Riwaya: Nitakupata tu

NITAKUPATA TU

SEHEMU YA 040

Neema alimuangalia masimba kwa muda bila kuongea kitu. Alikuwa akikiangalia kile ambacho kipo ndani yake. Maumivu, majonzi na hata machozi ni kitu ambacho alikisoma ndani ya macho ya Masimba. Kingine alichokiona ni hasira na utayari wa kufanya chochote. Hakuwa na lakuongea. Maneno yalimuishia mdomoni. Akashuhudia masimba akitoweka machoni mwake mithili ya mzimu. Akitembea akionyesha hakutaka mashauriano na mtu. Alikuwa katika safari ya kumfuata Mwamvita nyumbani kwake mbezi beach. Moyo wake ulijaa uchungu, alikuwa akitembea huku akibubujikwa na machozi. Alikuwa akilia hasa pale alipouona mwili wa mama yake ukifukiwa. Akajua hatamuona tena. Akajua hata muona mwanamke huyu aliyemjali sana. Bastola zake bado zilikuwa mahali tulivu. Akatembea mpaka kituo cha daladala. Akajivuta machozi kisha akatulia akisubiria daladala. Muda mfupi akaiona daladala ikija huku konda akipiganikiza vituo. Ilipodimama alikuwa wa kwanza kupanda. Baada ya kupanda akatulia kwenye siti akitizama nje kupitia dirishani. Kwa kuwa ulikuwa usiku , barabara haikuwa na foleni. Wakajikuta wakitumia dakika saba kufika mbezi Africana. Baada ya gari kusimama, masimba akashuka taratibu na kuanza kutembea taratibu kuelekea nyumba anayoishi Mwamvita. Alitembea kama mtu wakawaida na mwenye shughuli zake akipishana na watu na hata polisi wa Doria. Bado hakuwajali na bado hakuwatizama. Akaingia uchochoro fulani na kwenda kutokea mtaa wa pili sehemu ambayo alikuta panabar. Baada ya kutokea hapo kwenye bar, akasogea hapo na kutafuta kiti. Kwa kuwa ilikuwa sehemu kimya sana licha ya kuwa na bar, lakini pia aliiona kuwa ilikuwa sehemu nzuri yakutulia kuuvuta muda akiwasubiri watu wapungue aweze kuingia kwa Mwamvita kwa Urahisi. Baada ya kuvuta kiti akamuita mhudumu na kumuomba ampelekee mzinga wa Whisky. Mhudumu akafanya hivyo na muda mfupi baadae Masimba alikuwa akimimina kinywaji mdomoni huku macho yake yakicheza kila kona. Kwa kuwa sehemu aliyokaa ilikuwa na giza aliweza kuwaona wote waliokuwa wakiingia. Alitulia akiendelea kunywa taratibu mpaka saa saba kasoro usiku ndipo alipoondoka hapo akiifuata barabara inayoelekea nyumbani kwa Mwamvita. Alitembea kwa kufuata giza mpaka nyumba ya pili kutoka nyumba anayoishi Mwamvita. Akasimama hapo akiitizama vizuri nyumba anayoishi mwamvita. Nyumba yote ilikuwa giza kasoro taa moja tu ya chumba ndio ilionyesha kuwaka tu. Hilo alilitegemea kwa kuwa alijua baada ya tukio lile lazima mwamvita angejidhatiti. Akaondoka hapo sasa akipiga hatua kuelekea kule. Akauvuka uzia wa nyumba ile, akajikuta sasa akitazamana na nyumba ya mbaya wake.

Akatulia hapo kwa muda bila hata kufanya chochote. Alikuwa akifikiria ni nini afanye ili kuingia mle ndani. Kuwaka kwa taa moja katika jumba lile haikumfanya masimba ategeke. Siku zote aliamini kuwa chumba kilichowashwa taa hakikuwa na watu. Watu walikuwa katika chumba kingine kabisa. Hilo akaliamini na ndio lililomfanya asimame. Aliamini mwamvita alikuwa sehemu ndani ya nyumba na sio katika chumba kile kinachowaka Taa. Hilo likamfanya umakini uongezeke. Safari hii bastola aliishikiria mkononi. Akasogea mpaka kwenye ukuta wa Jengo lile. Akauangia ukuta ule kama atauweza. Baada ya kujiridhisha sasa alikuwa akiuparamia ukuta mfano wa nyani, muda mfupi akaangukiwa ndani pasipokutoa sauti. Baada ya kuanguka pale alijiinua haraka mpaka upande mwingine. Wakati akitembea alijikuta akijikwaa kwenye ndoo za bati. Ukelele ukatokea. Hilo likamuongoza masimba mpaka chini ya mti. Akajibanza hapo kuona kama kelele zile zingemleta mtu pale. Ni kweli hakuwa mbali na mawazo yake. Punde akawaona watu watatu wenye silaha wakitokea pande tofauti. Kila mmoja alikuwa akitokea upande wake. Katika kitu ambacho hakukitarajia ni kuwaona walinzi hao. Kwa mara ya kwanza Hili likamshangaza. Mwamvita kulindwa na watu wenye silaha nzito. Hata alipowaangalia watu hawa kwa uzuri aliwatambua kwa karibu. Kuwatambua huko kulampa picha ya kinachoendelea. Walinzi waliokuwepo pale walikuwa walinzi wanaomlinda Chief. Hilo lilimaanisha chief alikuwa hapo ndani. Hilo likamuongezea umakini. Wazo kuwa Chief alikuwa upande huu lilikigonga kichwa chake. Lakini akalitupilia mbali baada ya kuwaona watu wawili wakiufungua mlango na kuchungulia Alikuwa Chief akiwa sambamba na Mwamvita. Chief alikuwa kwenye Bajama huku Mwamvita akiwa kwenye mtandio mwepesi uliofungwa kihasarahasara. Bado macho ya masimba hayakutulia. Yalicheza na walinzi wote na hata wakati mwingine yakiwaangalia chief na mwamvita. Mpango wa kumuua mwamvita ulikuwa umekuwa mgumu kutokana na uwepo wa Chief. Akaaona haukuwa muda muafaka kwa siku ile. Hakutaka kumfanya chief aelewe kinachoendelea. Aliamua kuighairisha hukumu ya mwamvita akiipanga kufanyika siku inayofuata. Baada ya walinzi wale kuangalia na kutokuona kitu, wakaturudi kila mmoja katika nafasi yake. Ni muda huo masimba alipochupa na kutua nje kisha kutokomea gizani.

*****

Alimbeba France mikononi akiondoka katika nyumba ile ya siri. Ulikuwa usiku wa saa saba Teddy alipoamua kuondoka katika Jiji la dar es salaam akielekea arusha kabla ya kuvuka mpaka na mkuingia kenya. Alitembea usiku ule kuogopa kugundulika mpaka alipofika maeneo ya barabarani. Akasimamisha pikipiki na kujipakia kisha safari ya kibamba. Alitaka kwenda kulala chalinze iwe rahisi kuondoka pasipokujulikana. Hakujali kazini kwani aliomba likizo ya miezi miwili akisingizia kwenda kukaa matanga kwenye msiba wa mama mzazi wa mpenzi wake. Baada ya dakika kumi na tano alikuwa kibamba. Akashuka na kumlipa dereva wa pikipiki kabla ya kusogea mbele kidogo sehemu ambayo ilipaki gari aina ya Noah. Baada ya kuifikia ile gari mlango ukafunguliwa. Akampakia France kisha yeye na baada ya hapo gari ikang'oa na kuianza safari. Safari ya kuuhama mji kwa muda. Alijua hasira za masimba zingeisha mwilini mwake. Moyo wake ulikuwa ukivuja kwa maumivu. Machozi yalikuwa bado yakishuka. Hakujua mwisho kama ingekuwa vile. Tamaa ya pesa imeondoa utu wake. Sasa alikuwa akiukimbia mji alioupenda. Akimuacha mpenzi kwasababu ya tamaa. Hakutegemea hilo kabisa kichwani kwake.

*********

Ni asubuhi tulivu na yenye mawingu ya hapa na pale. Masimba alikuwa ametulia mahali akiitizama barabara na watu wake. Alikuwa hapo baada ya kuhaha usiku mzima akimtafuta Teddy pasipokumuona. Alikuwa hapo akiituliza akili yake akiwaza wapi ambapo teddy alikuwa amekwenda. Alijaribu kuwasiliana na Dee plus kumuuliza kama alikuwa na fununu kuhusu teddy na hata mtoto, lakini jibu alilopewa halikumridhisha. Kwamba teddy hakuonekana tokea mchana wa jana. Hilo likampa shaka kuhusu mwanawe france. Hakujua wapi teddy alikuwa amempeleka. Hilo likaendelea kumuumiza kichwa. Alichokifanya ni kuondoka pale na kuingia mtaani kunusa kama atapata chochote. Cha kwanza alichoamua ni kuelekea kijitonyama kuonana na Chief. Aliamua kufanya hivyo ili kujua alipo mwanawe na kuhusu kuweka angalizo katika watu kujua kuhusu mwanawe. Kuhusu france aliamua kumsaka kimya kimya. Aliwasili kijitonyama pale na kulakiwa kwa mshangao na baadhi ya wanausalama waliomtizama. Kila mmoja alikuwa na taarifa ya kuuawa kwa mama yake mzazi. Kwa nini yuko hapa? Yalikuwa maswali bila majibu. Salaam na pile zikachukua sehemu yake. Akawajibu kwa kichwa kisha kuingia ndani. Baada ya hapo akaongoza mpaka ofisini kwa Chief. Hapo akakutana na pole nyingine kutoka kwa sekretari wa Chief.

"Pole Masimba! !!...

"Nitapoa pale waliomuua mama yangu nitakapo tumbukuza risasi zangu kwenye vichwa vyao." alijibu masimba alimuacha Dada yule akishangaa.

"Mzee yupo ama katoka? Akauliza masimba. Kabla yule dada hajajibu mlango wa ofisi ya Chief Ukafunguliwa. Akatoka Mwamvita na Jimmy. Macho yao yakakutana na macho ya Masimba. MSHTUKO alioupata Mwamvita Ulishuhudiwa na kila mmoja pale. Chief ndiye aliyepigwa zaidi na butwaa. Macho ya Masimba yalikuwa yakimtizama Mwamvita. Alitamani kumuua mbele ya watu. Alitamani kumtafuna mbichi. Mikono yake ilikuwa ikitetemeka kwa hasira. Hilo Chief alilishuhudia hakuwahi kumuona kijana wake akiwa vile. Alihisi lolote litatokea, ni kweli mkono wa masimba ulikuwa ukishuka mahali alipohifadhi bastola yake. Tukio la kuuawa kwa mama yake likajirudia tena na tena kichwani kwake. Lakini chief alimuwahi na kumshika mkono akimtaka waingie ndani ya ofisi.
 
NITAKUPATA TU

SEHEMU YA 041

Chief hakukitegemea kile kilichotokea pale. Mshtuko wa mwamvita na mikono ya masimba kutetemeka kisha kushuka chini ilikuchomoa bastola, vilikuwa vitu vilivyomchanga. Yeye ni jasusi mwandamizi. Kilichotokea pale alihisi uwepo wa kitu kikubwa nyuma yao. Akamuangalia Masimba kwa makini sana. Alimuangalia akimsoma uso wake. Alichokutana nacho kikaitengeneza hofu, hofu ambayo hakujua ilipotoka. Ni vipi amuogope na kumjengea hofu kijana wake. Hilo likampa ujasiri wa kutaka kumuuliza Masimba. Wakati akitaka kuuliza, masimba akainua uso wake na kumtizama Chief. "machozi" ya machozi yalikuwa machoni kwa masimba yakishuka taratibu mashavuni. Chief akaendelea kupigwa butwaa. Masimba alikuwa akilia? Masimba anadondosha machozi? Ni kutokana na kifo cha mama yake au nikule kukutana kwao na Mwamvita? Kabla ya kupata majibu ya maswali yake. Masimba akainuka na kutoka ofisini huku nyuma akiubamiza mlango wa ofisi ya chifu kwa nguvu. Hata hili likikuwa Jipya kabisa kwake. Akauona uhasama kati ya Masimba na Mwamvita. Hilo likamfanya ahisi kuwa mwamvita na masimba wanajuana ama mwamvita anahusika na kifo cha mama wa Masimba. Akatamani kuuliza, alitamani kupata majibu kutoka kwa watu hawa wawili. Lakini sana sana kutoka kwa masimba ambaye alikuwa ni kijana wake. Hata yeye alianza kuhisi kitu kwenye kukutana kwake na Mwamvita kabla hawajawa wapenzi. Alijua ulikuwa mkutanishano wa kimipango. Ulikuwa ni mpango uliosukwa. Wazo hilo likamfanya atamani kuchukua simu yake ili kumpigia Mwamvita, lakini kabla hajafanya hivyo mlango ukafunguliwa.. akamuona Masimba akirudi mle ndani. Akamuangalia mkuu wake kwa muda kisha kwa sauti yenye Hasira akanena. "Ningejua Jana ningewaua pale mbezi. Nilikuwa na uwezo wa kuwaua wote kwa Risasi, lakini nilighairisha kutokana na uwepo wako. Watu waliotoka humu ndani ni wahusika katika mauaji ya waziri mkuu. Na hata mama yangu ameuawa kwa sababu ya hili suala. Wameuchukua uhai wa mama yangu kwa sababu ya hili suala. Nakamilisha ushahidi ili nimlete Jimmy hapa. Cha ajabu hata idara yetu inamtafuta lakini leo unamleta. Sasa sikia leo nakuletea kichwa cha Mpenzi wako mwamvita. Nitamuua kwa mkono wangu. Yeye ndiye aliyemshuti mama yangu mbele ya macho yangu. Nitamuuua. Hili nakwambia wewe na ukimwambia na kusababisha apotee nitakuua wewe. Nitakuua Chief Kama nilivyomuua Waziri mkuu kutoka na ujinga aliokuea akiufanya. Nimekwambia ili ujue kuwa sishindwi chochote." Aliongea masimba huku akilia. Aliondoka ndani ya ofisi akiwamuacha Chief katika mshangao. Mdomo uko wazi mshangao ukitawala usoni kwake. Kwamba Masimba ndio kamuua waziri, kwamba waziri alikuwa akifanya upuuzi, ni kweli ndio amefanya. Kwamba Mwamvita ndiye amemuua mama wa masimba mbele ya masimba? Lina ukweli kiasi gani hili? Jimmy anahusika na kifo cha waziri? Kwamba Masimba Jana Aliingia nyumbani kwa mwamvita? Yamekuwaje Haya? Masimba amechanganyikiwa? Yalikuwa maswali lukuki kichwani mwake. Katika maswali hayo kile cha mwisho ndicho kilichomtisha. Aliwalea vijana wake lakini kuna kipindi walimtia hofu.

Akainua simu na kupiga sehemu tatu tofauti. Baada ya hapo akatulia. Hazikupita dakika tano mlango ukafunguliwa. Aliyeingia ndani alikuwa mwanamke. Tena mwanamke ambaye hakuwahi kumjua. Huyu alikuwa amevalia buibui liliuficha mpaka uso wake. Mkonono alionyesha kushika kitu mfano wa CD. Chief akamuangalia mtu huyu kwa muda bila kuongea na mgeni wake. Mgeni huyu aliyemvamia ofisini kwake pasipo na taarifa. "Chukua hii cd.. kuna vingi vitakusaidia ikiwa ni pamoja na kumjua aliyemuua waziri mkuu." Aliongea mwanadada yule akiunyoosha mkono wake kumpa chief ile CD. Chief akamuangalia yule mwanamke kabla ya kuipokea CD na kuiweka kwenye Droo. Alikuwa katika kipindi kigumu sana. Imekuaje mtu huyu amepata ruhusa ya kuingia humu bila kuzuiwa.

*****

Wakati mwanamke yule mwenye baibui akiingia ofisini kwa mkurugenzi, masimba alikuwa amekaa ndani ya jengo lile Akitizama mlango wa ofisi ya Chief. Uingiaji wa mwanamke yule ulimtia wasiwasi kutokana vazi lake. Mwanzo alidhani labda ni kachero wa hapo, lakini alipotoka mara hii mawazo akayaondoa baada ya kuuona wasiwasi machoni kwa mgeni huyu wa Chief. Akamuacha amtangulie kwa mbele kisha yeye kufuata nyuma. Mtu yule alikuwa akitembea akigeuka kila wakati hofu yake akiona kama anatafutwa. Masimba bado alikuwa akimuangalia kwa umbali wa hatua kama Hamsini. Wakati mtu yule akiuendea mlango wa mwisho kabla hajalifikia geti, masimba alishapita kwa njia nyingine na kutokea sehemu tofauti kabisa na Eneo lile. Akatulia katikati ya watu wakiongea huku macho yake akitizima pale pale kwenye mlango. Alikuwa amemlia mashaka mwanamke yule. Alitambua alikuwa ametoka mahala na alikuja pale ofisini kwa Chief kuleta kitu fulani. Mashaka hayo yalitokana na mwanamke yule kuonekana ni mwenye wasiwasi wakati wa kuingia na hata kutoka. Muda mfupi akamuona yule mwanadada akitoka pake nje, akaanga angaza huku na huko. Baada ya muda akaonekana ikisimamisha tax kisha kuondoka eneo lile. Masimba akaendelea kutulia. Alijua na kuhisi kuwa mwanamke yule hakuwa peke yake. Alijua lazima kuna watu mahali fulani wakitimzama na kumfuatilia kwa kila kitu anachofanya. Aliendele kutulia akiangalia hilo. Ni kweli alichokuwa akikiwaza kwani baada ya dakika mbili kupita tokea mwanamama yule aondoke, akawaona watu watatu wakiondoka kutokana katika sehemu fulani na kuongoza wakitembea kama watu ambao hawakuwa wakijuana. Aliwaangalia watu wale akiwa bado amekaa hap0. Alikuwa amehisi uwepo wa mtu ama watu wengine eneo hilo. Ni kweli kama mwanzo wanaume wawili wengine wakasimama na kuanza kuondoka lakini hawa wakienda uelekeo tofauti na watu waliowatangulia. Hilo sasa likampa uhakika kwamba kina Jimmy ni wengi, licha ya wingi huo lakini aliamini Siku ilikuwa siku ya mwisho yaMwamvita kuivuta hewa ya mwenyezi Mungu. Alipohakikisha hapakuwa na watu wengine wakuwatilia shaka, masimba aliinuka na kusogea barabarani nia ikiwa ni kuisubiria tax iliyoondoka na yule mwanamke. Alisubiri kwa dakika kumi nzima lakini hakuiona ile tax ikirudi. Hilo likampa wasiwasi kuwa huwenda dereva yule ameshauawa mpaka wakati huo. Wakati akiliwaza hilo akaiona ile tax ikitokea kwa mbali. Kwa kuwa alikuwa amekalili namba za gari haikuwa shida. Alisimama barabarani na kupunga mkono. Baada ya hapo tax ikasimama. Masimba akaisogelea na kuufungua mlango wa nyuma. "Nipeleke ulipompeleka yule mwanamke. " aliongea masimba bila kuongeza neno lolote. Dereva akitii akawasha gari na safari ikaanza. Kila mmoja alikuwa kimya, dereva akiwaza pesa masimba alikuwa akiwaza kuhusu mwanamke aliyeingia na kutoka Ofisini kwa Chief. Kitu kwamba Chief amepelekewa kitu na kupewa shinikizo ni kitu pekee ambacho kiligonga kichwa chake. Hakuwahi kumuona wala kumjua mwanamke yule. Hilo likampa uhakika kuwa Jimmy alikuwa ameongeza watu wakumsaidia. Wakati wamefika Sinza kumekucha Masimba akamuona mwanamke akitembea pembezoni mwa barabara. Huyu alivaa suruali ya Jeans na Tishirt yake nyeupe. Chini alikuwa amevalia raba nyeupe sambamba na miwani ya juu ilionekana kwa watu wengine lakini kwa Masimba ikionekana ni miwani maalum inayovaliwa na majasusi. Licha ya mwanamke huyu kujibadilisha kimavazi lakini hakuweza kumpoteza masimba. Alikuwa ni mwanamke aliyetoka ofisini kwa chief muda mfupi uliopita. Akamwambia dereva yule wa Tax aisimamishe gari pembeni mwa kituo fulani cha tax. Dereva akatii kwa kusimamisha gari. Masimba akalipa kisha kushuka bila kuongea kitu. Muda wote macho yake yalikuwa kule kwa yule mwanamke. Alitembea kwa umakini akikwepa kuonekana. Safari ya mwanamke yule ikaishia kwenye saloon moja ya kike pale pale kumekucha. Masimba akatulia pembeni umbali wa hatua mia akiangalia kule kwenye saloon ile ya kike. Akasubiri kwa dakika kumi nzima lakini hakumuona mwanamke yule akitoka. Hilo likampa wasiwasi mkubwa sana, muda mfupi alikuwa akimuita kijana mmoja ambaye alikuwa anapiga Debe pale kituoni.

"Mambo vipi mzee!!? Akasalimu masimba baada ya kumuita mpiga debe.

"Fresh mkuu, nipe dili mwana." Akajibu mpiga debe yule.

"Kuna kitu nataka nikuulize lakini kabla sijakuuliza kamata hii."alisema masimba huku akumkabizi kijana yule noti ya Elfu kumi. Kijana yule akaipokea huku akimuangalia Masimba usoni.

"Duh respect mwana niulize tu nitakujibu kama nitakuwa najua chochote. Aliongea yule mpiga debe akionyesha kutabasamu kwa noti ile.

"Nahitaji kuhusu ile saloon pale. Akaongeza masimba huku akimuonyeshea kidole kuelekea ilipo saloon.

"Wewe ni Njagu au ni mwana usalama?" Akauliza yule teja huku akionyesha hofu kwa mbali. Hilo likamvutia Masimba. Akakiona kitu cha kufanya.

"Hapana mimi sio njagu wala Usalama wa Taifa. Mimi ni mtu wa kawaida. Nimekuja hapa na dada mmoja muda mfupi uliopita. Ameingia pale ndani lakini mpaka sasa simuoni akitoka." Alijieleza masimba akimtoa hofu. "Ooh wewe ndio umekuja na Dada V...? Aaah kwani hujui kinachoendelea mle ndani? Pale ni saloon kwa nje lakini palepale kuna mlango wa kutokea nyuma anbapo hapo kuna vigogo wengi wa serikali. Akajibu teja.

"Wanafanya nini Hao Vigogo? Au kuna danguro? Akauliza Masimba akijifanya hajui chochote kinachoendelea.

"Wewe kweli mgen.... akakatisha maongezi baada ya kumuona mwanamke mmoja akitoka. Hilo likamvutia Masimba kutizama kule. Macho yake yakavutiwa na mwanamke aliyetoka mle ndani. Hakuvutiwa kimapenzi bali alivutiwa kwa kuwa alikuwa ni mwanamke yule yule aliyeingia muda mfupi uliopita. Alionekana akuangaza huku na huko kama ni mwenyekutafutq kitu, punde akarudi tena ndani. Haikupita hata dakika, akawaona vijana wengine watatu tena wa kiume wakitoka. Hawa walionekana ni kama wale wakongo wanaokaa kwenye masaloon hapa mjini. Lakini muonekano wao haukufanana na watu hao. Masimba akaiona hatari ya kuendelea kuwa pale. Akamuomba Yule mpiga debe amuelekeze anapoishi ili aweze kurudi usiku kuongea naye chochote. Mpiga debe yule alimtajia Masimba mtaa na sehemu anayoishi. Baada ya hapo akatoa Noti mbili za elfu kumi kumi na kumpa huku akimuachia onyo la kutokumwambia yoyote kile walichoongea. Baada ya hapo Masimba akaondoka pale kurudi anapoishi kwa maandalizi ya kurudi usiku kwa maswali zaidi pia na kazi zaidi.

TUONANE JIONI
 
Dah masimba maliza wote alaf tutaisuka upya idara ya TISS na ww utakua chief wa TISS
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom