kumuacha Patra. Teddy akaongeza kilio pale mtoto yule alipolisogelea sanduku huku akilia. Hakuna ambaye hakulia, hakuna ambaye hakuguswa na kitendo kile. Hata masimba alikuwa akiliA, Hata Masimba alikuwa akitokwa na machozi. Alikuwa akimuangalia mtoto wa vicky kwa uchungu, alikuwa akimuangalia kwa hasira. Kama asingekuwa yeye mtoto yule asingekuwa akilia pale. Ujinga wa kutokujiandaa ama kuhisi hatari kumemfanya ampoteze vicky. Hilo likamuuma na kumuuma. Hata alipokumbuka kuwa alimkosa muuaji wa vicky alijiona kweli alikuwa mjinga. Mtu kama yeye hakupaswa kufanya ujinga kiasi kile. Hakupaswa kuufanya ujinga wa namna ile. Bado alimuangalia mtoto yule alivyokuwa akilia. Ni hapo alipokuwa akimuangalia Cleopatra ndipo alipokutanisha macho na Teddy. Wakatizamana katika aina fulani ya mashaka. Licha Teddy kumti zama masimba katika macho ya shari na kisasi, masimba yeye hakukionyesha hicho kabisa. Bado macho yake yalitengeneza neno mapenzi. Bado macho yake yalionyesha kuhitaji hili na lile. Bado macho yake yalionyesha kuumizwa na kilichokuwa kikiendelea. Macho yake yaliokuwa yakidondosha machozi ndiyo yaliyo mvuta teddy aliyekuwa bado akimtizama. "Masimba analia" lilikuwa neno la kwanza kukigonga kichwa chake, akaongeza udadisi katika kumuangalia huko. Ni kweli masimba aliumia na kuumizwa, ni kweli Masimba alionyesha kuteswa na kitu moyoni. Teddy akaiona hatia katika moyo wake, licha ya matendo yake lakini hakupenda kumuona mwanaume huyu akilia. Akasogea sambamba na patra kuelekea pale aliposimama Masimba. Lakini wakati bado akitembea kumfuata, akashuhudia masimba akiondoka eneo lile na kutokomea katikati ya waombelezaji. Ni wakati alipokuwa akiliangalia hilo akaipata taarifa ya kuuawa kwa mbunge wa kigamboni Bibie Grace Bwahama . Ni taarifa hii na uondokaji wa Masimba vilivyompa majibu kuwa mtaani na sehemu nyingine haziko salama. Mkono wa Masimba ulikuwa umeanza kutoa tiketi moja moja kwa kila mtu. Kwa mara ya kwanza moyo wake ukashikwa na ile hali ya mapenzi. Alikuwa akimpenda Masimba. Licha ya kashfa zote na Tuhuma anazorushiwa, lakini bado alimpenda Masimba. Ni kweli hata masimba alikuwa akimpenda yeye. Hata sms alizokuwa akitumiwa zilimuumiza na alijaribu kuchukua maamuzi ya kuachana naye. Lakini bado Teddy alikuwa moyoni mwake. Lakini Mbona Masimba Ana0ndoka katika mazishi ya Vicky? Lilikuwa swali ambalo halikupata majibu kwa wakati ule. Majibu Juu ya kuondoka kwake. Alitamani wabembelezane, alitamani waambiane na kunong'onezana. Lakini haikuwezekana kwa kuwa Masimba Hakuwepo pale. Akamuangalia patra kisha akatabasamu. Tabasamu la uchungu na la kuumiza.

***********

Hakuvumilia kumuangalia mtoto wa marehemu akilia, hakuvumilia kumuona teddy akilia kwa kosa alilosababisha. Damu ya Vicky ilikuwa mikononi mwake. Alihitaji kuilipa damu ya Vicky. Alihitaji kumuua mwanamke aliyemuua Vivky. Ni mawazo hayo yaliompa uamuzi wa kuelekea ofisini kwa mkurugenzi wa ujasusi kwa mara nyingine. Ila kabla ya safari hiyo aliamua kurudi tena katika Hoteli fulani ambayo walikuwepo watu wawili waliotiliwa shaka. Wanausalama wa kike walikuwa hapo wakibadilishana Zamu. Hata wale waliojifanya wauza mihogo ya kuchoma sambamba na Mahindi walikuwa nje ya hoteli wakihakikisha wanaigundua mienendo ya watu hawa waliokuja kama wageni. Safari hii hakutaka kupitia lango la mbele, bali alipitia Mlango wa nyuma ambao pia ulikuwa ukitizamwa na Wana Usalama kwa kila kinachoendelea hapo. Aliwapita wana usalama waliozagaa na kuuendea mlango, ukaufungua na kuingia ndani kisha kuufunga tena. Alifanya hivyo pasipokusalimia kwa watu aliowakuta hapo. Alipoingia ndani akajikuta akitokeza sehemu ya Jikoni. Hapo pia palikuwa na wanausalama kadhaa. Akawapita akitoka hapa na kuingia ndani kabisa ya Hotel. Alipoingia tu mbele kidogo akawaona watu wawili waliokaa lakini kwa kumpa mgongo. Kilichomvutia sio kukaa kwao katika eneo lile, ila ni kule kumuona Yule mtoto ambaye humuona akiwa na yule mama akiwa mmoja wao. Huku umakini ukiongezeka masimba akawapita na kusogea mbele zaidi pasipo kuonekana. Alipohakikisha watu hawa hawakumuona, alivuta kiti kilichokuwa pembeni akakaa hapo. Baada ya kukaa hapo haukupita Muda wanausalama wengine watatu wakaingia. Lakini uingiaji wao haukuwa ule uliozoeleka. Hawa waliingia kama wasafisha vyumba na watandikaji vitanda. Watu hawa wakipoingia mmoja akamfuata masimba na kuongea naye mawili matatu. Baada ya sekunde mbili wakaondoka na Masimba, hata waliporudi muda mfupi. Walirudi wakiwa tofauti. MASIMBA hakuwepo.

Ilikuwa ni mbinu iliyotumika ili kuwezesha masimba kuingia ndani kufanya uchunguzi wao. Kujifanya wafanya usafi ulikuwa ni mkakati uliosukwa ili kufanya kile ambacho walihitaji kukifanya. Masimba alikuwa ametulia sehemu macho yake yakiutizama Mlango katika Udadisi Wa Hali ya Juu. Alikuwa hapo akimsubiri mwanamke huyu ambaye aliamini ndiye huyu mwenye chumba hiki. Ndani ya Muda wa Sekunde kama Ishirini akauona Mlango ukifunguliwa, akaiona sura ya mwanamke ikichungulia. Ilikuwa sura ya mwanamke yule yule aliyemuua vicky. Masimba akaendelea kumtizama binti huyu. Hata pale alipoufungua mlango na kuingia kabisa kisha kuufunga tena mlango safari hii akiufunga kwa ndani, Masimba hakuinuka wala hakumfuata. Lakini binti alipoanza kuvua mavazi yake ndipo Hapo Masimba Alichokishuhudia kile ambacho hakuwa amekifikiria. Mtu huyu aliyeamini kuwa Alikuwa mwanamke Haikuwa hivyo. Huyu alikuwa mwanaume tena mwanaume aliyejengeka kimazoezi
 
NITAKUPATA TU

SEHEMU YA 065

Alikuwa mwanaume tena mwanaume mwenye mwili uliyojengeka kimazoezi. Hilo hakuwa amelitaraji. Mwanaume? Kumbe huyu hakuwa mwanamke. Hilo likampa mshangao, mshangao ambao ulizidi hasa pale mwanaume yule alipomaliza kuvua mavazi yake. Dakika moja iliyopita alikuwa akionekana kama mwanamke mrembo machoni kwa Masimba, hata pale mikadi beach alimuona kama malaika fulani. Macho yake yalikuwa yakimvutia kila mwanaume amtazamae. Licha ya hivyo kumbe hakuwa mwanamke kama alivyoonekana. Hilo likaongeza hamu ya kumjua huyu alikuwa nani, kwa nini alimuua Vicky? Hilo likamtoa pale alipokuwa amejificha kuelekea pale aliposimama mwanaume yule akijinasibu kama wa fanyavyo wasichana wengine. Bastola mkononi hatua za kunyata mfano wa paka. Bado mwanaume yule hakuwa amemuona, bado mwanaume yule hakuusikia mchakato wa viatu wala hatua. "Niliacha kukuua Mikadi Baada ya kumshuti yule mwansmke nia yangu ikiwa ni kukujua wewe ni nani. Umetoka wapi na umetumwa na nani? Kubwa Zaidi ni uzuri wako na muonekano wako ulinifanya nisite kuchukua maamuzi ili mradi nikukute sehemu niujue uzuri wako kiundani. Lakini kilichonishangaza ni kukuona hapa tena ukiwa umwanaume. Sasa nataka unijibu mwenyewe kwa kinywa chako. Ukileta ujuaji nitakusafirisha ukaungane na Vicky, Yule msichana uliyemuua pasipo na hatia. Sasa nijibu wewe ni nani? Umetoka wapi? Na unayafanya haya kwa kutumwa na nani? Aliongea masimba huku bastola yake ikiwa usawa wa kichwa cha mwanaume yule. Kitendo cha kuisikia sauti ile kutoka nyuma yake kilimshtua na kujikuta akiupoteza umakini katika hili. Kitendo cha kugunduliwa kwamba hakuwa mwanamke bali mwanaume hata hicho pia hakutegemea. Siku zote aliishi kama mwanamke na hata jamii ilitambua hivyo. Aliilinda siri ya muonekano wake kwa gharama kubwa sana. Alimuua kila mtu aliyemgundua na kuiigundua siri yake. Alisafiri katika nchi mbalimbali kufanya kazi za ndani kama mwanamke, kote huko aliua matajiri wake pasipo kugundulika. Lakini leo hii siri yake ilikuwa nje na pia alikuwa akitakiwa kueleza kile anachokifanya. Huyu ni nani? Ni swali lililopita kichwani kwake kwa kasi sana. Kumbe niligundulika wakati nikiua? Kumbe alikuwa na uwezo wa kunishuti na kunifuta hapa Duniani? Huyu ni nani? Yalikuwa mawazo yaliyopishana kichwani. Mawazo ambayo yalimchanganya na kuufanya ujasiri wake kuyeyuka. "Nasubiri majibu yako.." ni sauti kutoka kwa masimba iliyomshtua mwanaume huyu.

"Niambie kwanza wewe ni nani? Nami nitakujibu kila kitu unachohitaji kutoka kwangu." Akajibu yule mwanaume kwa sauti tulivu na kawaida sana. "Hupaswi kuuliza maswali, unachotakiwa ni wewe unijibu maswali yangu." Alisema masimba huku akimuangalia kwa umakini. "Sikiliza ni kwambie, huna sababu ya kukataa kunijibu.. nataka nikujue wewe ni nani kwanza na kwa nini unaniuliza maswali ya namna hiyo." Alizidi kuongea mtu yule akionyesha kutokujali. Akionyesha dharau za waziwazi. Hakujua huyu mtu alikuwa nani, hakujua anaongea na mtu ambaye mzaha kwake haukuwepo kabisa. Punde kidole kikafanya yake, risasi moja ikapenya kwenye paja la mtu huyu... Yowee la maumivu likamtoka. Alikuwa akianza kulalama hovyo. "Nitakuua kwa risasi moja moja ukiendelea kuniletea jeuri. Haya jibu maswali yangu." Aliongea Masimba Huku bastola bado ameielekeza kichwani kwa mtu huyu ambaye aliakuwa akilalama kwa maumivu. "Mimi sijui unachokisema.. wewe niue tu." Alijibu mtu yule akiendelea kuugulia maumivu.

"Kumbe unaniletea utani eeeh? Basi sina muda wa kupoteza." Aliongea masimba wakati huo huo akiachia Risasi tatu mfululizo ambazo zilimtupa mtu yule na kwenda kujibamiza ukutani. Alisogea na kumkuta tayari ni marehemu. Baada ya kujua tayari mtu huyu amekufa, akaanza kupekua sehemu tofauti ndani ya chumba kile. Upekuzi ambao ulimsaidia kupata Passports tatu zenye majina Tofauti. Bastola mbili pamoja na vitambulisho vitatu. Kati ya hizo bastola moja ilikuwa imetengenezwa urusi, huku nyingine ikitengenezwa Jamhuri ya Watu wa Czech. Zamani ikijulikana kama Czechslovakia. Pasipoti zilikuwa na majina ya watu watatu Tofauti. Moja ilikuwa na Jina la Veronica Senka ikionyesha ni Raia Wa Uganda. Nyingine ilikuwa na Jina la Janeth Omondi ambayo ilionekana kutolewa Kenya na passpoti ya tatu ilikuwa na Jina la Nusra Kassi akionekana kuwa ni Raia wa nchini kenya maeneo ya mombasa.

Hata vitamburisho vilikuwa na majina ambayo yalikuwa kwenye passipoti tena yakimuonyesha mtu huyu alikuwa ni mfanyakazi wa mamlaka ya bandari nchini kenya, uganda pamoja na Hapa Tanzania. Passpoti zake zilikuwa zimegongwa mihuri kutoka nchi kadhaa za kiafrika na hata ulaya. Baada ya kuridhika na vitu alivyopata akaamua kutoka hapo kwa kupitia Dirishani tayati kwa safari ya kuelekea Bandarini kuulizia jina la mtu huyu. Kichwani alitambua kuwa Jimmy alikuwa ameweka mizizi katika sehemu zote nyeti za nchi hii. Ilikuwa ni lazima kuing'oa mizizi ilikumuondoa katika Uso huu wa Dunia. Haikuwa kazi rahisi kuifanya lakini aliamini akianza kudili na mtu mmoja moja ni lazima atamuangusha Jimmy.

********

Aliingia bandarini na kulakiwa na msichana mmoja mweupe, mrefu na mwenye sura ya kuvutia. Macho yake makubwa na pua za kinyarwanda ni kitu pekee ambacho kilimfanya Masimba amuangalie mwanamke yule mara mbili mbili. Akavuta hatua mpaka pale kisha kwa sauti yake ya tatu akasabahi. "Habari yako Mrembo"?

"Salama tu kaka angu, karibu sana na sema shida yako nikusaidie. Aliongea msichana yule kwa sauti ambayo iliuburudisha moyo wa masimba.

"Naitwa John Raphael, natokea Hazina, nilikuwa nahitaji kumuona Mr Faudhi Facha Mkurugenzi muajiri wa Bandari. Alijibu Masimba huku akimuonyesha kitambulisho chake kinachoonyesha kweli ni mfanyakazi Wa hazina.
"Una miadi naye? Aliuliza binti yule.

"Sina miadi lakini ukimwambia kuna mtu anatoka hazina anataka kukuona atanielewa." Alijibu Masimba Huku macho yake yaliyozoea kugundua visivyogundulika ikitalii hapa mpaka kule.

"Nenda chumba cha Tano ghorofa ya tatu, hapo utakutana na sekretari wake atakusaidia." Alisema mwanamke huyu akimgandishia masimba macho usoni. "Nashukuru nikirudi nitakupitia nikakupe japo soda." Akaongea Masimba akimuacha mwanamke yule akielekea ghorofa ya tatu kwa mkurugenzi Muajiri. Alitembea kwa makini huku macho yake yakipita kwenye macho ya watu kugundua kama kuna macho yanamtizama kwa ghiliba. Lakini hapakuwa na hicho kitu. Kila mmoja alikuwa akiendelea na kazi kama kawaida. Alizipanda ngazi mpaka ghorofa ya tatu, akaongoza mpaka mlangoni mwa chumba husika. Akaugonga mlango kabla haujafunguliwa na binti mmoja mnene na mfupi mweusi. Kuingia na macho yao kutizamana na mwanamke huyu, akiona kitu machoni kwake. Macho ya Dada huyu yalikuwa yakizungumza hofu na wasiwasi. Kwa nini? Lilikuwa swali lililofuatiwa na Salamu.

"Karibu John.." alisema dada yule huku bado mshangao ukiwa usoni. "Ahsante bibie, bila shaka Taarifa yangu mnayo." Aliongea masimba akimuangalia zaidi mwanadada huyu. "Tumepigiwa simu kutoka mapokezi ndio maana umeona nimekuita Jina lako." Alijibu msichana yule.

"Ni utaratibu wa siku hizi au umeanza kwangu? Akauliza tena safari hii akihamisha macho usoni kwa mwanamke huyu na kuutizama mlango wa chumba cha mkurugenzi.

"Hapa sio kwako tu, hata wengine pia ni hivyo." Akajibu mwanamke yule. Lakini kwa masimba aliuona uongo wa Jibu hili. "Naweza kumuona mzeee? Akauliza Masimba.

"Yeah!, ingia anakusubiri." Alijibu msichana yule. Masimba hakuongea kitu zaidi ya kuongoza ndani kuelekea chumba cha mkurugenzi. Akaugonga mlango.. "pita kijana." Ilikuwa sauti kutoka ndani ya chumba. Masimba akausukuma mlango akaingia. Baada ya kuingia ndani akajikuta akitizama na Ofisi nadhifu iliyopangiliwa vizuri. Kaa hapo bwana masimba. Naona leo nina bahati ya kutembelewa na mtu kama wewe. Kufanya kazi hazina Sio kutu cha kawaida." Aliongee mzee yule akionyesha bashasha usoni. Kwa mtu kama masimba haikuwa bashasha, kwa mtu kama Masimba sauti ile haikuwa ikimaanishe kile ilichokusudia. Sauti ile ilikuwa na kitu ndani yake. Kitu kama dharau na hatakejeli. Hakujali hilo, akavuta kiti na kukaa. "Nashukuru sana mzee wangu, nami nimefarijika kukutana na mtu kama wewe. Naamini kuna mengi ambayo nitajifunza kwako." Naye akaongea Huku akimuangalia mzee yule usoni. Hofu na wasiwasi ni vitu viwili ambavyo vilikuwa ndani ya macho ya mzee huyu. "Okay, nakusikiliza kijana Wangu.." aliongea mzee yule akikaaa sawa.

"Nashukuru, kuna kitu ambacho nimekutana nacho leo hii huko nitokako, nikaamini nikija hapa kwako naweza kupata majibu ya maswali yangu." Aliongea masimba kwa upole huku akimtizama mzee yule. "Endelea Kijana...."
"Mzee kabla sijaendelea popote, naomba kumjua mtu huyu. Aliongea masimba akutoa moja ya kitambulisho kati ya vile vitatu na kumpa mzee.

Mzee yule akakipokea na kuanza kukitizama.. Mshtuko usio wa kawaida ukaonekana machoni mwake. Akainua kichwa kumuangalia Masimba. Akakutana na sura tofauti.. hii haikuwa sura iliyoingia hapa muda mfupi uliopita. Hii ilikuwa sura ya kazi. Sura inayomaanisha kile kinachotakiwa kumaanishwa
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom