Tukishasahaulika sasa tutakumbukwa lini?

TheForgotten Genious

JF-Expert Member
Jan 18, 2014
995
1,508
Na Maundu Mwingizi
Mwalimu wa Fasihi na muandishi wa vitabu.

Waswahili hunena, ukiwa na jambo unalopaswa kusema, kunyamaza ni sawa na kudanganya. Tangu nilipomaliza kutazama hafla ya Uzinduzi wa Ikulu mpya ya Chamwino, jijini Dodoma, nimejaribu kujizuia kusema chochote, lakini nahisi dukuduku likipanda toka kifuani hadi kooni kiasi cha kufanya nihisi koromeo limejaa mithili ya njiwa manga kwenye shamba la mpunga. Sina budi kufunua kinywa ili kupata ahueni. Walakini kabla sijasema chochote, naomba kuwaonesha japo kidogo umuhimu wa hafla zinazofanyika Ikulu au katika majilisi nyinginezo za Kiserikali katika kuhuisha na kukuza tasnia mbalimbali nchini.

Mwezi Januari 2021, katika hafla ya kuapishwa kwa Rais wa 46 wa Marekani, Joe Biden, mbali na wasanii wakubwa duniani kuhudhuria, pia alialikwa msichana mdogo wa miaka 22—mtunzi wa vitabu vya mashairi—aitwaye Amanda Gorman. Mshairi huyu hakualikwa tu kula karanga za Ikulu na kupiga picha, bali pia alipatiwa fursa ya kusoma shairi lake liitwalo The Hill we Climb, fursa ambayo—ndani ya siku ya moja tu—ilipelekea vitabu vyake viwili; Change Sings: Children Anthem na The Hill we Climb, kupanda chati na kushika nafasi mbili za juu kimauzo kwenye orodha ya Amazon. Fauka ya hayo, ndani ya siku hiyo hiyo moja, mamilioni ya wafuasi (followers) walifurika katika kurasa zake za mitandao ya kijamii. Mathalani, huko Twitter alikokuwa na wafuasi elfu saba tu, alifikisha zaidi ya wafuasi milioni mbili. Huko Instagram sasa ndiyo hakusemeki. Baada ya hafla hiyo, vyombo vikubwa vya habari kama CNN, BBC, Al-Jazeera, na vile vya mkondoni kama Oprah Show, nk., vilimsaka kwa udi na uvumba ili kufanya naye mahojiano yaliyokuwa na tija kubwa mno. Taasisi mbalimbali nchini Marekani, kama vile Morgan State University, zilimtafuta ili kutaka kumwajiri katika idara nyeti za masuala ya fasihi.

Mafanikio haya makubwa, yaliyochagizwa na kitendo kidogo tu cha Ikulu ya White House, kumwalika na kumpa fursa ya kuonekana mbele ya hadhira kubwa, hayakuishia tu kwa Amanda pekee, bali mrindimo wake uliitetemesha tasnia nzima ya watunzi wa vitabu nchini Marekani. Mauzo ya vitabu vingi yaliongezeka mara dufu na ilhali mzani wa hadhi ya watunzi ukipanda juu.

Kwa tukio hilo, Ikulu ya White House ilipeleka ujumbe Duniani, namna inavyothamini hadhi na kukuza vipaji vya watunzi wao wa vitabu, sanjari na juhudi zake katika kuhamasisha usomaji wa vitabu—kitu ambacho kinachochea maarifa katika bongo za watu wake, na kusisimua ubunifu katika ukuaji wa vipawa vyao. Tuulizane: ni akina "Amanda" wangapi nchini mwetu wanaofisha ubunifu wao na kuzika vipaji vyao kwa kukosa hamasa kutoka katika majukwaa makubwa ya wenye mamlaka!

Nililikumbuka tukio hilo la Amanda na Ikulu ya Marekani, baada ya moyo wangu kutamani kuwaona watunzi wa vitabu (riwaya, mashairi, nk)—kama walivyopanda jukwaani wanamuziki—nao wakipatiwa fursa hiyo adhimu na adimu kabisa katika Uzinduzi wa Ikulu mpya ya Chamwino. Lakini—waapi bwana wee—si tu hawakupata fursa ya kupanda jukwaani wala kutambuliwa hadharani, bali hata kualikwa tu ilishindikana. Walipuuzwa kabisa—au "kiungwana" tuseme walisahaulika.

Lakini, anapoalikwa Ommy Dimpoz, akasahulika mzee Shafi Adam Shafi (wa Kuli, Kasri ya Mwinyifuadi, Mbali na Nyumbani) huko ni kupuuzwa; anapoalikwa Christian Bella, akasahulika Hussein Tuwa (wa Mfadhili, Mkimbizi, Mdunguaji, nk) huko ni kupuuzwa; anapoalikwa Steve Nyerere, akasahulika Prof. Emanuel Mbogo (wa Watoto wa Mama Ntilie, Malkia Sitti bint Saad, nk) huko ni kupuuzwa; anapoalikwa Hajji Manara, akasahulika Richard Mabala (wa Hawa The Bus Driver, Mabala The Famer, nk), huko ni kupuuzwa. Sasa kwanini tunawapuuza—au tunawasahau—watu ambao kupitia kalamu zao wanalinda tamaduni zetu na kuchochea maarifa yetu? Umeshajiuliza ni kwa nini, wanenguaji na hata machawa wa wasanii wanaalikwa Bungeni halafu washindi wa tuzo za uandishi wa vitabu (riwaya, mashairi) za Safal-Cornell na Mwalimu Nyerere, wanasahaulika? Ni kupuuzwa tu.

Katika hali kama hiyo, unadhani kijana aliyewasoma akina Richard Mabala, Hussein Tuwa, kisha akaishia kuwaona tu Facebook na Twitter, anapokuja kuwaona Ommy Dimpoz na Steve Nyerere—wakiwa na Rais wa nchi—kwenye hafla kubwa za Kiserikali, atatamani kuja kuwa nani baadaye kati ya mwanamuziki na mwandishi? Atapenda kusoma vitabu au kusikiliza nyimbo? Sisemi kwamba hatuhitaji wanamuziki, waigizaji, nk, la hasha. Bali tunahitaji mchanyato wa wanasanaa na wanataaluma toka katika nyanja mbalimbali.

Hivi sasa tuna ombwe kubwa la watunzi wa kike katika tasnia ya vitabu nchini, kiasi kwamba wanawake wanakosa wa kuwasemea mambo yao kinaganaga. Sasa hebu pata picha, katika hafla ile ya Ikulu, mbele ya macho ya Rais, wangetambuliwa watunzi kama Zaynab Bahroon, Laura Pettie, Lilian Mbaga, Elizabeth Mramba, na wengineo, ni hamasa kubwa namna gani ingewafikia wasichana nchini ambao wanatamani kuwa watunzi wa vitabu, lakini hawaoni mwanga!

Watunzi wa vitabu (riwaya, mashairi, nk) wanazo kofia mbili vichwani mwao; moja, ni wanataaluma—kwa sababu vitabu vyao vinaandikwa kitaaluma na vinatumika katika shughuli za kitaaluma; pili, ni wana sanaa—kwa sababu vitabu vyao (riwaya, ushairi, nk), kama ilivyo kwa nyimbo na uigizaji, ni tanzu za fasihi. Na fasihi ni tanzu ya sanaa. Kwa hivyo, washairi na wanariwaya ni wasanii pia. Je, unayajua madhara ya kumsahau mtu ambaye asipoigusa jamii kitaaluma, ataigusa kisanaa? Sasa, kasumba hii imekuwa ikichipua kwa kasi mithilii ya uyoga kwenye kichuguu, kiasi kwamba si tu katika hafla za Ikulu, bali karibu hafla zote ambazo wana sanaa na wanataaluma mbalimbali hualikwa, watunzi wa vitabu (riwaya, mashairi, nk) husahaulika. Tunajenga taifa gani lisilo na hamasa ya kuandika wala tashwishi ya kusoma?

Nchi zilizoendelea Duniani zinawatunza na kuwatuza watunzi wao wa vitabu kwa wivu mkubwa. Chukua mfano, Rais Obama katika utawala wake, aliwalika Ikulu mamia ya watunzi wa vitabu kama vile akina Toni Morrison, Joyce Carol Oates, Daniel Aaron, Stephen King, na wengine wengi—na kuwatuza medani mbalimbali za kama sehemu ya kuheshimu na kutambua mchango wao katika jamii. Chukua mfano wa pili, mtunzi wa riwaya James Patterson, alipofikiria kuandika riwaya inayohusu masuala ya Urais na Ikulu, alimfikia Rais Bill Clinton na kumshawishi waandike kitabu kwa pamoja. Bill Clinton akakubali. Matokeo yake wakatoka na riwaya kabambe kabisa: The President is Missing na President's Daughter. Kwa heshima hii aliyopewa Patterson, unadhani ni vijana wangapi walikitafuta na kukisoma kitabu hiki? Ni vijana wangapi walitamani kuja kuwa kama Patterson? Bila viongozi kutengeneza fursa hizi hakuna atakayehamasika kufika mbali.

Hata hapa Bongo, miaka ile ambapo usomaji wa vitabu ulikuwa juu sana, haikutokea vile kwa nasibu tu, bali viongozi wa juu wa nchi yetu walishiriki kuamsha ari ya usomaji na kuchochea hadhi za watunzi. Utakumbuka mwalimu Nyerere alishirikiana sana na watunzi kama akina Kaluta Amri Abeid, Shaaban Robert, na wengineo tangu wakati wa kupigania uhuru na hata baada ya kuutwaa. Heshima ya watunzi hawa ikapaa kila kona. Kuna wakati Mwalimu alipata kuwa anawaalika Ikulu watunzi wa vitabu kama akina Elvis Musiba (aliyeandika simulizi za Willy Gamba), Ben R. Mtobwa (aliyeandika simulizi za Joram Kiango), na wengineo ili kupata nao kahawa na kupiga nao soga tu, kitu ambacho kilinyanyua hadhi za watunzi na thamani ya vitabu walivyoandika.

Unaweza kusema labda hiyo ni kwa sababu Mwalimu Nyerere mwenyewe alikuwa ni mtunzi wa vitabu. La hasha. Kuwa mtunzi pekee hakutoshi, bali wito na utambuzi juu ya tasnia hii nyeti kabisa. Chukua mfano huu: mwezi Machi 2017, Rais Magufuli alimteua mtunzi mahiri wa riwaya nchini, Dkt. Harrison Mwakyembe, kuwa Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo. Watunzi tukaamini kuwa sasa hata kama hatutofika chumbani, lakini tutatolewa msalani na kuwekwa walau barazani. Kumbe "mvinyo" ule ule uliowalevya wengi kiasi cha kudhani sanaa ni ya waimbaji na waigizaji tu, tayari ulikwishamlevya chakari Waziri huyu aliyetunga riwaya ya Pepo ya Mabwege. Mvinyo ule ukawa unamyumbisha tu huku na kule; ikawa leo akipepesukia Bongo Fleva kesho anawewesekea Bongo Muvi.

Kuna wakati, kwa kusaidiwa na mzee wetu mmoja, ambaye pia ni mtunzi wa riwaya, Wanariwaya kutoka Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira (Uwaridi) tuliweza kumfikia Dkt. Mwakyembe hadi ofisini kwake jijini Dodoma—na mabuku yetu makubwa yenye kushajiisha mapito yetu na kupambanua mahitaji yetu. Kilichotokea, kama mabuku yetu hayakufungiwa maandazi, basi tutakuwa ni wenye bahati sana.

Hatimaye leo tumempata Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Februari 2021, alihudhuria hafla ya utoaji tuzo za uandishi (riwaya na ushairi) za Mabati-Cornell na kuzungumza mengi yahusuyo uandishi na usomaji, akiwataja akina Mzee Hajji Gora, Shafi Adam Shafi, Mohammed Said Abdulla, na wengine wengi kuashiria namna alivyokuwa mkereketwa na mfurukutwa wa tasnia hii, sasa tusipopaza sauti zetu leo tutapaza lini? Na kama tutasahaulika wakati huu ambapo Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Bi Zuhra Yunus naye ni mtunzi mwenzetu wa vitabu—tutakumbukwa lini?.

Maundu Mwingizi,
Tabora, Tanzania.
 
Back
Top Bottom