NITAKUPATA TU
SEHEMU YA 056
Masimba hakujua tena kile kilichoendelea. Akaruhusu giza kuifuta Nuru ya macho yake. Akatulia na kutulia.
*****
Teddy alishangaa muda kakatika bila Masimba kufika nyumbani. Kwani walipoachana usiku ule alimwambia kuwa angerudi katika muda wa usiku ule. Lakini mpaka saa mbili ile hakuwa amemuona Masimba pale nyumbani. Hilo likampa shaka na wasiwasi mkubwa, alihisi masimba alikuwa kwenye hatari ama atakuwa ameshakufa. Kwa kuwa wakati wanaachana alimeambia anaelekea nyumbani kwa Chief.. Teddy Hakuona sababu ya kuendelea kukaa pale ndani. Alitaka kwenda kumtafuta Masimba, alitaka kuinasa habari kuhusu wapi alipo mwanaume wake. Akaondoka mle ndani akipanga kuelekea masaki. Masaki sehemu ambayo ilikuwa ya mwisho Masimba kusema kwamba anaelekea huko. Hakutaka kumuacha France, aliamua kumchukua na kuelekea naye huko. Japo ilikuwa ni hatari lakini asingemuacha mtoto katika jumba lile akiwa peke yake. Alijiandaa na kumuandaa France, muda mfupi baadae walikuwa Njiani akielekea Masaki. Kujua taarifa ya mtu sahihi kwake. Alifika masaki asubuhi ile na kupokelewa na Walinzi wa Chief. Akawasalimia na kuwaambia adhma yake ya kuonana na Chief. Simu ikapigwa moja kwa moja na majibu yalipokuja yakamkuta Teddy tayari yupo ndani akizikwea ngazi. Alihitaji kufahamu wapi alipoelekea Masimba baada ya kuondoka hapo. Alizimaliza ngazi na kutokea katika chumba maalum cha Chief. Aliingia akiwa katika sura yake nzuri lakini isiyokuwa na tabasamu. Macho yake yakakutana na macho ya Chief ambayo yalionyesha kuwa hayakupata mapumziko kwa muda mrefu. "Karibu Sana Mama..." aliongea Chief kwa sauti yake tulivu. "Ahsante Baba Yangu, nimekaribia lakini sikuja kukaa mzee.. nimekuja kukuulizia kuhusu muwendaji wako mkuu hajarudi jana." Aliongea Teddy macho yake yakimuangalia chief usoni kutafuta kitu machoni kwake. Alitaka kuumsoma Chief katika aina na mtindo aujuaye yeye. Lakini akakutana na macho ya chief yasio na hofu. Macho ya chief yaliyo yakawaida kabisa kuonyesha hakuwa na mashaka. "Teddy umepoteza uwezo wako uliokuwa nao mwanzo.. Teddy wa mwanzo anapotokewa na hali hiyo alianza kwanza kuutafuta ukweli.. Teddy yule hakuwa akifunga safari kuja ofisini ama hapa nyumbani. Aliitenda kazi ya kumtafuta kwa mikono yake mwenyewe. Umeingia wapi muwindaji wangu? aliongea Chief kwa sauti yenye umakini wa hali ya juu. Teddy akainua uso na kumtizama mzee kwa mara ya pili. Maneno ya chief yalikuwa na ukweli ndani yake. Hakuwahi kuja ofisini wala nyumbani kwa Chief. Aliutafuta ukweli mwenyewe. Hilo likamfanya ainuke na kumuaga chief. Alitaka kwenda kumtafuta Masimba na kumrudisha akiwa hai ama mfu. Alitambua Masimba atakuwa sehemu ametekwa ama kuuawa. Wakati anakaribia kutoka mlango wa mwisho wa jumba la mkurugenzi akaisikia Sauti ya Chief ikimuita. "Teddy Rudi ndani mara moja!!" Ilikuwa sauti ya Chief, mara hii ikionyesha haipo kwenye ukawaida. Teddy akageuka na kurudi ndani. Akitembea Huku macho yake yakipepesa huku na huko. Tofauti ya Chief ya safari hii ilimuonyesha kuwa chief ameipata habari mbaya. Alipomkaribia Chief, chief akanyoosha mkono na kumpa kikaratasi fulani. "Muwindaji wangu amefungiwa sehemu fulani pembezoni mwa Jiji.. Chukua hiyo namba, nenda kwa watu wa Mamlaka ya Mawasiliano Wakwambie hiyo namba imetuma ujumbe kutoka wapi. Nenda Ofisini waambie wakusaidie kupata taarifa ya namba hiyo." Aliongea Chief huku akigeuka kurudi ndani. Teddy hakusubiri, kile alichokuwa akikifikiria ndicho ambacho kimetokea. Akaliacha jengo la chief. Akatembea mpaka alipoiacha Gari yake. Akaufungua mlango wa gari na kujipakia. Safari yao ikaanza kuelekea kijitonyama.. njiani mawazo yaliendelea kumzonga juu ya kutekwa kwa masimba. Nani atakuwa amemteka? Je wamempeleka wapi? Aliyawaza yote huku akimuangalia France aliyekuwa amekaa pembeni. Akakumbuka kwamba alipewa namba na hakuifungua kuiangalia. Akaichukua karatasi ile na kukifungua. Punde alikuwa akiitizama namba ya mtu anayemfahamu. Mtu ambaye alimtambua na kumjua kiundani Zaidi. Alikuwa akiitizama namba ya suresh. Kengele ya tahadhali ikagonga kichwani.
Alitambua Jimmy na washirika wake ndio wako nyuma ya kutoweka kwa masimba. Hapo ndipo alipoipata hamu ya kuweka laini yake ya zamani. Aliwaza kufanya hivyo kwa kuwa aliamini angetumiwa ujumbe kutakiwa kufanya kitu kwa sababu ya kuachia Huru kwa Mpenzi wake. Akaegesha gari pembeni na kuitoa simu yake kisha kuipachika laini husika. Baada ya kuiweka na kukaa sawa.. Muda ule ule akaiona simu yake ikiita, alipoangalia Jina la mpigaji moyo ulimpiga paa baada ya kuona namba ya Chief. Haraka haraka akaipokea.. "hallow baba!!" Aliita Teddy.
"Umefika ofisini tayari? Aliuliza Chief akionyesha wasiwasi kwa sauti yake.
"Hapana, lakini nishamtambua na kuwatambua wote." Akajibu.
"Umewatambua na kuwajua? Ni kina nani? Wamenitumia ujumbe nikutafute nikwambie uupeleke mzigo wao ili tumchukue Masimba." Aliongea chief.
"Hawapelekewi chochote na Masimba atarudi akiwa hai na Salama. Niachie mzee hii ni vita yangu mimi. Masimba aliingia katika Hili kimakosa. Naomba ukae kimya na usijibu chochote." Aliongea Teddy na kukata simu. Sasa alikuwa akiingia kazini rasmi, alikuwa akiingia katika kazi nzito na ya Hatari. Aliujua ugumu na alitambua hatari yake. Hapo ndipo alipoamua kumpeleka France nyumbani kwa Chief. Alitaka kuwa huru katika kuifanya kazi yake. Alitaka kuwaonyesha kuwa hakuwahi kutishwa na akaogopa. Wakati akiwaza Hayo simu yake Ikaita. Kutizama namba ya mpigaji ilikuwa ni namba ile ile ya Suresh. Akaipokea na kuipeleka Sikioni. "Tunauhitaji Mzigo wetu, la sivyo utaiokota maiti ya mpenzi wako." Aliisikia sauti ya upande wa Pili ikiinguruma. Ilikuwa sauti tofauti na ya Suresh.. hii ilikuwa ngeni masikioni kwake. "Sileti chochote, hampati Chochote, na Masimba nitakuja kumchukua mimi mwenyewe." Alijibu Teddy.
Ukimya wa Ajabu ukatokea, kisha kicheko kikafuata. "Teddy wewe ni mdogo sana.. huwezi kupambana na sisi. Nakuonya usithubutu kufanya lolote utampoteza Masimba na hata wewe mwenyewe utapotea." Bado mtu wa upande wa pili alisikika akinguruma.
"Sijawahi kutishwa kisha nikaogopa. Nakipenda kifo na naipenda Damu pia. Nimeshatoka sehemu hatarishi kuliko. Sasa naomba nikwambie.. sitafanya chochote kile mnachohitaji, lakini ninachokisema ni kwamba Masimba atatoka na mzigo hautatoka. Mwambie Jimmy na Suresh sijawahi kushindwa kile ninachokiamua. Vita ndio imeanza." Aliongea Teddy kisha akakata simu. Aliuona uoga wa adui zake. Aliuona uoga wa kina Jimmy. Hili lilionyesha ni jinsi gani watu hawa walivyo waoga.
******
Alihisi kama yupo kwenye kina cha maji kilichommeza kiwiliwili chote. Kichwa chake pekee ndicho ambacho kilibaki. Hewa nzito na harufu mbaya ni vitu pekee vilivyomfanya aanze kufumbua macho yake taratibu na kutizama. Giza, ndio kitu cha kwanza kukutana nacho pale alipoyafumbua macho yake. Alijaribu kuangaza huku na kule kama ataona kitu chochote, lakini hakukiona chochote kile. Bado giza lilitanda kila kona. Akatulia kwa muda kuipa utulivu akili yake, alitaka kuipa muda wa kufikiria hatimaye kufanya maamuzi sahihi. Chumba alichofungiwa kilimpa majibu ya wapi alipo. Akaendelea kuwaza na kuwazua, akainuka pale chini na kukaa kitako. Akaitizama mikono yake ambayo haikufungwa na chochote kisha akacheka. Ni kosa kubwa kumuacha Jasusi mfano wake katika Uhuru wa aina yake. Kumuacha huru katika namna ile ilikuwa ni kumpa nafasi ya kufanya akitakacho. Aliamini angetoka katika muda wowote na katika namna yoyote. Punde akasikia nyayo za watu zaidi ya mmoja zikisogea kuelekea pale ndani. Masimba akarudi chini katika kuzuga kuwa bado hakurudiwa na fahamu. Kwa aina fulani ya kutizama akawaona watu wawili wakiingia ndani huku watatu waliokamatia bunduki nzito wakibaki mkononi wakiitizama kila hatua huku wakiwa tayari kwa chochote. Akaendelea kutulia wakati watu wale walipombeba na kuanza kutoka naye ndani ya chumba kile kinachoonekana kama kuzimu. Alitulia akiangalia kwa umakini, alilichunguza Jengo lile ili akianzisha Rabsha iwe ni rahisi kutoka.
Bado watu wale waliendelea kusonga mbele ndani ya jengo hilo. Wakaufikia mlango mmoja uliotengenezwa kwa chuma. Mmoja akabonyeza kitufe kimoja mara lango likafunguka. Macho ya masimba yakakutana na chumba ambacho ndani yake damu nzito na mabaki ya Binadamu vilisambaa kila kona. AKAJUA SASA ALIKUWA AKIINGIZWA KWENYE CHUMBA CHA MATESO. AKAUANDAA MWILI WAKE TAYARI KWA KUKABILIANA NA MATESO HAYO