H O F U
SEHAMU YA KUMI
MAMBO BADO
Ilikuwa yapata saa sita kasoro dakika kumi wakati Bon alipobisha hodi kwenye chumba cha Willy, huku akiwa na bastola mkononi tayari. Mike alikwenda kufungua. Akiwa tayari kabisa, aliruka haraka upande.
"Lo! Mungu wangu vipi?", Mike aliuliza baada ya kumwona Bon".
"Willy yuko wapi?", Bon aliuliza kabla ya kujibu.
"Amewafuata", Mike alijibu.
"Kama nusu saa hivi. Nyaso amempeleka na atarudi si muda mrefu. Rocky yuko wapi?", Mike aliuliza.
"Mike. Rocky ameuawa", Bon alijibu.
"Hapana", Mike alisema bila kuamini.
"Ukweli ni kwamba watu hawa ni majasusi wa hali ya juu. Twende tumfuate Willy. Huko njiani nimeona gari likielekea nyumbani kwa F.K. likiwa limejaa watu. Iwapo Willy yuko peke yake, atapata matatizo. Heri tumfuate kwani hatuwezi kumpotenza na Willy pia. Mambo mengine nitakueleza njiani. Kwani hatuna muda. Nyaso akirudi anaweza akatusubiri hapa hapa", Bon alisema.
Bila kusema neno Mike alichukua zana zake na wanaume wakatelemka chini. Mbele ya hoteli walipungia taksi na kupanda.
"Tupeleke Themi Hill", Bon alimwamrisha dereva. wakaondoka.
Willy alipopata fahamu kidogo akajikuta ndani ya chumba kikubwa. Alikuwa amefungwa kwenye mti mfano wa msalaba uliokuwa katikati ya chumba. Ingawa Willy alikuwa amepata fahamu huku akiumwa sana na kichwa, hakuonyesha kama amepata fahamu. Alifanya hivyo 'kununu muda' Alishangaa kukuta majasusi walikuwa bado hawajamuua. Hapo hapo aligundua kuwa walikuwa na sababu ya kumweka hai. Kwa kutumia sababu hiyo aliweza kununua muda zaidi. Alijikuta amefungwa barabara kiasi kwamba asingeweza hata kujitingisha.
Mara alisikia mlango unafunguliwa na taa kali zaidi zinawashwa na kuelekeza mwanga wake kwake. Pale pale Willy alitambua kuwa chumba kile kilikuwa chumba cha mateso. Alikuwa amevuliwa nguo zake zote na kubaki na chupi tu.
"Hecke, bila shaka umempiga sana mtu huyu, nusura umwue. Unajuwa mtu huyu tunamhitaji sana angalau kwa muda wa dakika tano zaidi akiwa hai", F.K alisema. Willy aliyasikia maneno hayo.
"Mtu huyu ni hatari sana F.K. Hecke alichofanya ni sawa sawa", mtu mmoja alisema na Willy akamsikia.
"Sharti turudishe fahamu yake maana yule mwenzake anaweza kuwa anajongea kwa wakati huu", F.K. alisema.
"P.G yuko nje tayari kumfungia kazi. Hecke na wewe nenda nje ukamsaidie P.G. kama ikibidi. Akidiliki kupitia njia ile ya chini kama alivyofanya mwanzo, huo ndio utakuwa mwisho wake, kwani nimemtegeshea bomu moja safi", George alijigamba.
"Hebu kwanza Hecke, nenda ukawashe ile swichi ya umeme ili umshitue mbwa huyu kwani amezirai muda mrefu", F.K. alimwamrisha Hecke. Willy akajiweka tayari huku akili yake ikifanya kazi haraka haraka. Hecke alikwenda akawasha swichi. Umeme ulimshitua Willy naye akajifanya kaupata fahamu tayari ili asiumizwe zaidi. Alipofungua macho alimwona F.K. amesimama mbele yake pamoja na George. Kule pembeni alimwona Hecke.
"Karibu kwetu Willy Gamba. Ni jambo lisilofurahisha kukukaribisha hapa nyumbani kwangu katika hali hii. Lakini umeyataka mwenyewe na kama ujuavyo msiba wa kujitakia hauna kilio. Haya, huyu hapa ni mwenzetu na kiongozi wetu Geoge ambaye anaongoza kikundi cha 'KULFUT' kilichotumwa kuja kuifundisha adabu Tanzania", F.K alisema akiwa anamtazama Willy. Baadaye alimgekia George.
"George, huyu ndiye Willy Gamba kama umewahi kumsikia. Ni bahati yake mbaya kwamba amekutana na wewe", F.K. alisema.
"Hata mimi nimefurahi kumwona, nimesikia habari zake nyingi. Nasikitika kumwona katika hali hii, hata anapokuwa amefikia mwisho wa maisha yake haya yote yametokana na nchi ya Tanzania kujiweka kimbelembele na kujiingiza kwenye mambo yasiyowahusu", George alijigamba.
Aliposikia hayo Willy alianza kuzungumza ilimradi aweze kusukuma wakati.
"F.K... ni lazima umweleze kaburu huyu swala la ukombozi Kusini mwa Afrika ni swala la Afrika huru nzima. Hivyo kwa watu kufa ili vizazi vilivyobaki viweze kuwa huru ni jambo takatifu. Kwa hiyo mimi sina wasiwasi na kufa".
"Hecke, hebu nenda huko nje ukamsaidie P.G. kumumaliza huyo mbwa mweusi mwingine kwani naona hawa wana vichwa vigumu kama vya paka", George alimrisha.
"Kitu kimoja ambacho unapaswa kuweka maanani Willy ni kwamba, mtu mweusi hawezi kujitawala. Sana sana atapata uhuru wa bendera lakini uchumi wenu utatawaliwa na mtu mweupe daima. Chukua mfano wa Tanzania ni nani anayefaidi matunda ya uhuru hapa kama siyo mzungu na mhindi?, Mhindi akiendesha Benz ni halali yake; thubutu mtu mweusi aendeshe Benz kama hakutiwa msukosuko. Sasa, kisa gani hata kupoteza maisha yenu kwa kupigania uhuru wa bendera ambao huna faida? kweli mtu mweusi hawezi...", F.K. alisema na kukatizwa.
"F.K. unazungumza maneno ya kitoto. Nchi huru za Afrika zinapigana dhidi ya ubaguzi kwa sababu hazitaki ubaguzi. Nyinyi wahindi mnaonekana kama watanzania machoni mwa watanzania. Mawazo yako katika kuhusu uhitilafiana kimapato ni jambo lililopo Ulimwenguni kote. Amini usiamini, kama usaliti wako utagunduliwa, hata kama mimi nitakuwa nimekufa, wahindi wenzako watakuwa wa kwanza kutamani kukurarua. Siyo wahindi wote wenye mawazo finyu kama yako", Willy alimwambia F.K.
"F.K. unamchelewesha huyu mtu. Hebu muulize atupe habari zetu halafu... Usiku unakwenda haraka sana", George alimwambia F.K.
"Kusema kweli Willy nilipenda kifo chako kije haraka. Hata hivyo huo ni uamzi wako. Kama utajibu swali langu, utakufa haraka bila kupata mateso. La hasha, utakufa pole pole na kwa uchungu mkubwa. Chumba hiki kina kila aina ya vifaa vya kutesea. Sina haja ya kukueleza kwani wewe mwenyewe ni mwenyekiti katika shughuli hii. Sasa jibu swali langu: Viongozi wa wapigania uhuru wamefichwa wapi?", F.K. aliuliza. Mara Willy aligundua kwamba mpango wa kuwaficha viongozi wa wapigania uhuru ulikuwa wa busara sana.
"Sijui. Kawatafute wewe mwenyewe. Kwani sisi tulipogundua hawa makaburu ulipowaficha ulituambia?", willy alijibu kwa kiburi. Jibu hilo liliwafanya wahamaki. George alimrukia Willy na kumtia makonde ya haraka haraka mpaka Willy akapoteza fahamu kwa muda.
"Sisi hatutaki mchezo. Tumekuja Tanzania kuwatia hofu na kiwewe. Jibu lako litatusaidia kuua viongozi peke yake kuliko kufagilia mbali umati wa watu na mji mzima wa Arusha. Kipigo tutakachotoa kitasikika mpaka huko ahera. Nyumba hii imejaa silaha za kisasa za kuweza kuuteketeza mji mzima. Sasa sema ama hakika utaumia", F.K. alisema kwa hasira. Willy alifahamu fika kwamba hakuna mtu ambaye angethubutu kumuua, kwani alijuwa wao walitaka kufahamu viongozi wa wapigania uhuru wako wapi. Hilo ndilo jambo muhimu lililokuwa limewaleta.
"Sijui walipo, fanya unavyotaka", Willy alijibu.
"Umeyataka mwenyewe", F.K. alijibu huku akitoa kitu mfano wa saa kutoka kwenye mfuko wa shati na kukiwasha. Mara Willy alijisikia moto unamchoma kutoka kwenye ncha ya kidole mpaka utosini. Alijaribu kuvumilia. Lakini uchungu ulizidi na Willy akaanza kupoteza fahamu. Bila ya kujifahamu Willy alitoa sauti kali.
"Aaaaaa! Nitakuelezeaaa!".
Wakati F.K na George wanamkabiri na kumtesa Willy katika kile chumba cha mateso, Bon na Mike walikuwa wamefika kwenye seng'enge ya jumba la F.K. tayari kwa mapambano makali.
"Tusipite kwa chini maana wanayo televisheni watatuona. Tupite njia ya kawaida ila tujuwe kuwa wanatusubiri", Bon alisema.
"Sawa", Mike alijibu.
"Pande zote mbili, kushoto na kulia zinayo madirisha makubwa. Jambo la kufanya ni kujitahidi kuingia na sisi tuonane huko ndani", Bon alimweleza Mike. Wote waliangaliana ili kupeana moyo.
"Jihadhari sana", Mike alimweleza Bon.
"Na wewe vile vile", Bon alijibu huku akimkumbuka marehemu Rocky aliyekuwa amemuaga kwa namna ile.
"Jambo la kwanza ni kuangalia kama Willy angali hai. Nina wasi wasi juu ya maisha yake", Bon alimnong'oneza Mike huku wakiachana. Mike alimuonyesha ishara ya kumwelewa Bon. Wakiwa wamejificha kwenye vivuli wanaume hao wawili walilisogelea jumba la F.K. kwa tahadhari na hamasa kubwa.
Mike aliambaa ambaa katika upande wake; mara alisimama kimya na kwa tahadhari alijaribu kusikia kila aina ya jambo ambalo lingetokea. P.G alikuwa upande wa kaskazini wa jumba lile. Mara alimwona Hecke aliyekuwa achunge upande wa kushoto wakati yeye P.G akichunga upande wa kulia.Wakati P.G alipokuwa anaambaa na ukuta wa kulia huku bastola mkononi. Mike naye alishafika kwenye ukuta ule ule akiangalia akiangalia namna ya kufungua dirisha bila kuwashitua watu waliokuwa ndani.
Mara P.G. alisikia jasho jembamba likimtoka. Pale pale alijuwa kuwa alikuwa katika hali ya hatari kwani hali hiyo humtokea mara tu hatari inapobisha hodi. Mike ambaye alikuwa amevaa nguo nyeusi alisogea mbali kidogo kutoka alipokuwa kwani naye alihisi kitu kinatembea karibu na ukuta ule. Alibana chini ya mti huku macho yake yamezoea giza. Mara alikia kitu kama mti kinakatika! Alipoangalia umbali wa mita mbili kutoka chini ya mti alipokuwa amesimama aliona kitu kinatingishika. Alipoangalia vizuri aliona mtu anasogea. Mike alisimama kama mti mkavu. P.G. naye alikuwa ananusa nusa huku na kule kama mbwa wa polisi huku bastola yake tayari kufyatuliwa wakati wowote.
Alipotembea na kufika sehemu ya mita moja kutoka mahali Mike alipokuwa amesimama, naye alisimama. Wakati huo huo Mike aliruka kama risasi. Alimkumba P.G. na wote wawili wakaanguka chini. Bastola ya P.G. ilianguka kando na kuzitema risasi zake. mlio wake haukusikika ndani ya jumba kwa sababu bastola ile ilikuwa na kiwambo cha kuzuia sauti. Walipoinuka, Mike alimtambua P.G. mara moja.
"Ni bahati iliyoje kwangu P.G.? Nilidhani umenikimbia huko Nairobi. Sasa mimi na wewe", Mike alisema na kumshangaza P.G. ambaye hakutarajia kukutana na Mike Arusha.
"Umejileta wewe mwenyewe kwenye kifo chako Mike Maina. Baada ya kukumaliza wewe nitarudi Nairobi. Kisha nitajibadilisha na kuhakikisha vile vikaragosi vyako kwenye ofisi yenu ambao walitaka kuharibu kazi yangu nawafagilia mbali. Kwa kutumia uwezo wangu wa kipesa, nitahakikisha Masoga anakuwa mkuu wa idara yenu..." P.G. alisema. Kisha alikatisha sentesi ili amchukue Mike kwa ghafla ili amtie 'mapigo ya kifo', kama yeye alivyokuwa anayaita. Lakini P.G. alipotupa mapigo yake hayo Mike aliyazua yote kwa ufundi wa hali ya juu.
"Nilimwahidi Mwaura kwamba nitalipa kisasi chake kwa mikono yangu mwenyewe. Sasa P.G. umekufa", Mike alisema na pale pale aliona sura ya maiti ya Mwaura ilivyokuwa imepigwa risasi. Mori ulimpanda. Alijisikia akipata nguvu zisizo kifani. Mike alimtia pigo la kifuani P.G. ambalo karibu lingemdondosha. Lakini alijitahidi na kurudishia mapigo makali sana. Mike aliteleza mpaka chini. P.G alivuta upanga wake ili ammalize Mike. Upanga ulikuwa umefichwa kiunoni. Huku akiamsha upanga, tayari kumkata Mike P.G. alisema.
"Burian Mike!", wakati huo huo Mike alijiviringisha na upanga ukamkosa, P.G. alijirusha na kujitayarisha tena kumkata Mike. Alimkosa mara ya pili na mara ya tatu. Mike aliruka na kuumpiga teke mkono ule wenye upanga ambao ulianguka chini. Mkono wa P.G. ulikuwa umevunjika. Maumivu yalikuwa makali na Mike alichukua nafasi hiyo. Mike alimtia P.G. kipigo cha mbavu ambazo zilivunjika. P.G. aliamua kujikakamua lakini akawa amezidiwa mbinu.
"P.G. Afrika itashinda na Afrika Kusini itaondokana na udhalimu wa ubaguzi wa rangi na kuwa huru chini ya wazalendo walio wengi. Ukiwa huko ahera utaona kuwa unyama wenu haufui dafu kwa wapigania haki. Hata Mwenyezi Mungu yuko kwenye upande wa wanyonge", Mike alimwambia P.G. ambaye alikuwa anatokwa damu puani na masikioni. Alijua alikuwa amekaribia mwisho wake lakini aliamua kama ni kufa ilibidi afe kiume. Alikusanya nguvu zake zilizobakia na kumrukia Mike. Lakini Mike alikuwa tayari. Hivyo alimpisha P.G. ambaye alijigonga kwenye ukuta na kuanguka chini. Mike alichukua ule upanga wa P.G. na kuutumia kumkata kichwa.
"Malipo ya dhambi ni mauti", Mike alisema huku akiwa ameinua upanga na kuangalia maiti ya P.G. Akiwa bado amepandwa na mori alivunja dirisha kwa kutumia upanga akiwa tayari kwa mapambano makali.
"Leo ni leo. Liwalo na liwe. Sisi na washenzi makaburu ", Mike alisema huku akipanda dirisha ili ajitose ndani.