Riwaya: Nitakupata tu

Riwaya: Nitakupata tu

Anayeikumbuka namba yake amcheki what's up, pengine kuna sababu. Sio kawaida yake huyu jamaa.
 
Ibra87 atakuwa anatatizo si kawaida kuwa kimya namna hii
 
NITAKUPATA TU

SEHEMU YA 052

Teddy akasimama akiwa ameduwaa akiutizama mwili wa mwanaume yule wa kizungu uliolala katikati ya dimbwi la damu. Nani amemuua mwanaume huyu? Nani anawaua watu hawa? Anawaua kwa sababu gani? Je wanaficha ushahidi? Yalikuwa maswali tata kichwani kwa teddy. Bado bastola ilikuwa mkononi akiinyoosha kuelekea kule ulipo lala mwili. Sasa akaamua kusogea akiwa makini kwa kila hatua. Akauruka mwili ule kisha kuingia ndani kabisa ya chumba cha mwanaume yule. Kuingia huko macho yake yakainasa vurugu, vurugu iliyofanywa kabla ya mwanaume yule kuuawa. Kila kitu kilikuwa chini ama kimevunjika ama kusambaa. Damu ilianzia ndani kabla ya sebuleni. Muonekano wa mtu yule aliyeuawa ilionyesha kuwa aliuawa akiwa kule sebuleni. Lakini kuvurugika kwa vitu sambamba na matone ya damu yalikivuruga kichwa cha teddy. Ilionyesha waliouawa walikuwa wawili. Ilionyesha aliyeuawa chumbani alikuwa mwingine. Ni hapo alipoipata hamu, hamu ya kumtafuta ama kumuona mtu mwingine aliyeuawa. Lakini angemtafutia wapi ikiwa hapakuwa na sehemu nyingine ya kutokea? Hapo ndipo alipoifanya akili yake kufanya kazi. Akatambua lazima kuna sehemu kuna mlango wa kupitia. Mlango ambao ndio uliotumiwa na watu kumficha huyu marehemu wa pili. Umakini ukaongezeka. Teddy akaangalia kila upande kama angeweza kugundua chochote. Lakini haikuwa rahisi. Haikuwa rahisi kwa kuwa hakuuona mlango wala alama yoyote iliomuonyesha kama kuna sehemu ya kupitia. Bado hakuamini alitaka kuhakikisha ukweli, mawazo yake yalimwambia ipo sehemu. Ni hapo wakati akiwaza hilo alipouona ufa ukutani. Lakini kilichomgutusha, huu haukuwa ufa wa kuonyesha dalili ya kubomoka kwa ukuta. Bali huu ulikuwa ufa wenye kunyooka kuonyesha kwamba ulitengenezwa maalum. Teddy akasogea huku umakini ukiwa katika kiwango cha juu. Alipoufikia ule ufa akafanya kama anaugusa ukuta, punde akashangaa ukuta ukijifungua. Akatupa macho ndani kwa chati, damu tena ilionekana mle ndani. Sasa akaamua kuingia kabisa kwenye chumba kile cha siri akiifuatilia ile damu. Damu iliyotapakaa katika chumba kile cha siri. Kuingia kwake ndani kukafuatiwa na tukio la kujifunga kwa ule ukuta. Punde akajikuta akitizamana na wanaume wanne walioshiba kama wacheza mieleka. Ni katika kasi ile ile teddy akataka kunyoosha bastola afyatue risasi. Lakini hakuwahi kulifanya hivyo. Kwani kwa wepesi wa unyoya, akajikuta akipokea mateke matatu mfululizo kutoka kwa mmoja kati ya wale wanaume wanne. bastola yake ilikuwa pembeni sasa alikuwa amesimama akiwa mikono mitupu. Wanaume wale wakamtizama kwa dhihaki. Wakamtizama wakimdharau. Muda mfupi wakaanza kumfuata wote kwa pamoja. Teddy akawa anarudi nyuma. Ni kipindi akigota ukutani ndipo alipouona ukuta ukifunguka tena. Akamuona mwanamume akiingia katika namna itiayo burudani Moyoni na Hata machoni. Mwanaume aliyeingia mfano wa kivuli. Teddy akataka kwenda kumkumbatia, lakini hakuweza kufanya hivyo. Hakuweza kwa kuwa uingiaji ule ulimpa kihoro. Kwanza hakuamini kama mtu huyu anaweza kuwa pale. Akamuangalia alivyokuwa akitembea, akahisi labda alikuwa akumtizama Joram kiango, akahisi huyu labda ni willy gamba.

Hata wanaume wale wanne walikuwa wameduwaa wakimwangalia kijana huyu aliyekuwa akiingia. Sio kwamba hawakumjua, sio kwamba hawakumuona, bali hawakutarajia hilo. Hawakutarajia ujaji wa mwanaume yule. Yule ambaye waliambiwa yupo tanga kwenye msiba wa mama yake. Lakini leo hii alikuwa mbele yao akitembea kama dume. Dume ambalo halikuonyesha hofu. Hata wao wakalishangaa na kuduwaa. Hawakumuangalia Teddy tena, wakamuache Teddy akinata na kuzunguka. Masimba akampita Teddy kisha kwenda kusimama mbele ya wanaume wale. Haikuchua hata sekunde katika tendo lile lililotendeka. Tendo lililowaacha wanaume wawili kati ya wanne wakianguka chini. Kila mmoja alikuwa akitoka damu kooni. Kisu kilikuwa kimepita kwenye shingo zao. Hili liliwashtua wanaume wawili waliobaki. Wakaamua Kujaribu bahati yao. Mmoja akatupa teke ambalo lilimpata Masimba na kusababisha bastola yake kuanguka. akabaki mikono mitupu. Ngumi zikapigwa katika aina fulani inayovutia. Licha ya kuwa na miili mikubwa lakini wanaume wale walikuwa wakiziweza ngumi. Yalikuwa mapambano yaliyodumu kwa Dakika Sita. Mapigano ambayo yalimfanya teddy ajisikie Hamu. Sio hamu ya tendo bali ilikuwa hamu ya kupambana. Lakini alipokuja kutizama Chini akaiona miili ya wanaume wale ikiwa sakafuni wakivuja damu. Baada ya kuwamaliza wale, masimba akamshika teddy na kumuongoza. "Hatutakiwi kuwa hapa, kuna mtu anatembea na sisi. Kuna mtu anaufuta ushahidi. Lazima tumjue." Aliongea masimba huku wakitokea mlango wa nyuma wa jengo lile kuelekea Nje. Wakatoka nje kabisa ya jumba lile. Ilikuwa safari ya kumtafuta mtu anayewazidi kwa kuwaua wale watu muhimu. Ni lazima wafanye hivyo. Safari hii ikaishia mpaka katika ile nyumba ya siri. Humo ndani wakapokewa na France sambamba na Salha. Hilo likaonyesha kumshtua Teddy. Hakutegemea kukutana na lile. Hakutegemea kumuona Salha sambamba na france pale ndani. Hapo akahisi kitu kikiupenya Moyo wake na kujikuta akitamani kuongea kitu. Sio kwamba alimuogopa Salha bali kitendo cha kumkuta pale akiwa na france ambaye alikuwa mikononi mwake ilimfedhehesha sana. Masimba aliligundua hilo mapema. Masimba aliugundua wivu katika uso wa teddy. Wivu sambamba na kutokuamini ni moja ya vitu vilivyomchanganya. Akamsogelea Teddy na kumkumbatia, "usihofu mama huyu ni mmoja kati yetu.. alichokifanya kumchukua France ilikuwa ni usalama wa mtoto sambamba na Familia. Watu hawa wangegundua hili tungempoteza Vicky sambamba na familia nzima.." aliongea Masimba. Teddy akanyamaza kwa muda, kisha akasogea na kumkumbatia france.

*******

Ulikuwa usiku wa manane pale Masimba alipokuwa mezani akikagua nyaraka alizopewa na yule mama wa ofisi ya waziri mkuu. Alikuwa akipekua moja baada ya nyingine. Akaisoma kwa makini na kupitia kila neno. Mawasiliano ya waziri mkuu na baadhi ya watu. Nyaraka muhimu za uingizaji na usambazaji wa biashara ya madawa ya kulevya. Biashara ya pembe za ndofu ni kitu ambacho kilikuwa kikifanywa na Ofisi ya waziri mkuu. Mikakati na mipango ya biashara hiyo ilisukwa kwa ustadi na watu wazito ndani ya serikali. Tembo, twiga na hata meno ya tembo vilisafirishwa kwenda china na watu wanaonekana kama Watalii. Kila mstari aliokuwa akiusoma alijikuta mwili ukimsisimka kutokana ya kile kilichomo ndani ya nyaraka zile. Waziri mkuu alikuwa ametengeneza genge la uharifu kwa kutumia cheo chake. Lasilimali za Nchi zilikuwa zikisafirishwa kila uchwao kwa kupitia mipakani na hata kwenye viwanja vya ndege. Hakikuwa kitu cha kawaida. Akainuka pale na kurudi chumbani. Moja kwa moja akaiendea simu yake, alipoichukua akatafuta namba ya chief. Sekunde mbili simu ilikuwa hewani. "Kuna tatizo kijana?" Aliongea chief kwa sauti ya usingizini. "Nipo kazini mkuu na unaitambua hii kazi. Nakuja muda mfupi hapo nataka unipeleke Ikulu." Akajibu masimba. "Ikulu muda huu? Hujui kuwa kuna sheria na taratibu zake za kuingia. Unadhani usalama wa ikulu wataturuhusu? Alijibu chief kwa aina ya swali. "Wewe ni nani hapa nchini? Mimi ni nani hapa nchini? Ongea na rais muda huu kuwa tunakwenda hapo." Alipomaliza kuongea hayo akakata simu bila kusubiri jibu la Mkurugenzi. Kisha akageuka kitandani kumuangalia Teddy Harry aliyekuwa amejiegemeza kitandani. Akakutana na macho ya teddy yakimtizama. Haya kuwa macho ya kawaida. Yalikuwa macho yanayohitaji kukijua kitu. Teddy alihitaji kuambiwa kitu. Masimba akamtizama sana.. punde walikuwa wamekumbatiana. "Naenda Ikulu mpenzi..Kuna kitu ambacho siwezi kubaki nacho hapa. Naomba uwe mlinzi wangu kwa nyuma yangu. Nataka umuangalie yule ambaye anatembea nasi. Hakikisha huonekani na wana usalama wengine." Aliongea huku akimuachia teddy na kuifuata bastola yake. Akatoka mle ndani akifuatana na Teddy tayari kwa safari ya kupeleka nyaraka Ikulu.
 
NITAKUPA TU

SEHEMU YA 053

ILikuwa safari ya kuelekea ikulu. Safari ambayo ilikuwa ni mwanzo wa kuupeleka ushahidi ambao utaweza kumshawishi rais wa nchi katika kuamini sababu za kuuawa Waziri mkuu. Alitoka na Teddy lakini muda fulani teddy akarudi kwa kupitia njia nyingine tayari kwa kuwa mtu wa nyuma ya Masimba. Huyu alikuwa ndiye mlinzi na mchunguzaji mkuu wa Masimba. Akarudi ndani kisha kutulia tuli. Masikio yake aliyatega huku na huko katika kuusikia mchakato hata wa sisiminzi. Akatulia kwa muda fulani bila kusikia chochote. Akainuka taratibu na kuurudisha mlango na kuelekea mbele zaidi. Wakati akiukaribia mlango akausikia mlango kama unafunguliwa Taratibu. Akachepuka pembeni na kutulia huku macho yakitizama mlangoni. Taratibu akakiona kivuli cha mtu kikitokea pale mlangoni. Mavazi aliyovaa sambamba na kiza kile hapakuwa na tofauti ya mfanano. Akakaza macho yake na kutizama kwa umakini Zaidi. Akamuona mtu akipita taratibu na kuuendea mlango. Kabla hajaufungua akaangaza huku na huko. Teddy bado alikuwa akimuangalia kwa ukaribu sana. Licha ya ukaribu huo lakini bado hakuwa amemgundua kwamba alikuwa ndani. Baada ya mtu yule kuangalia huku na huko akaufungua mlango kwa utaalamu ambao ulimfanya Teddy ahisi mtu huyu alikuwa ni jasusi kupindukia. Baada ya kuufungua mlango mtu yule akatoka tena safari hii akinyata mfano wa paka. Punde alikuwa akitokea juu ya ardhi. Baada ya kutokea hapo akatulia pembeni kuangalia kama alikuwa akifuatwa. Haikuwa hivyo, haikuwa hivyo kwa kuwa hapakuwa na mtu aliyekuwa akimfuatilia. Akainuka na kuianza safari. Wakati yeye akiondoka katika namna ile, pembeni kidogo alisimama Teddy akimuangalia mtu yule. Mtu ambaye mpaka kufikia pale hakuwa amemjua wala kumgundua kuwa alikuwa nani. Alipoondoka alipokuwa amejibanza, Teddy naye akafuatia nyuma kwa umakini. Ilikuwa ni lazima Teddy awe makini kwa kuwa alijua alikuwa akimfuatilia mtu ambaye ni mjuzi wa mambo yao. Alihakikisha mtu yule hampotei kwenye upeo wa macho yake. Alihakikisha mtu yule hampotei kabisa. Bastola mkononi akazidi kumfuatilia kwa umakini. Mtu yule alipofika karibu na barabara ya mandela. Akasimama kisha kitendo bila kuchelewa akaiona gari mmoja ikija kwa kasi na kusimama karibu kabisa na miguu ya mtu yule. Baada ya gari kusimama milango ikafunguliwa kwa kasi. Ni hapo alipokuwa akipanda ndani ya gari ndipo Teddy alipogundua mtu yule alikuwa nani. Ni wakati mtu yule anaupeleka mguu wake juu ili apande, kofia iliyomficha sura yake ikaanguka. Alikuwa Salha, alikuwa yule yule salha waliokuwa wakiishi naye. Salha aliyekuwa akiishi na France. Leo alikuwa akipakiwa kwenye gari fulani. Alikuwa akienda wapi? Kufanya nini? Na wale ni wakina nani? Yalikuwa maswali mfululizo kuchwani kwa Teddy. Maswali ambayo hayakupata majibu kwa wakati ule. Akabaki kuwa mtazamaji katika tukio lile, akiangalia namna atakavyoondoka hapo. Kwa wakati ule hakuwa na uwezo wa kujitokeza kwa kuwa sehemu yenyewe haikumruhusu. Punde akaiona gari ikiondoka kwa kasi akielekea buguruni. Hapo akakumbuka kumjulusha masimba juu ya kilichotokea. "Nimeona kikundi cha nyuki kimepita hapa na kuondoka na nyuki jike tunayeshi naye." Aliongea Teddy kwa Lugha ya Mafumbo. Lugha ambayo ilitumika sana katika masuala ya kijasusi. "Nimeona, nimewaona. Hapa tunapoongea nami nipo nyuma ya nyuki hawa pasipo wenyewe kujua. Cha kufanya naomba urudi mzingani ukamuondoe Nyuki mdogo." Alijibu masimba kwa lugha ile. Lugha ambayo waliifahamu wachache katika medani ile ya Kijasusi." Baada ya maongezi hayo na Masimba, Teddy akatii na kurudi nyumbani kama alivyoambiwa.

********

Gari aliyopanda SALHA sasa ilikuwa ikiiacha barabara ya maendela na kuchukua barabara ya uhuru. Safari ilikuwa ikiendelea huku gari hii ikionekana ikielekea kariakoo. Baada ya kuipita rozana na malapa, sasa ilikuwa ikielekea eneo la Ilala boma. Baada ya kufika Bungoni gari ikaingia kushoto na kuchukua barabara ya Kawawa. Sasa gari ilikuwa akielekea magomeni katika mwendo wa kasi sana. Bado masimba alikuwa nyuma akilifukuzia. Muda wote alikuwa ndani gari chakavu mali ya halmashauri ya Jiji la Dar es salam. Lililokuwa likitumika kama kubebea takataka Usiku. Bado alikuwa kwenye umakini mkubwa. Baada ya gari ile kufika maeneo ya kigogo roundabout akashuhudia ikiegeshwa pembeni, kisha watu watatu wakashuka. Baada ya watu wale kushuka na kuingia kwenye nyumba moja, akaishuhudia ile gari ikiondoka pasipo Salha kushuka. Hilo likampa utata kidogo, utata ambao hakujua wapi angeweza kuanza. Alihitaji sana kuwapata wale vijana. Alihitaji sana kujua wapi anapoelekea Salha. Alitakiwa akili yake iamue kufanya kitu kimoja, kitu ambacho kingempa muda wa kuwahi masaki. Akaona ni wakati wa kumfuata Salha. Shida yake alitaka kujua ni wapi Salha anaelekea. Uondokaji wake pale nyumbani haukuwa wa hatari. Kwa nini kutokumbeba france kisha kutembea umbali mrefu kutoka pale mafichoni kuifuata gari barabarani, Masimba Alijua salha hakutaka watu hawa wapajue pale mafichoni. Lakini vijana hawa ni kina nani? Nani yupo ndani ya gari Na Salha? Yalikuwa maswali mazito sana. Maswali ambayo yanahitaji majibu katika muda ule kabla hapajapambazuka. Jina la Falycious Benee lilikuwa la kwanza kumjia kuchwani mwake. Huyu alikuwa ni mwanaidara ambaye alikuwa akiifanya kazi kwa siri akiishi uswahilini. Muda wote alionekana kama mswahili lakini haikuwa hivyo. Kila alipokuwa akipita alikuwa kazini. Alikuwa akichukua hiki na kile. Akaichomoa simu yake na kuandika ujumbe mfupi ambao akautuma kwenye namba ya falycious. "Nyumba 0679 roundabouts nataka majibu yake ifikapo saa moja."... baada ya kuutuma ujumbe ule sasa akaamua kushuka kwenye gari lile chakavu na kukiendea kijiwe fulani cha pikipiki. Akamuita dereva mmoja pembeni na kuongea naye mawili matatu. Kitambulisho chake kikafuata sambamba na shilingi laki moja. Dereva akakubali kutoa pikipiki yake kumuachia Masimba. Kilikuwa kitendo kilichotendeka kwa dakika moja. Dakika ya pili Masimba alikuwa barabarani akiufuatilia ile gari. Pikipiki ilikuwa ikitembea katika utulivu wa hali ya juu. Bastola mbili bado zilimpa nguvu masimba ya kufuatilia. Hata wakati anafika kwenye makutano ya barabara ya morogoro, bado gari aliyopanda salha ilikuwa mbele ikitembea taratibu ikielekea maeneo ya magomeni. Masimba akaendelea kuwa makini kwa kila hatua. Wakaipita magomeni na sasa walikuwa wakielekea manzese. Hata walipoupita manzese bado gari ilizidi kusonga. Kufika shekilango ikaingia barabara hiyo na kwenda kuegesha gari nje ya maegesho ya Hotel ya Rombo View. Masimba akawapita na kuendelea kusonga mbele. Mbele kidogo akaisimamisha pikipiki kwenye bar fulani. Akamuita mlinzi na kumpa elfu kumi kisha kumuomba amlindie pikipiki. Baaada ya hapo akatembea kwa miguu kurudi nyuma kuuelekea Rombo view.

Baada ya kufika hapo akasimama kwa muda akiangaza, punde akamuona mlinzi akisogea na kutaka kumuuliza. Kitambulisho mkononi kwa Masimba kikamuacha mlinzi yule akirudi nyuma kwa woga. Baada ya mlinzi yule kusogea, masimba akaongoza moja kwa moja mpaka ndani ya Hotel. Hapo ndani akamkuta mtu wa mapokezi akimaliza kuandika vitu fulani. Akasogea mpaka pale.. "habari za saa hizi dada? : akasalimia masimba.

"Nzuri kakA! Nikusaidie nini? Akauliza mwanadada yule. "Nahitaji kujua watu waliongia sasa hivi wameelekea Chumba namba ngapi." Akajibu masimba taratibu akimuangalia yule mpangaji.

"Kaka hapa hatuna utaratibu huo wa kutoa siri za wateja." Alijibu yule msichana. Wakati wote macho ya masimba yalikuwa yakitizama kwa chati katika daftari lile. Macho yake yakatua kwenye jina la mtu anayejiita marlon. Chumba namba 045 A .. akajifanya anamuaga yule Dada na kushuka chini. Kabla hajatokea kwa Nje akageuka tena na kugeuza kurudi kule juu. Kufika pale mapokezi hakumuona yule Dada zaidi ya Matone ya damu na Mburuziko wa Mwili wa Binadamu. Bastola mkononi hatua kuelekea ulipo mburuziko zikafuata. Hatua kumi mbele ndani ya bafu zile akamkuta mhudumu amelala katikati ya Dimbwi la damu. Huku kisu kikiwa tumboni...

HII STORI INAWEZA KUBAKI KUWA KUMBUKUMBU NZURI KWANGU. ACHA NINYAMAZE MIKONO IFANYE KAZI
 
NITAKUPA TU

SEHEMU YA 053
HII STORI INAWEZA KUBAKI KUWA KUMBUKUMBU NZURI KWANGU. ACHA NINYAMAZE MIKONO IFANYE KAZI

Ni kweli Ibra, hii kazi ni nzuri, naamini Mungu atakuwezesha kuchapa kitabu ili ibaki kuwa kumbukumbu hata kwa vizazi vijavyo. Nasi tutajitahidi kuchangia.
 
Nna hasira sana lakini nguvu inagoma ila ucjali mkuu mungu atafanya wepesi inshaallah
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom