NITAKUPATA TU
SEHEMU YA 042
Hakutaka kugundulika mapema kwamba alikuwa katika viunga vile. Kutazama kwa mwanamke yule kulimpa mashaka kwamba kuna kitu atakuwa anakitafuta. Akamuaga teja yule na kuondoka katika eneo lile la Sinza. Safari hii akaamua kuelekea nyumbani ili aanze kwanza kumtafuta Teddy na kujua wapi alipo mwanawe France. Muda wote alikuwa akiikumbuka sura ya mama yake. Alijua mama yake angeamka siku yoyote na kuwa hai tena. Hakujua kuwa mama hakuamka na kamwe hataamka. Kwa mara ya kwanza tokea asubuhi akamkumbuka Dee plus. Alitaka kujua wapi alipofikia kuhusu wapi teddy alipo. Lakini hakutaka kufanya pale pale, alitaka kusubiri afike nyumbani kwanza ndipo angemtafuta. Alifika nyumbani kinondoni kigiza kikiwa ndio kwanza kinaimeza nuru ya mchana na kuukaribisha usiku huu tulivu kwa wengine. Nyumba yake ilikuwa kimya kuonyesha kutokutembelewa na mtu, achilia mbali kuishi watu. Aliiongoza mpaka getini bila wasiwasi, akajaribu kulisukuma geti la kuingilia, akashangaa likufunguka "mtego" lilikuwa neno la kwanza kutamkwa katika kinywa chake. Akafungua geti taratibu na kuingia ndani. Hapo akakutana na mwanga hafifu kutokana na kumezwa na kugiza kile cha saa moja usiku. Bado ukimya ulitawala na bado kengele za hatari ziliendelea kukigonga kichwa chake. Akatembea safari hiii bastola ikiwa mkononi. Alitembea taratibu akiufuata mlango wa kuingilia ndani ya nyumba. Akili yake ilikuwa ikimwambia kuna hatari. Mawazo yake yalikuwa yakimwambia kuhusu hatari. Hakutaka kupuuza katika hilo. Umakini ukaongezeka zaidi na zaidi. Alipoufikia mlango akajaribu kuufungua. Cha ajabu mlango ulifunguka kuonyesha kuwa haukuwa umefungwa. Akaingiza kichwa na kuchungulia ndani. Hapo akapokewa na giza tototo ambalo halikumsaidia kuona chochote. Akaufungua mlango zaidi akaingia mwili wote. Akatembea mpaka kwenye swichi na kuwasha taa zote mle ndani. Baada ya kuwashataa akajikuta akidhangaa baada ya kuona matone ya damu sakafuni. Hilo lilikuwa jambo ambalo hakulitegemea. Akaendelea kuangalia kwa umakini huku Bastola mkononi. Alitembea kufuata matone yale ya damu. Bastola ilikuwa ikitangulia. Kila alipokuwa akigeuka hata bastola iliangalia huko. Matone ya damu bado yaliendelea. Moyo wake ulikuwa ukidunda akihisi labda mwanawe France alikuwa ameuliwa na Teddy. Akahisi jasho likimvuja pale alipoyaona matone yale yakiishia nje ya mlango wa chumba chake. Hapo akasimama na kuivuta pumzi. Punde akausukuma mlango na kuangukia ndani. Macho yake yakatua Juu ya mwili wa mtu. Ukelele wa Hofu na uchungu ukamtoka. Dee plus alikuwa amelala kifudi fudi sakafuni, mwili wake ukiwa hautananiki kwa kuchakazwa na risasi. Akahisi bastola ikimponyoka na kudondoka chini. Hakuamini macho yake. Akausogelea mwili wa Dee Plus na kupiga magoti mbele yake. Mikono yake ikatamani kuushika mwili ule lakini mikono haikumruhusu. Alikuwa akitetemeka kwa hasira. Alikuwa akitetemeka kwa hofu ya kuuawa hata kwa wanawe. Alimtegemea Dee plus katika vita hii. Alimtegemea Dee plus katika kumsaidia hili. Leo alikuwa amepiga magoti mbele ya mwili wake. Ni jana tu walikuwa wakimzika mama yake, lakini leo na yeye alikuwa marehemu tena akiwa ameuliwa kinyama.
Masimba akautizama mwili wa Dee plus zaidi na zaidi. Wakati akiutizama mwili wa Dee, akakiona kitu mfano wa picha pembeni kwa mwili wa Dee. Huku mikono ikimtetemeka akanyoosha na kuichukua ile picha. Kuitizama tu, akahisi machozi yakimdondoka. Ilikuwa picha yake akiwa pamoja na watoto wake na mama yake pamoja na Tedy. Kilichomchanganya ni kukuta katika picha ile kuna sura za watu wawili zimepigiwa alama ya X. Sura ya kwanza ilikuwa ya mama yake mzazi. Picha ya pili ilikuwa ya mwanawe France. Ina maana France wamemuua? Lilikuwa swali lililomuasha masimba. Lilimuamsha kutoka kwenye kulia mpaka kwenye umasimba wake. Masimba yule ambaye hajawahi kukiogopa kifo. Akaitizama ile picha kwa muda, kisha achovya kidole chake kwenye Damu ya Dee plus na kuchora alama ya X kwenye picha ya Teddy. "Nitakuua Teddy, Nitakuua kabla ya jua la kesho." Alitamka masimba huku akiinuka akiutizama mwili wa Dee plus. Hakuwa akiamini mpaka muda ule. Mama kisha Dee plus harafu mwanawe France ndani ya siku mbili. Akaona huu ni wakati wakuacha kuutafuta ushahidi wa waziri mkuu katika uhusika wake katika biashara ya madawa ya kulevya. Alitaka kudili na uandaaji wa tiketi kwa sababu ya kuwasafirisha watu watano. Alikuwa ni lazima aandae tiketi hizo katika muda unaotakiwa. Ni lazima Mwamvita aondoke, ni lazima Jimmy apotee, Teddy lazima afutike katika uso huu wa Dunia. SURESH NA BEN nao wanatakiwa kwenye safari hiyo. Sasa hakutaka kwenda kwa yule teja, aliamua kumtafuta Mwamvita. Hawezi kumuacha aendelee kuivuta hewa wakati mama yake alikuwa amelala kaburini. Atamuachaje Teddy wakati alishaufumba mdomo wa france na Dee plus? Hakuwa tayari kuutafuta ushahidi. Alitaka kuua kwanza kisha ndio afanye alichotakiwa kufanya. Akaona amuarifu chief juu ya kifo cha Dee Plus. Akafanya hivyo katika muda ule, kisha akaongeza na kusisitiza kuhusu kile alichomwambia kuhusu Mwamvita. Chief akaitikia kanakwamba yeye ndiye alikuwa mfanyakazi wa chini. Akiitikia huku akihisi kuvurugwa kwa kile alichokisikia. Akauona umuhimu wa kuwaweka walinzi kadhaa katika chumba alichokazwa Mtoto wa Masimba. Sasa hakuwa akiwaamini hata watu wa chini yake. Alijikuta kila kitu akitaka kukifanya yeye. Hakutaka hili suala lifike popote. Aliamua kuuufumba mdomo wake huku akifuata angalizo alilopewa na Masimba la kutomwambia Mwamvita chochote. Sasa alikuwa amekaa kimya na kushika tama.
*****
Moyo wake haukuwa tayari kuwaacha watu hawa wakiwa hai. Alijaribu kumtafuta Mwamvita kila sehemu lakini hakufanikiwa kumuona popote pale. Hapo akaamua kumshirikisha Chief katika hili. Alitambua lazima kutakuwa na mawasiliano kati yao. Safari hii hakutaka kumpigia simu, alitaka kumfuata nyumbani kwake kwa kuwa alitaka kupata taarifa kwa kina. Akaondoka kule mafichoni kwake na kuelekea mpaka masaki. Kufika hapo akaambiwa Chief hayupo ameelekea ikulu kuitikia wito. Hilo likamfanya atulie kwa muda akitafakari nini cha kufanya. Alihitaji kujua alipo mwamvita na Hata Teddy. Lakini mpaka muda huo hapakuwa na fununu ya wapi walipo watu hawa. Hapo ndipo alipoona umuhimu wa kumfuata yule Teja kule Tandale kwa mtogole mtaa maarufu uitwao Yemen. Alihisi kama kwenda huko kunaweza kumpa taarifa ama kunusa chochote kinachohusiana na Mwamvita na Hata Teddy. Alipenya chochoro hii na Chochoro ile. Punde alikuwa amefika katika eneo hilo ambalo kwa hapa Dar es salaam liliogopeka sana Hasa kutokana na kuwa na wapiga kabali wenye uzoefu mkubwa kuliko sehemu yoyote hapa Tanzania. Akapita kwenye chochoro nyingine mpaka kuibukia kwenye nyumba ambayo alikuwa akiishi Teja yule. Ilikuwa nyumba nzuri ambayo kama ungewahi kuiona usingeamini Teja yule alikuwa akiishi katika nyumba ile. Ukimya ulikuwa umetawala huku kukionyesha kuwa Watu walikuwa wamelala mle ndani. Akaugonga mlango mara ya kwanza kisha mara ya pili. Akaisikia sauti kutoka ndani ikiuliza.
"Nani huyo?
Hakujibu bado alikuwa akuugonga mlango. Punde akasikia nyayo za mtu zikisogea mlangoni. Harafu komeo likasikika likifunguliwa kwa ndani. Sura ya mwanaume wa makamo ikatokea.
"Shikamoo mzee wangu!! Alisalimia Masimba.
"Marahaba, karibu ndani. Aliitikia mzee na kukaribisha. "Nilikuwa namuuliza Vickita Visenti kama yupo. Alisaili Masimba akimuangalia yule mzee usoni.
"Huyu kijana leo naona ameuliziwa sana. Muda sio mrefu walikuja mwanaume na mwanamke kumuuliziA, Sasa nakuona na wewe!!!. Nenda kule mwisho upande wa kulia ndio chumba chake kulipo." Alitoa maelezo yule mzee huku akimuonyesha masimba kwa kidole. Masimba akaingia ndani na kuongoza mpaka kule alipoelekezwa. Kufika mlangoni akasimama na kuchungulia ndani kupitia tundu la ufunguo. Jicho lake likatua kwenye mwili wa Yule teja akionyesha kulala. Baada ya kuona hivyo akaushika mlango na kuufunguq taratibu na kuingia. Kuingia kulikofuatana na Kutupa maji pale Kitandani. "MICHIRIZI YA DAMU" Ndicho kitu peker kilichoonekana pembeni mwa Vickita.
MASIMBA AKACHOKA