Riwaya: Nitakupata tu

Riwaya: Nitakupata tu

NITAKUPATA TU

SEHEMU YA 034

******
CHIEF ndio jina lililosomeka juu ya kioo cha simu yake. Hakuipokea kwa wakati ule. Macho yake yaliwatizama wenzake kisha kuitizama tena simu. Sio kwamba alikuwa akiogopa kuipokea simu bali hakuwa na la kumwambia mkuu wake. Akaiacha simu iendelee kuita mpaka ilipokata. Baada ya simu kukatika, kachero yule akauandika ujumbe kwa lugha ya mafumbo na kuutuma kwa Chief. Baada ya kumaliza hilo akamgeukia dereva wa tax. "Utaendelea kuishi hapa kwa Usalama wako mpaka pale hili jambo litakapokwisha." Baada ya kusema hilo makachero wale wakatoka mle ndani tayari kwa safari ya kwenda kuwatafuta Jimmy na Suresh.

*****

Ilikuwa yapata majira ya saa tatu na nusu usiku pale teddy aliposhuka kwenye bajaj pembezoni mwa ufukwe maarufu jijini dar es salaam, ufukwe wa coco beach. Baada ya kushuka hapo akaongoza taratibu mpaka sehemu mmoja iliyojitenga pekee akakaa na kutulia. Hakuwa hapo kwa sababu ya burudani bali alikuwa pale kwa minajili ya kuipa akili yake utulivu. Mambo yaliokuwa yakiendelea yalizidi kumchanganya na kuifanya akili yake ishindwe kufanya maamuzi. Ni mara tatu amenusurika kufa kwa kupigwa risasi, mara ya nne amenusurika kufa baada ya kugeukwa na wenzake kisha kumpoteza fahamu. Mpaka muda ule hakuwa akijua ni vipi ameokolewa katika kisanga kile. Hakujua ni vipi masimba amemtoa katika kifo ambacho kilipangwa kufanywa juu yake. Ni masimba huyu huyu alijitolea kila kitu na uwezo wake kuhakikisha yeye anarudi kwenye uhai. Hakumuacha pale alipowekwa matatani. Hata pale aliposhiriki kuua familia ya Asteria, bado masimba alimpa nafasi ya kubadilika. Licha ya hayo yote bado moyo wake ulikuwa katika mtihani mzito. Aliihitaji pesa na aliuhitaji mzigo wa madawa ya kulevya alionao Masimba. Aliutaka kwa njia yoyote. Hakuhitaji mzigo ule uingie mikononi mwa serikali. Aliutaka na aliuhitaji. Licha ya kuuhitaji huko, lakini hakujua angeweza kuutoaje mikononi mwa mwanaume yule. Hilo ndio lililomfanya afike usiku ule katika fukwe zile za coco beach kujaribu kuwaza hili na lile ili kupata majibu. Kichwa chake alikiinamisha chini huku mikono yake ikiuchezea mchanga. Mawazo yalikuwa yakipishana kichwani. Kuna kipindi katika akili yake alikuwa anawaza na kujilaumu kwa nini akutane na Masimba. Pesa zikaiteka akili yake, pesa zilimfanya aisahau nafasi ya masimba moyoni mwake. Aliihitaji pesa na aliuhitaji mzigo kwa gharama yoyote. Kwa mara ya kwanza akalikumbuka jina la mtu, mtu ambaye angeweza kupanga naye na kupata majibu. Lakini hakujua angewezaje kumpata huyu mtu. Kwani ulipita muda mrefu sana pasipokuonana. Akaichomoa simu yake mfukoni na kubonyeza namba fulani. Baadae simu upande wa pili ikasikika ikiita. Sekunde tatu baadae sauti nzito ikasikika upande wa pili. " Beni Bomphe naonge."

"Teddy killer hapa naongea, nakuhitaji kwenye fukwe za coco beach muda huu kama upo hapa Mjini." Akaingea teddy kisha kukata simu bila kusubiri jibu kutoka upande wa pili. Uso wake ulikuwa kwenye tabasamu matata sana, sasa uhakika wa kuupata mzigo alikuwa nao. Akaendelea kuwaza na kuwazua, baada ya dakika kumi na tano akamuona mtu akitembea taratibu katika fukwe zile. Kijana mweupe mwenye mwili uliojengeka kimazoezi alikuwa akiangaza huku na huko kama mwenye kutafuta mtu. Teddy akainuka na kumsogelea kijana yule. Muda mfupi baadae walikuwa wamesimama wakitizamana. "Habari za masiku Beni?" Akasabahi teddy.

"Nzuri mkuu, naona nchi imetingishwa." Akajibu beni huku akiongeza na maneno kadhaa. "Yeah! Ukiwa mshenzi lazima upate malipo ya kishenzi. Akajibu teddy huku uso wake ukionyesha kujua kila kitu.

"Usiniambie unamjua alietenda hili? Akaongeza ben huku akishindwa kuuficha mshangao.

"Yeah! Namjua! Alijibu kwa kifupi kisha akamuomba Ben waongee kile ambacho amemuitia.

Kwa shingo upande ben akakubali na kufuatana na teddy mpaka sehemu waliokuwa wamekaa mwanzo. "Nipe dili mama nitoweke hapa, watu kama sisi hatuonekani ovyo." Ben akatamka akimuangalia teddy. Teddy akamueleza ben kila kitu huku akificha vichache sana. Ni maelezo ambayo yalichukua dakika kama sita hivi. Baada ya maelezo yote kutoka kwa teddy, beni akatulia huku akimuangalia Ted usoni. Baadhi ya maneno kutoka kwa teddy hayakumuingia akilini. Aliujua uhusiano wao na masimba tokea ndio kwanza wanajiunga na idara ya ujasusi. Lakini haya ambayo yanatoka kinywani kwa teddy yalimuacha na kigugumizi. "Lazima tumuondoe masimba? Hata ikibidi hata familia yake tuitumie katika kuupata huu mzigo? Ni baadhi ya kauli ambazo zilimuacha Ben akiwaza.

"Kwahiyo unataka masimba asafirishwe? Hatimaye akauliza tena.

"Yeah nahitaji kuupata mzigo, kwahiyo ni lazima tumsafirishe. Pakitokea ugumu familia yake itahusika katika kutupa huu mzigo. Sina huruma wala mapenzi katika hili." Akajibu teddy huku kila kitu kikionyesha kuwa hakuwa akitania. Hilo pia halikutegemewa na ben. Lakini kwa kuwa aliitaka pesa Aliamua kukubaliana na teddy kuifanya kazi ile ambayo ilikuwa hatari. Alimjua masimba na aliujua ugumu wake. Kitendo tu cha kusikia kile alichokifanya kwa waziri mkuu ilimthibitishia ni kiasi gani ameingia kwenye vita nzito. Akamuangalia teddy kwa sekunde kadhaa kisha kwa sauti ya kujiamini akasema. "Nitaifanya hii kazi kwa moyo wangu wote. Ikiwa nitamuua masimba ama familia yake, basi damu yao itakuwa juu yako. Ikiwa ataniwahi mimi basi nadhani damu yangu pia itakuwa juu yako." Baada ya kuongea hilo akainuka na kuanza kuondoka huku hofu ikiwa imeutanda moyo wake. Hakupenda kupambana na mtu kama masimba, sio kwa kuogopa lakini alikuwa akimheshimu kama mtu aliyemfanikishia naye kufika pale.

*******

Alikuwa mfano wa simba aliyejeruhiwa, hakutaka kuwapa nafasi maafisa usalama kumtambua kama yeye ndiye aliyehusika na mauaji ya Waziri mkuu. Hilo likimlazimu masimba kutokulala kabisa kabisa akiwasaka Suresh, Jimmy na Mwamvita. Walikuwa watu pekee waliokuwa wakilifahamu hili. Alitaka kumalizana nao kwanza kabla ya kuangalia nini anatakiwa kukifanya. Usiku huu alikuwa maeneo ya sinza afrika sana akitizama kama anaweza kuwaona wabaya wake. Alikuwa ametulia akiendelea kunywa taratibu bia yake. Macho yake yalikuwa yakimtizama kila mmoja ambaye alikuwa akiingia ndani ya bar ile. Muda mwingi alitumia kuitazama saa yake. Muda ulikuwa ukisonga bila kumuona mtu wala kupata chochote kutoka kwa Dee plus. Kazi aliyompa ya kumfuatilia teddy bado haikuzaa matunda. Bado hakumuamini tena teddy. Aliutambua utamani wa teddy na hata mabadiliko yake. Licha ya kumtoa mkononi mwa kifo bado alijua ama kuhisi teddy anaweza kubadilika tena. Hilo likamfanya Masimba mpe dee plus kazi hiyo, kazi ya kuijua mienendo ya teddy. Hilo likampa ugumu wa kuamini kama hakuna chochote. Akauvuta muda akisubiri chochote. Punde mlio wa sms kwenye simu yake ukamgutusha kutoka mawazoni. Mkono ukazama mfukoni na kuibuka na simu. Sekunde moja iliitosha kuufungua ujumbe ule na kuusoma. "Wadudu wawili wamekaa ufukweni wakidonoa chini." Ulisomeka ujumbe. Ilikuwa lugha aliyoielewa, lugha ambayo ilimpa hamu ya kuwajua hao wadudu wawili na kile wanacho kidonoa.

"Ustawi" alijibu kwa neno hilo huku akiirudisha simu mfukoni. Lakini hazikupita hata dakika moja simu yake ikaita. Akaitoa tena mfukoni na kuangalia namba ya mpigaji. "CHIEF" ndio jina lililosomeka. Roho ikapaaa na damu kumsisika. Akapeleka kidole kwenye kitufe cha kijani kisha kuipeleka simu sikioni.

"Nakuhitaji nyumbani muda huu." Baada neno hilo simu ikakatwa. Masimba akaduwaa.hakuamini kupigiwa simu na mkuu wake wa kazi hasa ukiangalia jinsi alivyokuwa akisakwa. Niende? Lilikuwa swali pekee alilojiuliza. Lakini kabla hajapata jibu la swali lake akamuona Dee plus akiingia. Akampa ishara ya kumtaka asogee.. Dee Plus akasogea kisha bila kuongea kitu mfano wa picha na kumkabidhi Masimba
 
NITAKUPATA TU

SEHEMU YA 035

Akapewa kitu mfano wa picha, akaikunjua kutoka kwenye kitu kama gazeti na kuitupia macho. Akakutana na picha ya Mpenzi wake akiwa sambamba na mtu ambaye alimfahamu sana. Mtu ambaye alimkuza katika fani hadi kufikia hapo. Aliitizama picha kwa muda kisha akairudisha mikononi kwa Dee plus. "Hakikisha hawakupotei au hakikisha unakijua kile ambacho wamekizungumzia." Aliongea masimba akiunyoosha mkono. Dee plus aliichukua ile picha na kuondoka akimuacha masimba akiendelea kuburudika. Bado alihitaji kujua kile ambacho teddy na ben walikuzungumza pale ufukweni. Dee plus akaondoka safari hii akielekea katikati ya mji. Alitaka kuanza na ben kwanza. Kwa kuwa alikuwa na hisia kuhusu kikao cha pale ufukweni mwa bahari. Bastola mbili zilikuwa sehemu tofauti mwilini. Alimjua teddy na pia ben, licha ya kuwajua huko lakini hakuhofia kwa kuwa hata yeye alikuwa mmoja kati yao.

Picha ya teddy na ben wakiwa ufukweni mwa bahari ni kitu ambacho kilimjengea maswali masimba katika kichwa chake. Muonekano wa watu hawa katika picha aliyoitazama muda mfupi uliopita hapakuonekana ishara ya mapenzi juu yao. Ukaaji na jinsi walivyokuwa wakitizamana ilionyesha uwepo wa kitu nyeti kilichokuwa kikijadiliwa na watu hawa wawili. Hisia kwamba teddy anapanga mipango ovu juu yake ilikuwa akikigonga kichwa chake. Haikuwahi kutokea teddy na ben kuwa na ukaribu huu.. hilo likampa mashaka na wasiwasi. Hisia kwamba teddy bado hajabadilika bado ziliendelea kumsumbua. Akatamani kumfuata na kwenda kumuuliza kwa kuwa bado alimpenda sana. Hata alipokumbuka usaliti aliotendewa na watu wake, akahisi labda alimtafuta ben kwa ajili ya kumpa kazi ya kuwafutilia mbali jimmy na washirika wake. Vifo vya watu sita katika nyumba fulani ni ishara kuwa yupo mtu anayetembea naye kila sehemu. Kwa mara ya kwanza akawaza kuitumbukiza risasi kichwani kwa mwanamke huyu. Ni dhahiri kuwa mapenzi kwake tayari yalishakwisha. Akaendekea kuuvuta muda tena na tena. Wakati wa kuianza hii kazi hakuwaza kama angefika huku. Hakuwaza kama yangetokea haya. Kwa mara ya kwanza akakumbuka wito wa DG wa idara ya Ujasusi. Wito ambao kidogo ulionyesha kumtatiza katika kuukubali. Sekunde hii alikuwa amekaa akiwaza, sekunde ya pili alikuwa akiukaribia mlango wa kutokea tayari kwa safari ya kuelekea kwa Chief. Alitembea kwa miguu mpaka maeneo ya bamaga, hapo akachukua tax tayari kwa safari ya kuelekea masaki nyumbani kwa mkurugenzi. Muda wote alikuwa kimya wakati tax akisonga kuelekea masaki. Mara moja moja alikuwa akiangalia kwenye vioo vya pembeni kuona kama anafuatiliwa, lakini haikuwa hivyo. Hapakuwa na gari wala usafiri wa aina yoyote. Wakati tax inafika kwenye mataa ya Morocco, akaiona gari nyeupe kupitia kioo cha pembeni akiwafuatilia. Ingawa gari ile ilikuwa katikati ya magari mawili, lakini hilo halikumfanya asigundue kuwa inamfuatilia yeye kwa kuwa, wakati anatoka pale afrika sana, -hii gari aliipita ikiwa imeegeshwa pembezoni mwa barabara. Hakuongea kitu wala kuonyesha mabadiliko yoyote, dereva naye akaendelea kuendesha pasipokugundua kitu. Wakavuka mataa sasa wakielekea maeneo ya oysterbey. Alipoiangalia ile gari, akaiona nayo ikiendelea kusogea tena ikiwa katikati ya yale magari matatu . Hapo kengele za hatari zikaendelea kugonga kichwani mwake. Hisia kwamba yale magari matatu yalikuwa katika safari moja ikamjia. Kwa mara ya kwanza akajipapasa sehemu alipoihifadhi bastola yake. Baada ya kuhakikisha ipo akatabasu huku akimuomba dereva aelekee ulipo ubalozi wa ufaransa. Dereva akatii na kuuongeza mwendo, huku nyuma magari yale nayo yakaongeza.

Muda mfupi dereva akasimamisha gari pembeni mwa barabara. Masimba na dereva wote wakashuka, masimba akatia mkono wake mfukoni na kutoq noti mbili za elfu kumi kumi na kumpa yule dereva. Wakati dereva akijipapasa kutafuta chenji ya kumrudishia masimba. Muda ule ule gari zile zikawapita kwa mwendo ule ule, lakini kufika mbele kidogo zikaacha barabara inayokwenda posta, mbili zikaingia kushoto kwenye barabara inayokwenda Masaki nyingine moja ikapita kama inaelekea daraja la salenda. Kila kitu kilichokuwa kikitendeka pale kilimsisimua na kumfurahisha masimba. Kila kitu kilichokuwa kikitendeka ulikuwa ni mpango uliosukwa na DG wa Tiss. Alizijua gari na vile vile alizitambua mbinu husika. Hakuogopa tena.. dakika ile ile akaliacha eneo lile akiwa juu ya usafiri wa pikipiki.

*******

Ukimya ulikuwa umechukua nafasi yake kama kawaida katika eneo lote la masaki. Walinzi wa idara zote walikuwa wakizunguka kila kona kuwalinda viongozi wote. Makachero walikuwa kila sehemu wakinusa hiki na kufanya kile. Masimba alishuka umbali wa hatua hamsini kutoka yalipo makazi ya chief. Akatembea taratibu macho yake ya kitizama kila sehemu. Maafisa usalama na jeshi maalum la usalama wa taifa walikuwa wamezagaa kila upande wakiangalia usalama. Masimba akatembea kanakwamba hakuwa akiwaona walinzi na hata maafisa wengine. Akalikaribia geti, hapo akasimamishwa huku mitutu ya bunduki ikielekezwa kwake. Mtu mmoja alieonekana kama mkuu wa ulinzi akamsogelea masimba kwa ukaribu. Alipomfikia na kugundua alikuwa nani alimpa heshima kisha kumuongoza kuelekea ndani tayari kwa kukutana na Chief. Geti likafunguliwa masimba akaongozwa mpaka ndani pembeni kukiwa na watu maalum kutoka kikosi cha walinzi wa viongozi yaani VIP PROTECTION UNIT. Kufika ndani akaongozwa mpaka ndani ya jumba. Kuingia tu akukatana na macho ya chief mr godliving kimaro akimtizama. Hayakuwa macho ya kutisha machoni mwake, yalikuwa macho ya kawaida na macho ambayo hayakuwa na chochote. Wakaangaliana tena na tena, kila mmoja akimtizama mwenzake. "Shikamoo Mzee." Hatimaye masimba asabahi. Chief akaitika kwa kichwa kisha akampa ishara ya kukaa katika moja ya viti pale ndani. Masimba akakaa pasipo kubisha. Macho yake yalikuwa yakimuangalia Chief. Hata chief naye akawa ana muangalia usoni. "Bila shaka nadhani unajua kuhusu hiki kilichotokea hapa nchini. Mambo yamekuwa magumu sana, mashinikizo kutoka mamlaka za juu yamezidi. Mkuu wa nchi anataka kupata taarifa kuhusu hiki kifo. Lakini bado wenzako wameshindwa kupata chanzo cha kilicho nyuma ya hili tukio. Wote ambao tulidhani wangeweza kutufumbua katika hili nao huuawa katika mazingira ambayo nadhani ni kutaka kuuficha ukweli. Nimekuita hapa kukupa hii kazi, kushindwa kwa idara zetu za ujasusi ni aibu kwa nchi na kwa dunia. Mheshimiwa rais ametishia kuwaomba CIA NA MOSSAD katika kumgundua muuaji huyu ama chanzo mauaji hayo. Fanya ufanyavyo na kwa njia zako zote ili tufahamu hili. Unaruhusiwa kutumia chochote katika hili."aliongea chief akionekana kukerwa na hiki ambacho kinaendelea kutokea. "Masimba hakutaka kuongea kwa muda ule. Kichwa chake kilikuwa kikiifikiria kazi hii aliyopewa. Kazi ya kumtafuta muuaji wa waziri mkuu, muuaji ambaye alikuwa ni yeye mwenyewe. Akatamani kumjibu kwamba mimi ndiye muuaji, lakini akauacha huo mpango. Angejichunguzaje wakati muuaji alikuwa yeye? Hapo akauona umuhimu wa kuwawahi Jimmy, suresh na mwamvita. Alitambua watu hawa ndio watakuwa mashahidi juu ya maovu ya Hayati. "Unadhani mtuhumiwa wa mauaji aliyenusurika kufa kwa amri yako anaweza kuifanya kazi nzito kama hiyo tena akitumwa na watu wale wale wali0mtuhumu? Akauliza masimba masimba. . Safari hii akibadilika.

"Najua kwa nini nimekuita hapa, hayo mengine achana nayo, nimeunusa ukweli ndio maana kama mkuu wa idara nikakuita." Akajibu Chief.

"Sawa nitafanya naomba muda wa wiki mbili nitarudi hapa nikiwa na ushahidi ama mtuhumiwa mwenyewe. Ninachoomba ni ruhusa kutoka mamlaka za juu kuipekua nyumba zote zinazomilikiwa na marehemu." Lilikuwa ombi ambalo lilimduwaza chief. Hakulitegemea hilo. Akakaa kimya kama sekunde ishirini kisha kwa sauti yake akasema. "Sawa nitazingatia ombi lako." Baaada ya jibu hilo la chief, masimba akainuka na kutoka tayari kwa kuondoka huku akicheka kimoyomoyo.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom