mtoto wa mamantilie
New Member
- Feb 9, 2026
- 2
- 0
Usiku wa Mbuguni
Usiku wa Mbuguni haukuwa na sauti nyingi.Ni upepo tu uliokuwa ukipita juu ya mashimo ya migodi, ukibeba harufu ya vumbi na jasho la wachimbaji.
Amani alikuwa anakimbia.
Miguu yake ilikuwa imejaa vumbi jekundu, pumzi ikimkata kifuani kama kisu. Kila hatua aliyopiga ilimkumbusha kwamba mwili wake haukuwa na nguvu tena kama zamani. Ugonjwa uliokuwa umemtesa miezi kadhaa migodini ulikuwa umemla polepole.
Lakini hakuweza kusimama.
Mbali kidogo nyuma yake, taa za gari zilikatiza giza la usiku.
Aliangalia nyuma kwa sekunde moja tu.
Gari lilikuwa linakuja kwa kasi.
Amani alijua wale waliokuwa ndani ya gari hilo.
Hakuhitaji kuwaona.
Aliwajua.
Alijaribu kuongeza mwendo lakini miguu yake ilianza kulegea. Alifika karibu na shimo moja la mgodi lililoachwa wazi, akasimama kwa sekunde akipumua kwa nguvu.
Mawazo yakaanza kumrudia kichwani kama radi.
Arusha.
Kijiwe cha kahawa.
Kicheko cha Musa.
Halafu sauti ya Zawadi ikamjia kichwani.
"Amani, siku moja haya maisha yatakupeleka pabaya..."
Amani alifumba macho kwa sekunde moja.
Hakuwahi kufikiria mwisho wake ungekuwa hapa.
Si alipokimbia Arusha.
Si alipokuja Mbuguni kutafuta mahali pa kujificha.
Gari lilisimama mita chache nyuma yake.
Milango ikafunguka.
Watu watatu wakashuka.
Mmoja wao alibeba bastola.
“Amani,” sauti moja ilisema kwa utulivu.
“Bosi anasema umefanya kosa kubwa sana.”
Amani alicheka kwa uchungu kidogo.
“Kosa?” alisema kwa sauti dhaifu.
“Kosa langu lilikuwa kuamini kuna sehemu salama ya kukimbilia.”
Kimya kidogo kikapita kati yao.
Upepo ulipiga vumbi juu ya ardhi ya mgodi.
Amani alitazama mbali gizani, kana kwamba alikuwa anaona maisha yake yote yakipita mbele yake.
Arusha.
Musa.
Zawadi.
Halafu akasema polepole:
“Nilifikiri nikikimbia siasa… nitapata amani.”
Mtu aliyeshika bastola hakujibu.
Risasi ililia usiku ule.
Mwili wa Amani ukaanguka karibu na shimo la mgodi.
Upepo uliendelea kuvuma juu ya Mbuguni kana kwamba hakuna kitu kilichotokea.
Na mbali sana huko Arusha, watu waliendelea na maisha yao bila kujua kwamba hadithi ya Amani ilikuwa imefikia mwisho.
Lakini ukweli ni kwamba hadithi yake haikuanza hapa.
Ilianza miaka kadhaa nyuma, wakati taifa lilipoamini kwamba limepata raisi wa watu.