NITAKUPATA TU
SEHEMU YA 038
Mtunzi: Ibrahim Masimba
Whatsap: 0675191162
ILIPOISHIA
Tunaomba mzigo wetu la sivyo utakuta maiti za wanao pamoja na mama yako mzazi.
ENDELEA NAYO.
Kwa muda masimba akapigwa na bumbuwazi, butwaa la kutokuamini alichokisikia. Simu ilishakatwa na haikuwa ikipatikana tena. Mama yake na watoto wake Yaseer na France walikuwa chini ya himaya ya watu asio wajua. Hasira zikaendelea kuchemka ndani kwa ndani. Aliwapenda sana wanawe na hata mama yake. Hakupenda waguswe na kubughuziwa na mtu yoyote. Lakini leo kuna watu ambao wamekwenda kuugusa moyo wake na roho yake. Walikwenda kumtingisha na kumtia hofu. Walikwenda kuonyesha kuutaka mzigo kwa njia nyingine. Ni nani hawa wanacheza na watoto wangu? Ni nani hawa wanacheza na mama yangu? Yalikuwa mawazo yaliyomuondoa pale ndani. Alitaka kuondoka katika muda ule kuelekea kwao Handeni. Alitaka kuwahi kukabiliana na watu hawa. Mzigo ni wa nini kwangu? Watu wangu wanathamani kuliko hata huu mzigo. Wakati anaukaribia mlango wa kutokea akaisikia sauti ya Dee plus ikimuita. Hapo ndipo alipogutuka na kugundua kuwa Dee plus alikuwa pale ndani tena akiwa na mwanamke aliyeliwana damu. Akageuka na kumtizama Dee plus, macho yao yakaongea kwa sekunde mbili, sekunde ya tatu masimba alikuwa akiufungua mlango akiondoka pale kwa safari ya Tanga. Safari ya kuupeleka mzigo sababu ya kuwaokoa watu wake. Alitembea hasira ikichemka, alitembea kana kwamba ni kichaa. Bastola mbili zikiwa mwilini katika sehemu tofauti. Alikuwa ameingiq vitani rasmi, alikuwa ameingia kwenye mapambano. Teddy, mwamvita, suresh na jimmy ilikuwa ni lazima wafe. Ilikuwa ni lazima waondoke. Muda mfupi alikuwa sehemu moja katika nyumba yake ya Siri maeneo ya kijitonyama. Alikuwa ndani ya chumba akiuchukua ule mzigo tayari kwa kuupeleka sehemu husika. Alikuwa tayari kufanya kila kitu kwa sababu ya watoto na mama yake. Baada ya kuweka kila kitu katika hali nzuri, safari ya kuelekea Handeni ikaanza. Alikuwa katika kiwango kikubwa cha hasira, alimtoa teddy moyoni na hata rohoni. Alikuwa tayari kumuua kwa mikono yake mwenyewe. Alikuwa tayari kuufumua ubongo wa mwanamke huyu mpuuzi. Alitambua ni yeye ambaye alikuwa nyuma ya hili suala la kushikiliwa mateka kwa wazazi wake. Hakutaka kumwambia mtu yoyote zaidi ya Dee plus. Hata Chief hakutaka kumwambia kwa kuwa anaweza kuongea na wasaidizi wake wakaivujisha. Alitaka kupambana mwenyewe, alitaka hili suala liishe mikononi mwake. Suala la kifo cha waziri mkuu akaliweka pembeni kwanza. Mawazo yalikuwa kwa watoto wake na bibi yao. Wakati akipita kwenye daraja la wami akaliona gari likimpita kwa kasi sana. Mwendo wa gari lile ulimshangaza sana lakini kwa kuwa halikumhudu akaamua kuachana na mawazo kuhusu hilo. Akaendelea kuendesha gari kwa mwendo wa wastani. Wakati anafika mkata ili aingie kwenye barabara iendayo Handeni, mlio wa sms ukaingia kwenye simu yake. Akaitoa simu mfukoni, akakutana na Jina la My love juu ya kioo cha simu. Sms kutoka kwa Teddy hiyo ilimshtua. Akaufungua ujumbe ule huku moyo wake ukiwa na wasiwasi mkubwa. "Najua ushajua mpaka sasa mimi ni nani. Naomba upeleke mzigo ukiwa pekee yako, ujanja wowote utakaoufanya utakuja kuokota maiti za hawa vifaranga vyako." Ulisomeka ujumbe ule. Akaurudia kuusoma tena na tena. Hakutaka kuamini kama ulikuwa ukitoka kwa teddy mwanamke aliyekuwa akiimba mapenzi kila siku. Mwanamke aliyekuwa akimwambia Nakupenda kila siku. Akaurudia tena na Tena ulitumwa kweli na Teddy. "Nitakupata tu na Nitakuua kwa mkono wangu." Akajisemea mwenyewe huku akiirudisha simu mfukoni. Teddy alikuwa ameonyesha yeye ni nani katika hili. Aliamua kujiweka wazi. Akaipita mazingara na kuitafuta SUA. Gari ikatembea na kutembea katika mwendo wa kawaida.
******
Mji wa Vibaoni ulikuwa umepoa kwa ukimya, wakazi karibia wote walikuwa wamelala huku mbwa tu wakisikika wakibweka. Alitembea kwa miguu baada ya kuiacha gari sehemu ya mbali kidogo. Alitembea usiku ule akiwa na mavazi maalum ya kutembelea usiku. Kutoka kijiji cha kwambwembwele alipoiacha gari, akapitia barabara iendayo arusha eneo maarufu liitwalo kwa kadenge. Akatembea usiku ule pasipokukutana na kitu chochote mpaka alipotokea maeneo ya Shule ya Msingi mlimani (zamani alijulikana kama vibaoni) baada ya kufika hapo akatulia kwanza akiangalia nyumba yao. Macho yake yakawaona watu wawili ambao walikuwa wamesimama Nje ya nyumba yao. Aliendelea kuangalia mara akauona mwanga wa taa za gari ukisogea taratibu. Masimba akaendelea kidogo akitizama kwa makini. Akamuona mtu mwingine akitokea nyuma ya nyumba ya mzee Mauya. Baba mzazi wa Rukia Mauya. Baada ya kutoka mtu yule akaonekana akiisogelea gari ambayo ilikuwa tayari imesimama karibu na nyumba yao. Akaondoka pale na kupitia nyuma nyuma mpaka pembeni mwa uwanja wa shule ya msingi. Wakati huo watu wale bado walikuwa wamesimama huku mmoja wao akiongea na simu. Punde akauona mlango wa gari ile ukifunguliwa, wakashuka watu wawili ambao aliwatambua kwa haraka. Alikuwa mwamvita na Ben. Hata alipoiangalia gari ile vizuri aliitambua kuwa ni ile gari iliyompita kule wami. Baada ya watu wale kushuka akawaona wakiingia ndani ya nyumba yao kisha wakatoka wakiwa wanawasukuma watoto wake na mama yake. Wakati hilo likifanyika mlango mwingine wa gari ile ukafunguliwa. Safari hii alishuka teddy mkononi akiwa ameshikilia bastola. Kwa kuwa watoto na hata mama wa masimba walikuwa wakimjua,wakamkimbilia na kutaka kumkunbatia. Haikuwa hivyo, haikuwa hivyo kwa kuwa Teddy hakulitaka hilo. Akashudia wanawe wakipaa angani baada kupokea mapigo kutoka kwa teddy. Hakuvumilia hilo, muda huo huo alikuwa amechupa hewani na kuwadaka watoto wake kabla ya kufika chini. Akatua nao chini katikati ya watu wale huku mdomo wa bastola ukiwa kichwani kwa Teddy. Kilikuwa kitendo ambacho hakikutarajiwa na watu wale, kitendo ambacho kiliwaacha kwenye hamaniko. Wakati hilo likiendelea mama yake masimba akachoropoka na kutaka kukimbilia pale alipokuwa mwanawe. Hakumfikia wala kusogea.. Bastola ya Mwamvita Ikakohoa na wakati ule ule Masimba akamshuhudia mama yake akipaa juu na kuanguka chini. Damu zilikuwa zikivuja kifuani. Masimba hakuamini hilo, hakuamini kama chini pale amelala mama yake. Akakurupuka kukimbilia ulipolala mwili wa mama yake mzazi. Wakati huo huo wanakujiji nao walikuwa wakiinuka kutokana na kuusikia mlio wa bunduki. Baada ya kuona watu wameanza kuamka majumbani mwao, wakambeba mtoto mmoja na kuingia naye kwenye gari kisha kui0ndosha gari kwa mwendo wa kasi wakimuacha masimba akilia juu ya mwili wa mama yake.
Alikuwa haamini kama mama yake ndiyo yule aliyekuwa amelala pale chini damu ikivuja kama maji. "Mnala inuka chilonge. Usekunasa mnala wezi ukuluwo na walonge na yuhi? Inuka mnala." ( inuka mama tuongee, usiniache mama, wajukuu zako wataongea na nani? Inuka mama) alilalamika masimba huku akimtingisha mama yake. Lakini haikusaidia kitu, mama yake hakuwa na kauli tena. Alikuwa katika hatua za mwisho za uhai wake. Pale pale akashuhudia mama yake akikata kauli na kugeuza shingo. Muda mfupi akaacha kupumua. Mama yake alikuwa amekufa mikononi mwake. Mama yake alikuwa amekufa kwa ajili yake. Mwamvita alikuwa amemuua mama yake. Akashindwa kuongea kwa muda. Mama yake alikuwa amenyamaza kimya. Akainuka na kusimama pembeni akiuangalia mwili wa mama yake. Lakini alipoangalia pembeni hata mwanawe Yaseer alikuwa ameanguka akitokwa na damu puani, mdomoni na masikioni. Alikuwa amepoteza fahamu. Muda ule ule difenda ya polisi yenye askari kumi wenye silaha nzito ikawasili. Wakashuka na kuanza kupiga picha za tukio lile. Muda ule ule gari aina ya wagonjwa ikafika na kumchukua yaseer. Kila kitu kilitokea kwenye kipindi kifupi sana. Muda ambao ulibadilisha maisha ya masimba. Hakujua kama mwanawe atapona kutokana na pigo la Tedd na pia hata france naye hakujua kama atakuwa salama. Watu walikuwa wengi wameuzunguka mwili wa mama wa masimba. Mama ambaye alikuwa ni maarufu sana pale vibaoni na Handeni yote kwa ujumla. Vilio vikatawala huku watoto wa kike wa marehemu wa kipoteza fahamu kwa taarifa hiyo. Muda wote Masimba hakuwa akiongea taswira ya mwamvita akimshuti mama yake ilikuwa ikijirudia. Matundu matano ya risasi kifuani yaliuondoa uhai wa mama yake. Akaitamani iwe ndoto, aliitamani iwe kama hadithi ya kusadikika. Lakini mwamvita aliutoa uhai wa mama yake. Mbele ya macho yake ulilala mwili wa mwanamke mwenye thamani kuliko mwanamke yoyote duniani. Akainuka akipiga hatua kwa mara nyingine akielekea ulipolala mwili wa mama yake. Hakuufikia kama mwanzo, kizunguzungu kikali kikamfanya aanguke chini, macho yakaingiwa na Giza na hakuona kilichoendelea.
******
Alijifungia chumbani akilia kwa uchungu. Pembeni aliuweka mzinga wa pombe kali. Macho yake yalikuwa yamevimba kwa kilio na majuto. Mbele kidogo kwenye kitanda kidogo alikuwa amelala france mtoto wa masimba akitibiwa na Daktari binafsi. Taswira yake ikalikumbuka tukio la mwamvita kuruhusu risasi kumuua mama wa masimba. Akakumbuka kumuona mama yule akiinguka. Chozi likashuka na kushuka Zaidi. "Hukustahili Kufa mama yangu. Umenitendea mema sana tokea nilipokujua . Nisamehe mama yangu ni samehe kwa ujinga wangu. Aliongea Teddy akilia. Kichwani akavuta taswira ni hali gani alionayo masimba kwa muda ule. Akainuka na kutoka nje ya kile chumba. Safari yake ikaishia chumba kingine mle ndani. Akaichomoa bastola yake na kuinyanyua juu mdomo wa bastola ukagusa kichwani mwake. Teddy alitaka kujiua. Hakuweza kulivumilia lile. Kidole kikashuka mpaka kwenye kitufe cha kufyatulia risasi.
KESHO