Waandishi wa riwaya wa China wakuza mawasiliano ya fasihi kati ya China na Afrika

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,029
1,051
1716186364757.png


Mwandishi wa vitabu vya riwaya Abdulrazak Gurnah ambaye ni mzaliwa wa Zanzibar na sasa akiwa anaishi Uingereza, amekuwa gumzo kubwa duniani tangu wakati aliposhinda Tuzo ya Nobel ya Fasihi mwaka 2021. Sifa ya mwandishi huyu mwenye umri wa miaka 75 imesambaa kila mahali duniani na zaidi kuwafikia hata wadau wenzake ambao ni waandishi wa riwaya na washindi wa tuzo hii ya Fasihi ya Nobel akiwemo wa hapa China Bw. Mo Yan ambaye alishinda tuzo hii ya Nobel ya Fasihi mwaka 2012.

Ili kudumisha mashirikiano na mahusiano mema ya kiuandishi, Mwezi Machi mwaka huu wa 2024 Bw. Mo Yan akiwa profesa wa Chuo kikuu cha Ualimu cha Beijing alimwalika mdau mwenzake Abdulrazak Gurnah kuja China kuwasiliana na waandishi wenyeji kwenye ulimwengu wa fasihi wa China na kubadilishana mawazo kwenye nyanja ya fasihi ya China na Afrika.

Katika mawasiliano yao Bw. Mo Yan ambaye mwaka jana alitembelea nchi za Afrika Mashariki zikiwemo Tanzania na Kenya na kujionea utamaduni mpana wa nchi hizi, alisema amefurahishwa mno na ujio wa Bw. Gurnah kwa kuwa yeye ni shabiki wake namba moja. Bw. Mo Yan pia amesoma riwaya nyingi za Afrika zikiwemo zilizoandikwa na Ngũgĩ wa Thiong'o na Chinua Achebe.

Kwa kuwa China na Afrika zina mawasiliano mapana ya utamaduni na hasa ya fasihi, riwaya mbalimbali za Bw. Abdulrazak Gurnah tayari zimetafsiriwa kwa lugha ya Kichina na kuingia kwenye soko la China. Riwaya hizi zimependwa mno na kupokelewa kwa mikono miwili na Wachina huku zikipata mashabiki wengi zaidi hapa nchini China.

Akionesha kufurahishwa na hatua hii ya wanafasihi wa China kuteua vitabu vyake na kuvitafsiri kwa lugha ya Kichina Bw. Gurnah anasema hakuwahi kufikiria kwamba siku moja wasomaji wa China nao pia watapata ladha na hisia wanazozipata watu wa Afrika kupitia hadithi zake mbalimbali.

“Watu wote duniani tunajuana kwa njia mbalimbali, tunasikia habari za nchi fulani, tunasoma vitabu vilivyoandikwa kuhusu maisha ya watu. Mimi ninasoma vitabu vya China, vitabu vya Kirusi, vya Kiingereza, na kila ukisoma vitabu unafahamu zaidi. Basi ikiwa watu wa hapa China watasoma vitabu vyangu zaidi, watafahamu maisha yetu zaidi.” Alisema Bw Gurnah

Katika kazi yake ya uandishi ya zaidi ya miaka thelathini, Gurnah ameandika riwaya 10. Katika nusu ya pili ya mwaka 2022, Ofisi ya Uchapishaji wa Tafsiri ya Shanghai ilizindua tafsiri za Kichina za kazi bora tano za Gurnah zikiwa ni pamoja na "Paradise", "By the Sea", "Afterlife", "In Praise of Silence" na " The Last Gift ". Wakati huohuo tafsiri za Kichina za kazi nyingine tano za Gurnah ambazo ni "Gravel Heart", "Dotty", "Abandonment", "Memory of Parting" na "Pilgrim's Road", zilitolewa wakati wa Maonesho ya Vitabu ya 2023 ya Shanghai.

Ingawa vitabu vya Bw. Gurnah kimsingi vimeuzwa sana hapa nchini China, riwaya zake 10 zinachambua masuala yaliyo karibu sana na mioyo ya Wazanzibari. Katika kazi zake, anaangazia watu binafsi, vikundi na jamii ambazo zimesambaratika kutokana na mabadiliko makubwa yanayotokea katika jamii. Bw. Gurnah anatumia mtindo tulivu wa uandishi akiwa amebeba kumbukumbu nzito zenye machungu, na kuweka bayana athari za ukoloni na maisha ya wakimbizi walionaswa katikati ya tamaduni tofauti na migawanyiko ya kibara. Labda Amejikita kuandika aina hii ya hadithi kwasababu na yeye kwa namna fulani amepitia machungu haya.

“Nimeandika hadithi za historia, na za watu wakimbizi au watu waliohama kwani tufahamu kuwa wengine wamehama kwasababu imewabidi wahame, wengine wamehama kwasababu wametaka maisha mengine mapya. Ni kitu ambacho dunia nzima sasa tunaona kikitokea. Watu wengi kutoka Afrika wanakwenda nchi za Ulaya, wanakwenda nchi za Marekani. Kwa hiyo mimi naandika kitu ambacho kinatokea kila siku katika maisha yetu. Na mie pia kimenigusa na ni kama vile nafahamu kwa undani kwasababu mimi ninayo hadithi yangu inayohusiana na mambo hayo.”

Gurnah, aliyezaliwa mwaka 1948, aliondoka Zanzibar na kuhamia Uingereza katika miaka ya 1960. Alipata shahada ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Kent na kubaki chuoni kuendelea kufundisha. Kwa miaka mingi, profesa huyu wa fasihi amekuwa na athari kubwa kwa wanafunzi wake wa huko.
 
Kwanini kuwatupia mzigo Israel? Inawezekana rubani ni gaidi aliamua kujitoa muhanga.
 
Ikiwezakana china waonde hii elimu ya mzungu huku Africa inatuletea feminists.
 
Back
Top Bottom