Riwaya: Kiguu na njia

Duhhh ninouma
 
Sikuonana na Chifu hadi baada ya siku tatu. Zikiwa siku za kula vizuri, kulala vizuri na kupumzika, huku tayari nimepewa nguo na viatu vipya, nywele zangu zikiwa zimekatwa vizuri, nilimwona Chifu akinitazama kwa makini kabla ya kutikisa kichwa kama alivyofanya mkewe na kisha kutabasamu.

Nilikuwa nimepelekwa kukutana naye katika ‘Ikulu’ yake, chumba kikubwa chenye viti vipatavyo mia moja vilivyoelekea kwenye kiti chake cha enzi, ambacho kilichongwa kwa mbao za mpingu na fundi anayejua kila aina ya nakshi. Sehemu kubwa ya kiti hicho kilimeremeta kwa aina fulani ya mawe ambayo baadaye nilikuja kufahamu kuwa ni almasi.
Chifu alikuwa amekikalia kiti hicho, mimi nikiwa nimesimama wima mbele yake. Tulikuwa wawili tu chumbani humo baada ya walinzi ambao huwa wako nyuma yake siku zote kuamriwa kuondoka.

“Karibu mwanangu!” Chifu alitamka baada ya kunitazama kwa muda mrefu. “Karibu katika himaya ya Masanja mwana Kasanga, Msukuma halisi aliyewashinda wavamizi na wahamiaji wote. Jisikie uko nyumbani.”
Nilitikisa kichwa kumkubalia ingawa nilikuwa sijamwelewa.

“Hata hivyo, ningependa kukufahamu vizuri, wewe ni nani, kabila gani, ulikuwa ukitokea wapi na kwenda wapi kabla vijana wangu hawajakuleta hapa?” Chifu aliniamuru. Sauti yake ilionyesha upole na upendo kama ya mkewe. Ikanitia moyo.

Nilieleza ukweli juu ya kwetu, Buha, ambako nilizaliwa na kukulia. Kwa hofu kuwa ule mweleka ulikuwa umemwua padri Backhove na kwamba habari za kifo chake zilikwishawafikia huku, nilidanganya juu ya maisha yangu ya elimu. Nilimwambia Chifu kuwa ingawa nilifuata elimu huko kwa Wahaya niliishia kuvua samaki katika ziwa kwa kukosa mtu wa kunisomesha.

Kwa mshangao wangu habari hiyo ilimfurahisha sana Chifu. Alipotabasamu, akacheka kabla hajakohoa kwa kupaliwa na kicheko chake. Baadaye alisema, “Mungu amekuleta nyumbani, upate elimu uliyokuwa ukiitafuta. Utasoma shule ya watoto wa Machifu. Kama ubongo wako unachemka barabara utafika hadi Ulaya. Utakuwa Cheyo lakini Cheyo ataendelea kuwa Cheyo.”

Sikumwelewa. Nikamtumbulia macho ya mshangao na kutoamini, macho yaliyojaa maswali ambayo Chifu aliyaona na akaamua kuyajibu, “Nitakuibia siri moja. Nataka ibakie siri, kati yangu na wewe tu. Unaweza kutunza siri?”
Nilikubali.

“Pamoja na umri huu,” Chifu alisema. “Pamoja na kuwa na wake tele hadi leo nimejaliwa kupata mtoto mmoja tu, wa kiume. Anaitwa Cheyo. Tena ana umri kama wako.” Alisita kidogo kabla hajaongeza, “Himaya yangu iko mashakani. Nikifa himaya itapotea mali zangu zitaparanganyika. Hivyo, walipokuja wazungu kutaka kumchukua mwanangu huyu wa pekee ili wampeleke nchi ya mbali akapate elimu, naona tukio hilo litaiweka mashakani zaidi himaya yangu. Nani atarithi Ufalme wangu?”

“Na hata kama akirudi, akiwa amepoteza maadili ya utawala na mila za kabila langu na kuambulia tamaduni za mila za wageni nitakuwa nimejiweka katika nafasi gani?” Chifu alihoji na kuishia kujijibu mwenyewe, “Hapana. Nimekataa. Cheyo ni mwanangu. Nitamlea na kumfundisha mwenyewe. Sitaki kuchekwa na Machifu wenzangu wenye watoto lukuki.”
Alisita kwa muda akiwa amejiinamia. Alipoinuka alinikazia macho, “Mwanangu,” akasema “Ni hapo unapoingia katika familia. Kama kweli unataka elimu, kama kweli unaweza, nitakupeleka wewe badala yake. Utatumia jina langu na hadhi yangu. Utalelewa kwa upendo na amani maisha yako yote, kama mtoto wangu wa damu.”

Alinikazia tena macho, kwa muda mrefu kama anayejaribu kuusoma moyo wangu. Kisha akaniuliza taratibu, “Unasemaje?”

Niseme nini? Kwanza sikulitegemea swali hilo. Lakini sikutegemea kabisa kuwa matokeo ya kutekwa kwangu majuzi yangekuwa habari njema kama hiyo. Shule! Ni kitu nilichoondokea kukipenda kuliko chochote kile katika uhai wangu. Jambo lililofanya nishindwe kuamini iwapo nilichokuwa nimesikia ilikuwa ukweli au niko ndotoni. Niseme nini? Sikuwa na la kusema zaidi ya kuhisi machozi ya furaha yakinitoka na kuteleza juu ya mashavu yangu. Nilijaribu kuyafuta kwa mkono wangu ambao pia ulikuwa ukitetemeka.
Chifu hakuhitaji sauti yangu kupata jibu langu. Alielewa. Akainuka na kunikumbatia. “Hutajutia uamuzi wako. Naapa…” alininong’oneza.

Siku mbili tatu zilizofuata zilikuwa za maandalizi ya safari. Niliandaliwa vizuri sana kwa kufundishwa historia ya ukoo na majina ya mababu zao, ambao walikuwa wangu pia. Nilitakiwa kukariri majina hayo pamoja na mambo mengine tele ya kifamilia, kiukoo na kikabila. Haikuwa kazi rahisi.

Kiafya niliandaliwa pia. Ilikuwa nile mayai sita, kuku mmoja, ugali au ndizi za kutosha na kunywa kibuyu kimoja cha maziwa kila siku. “Ili ukifika pale ufanane na mtoto wa Chifu,” mzee Masanja alisisitiza. Amri hiyo iliambatana na kulala mapema, kuoga mara mbili kutwa, kuchana nywele zangu na kujipaka mafuta ya mgando mwili mzima. Hilo liliambatana na kununuliwa nguo za maana, viatu vya bei, mfuko wa safari na noti ya shilingi kumi ambayo Chifu alisema ni ya ‘kulinda mfuko.’

Matokeo ya kazi hiyo yalimshangaza kila mtu, ikiwa pamoja na mimi mwenyewe. Liliibuka dume lililopanda juu, lenye maungo yenye nguvu na afya tele, dume ambalo ile sura ya hofu na mashaka ilitoweka, nafasi yake ikachukuliwa na sura ya ucheshi, iliyojaa matumaini. Sura ya Mtanganyika halisi, aliyependwa na kupendeza kwa kila aliyemtia machoni. Sura ya Mtukwao au Petro mwana wa Karimanzira, mjukuu wa Kionambali. Hapana, sasa nilikuwa Cheyo mwana Masanja mwana Kasanga!

Nilikuwa mimi yuleyule, lakini mpya! Msomi mtarajiwa!
Pamoja na maandalizi hayo ya kusisimua, kitu kimoja kilikuwa kikisumbua sana akili yangu. Toka nilipokuja katika familia hiyo na kupewa nafasi ya kuwa mwana familia na fursa ya kupata elimu sikuwa nimebahatika kukutana ana kwa ana na mrithi halali wa familia, ambaye nafasi yake ya elimu nilielekea kuipokonya. Ningependa sana kumwona mtu huyu. Nijue ni mtu wa aina gani kitabia na kimaumbile. Lakini zaidi ningependa kujua msimamo na fikra zake juu ya uamuzi wa baba yake wa kumnyima fursa ya elimu ili awe mrithi na Chifu wa baadaye wa eneo hili.
Nilipata kumuuliza Chifu juu ya hilo, iwapo mwanawe ameridhia maamuzi hayo au la, lakini, kwa mshangao nilimwona Chifu akionyesha dalili za kukasirika kabla hajanijibu kwa mkato, “Yule ni mwanangu. Atafuata matakwa yangu,” jibu ambalo lilinitia mashaka zaidi.

Nilipopata wasaa nilimuuliza bi mkubwa juu ya jambo hilo. “Ni kweli mwanao hataki shule. Ni kweli atafurahi akisikia kuwa nakwenda kule kutumia jina lake na nafasi yake kujipatia elimu? Halafu yuko wapi mbona hajaonekana?”
Mama Chifu alinifumbua macho kidogo. Alisema, “Cheyo alikuwa anapenda shule. Hiyo sio siri. Lakini anatupenda zaidi wazazi wake. Hawezi kututupa kwa ajili ya kujua kusoma na kuandika. Alikubaliana na baba yake na ameachana na ndoto zote za kwenda shule. Amejiandaa kuja kuchukua nafasi yake mara Mungu atakapomchukua baba yake.”
“Yuko wapi?” nilimuuliza.

Nilimwona mama akisita kidogo. Baadaye alisema, “Nitakuibia siri. Chifu amemficha, hadi suala hili litakapokwisha.”
“Amemficha wapi?” nilisisitiza.

“Amemsafirisha. Yuko Misungwi kwa wajomba zake. Watamrudisha hapa mara wewe utakapoondoka na kuingia shule ili Wazungu waache kutuma matarishi wa kumtaka Chifu apeleke mtoto wake shule.”
Kiasi nilifarijika, walao kwa kuelewa ukweli.

Hata hivyo, usiku wa kuamkia safari yangu mashaka yangu yaliibuka pale mmoja wa wajomba hao wa Misungwi alipofika kwa Chifu akiwa na taarifa ambayo ilimchanganya Chifu mwenyewe na kila mtu katika familia hiyo. Kwamba Cheyo alikuwa ametoweka kwa wajomba zake na hajulikani aliko!

Chifu aliduwaa. Alimtolea shemeji huyo macho makali, yaliyojaa hasira. “Kwa nini hamkumwangalia?” alifoka. “Mtafuteni, arudi hapa!” aliamuru.
 
KWA ANAYEKIHITAJI KITABU HIKI CHA KIGUU NA NJIA NA VINGINE VYA BEN MTOBWA KAMA DAR ES SALAAM USIKU, SALAMU TOKA KUZIMU, TUTARUDI NA ROHO ZETU NA VINGINE VINGI, NITAFUTE KWA KUPITIA 0712504985 AU 0763044459. KARIBUNI.
SURA YA SITA
Kwa treni hadi Tabora
Safari ya Mwanza hadi Tabora ilikuwa ya kusisimua sana. Ilikuwa safari yangu ya kwanza maishani kusafiri bila kutumia nguvu za miguu au mikono yangu. Toka Kigoma hadi Kagera hadi Mwanza nilitumia mikono au miguu yangu. Toka Kigoma hadi Kagera hadi Mwanza nilitumia mikono yangu kupiga makasia hadi tulipowasili majuzi. Safari hii kazi yangu ilikuwa kukaa kitako, kando ya dirisha, huku macho yangu yakifaidi kilometa zote 453 za safari kwa kuburudishwa na mazingira aina aina.
Tulisafiri kwa aina mpya ya usafiri iliyotambulishwa nchini na utawala wa Mjerumani, gari moshi. Ujenzi wa reli, vyuma imara ambavyo vilitumiwa na gari moshi hiyo kuteleza juu yake, ambao ulianza huko Darisalama mwaka 1912 uliweza kufika Mwanza 1923, ikiwa moja ya matawi ya reli hiyo lililoanzia Tabora. Reli hiyo, maarufu kama reli ya kati inayokata nchi toka mashariki hadi magharibi na toka kaskazini hadi kusini inakadiriwa kuwa na urefu wa kilomita 2600. Ni moja kati ya kumbukumbu za utawala wa Mjerumani, ambazo kamwe hazitafutika katika historia ya nchi hii.
Reli hii ni kiungo pekee muhimu kinachoiunganisha nchi toka bahari ya hindi kwa upande mmoja hadi ziwa la Tanganyika kwa upande wa pili, jambo linaloifanya iwe tegemeo kubwa kwa usafirishaji wa watu na mizigo si kwa nchi yetu pekee bali pamoja na zile za Burundi, Kongo na Rwanda pia.
Licha ya sababu hizo za kiuchumi reli ilikuwa pia mshirika mkubwa katika masuala ya kiutamaduni na kijamiii nchini. Kwanza iliwezesha makabila yapatayo mia na ishirini ya Tanganyika kufahamiana kwa urahisi. Mzaramo wa pwani angeweza kukutana na Mmanyema wa Kigoma, au Mchaga wa Kilimanjaro kufahamiana na Mfipa wa Mpanda kwa urahisi zaidi ya siku zile za akina Livingstone kutumia miaka maporini toka pwani ya Bahari ya Hindi hadi pwani ya ziwa Tanganyika.
Na hilo halikuwa kwa makabila ya ndani tu. Ujenzi wa reli hiyo ulimfanya mkoloni wa Kijerumani alete vibarua wengi wa kazi hiyo toka nchini India. Hawa ni chanzo cha msamiatai wa ‘kuli’ neno lililozaliwa kutokana na lile la kiingereza ‘Coolie’ wakatii huo likitumiwa kama kashfa kwa vibarua wasio na ujuzi wowote. ‘Kuli’ haikutofautiana sana na ‘manamba’ wa hapa nyumbani ambao walikamwatwa kwa visingizio mbalimbali kubwa ikiwa kushindwa kulipa kodi ya kichwa, na kupelekwa kufanya kazi za mikono katika mashamba ya mkonge kaskazini magharibi mwa nchi yetu.
Kuli’ wengi walitoka India, ama walinogewa, ama hawakuwa na uwezo wa kurudi kwao, ama yote mawili, wakaishia kuwa wakazi wa hapa. Leo hii jamii mpya ya akina Gulamali, Manji, Adamjee; na kadhalika inapatikana sehemu yoyote ya Tanganyika; hasa vijijini.
Jing – janga – jing – jang – jing - jang garimoshi lilihangaika kuvuta mabehewa sita wa abiria na manne ya mizigo yaliyofanya tuwe kama joka refu linaloteleza kwa kujikongoja. Injini ya garimoshi hilo, ambayo sikuhitaji kuambiwa kuwa ilikuwa ikitumia kuni kutengenezea mvuke wa kuiendesha ilikuwa ikitoa moshi mwingi na mzito sana. Moshi ambao ulilala juu ya treni kama wingu jeusi lisilopendeza machoni. Nadhani hiyo ni sababu pekee iliyowafanya waswahili waamue kuita usafiri huo wa ‘garimoshi.’
Nikiwa nimeketi raha mustarehe dirishani pangu nililitazama kwa masikitiko ziwa nililolipenda la Nyanza likitokomea machoni mwangu taratibu. Ziwa hilo lilinilea, lilinihifadhi na kunifadhili kwa muda wa kutosha. Ndilo lililonifundisha kuogelea na kutafuta pesa. Ziwa lililonitoa Kagera na kunifikisha Mwanza. Hilo ndilo ziwa ambalo leo naliacha bila kuwa na uhakika wa kuliona tena. “Nitarudi!” nilinong’ona taratibu.
“Nini?” jirani yangu, mzee wa makamo ambaye tulichangia kiti, alinihoji akidhani nazungumza naye.
Sikumjibu.
Tukapinda na kupenya katikati ya majabali marefu mfano wa milima. Tuliacha jabali moja baada ya jingine, mbuyu mmoja baada ya mwingine huku tukivuka vijito na mito ya hapa na pale.
Mara tukazama katika mapori na misitu mikubwa, kwa mbali tukawaona wanyama mbalimbali kama ngedere waliokuwa wakirukaruka kwenye miti au mbuzimawe ambao walirandaranda juu ya majabali ya hapa na pale. Katika eneo moja lenye mabwawa tuliwaona ndege aina ya flamingo wenye miguu mirefu na midomo myekundu wakiwinda samaki au wadudu ndani ya maji hayo. Ndege wengine, aina mbalimbali pia walikuwa wakiruka huku na huko kama wanaotushangaa au kutushangilia hadi tulipotokomea.
“Mantare!” Yule jirani yangu aliropoka.
Ikawa zamu yangu kumshangaa, “Nini?” nilimuuliza.
“Tumefika stesheni ya Mantare,” alifafanua.
Kweli. Nililiona garimoshi likipunguza mwendo na hatimaye kusimama kando ya nyumba mbalimbali ambazo zilionekana kuwa za wafanyakazi wa reli hiyo.
Palikuwa na purukushani fulani, watu wakipanda wengine wakishuka. Miongoni mwa watu hao walikuwepo pia wafanyabiashara wenye bidhaa mbalimbali kama vyakula, mapambo na mifugo. Walionunua walinunua, wasionunua tulijifanya hatuoni.
Tulisimama hapo kwa dakika kumi tu. Mara garimoshi hilo lilianza tena safari yake kwa mwendo wake wenye maringo, taratibu kama halitaki na baada ya kuchochea huku likikohoa kwa uzito wa mabehewa.
“Kwimba!” mzee aliropoka tena. Nilikuwa nimeanza kusinzia. Nikafunga macho na kuona tukiingia katika stesheni nyingine. Nikatoa kichwa dirishani na kuwatazama wanaoshuka na kupanda.
Tukaondoka.
Jirani yangu huyo alikuwa amejipa kibarua. Kila tulipokaribia kituo fulani nilimsikia akitamka kwa nguvu, “Malya,” kisha “Seke.” Sikufumbua macho yangu hadi pale aliponitikisa kwa nguvu huku akiniambia, “Amka tumefika Shinyanga!”
nilifumbua macho. Jina la Shinyanga lilikuwa na uzito wake katika kumbukumbu zangu. Hata hivyo, nilimwambia taratibu “Siendi Shinyanga. Nakwenda zangu Tabora.”
“Tabora! Kuna nini Tabora?”
Sikumwelewa, “Kuna nini Tabora?” nikamjibu kwa swali jingine. “Kwani Shinyanga kuna nini?”
Kumbe mzee alikuwa na hamu ya maongezi. Alianza kwa kutabasamu. Baadaye aliporomosha sifa za Shinyanga. “Kuna kila kitu ambacho binadamu anahitaji. Ardhi bora yenye rutuba tele. Misitu imejaa wanyama kila aina. Ng’ombe wa hapa wamenenepa na wanatoa maziwa mengi kuliko popote pale. Hata Wazungu wengi siku hizi wanatembelea milima yetu mara kwa mara. Kuna fununu kuwa huko ardhini kuna mali nyingi ambazo huko kwao ni utajiri mkubwa.”
Nilitabasamu lakini sikumjibu. Sikuwa na jibu la haraka.
“Enhe na Tabora?” alihoji.
“Tabora nini?” nilimuuliza.
“Kuna nini Tabora?”
Niliamua kumnyamazisha kwa kumpa kile ambacho nilikipata vitabuni, ambacho nina hakika kuwa alikuwa hakijui. “Tukianza na reli hii tunayoitumia sasa. Roho yake iko Tabora.”
“Kwa vipi?” alihoji akicheka.
“Tabora ni kituo pekee muhimu sana. Pale Tabora ndipo ambapo reli hii inajigawa, moja ikienda Kigoma, ambako inafika hadi ziwa Tanganyika linalotuunganisha na nchi za Kongo, Burundi na Zambia. Pia, kuna reli inayokwenda hadi Mpanda, kusini mwa nchi yetu.”
Wakati akitafakari hilo nilimpa la pili.
“Unaijua eropleni?” nilimuuliza.
“Ndege Ulaya!” alisema akicheka. “Sio naijua, nimeipanda mara nyingi.”
“Kutoka wapi kwenda wapi?” nilimuuliza kwa mshangao.
“Burma,” alinijibu. “Kwenye vita kuu ya kwanza nilikuwa mmoja wa wapiganaji tuliorushwa kwa ndege kwenda kusaidia wenzetu waliozingirwa na maadui,” alisita kidogo kabla ya kuniuliza, “Ndege ina uhusiano gani na Tabora?”
“Tarehe 22 Julai mwaka 1920 ndege ya kwanza kutua nchini Tanganyika ilitua katika uwanja wa ndege Tabora. Ndege hiyo ndogo ya Mwingereza iliruka toka Nairobi Kenya hadi hapa na kuweka historia ya pekee kwa nchi ya Tabora.
Mzee alicheka. “Hilo tu?” aliniuliza.
“Yako mengi, “ nilimjibu. “Yule kiboko wa Waarabu, Mtemi Milambo, aliishi katika ngome yake Iselemagazi iliyokuwa Tabora. Yule Mwingereza Davidi Livingstone aliyekataa kurudishwa kwao na akafia Zambia alipata kuishi Tabora kwa muda, kabla hajahamisha makazi yake Ujiji, Kigoma. Tabora ulikuwa mmoja kati ya miji michache nchini iliyokuwa na watu wengi, toka miaka ya 1700, mji mdogo huo?”
Mzee aliyatafakari maneno yangu. “kichwa chako kinafanya kazi vizuri sana, mjukuu wangu. Naweza kutabiri unakwenda Tabora kufanya nini.”
“Naenda kufanya nini?” nilimjaribu.
“Kusoma,” alinijibu. “Kweli au uongo?”
“Kweli tupu.”
Mzee akacheka kabla hajaongeza, “Naweza hata kukuambia jina la shule unayokwenda.”
“Shule gani?”
“Unakwenda Tabora School. Shule ya misheni inayopokea watoto wa machifu. Kweli au uongo?”
“Ni kweli,” nilimjibu kwa mashangao. “Umejuaje mzee?”
“Uzee dawa. Uzee ni kuona mengi ni kuona mbali. Jinsi ulivyovaa, jinsi ulivyotulia, jinsi unavyoongea, ni wazi kuwa wewe ni mtoto wa Chifu. Na nina imani kuwa utafika mbali katika safari yako ya maisha.”
Nilitamani kucheka, nilitamani kulia. Sikujua nifanye lipi katika hayo. Kwa mara ya kwanza, baada ya muda mrefu nikamkumbuka babu yangu, mzee Kionambali.
Mtoto wa Chifu!
 
KWA ANAYEKIHITAJI KITABU HIKI CHA KIGUU NA NJIA NA VINGINE VYA BEN MTOBWA KAMA DAR ES SALAAM USIKU, SALAMU TOKA KUZIMU, TUTARUDI NA ROHO ZETU NA VINGINE VINGI, NITAFUTE KWA KUPITIA 0712504985 AU 0763044459. KARIBUNI.

Tulifika Tabora siku mbili baadaye.
Stesheni ya Tabora ni sehemu moja yenye kila aina ya pilikapilika. Ilikuwa na watu wengi wenye purukushani hii na ile, huyu akihangaika kupanda behewa, huyu akishuka, yule akibadili behewa kuhamia lile, huyu akipiga kelele kuuza asali na bidhaa nyingine na kadhalika na kadhalika. Lakini purukushani kubwa zaidi ilikuwa ya magarimoshi yenyewe. Vichwa vilikuwa vingi mno, vikienda hapa au pale, kuhamia reli hii au ile huku vikicheua moshi na honi za mara kwa mara, hali iliyofanya pawe mahala ambapo mtu asingependa kukaa kwa muda mrefu.
Nilishuka, nikachukua mzigo wangu na kutoka nje ya stesheni. Huko nje kitu cha kwanza kilichovuta macho yangu ni wingi wa maembe. Barabara nzima toka stesheni hadi mjini zilizingirwa na miembe mikubwa, kila upande kwa namna iliyofanya iwe na kivuli murua cha kusisimua. Nilipiga hatua moja kwenda nyingine kuifuata barabara hiyo ya aina yake. Kila hatua ilinifanya nione kuwa wingi huo wa miembe haukuwa wa kando ya barabara pekee. Mapori yote ya mji yalitawaliwa na miembe mingi, mikubwa, ambayo baadhi ilikuwa na maembe yaliyoiva, ambayo yalionyesha kuwa watoto wa mji huo walishachoka kuyala.
Mji wa Tabora ulikuwa mdogomdogo, wenye nyumba za kawaida, ambazo hazikutofautiana sana na zile za Mwanza. Tofauti pekee kubwa niliyoiona ni mavazi na lafudhi. Kimavazi nilishangaa kuona watu wengi wakiwa wamevaa mavazi yenye asili ya Kiarabu, kanzu nyeupe na kiko mdomoni kwa wanaume na baibui jeusi lililofunika moja ya kumi ya mwili isipokuwa sehemu ndogo ya uso kwa wanawake. Katika mazungumzo yao nilibaini pia kuwa lafudhi ya wengi wao ilikuwa ya Pwani zaidi. Japo walizungumza kwa namna iliyofanya nihisi ama wanaibembeleza lugha ama inateleza kwenye ndimi zao.
‘Karibu Tabora mwanangu!’ nilijikaribisha.
Nikauliza njia ya kwenda shule ya Tabora School. Nikaelekezwa. Nikaifuata njia hiyo taratibu, mzigo mkononi, mluzi mdomoni, ndoto za mafanikio zikiwa tele moyoni.
Nilipokelewa na mlinzi nje ya geti la kuingilia shuleni. Nikajitambulisha kwake. Alinifungulia geti na kunielekeza iliko ofisi ya mkuu wa shule. Nilikwenda kwa mwendo wa kujiamini, huku nikiwa tayari nimetoa barua yangu ya utambulisho toka kwa ‘baba yangu,’
Chifu Masanja mwana Kasanga. Wanafunzi wenzangu tayari walikuwa madarasani. Niliweza kuwasikia baadhi ya walimu wakifoka kwa sauti kubwa katika jitihada za kujaribu kuingiza kitu fulani katika vichwa vigumu vya wanafunzi.
Karani wa mkuu wa shule alinipokea, akaipokea barua yangu na kuiingiza chumbani kwa bosi wake. Muda mfupi baadaye niliitwa katika ofisi hiyo.
Mkuu wa shule alikuwa Mzungu. Mtu mnene miraba minne, ambaye angefaa zaidi kuwa mwalimu wa ngumi badala ya taaluma. Nilimkuta kasimama nyuma ya meza yake, barua yangu ikiwa mkononi mwake. Alinikazia macho makali kwa dakika moja au mbili kabla hajatamka neno moja tu “Keti.” Nikaketi kwenye kimoja wapo cha viti viwili vilivyomuelekea mwalimu mkuu, miguu yangu ikianza kupoteza nguvu, mikono ikianza kutetemeka kwa sababu ambayo sikuifahamu.
“Barua yako hii?” alinihoji baadaye.
“Ndiyo.”
“Umeipata wapi?”
“Kwa nini? Nimepewa na Chifu… baba… nikuletee.”
“Chifu nani?”
“Masanja mwana Kasanga.”
Mkuu huyo wa shule alinitazama kabla hajaongeza swali jingine, “Unaitwa nani?”
Nusura nitaje jina langu halisi. “Cheyo,” nikatamka.
Nilimwona mkuu wa shule akizidi kushangaa. Mara akawa kama kakumbuka jambo. Akatoka na kumnong’oneza jambo karani wake. Kisha akarudi na kuketi. Muda mfupi baadaye mlango uligongwa, mwanafunzi mmoja akaingia na kuelekezwa kuketi kiti cha pili kilichokuwa wazi.
Mkuu wa shule alimkazia macho kama alivyofanya kwangu kabla ya kumuuliza, “Ulisema wewe ni nani, unatoka wapi na baba yako ni nani?”
“Naitwa Cheyo. Kwetu Mwanza. Mimi ni mtoto wa Chifu Masanja mwana Kasanga.”
Miguu yangu iliishiwa nguvu. Nilitamani ardhi ipasuke, inimeze yaishe. Ardhi haikufanya hivyo. Nikahisi nimeanza kutetemeka mwili mzima, jasho jembaba likinitoka.
Mkuu wa shule alikuwa akinitazama kwa makini.
“Nani anasema uongo, nani anasema ukweli kati yenu?” aliniuliza. “Juzi tu,” aliongeza. “Alikuja huyu kijana, akatuambia kwamba anaitwa Cheyo na ni mtoto wa chifu Masanja. Kwa maelezo yake baba yake hataki aje shule, anataka akae nyumbani kusubiri kurithi Uchifu wake atakapokufa. Kwamba amekuja hapa shuleni kwa kutoroka baada ya jitihada za kumsihi baba yake kumruhusu kushindikana. Na kwa jina na nafasi yake ilikuwa wazi bado tumempokea na kumruhusu kuendelea na masomo. Leo umekuja wewe. Unadai wewe ni Cheyo mtoto wa Chifu Masanja na una barua yake ya kuomba upokelewe hapa. Nataka kujua nani mkweli nani mwongo kati yenu,” aliniuliza akitutazama kwa zamu. Cheyo naye alishangaa. Akageuka kunitazama. Nilijitahidi kuinua uso wangu nimtazame pia, ilikuwa kazi ngumu kuliko zote nilizopata kufanya. Hicho kidogo nilichobahatika kuona katika uso wake kilionyesha wazi kuwa si kwamba hatufahamiani tu, bali pia tulikuwa hatufanani kwa namna yoyote ile. Pale ambapo mimi nilikuwa mng’avu yeye alikuwa mweusi tii, pale nilipokuwa mrefu yeye alikuwa mfupi na mwenye kiribatumbo.
 

Similar Discussions

Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…