Riwaya: Kiguu na njia

Duhhh ninouma
Wote tulitazamana. Macho yangu yalikutana na yale ya Byabato ambayo yalinitazama kwa namna ya kunisuta na kunidhihaki. Macho yaliyokuwa yakisema, “Unajua kuwa najua kuwa ni yako!”

ENDELEAAAAA...
“Nitauliza kwa mara ya tatu,” Padri aliendelea. “Nani kati yenu aliyedondosha hirizi hii jana?”
Macho ya Byabato yalikuwa yameganda juu ya macho yangu, yakinicheka. Sikuweza kustahimili zaidi. Niliinua mkono wangu juu na kisha kusimama huku nikijibu taratibu, “Ni yangu, Padri.”
Si Padri wala wanafunzi wenzangu walioamini masikio yao. Kwa darasa langu, kwa shule nzima na hata jamii nzima ya eneo hilo mimi nilikuwa mfano bora zaidi kimasomo na kikanisa. Nilikuwa hata nikiwasaidia mashemasi katika huduma ndogo ndogo za kanisa.
“Ni yako?” Padri aliniuliza tena, kana kwamba alitaka nibadili kauli na kuikana hirizi yangu. Sikuwa tayari kwa hilo.
“Unajua kuwa mwili wako ni hekalu la Mungu? Aliniuliza Padri.
“Najua!”
“Kwa nini basi unavaa uchafu? Kwa nini unahifadhi dhambi na kuishi nayo? Hutaki kuingia katika ufalme wa Mungu?”
Sikumjibu.
“Sio neno,” Padri aliendelea. “Leo Bwana amefanya muujiza kwa ajili yako. Ameifichua hirizi hii chafu, ambayo umeivaa kwa muda mrefu, ili ujitakase upya. Tutawasha moto hapo nje, utaichoma hirizi hii kwa mkono wako mwenyewe. Kisha tutakuombea na kukubariki kwa kitendo hicho cha kuachana na upagani milele.”
Tulitolewa nje. Zikaletwa kuni, moto ukawashwa. Huku wenzangu wakiimba pambio mbalimbali, mimi na Padri Backhove tulisimama mbele ya kadamnasi hiyo, mikononi mwake akiwa na Biblia na hirizi yangu.
“Wakati nikianza kusali, ichukue hirizi hii uitupe ndani ya moto ukitamka maneno yafuatayo ‘Shetani nakuteketeza sasa na milele, kwa jina la Yesu’ Umeelewa?”
Niliitikia kwa kichwa.
Nyimbo zilipamba moto. Sauti ya Padri akisoma sala ilisikika waziwazi. Lakini mkono wangu uliokuwa na hirizi uliishiwa nguvu huku nikitetemeka mwili mzima. Niliishikilia kwa zaidi ya dakika mbili, nikiining’iniza juu ya miale murua ya moto huo lakini vidole vyangu vilielekea kunigomea. Hisia zangu zilikwenda mbali sana toka hapo. Zilisafiri hadi usiku ule tulipoagana na babu uchochoroni. Masikio yangu yalisafiri pia. Yalikuwa pamoja nami huko uchochoroni, gizani, yakimsikia babu akisema; Hii ni hirizi ya bahati. Ilinde nayo itakulinda maishani mwako. Sauti hiyo ilikuwa wazi wazi kabisa masikioni mwangu.
“Ichome!” Padri alikatiza sala na kuniambia kwa ukali.
“Siwezi!” Nilimjibu.
“Huwezi nini?” aliniuliza kwa mshangao. “Tupa uchafu huo ndani ya moto!” nilishindwa kabisa kuviamini vidole vyangu kufanya hivyo. Mara nikageuka na kuanza kuondoka. Padri hakuyaamini macho yake. Akanifuata na kujaribu kunishika. Nikamsukuma.
Padri Backhove alikuwa mtu mnene na mzito sana. Lakini hakuwa na nguvu nyingi. Nilimsukuma kidogo tu, lakini akaanguka chali, kama gunia. Sehemu ya kanzu yake ndefu, iliyofika miguuni iliangukia ndani ya moto huo na kuanza kuungua.
“Nakufa!” Padri alipiga kelele akijiviringisha huku na kule katika jitihada za kujizoa ainuke toka mavumbini hapo.
Nilishikwa na hofu kubwa. Wakati wenzangu wakihangaika kuzima moto katika mwili wa padri, wengine wakijaribu kuinua mwili wake wenye zaidi ya kilo mia na sitini mimi nilianza kukimbia kwa nguvu zangu zote huku nikihisi sauti za watu wanaonifuata wakizomea nyuma yangu. Sikugeuka wala kusimama hadi nilipofika vichakani, mbali sana, ambako niliamini mtu yeyote asiye na uwezo wa kukimbia kama mimi na ujuzi wa mambo ya porini kama mimi, asingeweza kunipata.
* * *​
Nilijipumzisha kwa muda chini ya kivuli cha mti aina ya mvule, ulioonekana kupevuka sana. Nikaketi na kuegemea shina lake huku nikiitumia akili yangu kutafakari mustakabali wa maisha yangu baada ya tukio lile. Moyo wangu ulijaa kiza, hofu kubwa ikiwa imetanda katika nafsi yangu kwa kufikiria tu uzito wa mkasa ule.
Sikuwa na hakika kama padre Backhove alikuwa hai au la kwa moto na mweleka ule. Hata hivyo, hakika niliyokuwa nayo ni kwamba alikuwa ameathirika sana kimwili na kisaikolojia. Kwa vyovyote vile kama angenitia mkononi adhabu ambayo ningeipata isingekuwa kifani. Wazo ambalo lilinifanya nisahau kabisa ndoto ya kurudi shuleni pale na kuomba msamaha.
Zaidi ya hayo, hata kama ningerudi na kusamehewa ningeishi maisha gani shuleni pale bila kuwa kituko na kichekesho kwa kila mtu kwa miaka nenda miaka rudi? Sikuwa radhi kwa hilo.
Halafu, hata kama ungetokea muujiza nirejee shule na yote mengine yasahauliwe, jambo moja tu lisingeweza kusahauliwa kamwe. Hirizi. Kwa vyovyote vile msamaha wangu na kutakasika kwangu kungeendana na kuiteketeza hirizi ile hadharani, hirizi ambayo ni urithi wangu pekee! Kiungo cha mwisho kati yangu na familia yangu!
Mara nikaikumbuka hirizi hiyo! Iko wapi? Nilijiuliza nikitia mkono wangu mfukoni kuitafuta. Haikuwemo. Nilikagua mifuko yangu yote na kujipapasa mwili mzima, wapi. Hirizi yangu ilikuwa imepotea, bila shaka katika zile purukushani za kukimbia!
Nilihisi nikiishiwa nguvu. Kwa muda nilipoteza mapigo kadhaa ya moyo, huku macho yakiingia kiza. Hirizi yangu ambayo ilikuwa kila kitu maishani mwangu. Hirizi ambayo ilisababisha nipoteze kila kitu maishani mwangu! Imepotea!
Wanasema binadamu katika uhai wake, anaweza kufa kidogo! Kama madai hayo ni ya kweli basi mimi Petro Kionambali, siku hiyo, chini ya mti ule wa mvule nilikufa kidogo.
Na hata pale uhai uliponirejea sikuwa mtu yuleyule tena. Sikuwa na pa kwenda. Nisingeweza kurudi Kashozi kwa mzee Buberwa na kumsimulia kuwa nimeshindwa shule kwa ajili ya hirizi. Kadhalika, nisingeweza kurudi kwetu Buha na kumwambia babu na wazazi wangu kuwa nimeacha shule kwa ajili ya hirizi ambayo haipo tena. Shule nako kusingeendeka. Iko wapi hirizi tuichome? Ningeulizwa kabla ya mengine yote. Imepotea! Lingekuwa jibu langu. Nani ambaye angeniamini? Zaidi nani ambaye angenithamini? Haikuwepo namna.
Ghafla nikajiona yatima. Hapana, nilikuwa mwana mpotevu, asiye na mbele wala nyuma.
Nikainuka na kujitazama. Tayari nilikuwa kijana mrefu kuliko watu wote katika familia yangu. Nilikuwa mwembamba lakini mkakamavu. Mikono yangu ilikuwa na nguvu, miguu yangu ikiwa na uwezo. Zaidi ya kaptula, shati na viatu nilivyovaa sikuwa na chochote mkononi wala mfukoni mwangu. Nilikuwa masikini. Lakini nilijiamini. Afya yangu, elimu yangu na ari yangu vilifanya niamue jambo moja; sirudi kwetu wala sirudi shule. Nitapiga mguu, kutafuta maisha upya. Hata kama nitafika mwisho wa dunia!
* * *​
Nilipiga mguu kuelekea Kanazi. Nilifika usiku sana. Kwa kuhofia kuwa habari zangu zilishafika hapo nililala porini, juu ya mti. Alfajiri nilianza tena safari. Kiguu na njia hadi Muhutwe. Hapo niliomba hifadhi kwa wavuvi waliokuwa wamejenga vibanda vyao pwani. Hawakuwa na hiyana, ingawa mavazi ya shule niliyoyavaa yalifanya wanishuku kuwa nimetoroka shule. Sikukosa uwongo wa kuwaambia hata mashaka juu yangu yakaisha.
Katika elimu yangu fupi shuleni nilikuwa nimepata ufahamu wa kutosha wa Jiografia. Baada ya kughairi kurudi kwetu au kwenda kwa mzee Buberwa niliamua kwenda nchi ya Wasukuma. Mengi yalikuwa yakizungumzwa juu ya nchi hiyo ambayo nilitamani kuyaona kwa macho.
Zilikuwepo hadithi za Msukuma aliyeitwa Ng’wanamalundi ambaye alisemekana kuwa mganga aliyewashinda wachawi wote kwa kutumia ngoma zake. Mtu huyo wa miujiza alisemekana pia kuwa alikuwa na macho yenye nguvu za ajabu, ambayo yaliweza kukausha miti na hata binadamu aliowakazia macho, jambo lililopelekea awe akitembea huku akiwa amejifunga kitambaa usoni kufunika macho yake. Mtu huyo alidaiwa kuwa katika moja ya hafla zake alipata kukausha msitu mkubwa na mamia ya watu waliokuwa mbele yake. Jambo hilo liliifanya serikali ya mkoloni imkamate na kumhukumu kunyongwa. Lakini hakuna aliyethubutu, kwani kabla ya hukumu hiyo kutekelezwa alifungwa katika kimojawapo cha visiwa vidogovidogo vilivyo baharini katika pwani ya Bahari ya Hindi, huko Dar es Salaam. Hata hivyo, ilielezwa kuwa Ng’wanamalundi huyo kila jioni alionekana katika vilabu vya pombe Dar es Salaam akiwa amevuka bahari kwa kutembea juu ya maji. Wakoloni wakalazimika kumwachia.
Sifa nyingine ya nchi ya Wasukuma ni zile hadithi kuwa kulikuwa na milima ya mawe, ama majini ama nchi kavu. Baadhi ya milima hiyo ilielezewa kuwa ilikuwa katika maumbile ya binadamu, ikiwa imesimama miaka nenda rudi kama inayosubiri mwujiza fulani utokee, ili ipate uhai na kuanza kutembea kama binadamu wengine.
Nchi hiyo pia ilikuwa ikisifiwa sana kwa ukubwa wa ardhi na wingi wa rutuba yake. Kilimo cha mazao ya chakula na yale ya biashara kama pamba na katani kilielezewa kuwa hakikupata kumtupa mtu. Kwa bahati mbaya, mimi sikupata kuwa mkulima wa haja. Wala sikuona kama ningeweza kuwa na ustahimilivu wa kulima leo kusubiri mavuno miezi au miaka kadhaa baadaye. Mimi nilikuwa mtu wa maji. Mtu wa kutupa nyavu na kuzitupa huku tayari zimejaa samaki! Hivyo, sababu kubwa iliyonipa msukumo wa kutamani kufika huko hasa lilikuwa ziwa. Jiografia yangu ilionyesha kuwa Wahaya na Wasukuma walichangia ziwa hili. Wakati Wahaya wakiwa Magharibi wakilitumia kwa shughuli zilezile.
Kwa kuzingatia hali yangu ya kutokuwa na kazi wala ujuzi wowote wa kuweza kupata ajira nyingine nililichukulia ziwa hili kuwa mkombozi wangu pekee. Nilitegemea ziwa liniajiri, linilee, kwani taaluma ya uvuvi niliyoipata katika likizo zangu ilitosha kabisa kunipatia ajira hiyo.
Ni kwa mtazamo huo ndipo nilipojikuta nikijiunga na vikundi mbalimbali vya uvuvi kwa lengo la kujipatia fedha. Siku zote za uvuvi wangu nilifuata ziwa kuelekea upande wa kushoto kwangu badala ya upande wa kulia. Kama ningeelekea kushoto, ningelazimika kufika Uganda na baadaye Kenya, kabla ya kuingia Tarime, Musoma, Bunda hadi kufika Mwanza. Ingekuwa safari ndefu isiyo na sababu yoyote.
Mimi nilielekea kulia. Nilivua katika pwani na visiwa mbalimbali kama Bambire, Iroba, Rubondo na Nyamiende. Ilikuwa safari ndefu na ngumu sana. Takribani mwaka mzima uliishia njiani. Ama nilikwamishwa na ukosefu wa majahazi yanayoelekea huko nilikokuwa nikielekea, ama upepo mkali wa siku kadhaa ziwani ulifunga kabisa njia. Msimu wa masika ulioambatana na mvua kubwa za radi na mingurumo ya kutisha ni miongoni mwa sababu nyingine iliyonichelewesha njiani. Nililazimika kusubiri kwa zaidi ya miezi minne katika kijiji fulani huko Biharamulo.
Urefu huo wa safari ulikuwa na faida moja. Kwanza, ulinipa fursa ya kupata ukomavu na uvumilivu mkubwa katika pilikapilika za ziwani na nchi kavu. Ningeweza kuvumilia mvua ya siku mbili au tatu ikinipiga mwilini, niliweza kustahimili jua kali linalochoma kama mkaa wa moto. Niliweza pia kuipuuza njaa kwa muda mrefu. Zaidi, mwili wangu ulijenga uwezo mkubwa wa kuyashinda maradhi madogomadogo kama homa au tumbo bila haja ya kutumia dawa za madukani au mitishamba tele niliyopata kuelekezwa na babu.
Faida nyingine kubwa niliyoipata kutokana na urefu wa safari hiyo ilikuwa udugu. Nilikutana na watu mbalimbali, nikashirikiana nao kwa hili na lile na kujikuta nimepata ndugu na marafiki tele, ambao kila nilipoondoka kuendelea na safari yangu walisikitika sana, lakini haikuwa kabla ya kunitakia kheri na baraka za safari.
Nilikosa raha kiasi pale tulipofika kisiwa cha Kome tukikaribia kabisa Mwanza. Rafiki zangu hao walishauri tubadili mwelekeo na kwenda kwanza Ukerewe. Tulifika Nansio. Tukafanya shughuli zetu za uvuvi hapa na pale, katika kijiji hiki na kile hadi tukajikuta tumeingia katika kisiwa kingine kidogo kiitwacho Ukara.
Ulipata kuona au kusikia juu ya mawe yanayocheza muziki? Kama hujapata hata kusikia mwenzio niliyaona kwa macho yangu katika kisiwa hicho cha Ukara. Kisiwa hicho kina mawe yaliyokaa kiajabu ajabu. Mtu anaweza kufikiria kuwa yalipangwa na binadamu, kwani baadhi yako juu ya mengine, yakiwa yamegusana kwa sehemu ndogo sana lakini hayadondoki si kwa mawimbi wala dhoruba la ziwani. Nilikuwa nikiyakodolea macho mara kwa mara mawe yale hadi mwenzangu mmoja aliposema, “Unashangaa kuyaona yalivyokaa, jee ukiyaona yanacheza?”
Nilidhani ni mzaha. Tulipobishana jamaa hawa walinipeleka katika kijiji cha Kome, ambako tulipata mwenyeji aliyetupeleka eneo la Kululibha yalipo mawe haya ya ajabu. Mwenyeji wetu alitoa amri kwa lugha yake ya Kikara. Mara mawe hayo yakaanza kucheza kama watoto mapacha moja juu ya jingine. Hadi leo sijui ni kitu gani kilichotokea hadi mawe hayo yamtii binadamu.
Lakini huo si muujiza pekee wa Ukara. Pale kijijini kuna kisu chenye makali pande mbili. Unapotokea uhalifu wa aina yoyote watuhumiwa hupelekwa kwa mtaalamu na kuamriwa kukalia kisu hicho. Lakini si kwa mhalifu. Yeye hukatwa mara moja, hata awe amevaa nguo nzito kiasi gani. Kwa yale niliyoyaona, ya mawe kucheza, sikuwa na ubishi wowote kwa jambo hilo.
Maajabu mengine ambayo niliyaona kwa macho yangu, ni mti mmoja kijijini Chilabi huko Ukara. Mti huo ulipigwa na radi ukang’oka. Wenyeji wakaanza kujipanga ili waupasue mbao na kuni. Wakati kabla kazi hiyo haijaanza, mti huo ulisimama na kuota tena palepale ulipokuwa awali. Hata hivyo, haukuwa na majani. Mti huo upo hadi leo. Niliutazama, nikaupapasa. Unaonekana mkavu lakini unaishi.
Maajabu hayo yalifanya tulipoanza tena safari ya Mwanza niwe nimechangamka zaidi.
 
Sikuonana na Chifu hadi baada ya siku tatu. Zikiwa siku za kula vizuri, kulala vizuri na kupumzika, huku tayari nimepewa nguo na viatu vipya, nywele zangu zikiwa zimekatwa vizuri, nilimwona Chifu akinitazama kwa makini kabla ya kutikisa kichwa kama alivyofanya mkewe na kisha kutabasamu.

Nilikuwa nimepelekwa kukutana naye katika ‘Ikulu’ yake, chumba kikubwa chenye viti vipatavyo mia moja vilivyoelekea kwenye kiti chake cha enzi, ambacho kilichongwa kwa mbao za mpingu na fundi anayejua kila aina ya nakshi. Sehemu kubwa ya kiti hicho kilimeremeta kwa aina fulani ya mawe ambayo baadaye nilikuja kufahamu kuwa ni almasi.
Chifu alikuwa amekikalia kiti hicho, mimi nikiwa nimesimama wima mbele yake. Tulikuwa wawili tu chumbani humo baada ya walinzi ambao huwa wako nyuma yake siku zote kuamriwa kuondoka.

“Karibu mwanangu!” Chifu alitamka baada ya kunitazama kwa muda mrefu. “Karibu katika himaya ya Masanja mwana Kasanga, Msukuma halisi aliyewashinda wavamizi na wahamiaji wote. Jisikie uko nyumbani.”
Nilitikisa kichwa kumkubalia ingawa nilikuwa sijamwelewa.

“Hata hivyo, ningependa kukufahamu vizuri, wewe ni nani, kabila gani, ulikuwa ukitokea wapi na kwenda wapi kabla vijana wangu hawajakuleta hapa?” Chifu aliniamuru. Sauti yake ilionyesha upole na upendo kama ya mkewe. Ikanitia moyo.

Nilieleza ukweli juu ya kwetu, Buha, ambako nilizaliwa na kukulia. Kwa hofu kuwa ule mweleka ulikuwa umemwua padri Backhove na kwamba habari za kifo chake zilikwishawafikia huku, nilidanganya juu ya maisha yangu ya elimu. Nilimwambia Chifu kuwa ingawa nilifuata elimu huko kwa Wahaya niliishia kuvua samaki katika ziwa kwa kukosa mtu wa kunisomesha.

Kwa mshangao wangu habari hiyo ilimfurahisha sana Chifu. Alipotabasamu, akacheka kabla hajakohoa kwa kupaliwa na kicheko chake. Baadaye alisema, “Mungu amekuleta nyumbani, upate elimu uliyokuwa ukiitafuta. Utasoma shule ya watoto wa Machifu. Kama ubongo wako unachemka barabara utafika hadi Ulaya. Utakuwa Cheyo lakini Cheyo ataendelea kuwa Cheyo.”

Sikumwelewa. Nikamtumbulia macho ya mshangao na kutoamini, macho yaliyojaa maswali ambayo Chifu aliyaona na akaamua kuyajibu, “Nitakuibia siri moja. Nataka ibakie siri, kati yangu na wewe tu. Unaweza kutunza siri?”
Nilikubali.

“Pamoja na umri huu,” Chifu alisema. “Pamoja na kuwa na wake tele hadi leo nimejaliwa kupata mtoto mmoja tu, wa kiume. Anaitwa Cheyo. Tena ana umri kama wako.” Alisita kidogo kabla hajaongeza, “Himaya yangu iko mashakani. Nikifa himaya itapotea mali zangu zitaparanganyika. Hivyo, walipokuja wazungu kutaka kumchukua mwanangu huyu wa pekee ili wampeleke nchi ya mbali akapate elimu, naona tukio hilo litaiweka mashakani zaidi himaya yangu. Nani atarithi Ufalme wangu?”

“Na hata kama akirudi, akiwa amepoteza maadili ya utawala na mila za kabila langu na kuambulia tamaduni za mila za wageni nitakuwa nimejiweka katika nafasi gani?” Chifu alihoji na kuishia kujijibu mwenyewe, “Hapana. Nimekataa. Cheyo ni mwanangu. Nitamlea na kumfundisha mwenyewe. Sitaki kuchekwa na Machifu wenzangu wenye watoto lukuki.”
Alisita kwa muda akiwa amejiinamia. Alipoinuka alinikazia macho, “Mwanangu,” akasema “Ni hapo unapoingia katika familia. Kama kweli unataka elimu, kama kweli unaweza, nitakupeleka wewe badala yake. Utatumia jina langu na hadhi yangu. Utalelewa kwa upendo na amani maisha yako yote, kama mtoto wangu wa damu.”

Alinikazia tena macho, kwa muda mrefu kama anayejaribu kuusoma moyo wangu. Kisha akaniuliza taratibu, “Unasemaje?”

Niseme nini? Kwanza sikulitegemea swali hilo. Lakini sikutegemea kabisa kuwa matokeo ya kutekwa kwangu majuzi yangekuwa habari njema kama hiyo. Shule! Ni kitu nilichoondokea kukipenda kuliko chochote kile katika uhai wangu. Jambo lililofanya nishindwe kuamini iwapo nilichokuwa nimesikia ilikuwa ukweli au niko ndotoni. Niseme nini? Sikuwa na la kusema zaidi ya kuhisi machozi ya furaha yakinitoka na kuteleza juu ya mashavu yangu. Nilijaribu kuyafuta kwa mkono wangu ambao pia ulikuwa ukitetemeka.
Chifu hakuhitaji sauti yangu kupata jibu langu. Alielewa. Akainuka na kunikumbatia. “Hutajutia uamuzi wako. Naapa…” alininong’oneza.

Siku mbili tatu zilizofuata zilikuwa za maandalizi ya safari. Niliandaliwa vizuri sana kwa kufundishwa historia ya ukoo na majina ya mababu zao, ambao walikuwa wangu pia. Nilitakiwa kukariri majina hayo pamoja na mambo mengine tele ya kifamilia, kiukoo na kikabila. Haikuwa kazi rahisi.

Kiafya niliandaliwa pia. Ilikuwa nile mayai sita, kuku mmoja, ugali au ndizi za kutosha na kunywa kibuyu kimoja cha maziwa kila siku. “Ili ukifika pale ufanane na mtoto wa Chifu,” mzee Masanja alisisitiza. Amri hiyo iliambatana na kulala mapema, kuoga mara mbili kutwa, kuchana nywele zangu na kujipaka mafuta ya mgando mwili mzima. Hilo liliambatana na kununuliwa nguo za maana, viatu vya bei, mfuko wa safari na noti ya shilingi kumi ambayo Chifu alisema ni ya ‘kulinda mfuko.’

Matokeo ya kazi hiyo yalimshangaza kila mtu, ikiwa pamoja na mimi mwenyewe. Liliibuka dume lililopanda juu, lenye maungo yenye nguvu na afya tele, dume ambalo ile sura ya hofu na mashaka ilitoweka, nafasi yake ikachukuliwa na sura ya ucheshi, iliyojaa matumaini. Sura ya Mtanganyika halisi, aliyependwa na kupendeza kwa kila aliyemtia machoni. Sura ya Mtukwao au Petro mwana wa Karimanzira, mjukuu wa Kionambali. Hapana, sasa nilikuwa Cheyo mwana Masanja mwana Kasanga!

Nilikuwa mimi yuleyule, lakini mpya! Msomi mtarajiwa!
Pamoja na maandalizi hayo ya kusisimua, kitu kimoja kilikuwa kikisumbua sana akili yangu. Toka nilipokuja katika familia hiyo na kupewa nafasi ya kuwa mwana familia na fursa ya kupata elimu sikuwa nimebahatika kukutana ana kwa ana na mrithi halali wa familia, ambaye nafasi yake ya elimu nilielekea kuipokonya. Ningependa sana kumwona mtu huyu. Nijue ni mtu wa aina gani kitabia na kimaumbile. Lakini zaidi ningependa kujua msimamo na fikra zake juu ya uamuzi wa baba yake wa kumnyima fursa ya elimu ili awe mrithi na Chifu wa baadaye wa eneo hili.
Nilipata kumuuliza Chifu juu ya hilo, iwapo mwanawe ameridhia maamuzi hayo au la, lakini, kwa mshangao nilimwona Chifu akionyesha dalili za kukasirika kabla hajanijibu kwa mkato, “Yule ni mwanangu. Atafuata matakwa yangu,” jibu ambalo lilinitia mashaka zaidi.

Nilipopata wasaa nilimuuliza bi mkubwa juu ya jambo hilo. “Ni kweli mwanao hataki shule. Ni kweli atafurahi akisikia kuwa nakwenda kule kutumia jina lake na nafasi yake kujipatia elimu? Halafu yuko wapi mbona hajaonekana?”
Mama Chifu alinifumbua macho kidogo. Alisema, “Cheyo alikuwa anapenda shule. Hiyo sio siri. Lakini anatupenda zaidi wazazi wake. Hawezi kututupa kwa ajili ya kujua kusoma na kuandika. Alikubaliana na baba yake na ameachana na ndoto zote za kwenda shule. Amejiandaa kuja kuchukua nafasi yake mara Mungu atakapomchukua baba yake.”
“Yuko wapi?” nilimuuliza.

Nilimwona mama akisita kidogo. Baadaye alisema, “Nitakuibia siri. Chifu amemficha, hadi suala hili litakapokwisha.”
“Amemficha wapi?” nilisisitiza.

“Amemsafirisha. Yuko Misungwi kwa wajomba zake. Watamrudisha hapa mara wewe utakapoondoka na kuingia shule ili Wazungu waache kutuma matarishi wa kumtaka Chifu apeleke mtoto wake shule.”
Kiasi nilifarijika, walao kwa kuelewa ukweli.

Hata hivyo, usiku wa kuamkia safari yangu mashaka yangu yaliibuka pale mmoja wa wajomba hao wa Misungwi alipofika kwa Chifu akiwa na taarifa ambayo ilimchanganya Chifu mwenyewe na kila mtu katika familia hiyo. Kwamba Cheyo alikuwa ametoweka kwa wajomba zake na hajulikani aliko!

Chifu aliduwaa. Alimtolea shemeji huyo macho makali, yaliyojaa hasira. “Kwa nini hamkumwangalia?” alifoka. “Mtafuteni, arudi hapa!” aliamuru.
 
KWA ANAYEKIHITAJI KITABU HIKI CHA KIGUU NA NJIA NA VINGINE VYA BEN MTOBWA KAMA DAR ES SALAAM USIKU, SALAMU TOKA KUZIMU, TUTARUDI NA ROHO ZETU NA VINGINE VINGI, NITAFUTE KWA KUPITIA 0712504985 AU 0763044459. KARIBUNI.
SURA YA SITA
Kwa treni hadi Tabora
Safari ya Mwanza hadi Tabora ilikuwa ya kusisimua sana. Ilikuwa safari yangu ya kwanza maishani kusafiri bila kutumia nguvu za miguu au mikono yangu. Toka Kigoma hadi Kagera hadi Mwanza nilitumia mikono au miguu yangu. Toka Kigoma hadi Kagera hadi Mwanza nilitumia mikono yangu kupiga makasia hadi tulipowasili majuzi. Safari hii kazi yangu ilikuwa kukaa kitako, kando ya dirisha, huku macho yangu yakifaidi kilometa zote 453 za safari kwa kuburudishwa na mazingira aina aina.
Tulisafiri kwa aina mpya ya usafiri iliyotambulishwa nchini na utawala wa Mjerumani, gari moshi. Ujenzi wa reli, vyuma imara ambavyo vilitumiwa na gari moshi hiyo kuteleza juu yake, ambao ulianza huko Darisalama mwaka 1912 uliweza kufika Mwanza 1923, ikiwa moja ya matawi ya reli hiyo lililoanzia Tabora. Reli hiyo, maarufu kama reli ya kati inayokata nchi toka mashariki hadi magharibi na toka kaskazini hadi kusini inakadiriwa kuwa na urefu wa kilomita 2600. Ni moja kati ya kumbukumbu za utawala wa Mjerumani, ambazo kamwe hazitafutika katika historia ya nchi hii.
Reli hii ni kiungo pekee muhimu kinachoiunganisha nchi toka bahari ya hindi kwa upande mmoja hadi ziwa la Tanganyika kwa upande wa pili, jambo linaloifanya iwe tegemeo kubwa kwa usafirishaji wa watu na mizigo si kwa nchi yetu pekee bali pamoja na zile za Burundi, Kongo na Rwanda pia.
Licha ya sababu hizo za kiuchumi reli ilikuwa pia mshirika mkubwa katika masuala ya kiutamaduni na kijamiii nchini. Kwanza iliwezesha makabila yapatayo mia na ishirini ya Tanganyika kufahamiana kwa urahisi. Mzaramo wa pwani angeweza kukutana na Mmanyema wa Kigoma, au Mchaga wa Kilimanjaro kufahamiana na Mfipa wa Mpanda kwa urahisi zaidi ya siku zile za akina Livingstone kutumia miaka maporini toka pwani ya Bahari ya Hindi hadi pwani ya ziwa Tanganyika.
Na hilo halikuwa kwa makabila ya ndani tu. Ujenzi wa reli hiyo ulimfanya mkoloni wa Kijerumani alete vibarua wengi wa kazi hiyo toka nchini India. Hawa ni chanzo cha msamiatai wa ‘kuli’ neno lililozaliwa kutokana na lile la kiingereza ‘Coolie’ wakatii huo likitumiwa kama kashfa kwa vibarua wasio na ujuzi wowote. ‘Kuli’ haikutofautiana sana na ‘manamba’ wa hapa nyumbani ambao walikamwatwa kwa visingizio mbalimbali kubwa ikiwa kushindwa kulipa kodi ya kichwa, na kupelekwa kufanya kazi za mikono katika mashamba ya mkonge kaskazini magharibi mwa nchi yetu.
Kuli’ wengi walitoka India, ama walinogewa, ama hawakuwa na uwezo wa kurudi kwao, ama yote mawili, wakaishia kuwa wakazi wa hapa. Leo hii jamii mpya ya akina Gulamali, Manji, Adamjee; na kadhalika inapatikana sehemu yoyote ya Tanganyika; hasa vijijini.
Jing – janga – jing – jang – jing - jang garimoshi lilihangaika kuvuta mabehewa sita wa abiria na manne ya mizigo yaliyofanya tuwe kama joka refu linaloteleza kwa kujikongoja. Injini ya garimoshi hilo, ambayo sikuhitaji kuambiwa kuwa ilikuwa ikitumia kuni kutengenezea mvuke wa kuiendesha ilikuwa ikitoa moshi mwingi na mzito sana. Moshi ambao ulilala juu ya treni kama wingu jeusi lisilopendeza machoni. Nadhani hiyo ni sababu pekee iliyowafanya waswahili waamue kuita usafiri huo wa ‘garimoshi.’
Nikiwa nimeketi raha mustarehe dirishani pangu nililitazama kwa masikitiko ziwa nililolipenda la Nyanza likitokomea machoni mwangu taratibu. Ziwa hilo lilinilea, lilinihifadhi na kunifadhili kwa muda wa kutosha. Ndilo lililonifundisha kuogelea na kutafuta pesa. Ziwa lililonitoa Kagera na kunifikisha Mwanza. Hilo ndilo ziwa ambalo leo naliacha bila kuwa na uhakika wa kuliona tena. “Nitarudi!” nilinong’ona taratibu.
“Nini?” jirani yangu, mzee wa makamo ambaye tulichangia kiti, alinihoji akidhani nazungumza naye.
Sikumjibu.
Tukapinda na kupenya katikati ya majabali marefu mfano wa milima. Tuliacha jabali moja baada ya jingine, mbuyu mmoja baada ya mwingine huku tukivuka vijito na mito ya hapa na pale.
Mara tukazama katika mapori na misitu mikubwa, kwa mbali tukawaona wanyama mbalimbali kama ngedere waliokuwa wakirukaruka kwenye miti au mbuzimawe ambao walirandaranda juu ya majabali ya hapa na pale. Katika eneo moja lenye mabwawa tuliwaona ndege aina ya flamingo wenye miguu mirefu na midomo myekundu wakiwinda samaki au wadudu ndani ya maji hayo. Ndege wengine, aina mbalimbali pia walikuwa wakiruka huku na huko kama wanaotushangaa au kutushangilia hadi tulipotokomea.
“Mantare!” Yule jirani yangu aliropoka.
Ikawa zamu yangu kumshangaa, “Nini?” nilimuuliza.
“Tumefika stesheni ya Mantare,” alifafanua.
Kweli. Nililiona garimoshi likipunguza mwendo na hatimaye kusimama kando ya nyumba mbalimbali ambazo zilionekana kuwa za wafanyakazi wa reli hiyo.
Palikuwa na purukushani fulani, watu wakipanda wengine wakishuka. Miongoni mwa watu hao walikuwepo pia wafanyabiashara wenye bidhaa mbalimbali kama vyakula, mapambo na mifugo. Walionunua walinunua, wasionunua tulijifanya hatuoni.
Tulisimama hapo kwa dakika kumi tu. Mara garimoshi hilo lilianza tena safari yake kwa mwendo wake wenye maringo, taratibu kama halitaki na baada ya kuchochea huku likikohoa kwa uzito wa mabehewa.
“Kwimba!” mzee aliropoka tena. Nilikuwa nimeanza kusinzia. Nikafunga macho na kuona tukiingia katika stesheni nyingine. Nikatoa kichwa dirishani na kuwatazama wanaoshuka na kupanda.
Tukaondoka.
Jirani yangu huyo alikuwa amejipa kibarua. Kila tulipokaribia kituo fulani nilimsikia akitamka kwa nguvu, “Malya,” kisha “Seke.” Sikufumbua macho yangu hadi pale aliponitikisa kwa nguvu huku akiniambia, “Amka tumefika Shinyanga!”
nilifumbua macho. Jina la Shinyanga lilikuwa na uzito wake katika kumbukumbu zangu. Hata hivyo, nilimwambia taratibu “Siendi Shinyanga. Nakwenda zangu Tabora.”
“Tabora! Kuna nini Tabora?”
Sikumwelewa, “Kuna nini Tabora?” nikamjibu kwa swali jingine. “Kwani Shinyanga kuna nini?”
Kumbe mzee alikuwa na hamu ya maongezi. Alianza kwa kutabasamu. Baadaye aliporomosha sifa za Shinyanga. “Kuna kila kitu ambacho binadamu anahitaji. Ardhi bora yenye rutuba tele. Misitu imejaa wanyama kila aina. Ng’ombe wa hapa wamenenepa na wanatoa maziwa mengi kuliko popote pale. Hata Wazungu wengi siku hizi wanatembelea milima yetu mara kwa mara. Kuna fununu kuwa huko ardhini kuna mali nyingi ambazo huko kwao ni utajiri mkubwa.”
Nilitabasamu lakini sikumjibu. Sikuwa na jibu la haraka.
“Enhe na Tabora?” alihoji.
“Tabora nini?” nilimuuliza.
“Kuna nini Tabora?”
Niliamua kumnyamazisha kwa kumpa kile ambacho nilikipata vitabuni, ambacho nina hakika kuwa alikuwa hakijui. “Tukianza na reli hii tunayoitumia sasa. Roho yake iko Tabora.”
“Kwa vipi?” alihoji akicheka.
“Tabora ni kituo pekee muhimu sana. Pale Tabora ndipo ambapo reli hii inajigawa, moja ikienda Kigoma, ambako inafika hadi ziwa Tanganyika linalotuunganisha na nchi za Kongo, Burundi na Zambia. Pia, kuna reli inayokwenda hadi Mpanda, kusini mwa nchi yetu.”
Wakati akitafakari hilo nilimpa la pili.
“Unaijua eropleni?” nilimuuliza.
“Ndege Ulaya!” alisema akicheka. “Sio naijua, nimeipanda mara nyingi.”
“Kutoka wapi kwenda wapi?” nilimuuliza kwa mshangao.
“Burma,” alinijibu. “Kwenye vita kuu ya kwanza nilikuwa mmoja wa wapiganaji tuliorushwa kwa ndege kwenda kusaidia wenzetu waliozingirwa na maadui,” alisita kidogo kabla ya kuniuliza, “Ndege ina uhusiano gani na Tabora?”
“Tarehe 22 Julai mwaka 1920 ndege ya kwanza kutua nchini Tanganyika ilitua katika uwanja wa ndege Tabora. Ndege hiyo ndogo ya Mwingereza iliruka toka Nairobi Kenya hadi hapa na kuweka historia ya pekee kwa nchi ya Tabora.
Mzee alicheka. “Hilo tu?” aliniuliza.
“Yako mengi, “ nilimjibu. “Yule kiboko wa Waarabu, Mtemi Milambo, aliishi katika ngome yake Iselemagazi iliyokuwa Tabora. Yule Mwingereza Davidi Livingstone aliyekataa kurudishwa kwao na akafia Zambia alipata kuishi Tabora kwa muda, kabla hajahamisha makazi yake Ujiji, Kigoma. Tabora ulikuwa mmoja kati ya miji michache nchini iliyokuwa na watu wengi, toka miaka ya 1700, mji mdogo huo?”
Mzee aliyatafakari maneno yangu. “kichwa chako kinafanya kazi vizuri sana, mjukuu wangu. Naweza kutabiri unakwenda Tabora kufanya nini.”
“Naenda kufanya nini?” nilimjaribu.
“Kusoma,” alinijibu. “Kweli au uongo?”
“Kweli tupu.”
Mzee akacheka kabla hajaongeza, “Naweza hata kukuambia jina la shule unayokwenda.”
“Shule gani?”
“Unakwenda Tabora School. Shule ya misheni inayopokea watoto wa machifu. Kweli au uongo?”
“Ni kweli,” nilimjibu kwa mashangao. “Umejuaje mzee?”
“Uzee dawa. Uzee ni kuona mengi ni kuona mbali. Jinsi ulivyovaa, jinsi ulivyotulia, jinsi unavyoongea, ni wazi kuwa wewe ni mtoto wa Chifu. Na nina imani kuwa utafika mbali katika safari yako ya maisha.”
Nilitamani kucheka, nilitamani kulia. Sikujua nifanye lipi katika hayo. Kwa mara ya kwanza, baada ya muda mrefu nikamkumbuka babu yangu, mzee Kionambali.
Mtoto wa Chifu!
 
KWA ANAYEKIHITAJI KITABU HIKI CHA KIGUU NA NJIA NA VINGINE VYA BEN MTOBWA KAMA DAR ES SALAAM USIKU, SALAMU TOKA KUZIMU, TUTARUDI NA ROHO ZETU NA VINGINE VINGI, NITAFUTE KWA KUPITIA 0712504985 AU 0763044459. KARIBUNI.

Tulifika Tabora siku mbili baadaye.
Stesheni ya Tabora ni sehemu moja yenye kila aina ya pilikapilika. Ilikuwa na watu wengi wenye purukushani hii na ile, huyu akihangaika kupanda behewa, huyu akishuka, yule akibadili behewa kuhamia lile, huyu akipiga kelele kuuza asali na bidhaa nyingine na kadhalika na kadhalika. Lakini purukushani kubwa zaidi ilikuwa ya magarimoshi yenyewe. Vichwa vilikuwa vingi mno, vikienda hapa au pale, kuhamia reli hii au ile huku vikicheua moshi na honi za mara kwa mara, hali iliyofanya pawe mahala ambapo mtu asingependa kukaa kwa muda mrefu.
Nilishuka, nikachukua mzigo wangu na kutoka nje ya stesheni. Huko nje kitu cha kwanza kilichovuta macho yangu ni wingi wa maembe. Barabara nzima toka stesheni hadi mjini zilizingirwa na miembe mikubwa, kila upande kwa namna iliyofanya iwe na kivuli murua cha kusisimua. Nilipiga hatua moja kwenda nyingine kuifuata barabara hiyo ya aina yake. Kila hatua ilinifanya nione kuwa wingi huo wa miembe haukuwa wa kando ya barabara pekee. Mapori yote ya mji yalitawaliwa na miembe mingi, mikubwa, ambayo baadhi ilikuwa na maembe yaliyoiva, ambayo yalionyesha kuwa watoto wa mji huo walishachoka kuyala.
Mji wa Tabora ulikuwa mdogomdogo, wenye nyumba za kawaida, ambazo hazikutofautiana sana na zile za Mwanza. Tofauti pekee kubwa niliyoiona ni mavazi na lafudhi. Kimavazi nilishangaa kuona watu wengi wakiwa wamevaa mavazi yenye asili ya Kiarabu, kanzu nyeupe na kiko mdomoni kwa wanaume na baibui jeusi lililofunika moja ya kumi ya mwili isipokuwa sehemu ndogo ya uso kwa wanawake. Katika mazungumzo yao nilibaini pia kuwa lafudhi ya wengi wao ilikuwa ya Pwani zaidi. Japo walizungumza kwa namna iliyofanya nihisi ama wanaibembeleza lugha ama inateleza kwenye ndimi zao.
‘Karibu Tabora mwanangu!’ nilijikaribisha.
Nikauliza njia ya kwenda shule ya Tabora School. Nikaelekezwa. Nikaifuata njia hiyo taratibu, mzigo mkononi, mluzi mdomoni, ndoto za mafanikio zikiwa tele moyoni.
Nilipokelewa na mlinzi nje ya geti la kuingilia shuleni. Nikajitambulisha kwake. Alinifungulia geti na kunielekeza iliko ofisi ya mkuu wa shule. Nilikwenda kwa mwendo wa kujiamini, huku nikiwa tayari nimetoa barua yangu ya utambulisho toka kwa ‘baba yangu,’
Chifu Masanja mwana Kasanga. Wanafunzi wenzangu tayari walikuwa madarasani. Niliweza kuwasikia baadhi ya walimu wakifoka kwa sauti kubwa katika jitihada za kujaribu kuingiza kitu fulani katika vichwa vigumu vya wanafunzi.
Karani wa mkuu wa shule alinipokea, akaipokea barua yangu na kuiingiza chumbani kwa bosi wake. Muda mfupi baadaye niliitwa katika ofisi hiyo.
Mkuu wa shule alikuwa Mzungu. Mtu mnene miraba minne, ambaye angefaa zaidi kuwa mwalimu wa ngumi badala ya taaluma. Nilimkuta kasimama nyuma ya meza yake, barua yangu ikiwa mkononi mwake. Alinikazia macho makali kwa dakika moja au mbili kabla hajatamka neno moja tu “Keti.” Nikaketi kwenye kimoja wapo cha viti viwili vilivyomuelekea mwalimu mkuu, miguu yangu ikianza kupoteza nguvu, mikono ikianza kutetemeka kwa sababu ambayo sikuifahamu.
“Barua yako hii?” alinihoji baadaye.
“Ndiyo.”
“Umeipata wapi?”
“Kwa nini? Nimepewa na Chifu… baba… nikuletee.”
“Chifu nani?”
“Masanja mwana Kasanga.”
Mkuu huyo wa shule alinitazama kabla hajaongeza swali jingine, “Unaitwa nani?”
Nusura nitaje jina langu halisi. “Cheyo,” nikatamka.
Nilimwona mkuu wa shule akizidi kushangaa. Mara akawa kama kakumbuka jambo. Akatoka na kumnong’oneza jambo karani wake. Kisha akarudi na kuketi. Muda mfupi baadaye mlango uligongwa, mwanafunzi mmoja akaingia na kuelekezwa kuketi kiti cha pili kilichokuwa wazi.
Mkuu wa shule alimkazia macho kama alivyofanya kwangu kabla ya kumuuliza, “Ulisema wewe ni nani, unatoka wapi na baba yako ni nani?”
“Naitwa Cheyo. Kwetu Mwanza. Mimi ni mtoto wa Chifu Masanja mwana Kasanga.”
Miguu yangu iliishiwa nguvu. Nilitamani ardhi ipasuke, inimeze yaishe. Ardhi haikufanya hivyo. Nikahisi nimeanza kutetemeka mwili mzima, jasho jembaba likinitoka.
Mkuu wa shule alikuwa akinitazama kwa makini.
“Nani anasema uongo, nani anasema ukweli kati yenu?” aliniuliza. “Juzi tu,” aliongeza. “Alikuja huyu kijana, akatuambia kwamba anaitwa Cheyo na ni mtoto wa chifu Masanja. Kwa maelezo yake baba yake hataki aje shule, anataka akae nyumbani kusubiri kurithi Uchifu wake atakapokufa. Kwamba amekuja hapa shuleni kwa kutoroka baada ya jitihada za kumsihi baba yake kumruhusu kushindikana. Na kwa jina na nafasi yake ilikuwa wazi bado tumempokea na kumruhusu kuendelea na masomo. Leo umekuja wewe. Unadai wewe ni Cheyo mtoto wa Chifu Masanja na una barua yake ya kuomba upokelewe hapa. Nataka kujua nani mkweli nani mwongo kati yenu,” aliniuliza akitutazama kwa zamu. Cheyo naye alishangaa. Akageuka kunitazama. Nilijitahidi kuinua uso wangu nimtazame pia, ilikuwa kazi ngumu kuliko zote nilizopata kufanya. Hicho kidogo nilichobahatika kuona katika uso wake kilionyesha wazi kuwa si kwamba hatufahamiani tu, bali pia tulikuwa hatufanani kwa namna yoyote ile. Pale ambapo mimi nilikuwa mng’avu yeye alikuwa mweusi tii, pale nilipokuwa mrefu yeye alikuwa mfupi na mwenye kiribatumbo.
 

Similar Discussions

14 Reactions
Reply
Back
Top Bottom