Riwaya: Kiguu na njia

Riwaya: Kiguu na njia

hii nimeipenda kwasababu nimepata historia yetu wapare japo kidogo
SURA YA KUMI NA SABA

Kilimanjaro, Paa la Afrika

Nilikuwa nimesikia mengi juu ya Kilimanjaro, mlima mrefu kuliko wote barani Afrika. Hali kadhalika, nilisoma mengi na kutazama picha nyingi zilizoonyesha mlima huo. Lakini katika yote hayo niliyosikia au kuona kwenye picha hakukuwepo lolote lililoniacha nisiweze kupigwa na butwaa huku nikiwa siyaamini macho yangu pale nilipoutia machoni mlima huu. Kwa kweli, ni mlima ambao lazima uuone, kusimuliwa pekee kulikuwa hakutoshi.

Ilikuwa ndio kwanza nashuka toka katika basi lililonileta mjini hapo, macho yangu yalipopokelewa na utukufu ule. Ujio wangu Kilimanjaro ukiwa umefanyika bila matarajio baada ya yale mapokezi ya kutisha niliyoyapata Singida. Mapokezi ya kulazwa chumba kimoja na fisi.

Ni mawazo hayo yaliyofanya Singida kama nuksi nyingine iliyokuwa ikinisubiri. Hali iliyopelekea baada ya siku mbili tatu za kuzurula mjini hapo nipande basi lililonileta Kilimanjaro, kwa matarajio ya kupata kazi au biashara yoyote ambayo ingeniwezesha kupata chochote ili nitimize azma yangu ya kurudi nyumbani. Azma ambayo umuhimu wake uliongezeka siku baada ya siku.

Mlima ulisimama pale kwa kiburi na fahari zote. Ulikuwa peke yake, ukiwa umechomoza hadi juu ya mawingu, kiasi cha kujionyesha vizuri popote uliposimama katika eneo la miji kama Moshi, arusha na vitongoji vyake. Ukiwa umepambwa kwa theluthi iliyokuwa ikimeremeta kileleni, Kilimanjaro ulisimama pale, peke yake, kama mfalme aliyevalia taji lake ambaye hakuwa na mpinzani. Hapana, alionekana zaidi kama malkia mwenye majivuno, aliyevalia mapambo yake yote, ambaye hakupenda kujichanganya na watu wengine. Sijui ningeukodolea macho kwa muda gani mlima huo kama nisingehisi kushikwa bega huku sauti ya mtu mmoja ikisema, “Angalia, yasije yakakukuta yaliyomkuta Rebmen kwa kuushangaa mlima huo.”

Nikazinduka. Nikayaondoa macho yangu toka kileleni na kumtazama msemaji. Alikuwa mpita njia tu, mvulana aliyevaa mavazi ya shule, mfuko wa madaftari yake ukiwa kwapani. Alikuwa akitabasamu.

“Rebmen gani?” nilimuuliza.

“John Rebmen. Yule Mjerumani aliyekuwa Mzungu wa kwanza kuutia machoni mlima huu,” alifafanua.

Nikalikumbuka jina hilo. Nikakumbuka pia tarehe na mwaka ambao Rebmen aliuona mlima huo kwa mara ya kwanza. Ilikuwa Mei 11, 1848.

“Rebmen alifanya nini?” niliuliza.

“Hukumbuki?” mwanafunzi huyo alinihoji. “Hukumbuki yaliyompata? Hukumbuki kuwa aliibiwa mfuko wake uliokuwa na fedha zake, nyaraka zake na kumbukumbu zote za safari yake? Ulivyokuwa umeduwaa pale wewe pia ungeweza kuporwa huo mfuko wako bila kujijua”

Nikacheka. Nilikumbuka kusoma tukio hilo kwenye kitabu cha mwandishi mmoja. Nadhani alikuwa Rebmen mwenyewe aliyeandika. Kwamba akiwa Kilimanjaro, maeneo ya kibosho, aliibiwa mfuko wake uliokuwa na fedha zake zote na nyaraka zake zote muhimu. Siku hizi watani wa Wachaga, hasa Wapare, hulitumia tukio hilo kuwadhihaki Wachaga kuwa kwa ajili ya tukio lile Rebmen aliyekuwa mmisionari aliwalaani hata wakawa watu wa kupenda na kuabudu sana pesa kuliko utu. ‘Mchaga mzuri ni aliyekufa tu,’ ni moja ya kauli zinazoendana na utani huo.

Ingawa sikumbuki kama kweli Rebmen aliibiwa wakati akiushangaa mlima lakini bado nisingeweza kumlaumu. Kwa mtu kama yeye, aliyetoka mbali sana na ambaye hakupata kusikia wala kuona picha ya mlima huo kama mimi, kuduwaa kiasi cha kuibiwa begi lake kamwe lisingekuwa jambo la ajabu. Kitendo cha ardhi kuchomoza hadi meta 5894 juu usawa wa bahari, huku ukiwa umesimama peke yako siyo jambo la kawaida. Aidha, ile theluji kileleni na historia ya milipuko ya volkano katika vilele vyake vitatu vya Kibo, Mawenzi na Shira ni sababu nyingine za kihistoria ambazo zitamfanya mtazamaji aukodolee macho hata kuweza kuporwa begi lake.

Hata hivyo, kauli ya mtoto yule wa shule ilinifanya nianze tena kutembea mitaani, begi mkononi, macho yakiwa hayakomi kurudi kwenye kilele cha mlima mara kwa mara.

Mji huu wa Moshi, ulio mbali kwa kilomita 580 toka Dar es Salaam na 76 toka Arusha, uko kilomita 890 toka usawa wa bahari. Hesabu ya watu wa mwaka 1948 ilionyesha kuwa mkoa mzima wa Kilimanjaro ulikuwa na idadi ya watu wapatao 267,700.

Hiyo ilikuwa sehemu ya akiba yangu ya kumbukumbu juu ya Kilimanjaro. Sehemu nyingine ilikuwa juu ya mkazi mkuu wa mkoa huo, Mchaga. Wakati watu wengi walifahamu kuwa Wachaga ni kabila moja, linaloongea lugha moja, mimi nilikuwa na taarifa tofauti. Wakiishi kusini mwa mlima Kilimanjaro Wachaga ni mkusanyiko wa makabila mbalimbali, wanaozungumza lugha mbalimbali wakiwa wametoka katika maeneo mbalimbali kwa nyakati mbalimbali. Watu hawa, ambao kwa bahati wote ni wabantu, baadhi yao wanafananishwa na Wakamba wa Kenya kwa siha na lafudhi. Wengine wanafananishwa na wataveta na hata watu wa Niger na Kongo. Wataalamu wanahisi watu hawa walivutwa na hali ya hewa, mbali na utajiri wa misitu kwenye mteremko wa mlima tangu karne ya kumi na saba. Hali iliyowawezesha kuwa wakulima wakubwa wa mibuni kama zao la biashara na migomba kwa ajili ya chakula.

Miongoni mwa makabila yanayounda Wachaga ni pamoja na Warombo, Wamachame, Wavunjo na Wamarangu. Inaaminika kuwa katika zama zile za kuhamia Kilimanjaro makabila haya, ambayo yalikuwa na falme tofauti kama zilivyo lugha na tamaduni zao walipigana vita mara kwa mara. Kabila jingine maarufu Kilimanjaro, Wapare, lilitumia fursa hiyo kwa manufaa yao kiuchumi. Inaaminika Wapare walikuwa wafua vyuma mashuhuri ambao koo mbalimbali za Wachaga ziliwategemea kuundiwa silaha mbalimbali kama mikuki mishale na mapanga kwa minajili ya kujipatia ushindi dhidi ya koo nyingine.

Nilijikumbusha hayo wakati nikitembea taratibu toka kituoni hapo nikifuata barabara ambayo sikuifahamu, wala sikuwa na haraka ya kuifahamu. Nilikuwa nimejikumbusha nguo zangu za kazi, kaptula na shati la kaki murua ya Marekani, viatu vizito vya dhoruba na soksi nyeusi. Nywele zangu, kama kawaida, zilikuwa fupi zilizochongwa vizuri. Nadhani nilionekana mrefu kuliko watu wengi eneo hilo. Nadhani pia ngozi yangu ya maji ya kunde, usafi wa mwili wangu na utulivu wangu wakati nikivuta hatua moja baada ya nyingine kutoka kituoni hapo ni miongoni mwa vitu vilivyovutia macho ya wapita njia dhidi yangu. Niliona nikitazamwatazamwa kuliko kawaida, baadhi ya watu walinong’onezana huku vidole vikielekezwa kwangu.

Halafu likatokea jambo ambalo halikupata kutembelea fikra zangu. Kundi kubwa la kinamama liliibuka toka mahala fulani kituoni hapo na kunifuata mbio. Waliponifikia walianza kuimba huku wakipiga makofi na vigelegele.

Babaaa baba huyoo….

Babaa baba huyo…. Baba…


Sikuelewa. Nilisimama na kugeuka huku na huko nikitazama nani anapokelewa na kushangiliwa kiasi hicho.

Hakuwa mwingine zaidi yangu. Walikuwa tayari wamenizingira, mfuko wangu ukapokonywa na mama mmoja kuamua kuubebea yeye. Waliendelea kuimba.

“Karibu sana baba,” mmoja wao alisema huku akinikumbatia.

Nilizidi kuchanganyikiwa. Ama wana wazimu ama mimi napata wazimu! Niliwaza nikijaribu kujibabadua toka katika mikono ya mama huyo.

“Vipi… kuna nini?” nilijaribu kuuliza. Sikusikika. Kelele zilikuwa nyingi. Yule aliyenikumbatia kwanza aliwageukia wenzake na kuwaambia, “Mnaona? Niliwaambia ni mtu mwenye haya sana.” Akawageukia vijana wa kiume waliokuwa kando na kuwauliza, “Mbona hamchangamki? Mpokeeni kishujaa shujaa wetu.”

Kauli hiyo ilifuatiwa na vijana hao wa kiume kunivamia, wawili kati yao wakaniinua na kunibeba juu wakiniongoza njia kunipeleka walikokujua. Katika maongezi yao nilisikia mmoja akisemea, “Nilidhani Nyerere ni jitu kubwa, linalotisha na kuwatetemesha wakoloni. Kumbe ni mtu wa kawaida…”

Ndipo nikaelewa. Walikuwa wamenifananisha na Nyerere!

Wakati huo vuguvugu la kudai uhuru likiwa linazidi kupamba moto majina ya akina Julius Nyerere, Oscara Kambona, Bibi Titi Mohamed na wengineo yalikuwa yametawala sana katika vyombo vya habari. Nyerere, ambaye wakati huo alikuwa mwalimu wa shule moja ya sekondari kule Tabora alifahamika zaidi kutokana na maandishi yake katika vyombo vya habari hasa magazeti akiwa msomi aliyefika hadi Makerere, Uganda. Nyerere aliwaandaa Watanganyika kujitawala. Alisema na alisikika sana.

Sikupata kufikiria kama ingetokea siku mimi, Kiguu na Njia nikapokelewa kwa heshima kiasi hicho. Hivyo, lazima nikiri kuwa kwa kiasi fulani nilifurahia nafasi hiyo ya kubebwa. Lakini pia, kwa ajili ya kelele na imani yao kuwa nina haya nilijua wasingeamini chochote ambacho ningewaambia. Nikaamua kutulia tuli juu ya mabega yao nikicheka kimoyomoyo.

Msafara huo uliishia katika nyumba moja ya wageni, mtaa wa tatu kutoka katika kituo hicho. Nilipelekwa moja kwa moja katika chumba maalum kilichoandaliwa kwa ajili ‘yangu’. Kilikuwa na bafu na choo chumbani humo. Mfuko wangu wa safari tayari uliwekwa juu ya meza, salama salimini. Yule mama aliyejipa uenyeji zaidi yangu alisema, “Baba, oga upumzike kidogo. Bibi Titi alifika jana. Nitamwarifu juu ya ujio wako, pengine mtapenda kuteta kidogo kabla ya kuanza safari ya Machame. Chifu Abdieli Shangai atakuwa tayari amewasubiri.”

“Lakini mimi sio Nyerere,” nilimwonya. “Naitwa…” hakusubiri hata nitaje jina langu. Badala yake aliangua kicheko, akipuuza alichokichukulia kama mzaha wangu. Akatoka huku akiufunga mlango nyuma yake.

Sikuwa na jinsi. Nikaoga. Nikapaka mafuta na kuvuta zile nguo zangu za safari. Nikavaa suruali na shati safi. Nikatia tai na koti juu. Nilifanya hayo kwa uangalifu mkubwa bila kuchafua bafu wala kuvuruga kitanda ili mweye chumba chake halisi atakapotokea akikute kikiwa kisafi.

Wakati nikijiandaa kutoka, nikiwa na dhati ya kuwahakikishia kuwa mimi sikuwa Nyerere, mlango uligongwa nikaufungua. Bibi Titi Mohamed alikuwa pale. Sikuhitaji kutambulishwa. Alikuwa mwanamke mfupi, mnene, mwenye macho maangavu.

“Julius, umeruka kwa ndege? Nilidhani ungefika hapa jioni,” alisema kwa sauti yenye mamlaka. Sauti hiyo ilififia ghafla aliponitazama usoni na kubaini kuwa mimi sikuwa Julius Nyerere waliyekuwa wakimtegemea.

“Nimejitahidi sana kuwaambia mimi sio Nyerere, hawakukubali,” nilijitetea. “Ni kama nimetekwa nyara na kuletwa hapa,” niliongeza.

Bibi Titi aliangua kicheko. Aligeuka kuwatazama wenyeji wetu waliosimama nyuma yake kunisubiri. Kicheko chake kilizungumza kila kitu. Akageuka tena kunitazama, “Pole sana bwana. Ni kweli umefanana sana na mwalimu. Kwa mtu asiyemfahamu vizuri kuwafananisha si ajabu.”

Sikumjibu. Sikuwa na la kujibu zaidi ya kutabasamu.

“Ulikuwa ufikie wapi?” aliniuliza.

“Nilikuwa natafuta mahali pa kupanga.”

“Basi unaweza kulala hapa,” aliniambia. “Malaika wako amekwishakukuongoza hadi chumbani humu, huna sababu ya kupingana naye. Pumzika, baadaye tutakaa tuzungumze. Si ajabu mola kakuleta mikononi mwetu kwa sababu maalum.”

Sikuwa na sababu ya kukataa.

* * *​

Kwa mujibu wa maelezo niliyoyapata baadaye, vuguvugu la wagombea uhuru nchini, chama cha TANU ambacho kilikuwa kimeanzishwa kutokana na TAA kulikuwa na matatizo katika kanda hiyo ya mashariki, hasa Kilimanjaro. Kwa mujibu wa maelezo hayo, matatizo hayo hayakuhusiana na chama kukubalika au kutokukubalika eneo hilo bali yalitokana na mvutano ndani ya Wachaga wenyewe.

Baada ya ule mvutano na mapigano ya makabila mbalimbali yanayounda Uchaga ulifika wakati pamoja na kukubaliana kuwa kitu kimoja. Uamuzi huo ulifuatiliwa na kumteua Mangi mkuu kama msimamizi na msemaji rasmi wa masuala ya Wachaga. Mangi mkuu huyu aliyekuwa na makao yake huko Marangu aliwekwa juu ya viongozi wengine wote wa kikabila.

Hata hivyo, ule mzimu wa chuki na kutokutamaniana miongoni mwao, ingawa ulizikwa, bado haukufa. Ni kama ulizikwa hai. Ujio wa Mjerumani, ambaye alifuata nyayo za mpelelezi wao Rebmen, ulifanyika Kilimanjaro iwe chaguo lao la awali, wakati machifu wengine wakisita kuwapokea. Mangi Sina wa Kibisho, miaka ya 1890 akiwa amejizatiti kiuchumi kwa kilimo na ufugaji, alikuwa pia ameimarisha jeshi lake ambalo lilikuwa kero kubwa kwa utawala wa wajerumani. Awali ya hapo Wajerumani hao, chini ya uongozi wa Karl Peters, waliendesha utawala wa kinyama na ukatili mkubwa Kilimanjaro, hali iliyopelekea April 25, 1887 gavana huyo katili afukuzwe kazi na serikali yake.

Lakini miaka mitatu baadaye, Machi 2, 1890 Wajerumani hao waliwanyonga hadharani, mjini Moshi, viongozi tisa wa kikabila. Viongozi mashuhuri kati ya waliopoteza maisha siku hiyo wakiwa Mollelia wa Kibosho, Ngalami na Meli wa Moshi. Madai ya Wajerumani kwa kitendo hicho yakiwa kwamba viongozi hao walikuwa wakiwavurugia jitihada za uongozi wao Kilimanjaro.

Hivyo, mkataba ambao Mangi Rindi wa Chaga aliingia na Mjerumani miaka mitano kabla ya kitendo hicho cha kikatili, na kuufanya mji wa Moshi kuwa kituo kikubwa cha biashara ya ndovu na watumwa kati yake na Zanzibar, lilikuwa pigo jingine katika jitihada za kuifanya Kilimanjaro kuwa na sauti moja.

Ujio wa vuguvugu la kupigania uhuru kukawa kama msumari wa mwisho kwenye jeneza la jitihada hizo. Wakati huo tayari yakiwepo malumbano makubwa ya iwapo kulikuwa na uhalali na haja ya Mangi mkuu kuendelea kutoka katika ukoo na kabila moja na cheo hicho kiende kwa kupokezana au la. Mangi mkuu, wakati huo Chifu, Thomas Mareale na kambi yake walishikilia msimamo wao. Kwa upande mwingine, machifu kama Abdiel Shangali walilipinga hilo kwa vitendo. Wasomi wengi wakiwa nyuma yake, Shangali alitumia fursa hiyo ya mparanganyiko kuunga mkono TANU na kuwekeza kimsimamo mikononi mwa mkewe Solomon Eliofoo, aliyekuwa ametokea masomoni Uingereza na Marekani na kurudi na kuanzishwa tawi la TANU Machame.

Lilikuwa tatizo zito kwa Chifu Mareale. Jitihada zake za kuwekeza kwa Petro Njau hazikuzaa matunda yaliyotarajiwa, hali iliyopelekea uhusiano wake na TANU ulegelege. Ingawa yeye binafsi aliwasiliana sana na Nyerere na wakati fulani kumtaka aje Kilimanjaro kuzungumza na Machifu wote bado alionekana kama mtu aliyekuwa njia panda. Hali ambayo baadaye ilishusha umaarufu wake, lakini hadhi yake na nafasi yake katika historia kamwe haikupata kufutika.

Kwa upande mwingine, Kilimanjaro haikuwa na njaa sana ya uhuru kama zilivyokuwa sehemu nyingine za Tanganyika. Kiuchumi alikuwa mbali zaidi. Kilimo cha mibuni kilikuwa kimeanzishwa katika eneo hilo tangu mwaka 1919 na kushika kasi 1930 na kuendelea. Hali hiyo iliambatana na kuanzishwa kwa vyama vya ushirika, ikiwa nchi ya Kwanza Afrika kuwa na mfumo huo. Hali ya hewa na ujio wa mapema wa wakoloni katika maeneo hayo pia ilikuwa neema nyingine kwao. Walipata shule nyingi na bora zaidi mapema.

Huduma za matibabu, barabara na maji pia walizijua kabla ya maeneo mengi ya nchi kufikiriwa.

Hivyo, inaweza kueleweka pale ‘Mshumbue’ Mangi mkuu Thomas Lenana Mlanga Mareale II aliponukuliwa akishuku kuwa Nyerere ‘alikuwa akinikwepa,’ na kwamba alimsahau katika harakati za uhuru. Hata hivyo, Mangi mkuu huyu aliendesha harakati mbalimbali za kisiasa ndani na nje, ikiwa pamoja na kumlipa wakili ambaye alimtetea Kenyatta wa Kenya hadi akaachiwa toka kifungoni wakati akituhumiwa kujihusisha na Mau Mau.

“Hivyo, ni sehemu fupi ya historia ya uchagani kaka yangu,” Bibi Titi Mohamed alisema baada ya maelezo hayo ambayo niliyaunganisha na kujaribu kuyaweka katika mtiririko mmoja baada ya huyu kusema hili, huyu lile nikijumuisha na yale yaliyokuwa katika kumbukumbu zangu.

Tulikuwa katika ukumbi wa hoteli hiyo. Watu wapatao wanane, wakiwemo wanawake watano, Bibi Titi na wawili wengine kati ya wale walionipokea pale kituo cha mabasi. Nilionekana kama muujiza. Nadhani hata kama angekuwa Nyerere mwenyewe hangepata idadi kubwa ya watu waliokuwa wakiingia na kutoka kwa nia ya kumwona ‘mtu aliyefanana na Nyerere’. Wingi wa watu hao wakiwa kina mama ambao walicheka na kujicheka sana kwa kosa la kunichanganya na kijana huyo aliyekuwa akitajwatajwa sana. Nadhani kwa namna fulani walidhibitiwa, kwani baadaye tuliketi na kuingia katika maongezi marefu, yaliyoongozwa zaidi na Bibi Titi, mwanamama msemaji sana, mwingi wa vichekesho huku akiwa pia msikilizaji mzuri.

“Wachaga wana historia tofauti na sehemu nyingi za nchi,” Bibi Titi aliongeza. “Sisi watu wa Pwani tuna historia inayotofautiana kwa kiasi kikubwa na wao. Nadhani wageni wengi waliotembelea makwetu toka enzi za enzi waliacha athari nyingi miongoni mwetu zaidi ya Uchagani ambako ni mbali kutokea Pwani.”

“Nadhani,” niliunga mkono. “Maana toka Waarabu, Wareno, Wajerumani na baadaye Waingereza wenyeji wao wa awali ni nyie tu.”

“Bibi Titi alitabasamu. “Tuyaache hayo,” alisema. “Hebu na wewe tuambie yako tukusikie. Ilikuwaje ukafananishwa na bwana Julius?” alinihoji.

“Kwa kweli sijui. Simjui Julius wala sijapata kumtia machoni labda imetokea tu tukafanana maana duniani wawili wawili,” nilimjibu.

“Huna udugu naye?”

“Hata kidogo.”

“Wewe ni Mzanaki?”

"Wala.”

“Kumbe nini basi.”

“Mie Muha. Natokea kigoma.”

Hufanani na Waha. Utakuwa Mmanyema.” Bibi Titi alidai. “Lakini hilo halina haja kwa sasa,” aliongeza. “Kama hutajali, tuambie wewe ni nani, unatokea wapi na unaelekea wapi.”

Nikawatajia jina langu. Nilitaja pia kazi niliyowahi kufanya ambayo sasa sikuwa nayo. Walivutiwa na taarifa ya safari za hapa na pale katika miji na vijiji mbalimbali vya Bonde la Ufa pamoja na mbuga za wanyama.

“Hujapata kufikiria kujiunga na harakati za kupigania uhuru?” Bibi Titi aliuliza. Akaongeza, “Maana wewe unaonekana ni mtu wa watu. Halafu, unatembea sana. Lakini la muhimu zaidi ni kwamba tungependa kupata mtu wa kwenda kuhamasisha harakati hizi huko kwenu. Ndiyo kuna watu tayari, lakini hawatoshi. Kumg’oa mkoloni siyo mchezo. Inahitajika kila silaha na kila askari.”

Wazo hilo halikupata kunitembelea akilini. Sikuwa na hakika kama mimi ni mtu wa kupanda jukwaani, mbele ya kadamnasi na kuanza kujinadi kuwa mimi ni bora zaidi ya wengine, au kumnadi mtu mwingine kwamba anafaa kuliko mwingine. Kwa ujumla sikupata kuwa na ndoto ya kuwa mwanasiasa maishani mwangu.

Bibi Titi alisoma hayo katika macho yangu. Akatabasamu. “Ni jambo linalohitaji kulifikiria.” Alinena. “Harakati zetu bado ni changa. Hakuna fedha za kulipa mtu wala kulipwa. Kwa ujumla tunajitolea. Tunachopigania ni uhuru. Ukipatikana kila mtu atakula matunda ya uhuru.”

Alisita, akaitazama saa yake. “Nadhani basi alilopanda Mwalimu linakaribia kufika. Nisingependa akina mama wakampokee mtu mwingine. Naenda mwenyewe kumpokea. Atafikia hoteli hiihii. Nitakukutanisha naye, pamoja na Kambona, ili uzungumze nao. Nadhani utakuwa tayari umefanya uamuzi.”

Akainuka na kuondoka, alifuatana na wale kina mama wengine na wanaume wawili.

Nilibakia na watu wawili mmoja alikuwa mtu mfupi, mweupe, ambaye kama si kwa ajili ya mvi mbili tatu kichwani ungeweza kumfikiria kuwa ni mtoto mdogo, ingawa umri wake ulizidi wangu kwa mbali sana. Hakuonekana kuwa Mchaga. Na hakuchelewa kunithibitishia hilo pale alipozungumza na mara moja nikabaini lafudhi yake kuwa ya Kipare zaidi.

“Ni kweli mimi ni Mpare,” alijibu swali langu. “Nimeungana na hawa watani wangu wajanjawajanja, katika harakati hizi za kupigania uhuru. Tatizo ni hapo utakapopatikana huo uhuru. Mchaga atapenda kuuteka nyara uwe wake, maana Mchaga mzuri ni yule aliyekufa tu.” Alisema akimtazama Mchaga.

Yule Mchaga akacheka. Yeye pia alinizidi umri. Alikuwa amevaa suti ya kijivu, tai shingoni na alishikilia mkoba wa nyaraka mkononi. Uso wake uliojaza ulipambwa na miwani. Hali iliyompa sura ya usomi.

“Achana na wajukuu wetu hao,” aliniambia. “Hao wameshindikana kabisa. Mpare anapata kesi ya kuku, ama kwa kuiba au kuibiwa. Atauza hata ng’ombe ili ashinde kesi hiyo. Kuna mtu hapo?”

Mie pia nililazimika kucheka.

Waliagiza vinywaji. Wao walikunywa bia mimi nilikunywa soda.

“Bia?” alihoji mmojawao.

“Sinywi.”

“Kwa nini? Unaumwa?”

“Hapana. Sijawahi kunywa toka nizaliwe.”

Walinitazama kwa mshangao kana kwamba nimewaambia jambo la ajabu kuliko yote waliyopata kuyasikia.

“Kwa umri huo?” Yule Mchaga aliuliza, “Huo ni umri wa kunywa vitu vya kiutu uzima.” Aliongeza.

“Tatizo ni kwamba sijapata kuitamani wala kuifiria. Halafu bei yake kubwa mara tatu kuliko soda.” Nilijitetea.

“Acha ubahili wa Kipare,” Mchaga alisema akicheka.

Mpare alicheka pia. Lakini alihamisha maongezi na kunitaka nimsimulie juu ya safari zangu za maporini. “Huko ulikokwenda kuna wanyama?”

“Wengi tu.” Nilimjibu “Unaweza kukutana na kundi la nyati wengi kama Ng’ombe wanaofugwa, kundi la twiga utadhani wako kwenye maonyesho na pundamilia kana kwamba wana sherehe.”

“Tembo?”

“Wengi kupita kiasi”

“Vifaru?”

“Wengi tu.”

“Umepata kuwaona kwa macho yako?”

“Mara nyingi tu.” Nilimjibu.

Mchaga alijaribu kuingilia kati, lakini Mpare alimkatisha kwa maswali yake juu ya wanyama na maeneo tuliyotembelea. Nilipomtajia kuyafahamu kwangu vyema maeneo ya Manyara, Ngorongoro na Tarangire alionekana kuvutiwa zaidi. Nilihisi kuona dalili za udenda zikielekea kudondoka toka mdomoni mwake. Sikuwa na hakika kama niliona vizuri.

“Itabidi tuzungumze kama wanaume baadaye,” aliniambia. “Unatarajia kuondoka lini?”

“Sina haraka,” nilimjibu. “Nitapenda kufika Arusha pia kabla ya kurejea maporini,” niliongeza.

“Nitakupeleka.” Alidakia. “Mimi ni mwenyeji Arusha kuliko hapa Moshi. Hutohitaji kulala au kula hotelini.”

Mchaga aliangua kicheko cha dhihaka, kicheko kilichofuatiwa na “Ndugu yangu umekwisha. Mpare ajitolee kukupeleka Arusha, akupe malazi na chakula! Kuna jambo hapo,” alisema.

“Atakwisha yeye,” nilijibu, “Maana siye Wamanyema tuna historia ya kula watu. Nitamla mzimamzima kabla yeye hajanila,” kauli ambayo iliniangusha kicheko kirefu.

“Lakini Wapare unawajua vizuri? Wana maradhi yasiyo na dawa ya uchoyo. Wewe na yeye mtakufa njaa hata kabla hujafikiria kumla, huku mkiwa na fedha mfukoni,” aliongeza na hivyo kuongeza kicheko. Sikujua mengi juu ya Wapare zaidi ya ukweli kuwa ni kabila jingine kubwa la Kilimanjaro, wanaishi katika miteremko ya milima ambayo ni sehemu ya mlima Kilimanjaro, na kwamba wao pia wamegawanyika katika sehemu kuu mbili, Wapare wanaozungumza Kingweno, wanaoishi kaskazini na Wachasu waishio Usangi, Kusini. Lugha zao zina aina fulani ya kulandana na zile za Wataveta na Asu wa Kenya.

Enzi za kale Wapare walisifika kwa uganga wa mvua na uhunzi. Uhakika kuwa kabila hili ni la kale ni pale nilipowahi kuona kitabu kitakatifu cha Biblia iliyoandikwa kwa lugha ya Kipare, kilichochapishwa mwaka 1910. Pamoja na ujio huo wa dini za kisasa Wapare waliendelea na tiba mbalimbali za asili kama maziwa ya Konda badala ya mama kumtibu mtoto mwenye wintu, maradhi ya sangasi yaliyoharibu vinywa vya watoto, majani yaliyoitwa more yaliyotibu ‘Kirumu,’ ‘kiruti’ au ‘kinyoka’, maradhi ya macho kwa watoto wadogo.

Historia ya dini za kigeni Upareni inaanza na mmisheni Jakob Janssen Dannholz, Mjerumani wa madhehebu ya kiluteri ambaye mwaka 1907 alianzisha ‘kazi ya bwana’ huko Mbaga, Upare ya kusini. Aliishi hapo hadi alipokamatwa na kuchukuliwa na Waingereza kama mfungwa wa kivita hadi katika kambi yao ya Misri ambako alifariki mwaka mmoja baadaye. Alifariki na umri wa miaka arobaini lakini kazi aliyoianzisha iliishi, ikakua na inaendelea kukua hadi leo.

Kinyume na makabila mengi nchini, wanawake wa Kipare walikuwa mstari wa mbele, pengine kuliko wanaume zao, katika harakati za kupigania uhuru na haki zao. Kumbukumbu zangu toka vitabuni zilinikumbusha mwaka 1946, kule Usangi, pale maelfu ya akina mama walipoibuka na kuanzisha vurumai kubwa wakipinga kulipa kodi. Tukio hilo liliibuka pale Chifu mmoja alipotembelewa na mkuu wa wilaya kwa ajili ya majadiliano. Umati wa wanawake wapatao mia tano waliizingira nyumba hiyo kutaka ufafanuzi juu ya utaratibu wa kodi ambao hawakuafikiana nao. Mkuu huyo alipojaribu kuondoka bila kuwapa ufafanuzi walipandwa na hasira, walianzisha nyimbo huku wengine wakiipiga mawe nyumba hiyo ya Chifu. Tukio hilo lilifuatiwa na maelfu ya wanawake kujiunga katika vuguvugu hilo ambalo lilitikisa serikali ya mkoloni.

Kama Wachaga, Wapare pia walikuwa katika mstari wa mbele katika kuiunga mkono TAA na baadaye TANU katika mapambano ya kudai kujitawala. Hali hiyo inachukuliwa kuwa ilisaidia kuondoka wazo la kuibuka kwa chama cha kikabila ambacho kingeweza kuwa chini ya ‘PARE UNISI’ ambayo ilikuwa na nguvu nyingi kutokana na mchango wa kiuchumi iliyotokana na kilimo cha mibuni, katani na chai.

“Unasemaje?”

Mpare alinizindua. Nikamtazama.

“Naona uko mbali sana,” aliongeza. “Nilikuuliza unadhani tuondoke lini kwenda Arusha?”

“Nilikuambia sina haraka, kwani hatuonani tena baada ya leo?” nikamuuliza.

“Tutaonana. Bila shaka yoyote.”

Mara akina mama walikwenda stendi kumpokea mwalimu wakaanza kurudi, mmoja baada ya mwingine. Hawakuwa na furaha kama ile waliyoonyesha wakati wakinipokea mimi. Hatukuchelewa kuelewa sababu.

Mwalimu Nyerere hakutokea.

Mchaga aliyekuwa kimya muda mwingi, akishughulikia kinywaji chake alitabasamu kidogo akinitazama. Kisha akasema, “Maadam Nyerere hakuja, na wewe umefanana naye, tutaendelea kukuita Nyerere. Unasemaje?”

Sikumbuki kama nilimjibu.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom