HOFU
SEHEMU YA TISA
KABLA YA USIKU WA MANANE
Wakati Willy na Nyaso walipokuwa wanaelekea New Arusha Hoteli. F.K. alikuwa amewasili nyumbani kwake. Alikuwa akiwaeleza wenzake kazi aliyokuwa ameifanya.
"Kazi mliyonituma nimeimaliza tayari", F.K alisema.
"Vema", George alijibu.
"Sasa ni saa tatu na dakika kumi, mipango yetu itaanza saa ngapi?", P.G aliuliza.
"Hebu nisikilize kwa makini", George alieleza. "Nilikuwa kwenye chumba cha habari na nimewasiliana na Kamanda wa KULFUT huko Afrika ya Kusini. Nilipompa habari kuwa tayari tumepoteza watu wawili alikasirika sana na kuniambia kwamba asingependa kusikia kitu kama kile tena. Alisema jambo hilo lilikuwa kinyume cha nia ya matakwa ya Serikali ya Afrika Kusini ambayo ni kuleta 'hofu' isiyoelezeka dhidi ya wapigania uhuru, nchi zilizokuwa mstari wa mbele na Afrika huru kwa ujumla.
"Ameongeza kuwa usiku wa leo lazima uwe usiku wa kazi. Hapo kesho Kamanda anataka kusikia habari za kilio kutoka Tanzania na Afrika nzima. Kama mjuavyo mkutano wa wapigania uhuru umepangwa kuanza kesho saa tatu. Lakini amri tuliyopewa ni kwamba mkutano huo usiwepo, na badala yake kuwe na vilio. Wale watakaokuwa wamesalimika watakuwa wanaikimbia Tanzania bila mpangilio wowote. Wakati dunia nzima itakapokuwa inalaani kipigo tutakachokitoa kwa Tanzania, majeshi yetu ya Serikali ya Afrika Kusini yatavamia Msumbiji, Botswana, Zambia, Zimbabwe na Angola hapo kesho. Watu wa nchi hizo watabaki wamechanganyikiwa. Wakati dunia nzima inagwaya, jeshi letu la polisi litafyekelea mbali watu weusi wenye kuleta ghasia ndani ya Afrika Kusini. Tutawachinja kama kuku na hivyo kuzima kabisa maasi wanayoita ukombozi".
"Ndio mnaona umuhimu wa kushinda katika mapambano yetu. Kamanda wetu amenipa majina ya viongozi wanne wa wapigania uhuru. Ameongeza kwamba hao wakiuawa wote kwa siku moja, itakuwa ni kipigo cha kutosha hata kuzima vugu vugu la maasi katika Afrika kwa muda mrefu. Majina ya viongozi hao ni Mbeki, Jamana, Ntamazi na Basweka. Je, F.K una habari kuwa watu hawa wamewasili?".
"Ndiyo, wote hawa wamefikia Maunt Meru Hoteli na namba za vyumba vyao ni hizi hapa", F.K alisema huku akimpa kijikaratasi chenye maelezo kamili juu ya viongozi wake.
"Umefanya kazi nzuri, F.K", George alimpongeza F.K.
"Ahsante, kazi nzuri lazima ifanyike George ili lengo letu liweze kutimizwa", F.K alisema.
"Sina shaka", George alisema. "Viongozi hawa wanalindwa sana. Askari polisi, maafisa usalama na hao wapelelezi mashuhuri watatu wamewazunguka viongozi hao, hasa kutokana na mambo yaliyotokea jana. Tumshukuru F.K kwa kuhakikisha usalama wetu na kukaa bila adui kujua tuko wapi huku tukipata habari bila matatizo".
"Hayo yote ni matunda ya mafunzo yako thabiti, kama Mwalimu wangu", F.K alijibu kwa unyenyekevu.
"Hivyo", George alieleza. "Mpango ni kama ifuatavyo; kwanza kabila lazima tuwakorofishe hawa wapelelezi watatu. Bila kufanya hivyo, kazi yetu ya kuwafyekelea mbali viongozi hawa itakuwa ngumu. Kwa hiyo, mimi nimepanga kwamba ni lazima Willy Gamba auawe leo kabla ya usiku wa manane, inaonekana huyu ndiye ngao ya wengine waliobaki. Yeye akiuawa wenzake watabaki wamegwaya na kuchanganyikiwa wasijue la kufanya. Hawataweza kuchukua hatua yoyote kwa leo kwani watahitaji muda mrefu kutayarisha mpango mpya, bila kuwa na Willy Gamba. Hii itatupatia muda sisi kufunga kazi, Kabla ya jua kuchomoza, kazi yetu itakuwa imekamilika".
"Mtu huyu atauawa vipi", P.G aliuliza.
"Mpango wa kumuua Willy utakuwa kama ifuatavyo, F.K na vijana watatu watakwenda nyumbani kwa mzee Hamisi. F.K alieleza kwamba familia ya mzee Hamisi iko likizo, hivyo yeye anakaa peke yake kwa wakati huu. Vile vile tunafahamu kuwa Willy na mzee Hamisi wanafanya kazi bega kwa bega, kwani habari zote kutoka kwa bosi wa Willy zinapitia ofisini kwa mzee Hamisi. Hivyo F.K na wenzake watamlazimisha mzee Hamisi amwite Willy Gamba kwa simu toka hapo hotelini kwake. Mzee Hamisi atalazimishwa kumwambia Willy aje nyumbani kwake ili ampe habari muhimu sana kutoka kwa bosi wake. Bila shaka Willy atakuja na mtego wetu utamnasa. Atauawa tu", George alisema huku akitabasamu alipoona nyusa za wenzake zimejaa furaha baada ya kusikia mpango wake.
"Kweli naamini unastahili kuwa kiongozi wetu", Dave alisema. "Kwenye mtego kama huu hata mimi ningenasa tu".
"Lakini vijana watatu hawatoshi, mtu huyu ni mbaya sana", F.K alisema kwa sauti ya woga.
"Oke, nitakwenda nao mimi mwenyewe", Dave alijigamba.
"Hapana", George aliingilia kati. "F.K atakwenda na hao vijana, bali tu tutamwongeza mmoja zaidi ili wawe wanne. Wewe mwenyewe Dave unajuwa kwamba vijana wetu wanao ujuzi mkubwa. Vile vile mfahamu kuwa wakati Willy akiitwa kwa mzee Hamisi hatachukua tahadhari kubwa, kwani hatahisi kitu chochote kibaya. Hivyo kazi yao itakuwa rahisi kama mtelemko. Mara tu baada ya mzee Hamisi kumwita Willy, naye lazima auawe. Baada kumuua Willy vijana wetu watarudi huku haraka kwa kazi nyingine ya baada ya usiku wa manane. Mimi, P.G na vijana wawili tutakwenda kukagua mazingira Maunt Meru Hoteli na vile vile jumba la Kimataifa ambamo mkutano unatarajiwa kufanyika. Tunataka kutega mabomu ya masaa kwenye sehemu hiyo. "Kwa hiyo F.K, baada ya kumwita Willy na kumuua Hamisi, kazi nyingine utawaachia vijana. Wewe utachukua gari la Hamisi kwani litahakikisha usalama zaidi, halafu utufuate Maunt Meru Hoteli ili utuonyeshe chumba cha mikutano ambamo tunatarajia kutega mabomu. Baada ya kumuua Willy. Vijana warudi huku haraka kwa gari lako. Wewe Dave utabaki hapa na vijana watatu mkisubiri kazi yenyewe ya usiku wa manane. Mipango zaidi nitawajulisha saa tano usiku wakati tukijitayarisha kwenda kwenye mapambano yenyewe. Naamini nyote mmenielewa?".
"Mpango ni barabara kabisa", Dave alisema huku akijinyoosha nyoosha.
"Hivi ni kwanini mnataka kutega mabomu? Si hawa watu tutawaangamiza usiku huu ili mkutano usifanyike kesho?", P.G aliuliza.
"Katika kazi hii hakuna kuacha mwana hata kidogo, kama hatukufanikiwa kuwauwa wote kwa leo, basi wale watakaodiriki kuendelea na mkutano kesho, nao watauawa vile vile", George alijibu huku akitabasamu.
"Baada ya kufunga kazi sisi tutaondoka vipi hapa?", Dave aliuliza.
"Usiwe na wasiwasi", George alijibu. "Mipango yote imeshakamilishwa na F.K; ukipata muda ingia chumba namba kumi".
"Haya, twende kazini vijana. Mungu atusaidie", P.G alisema.
"Amin!", wengine walijibu kwa pamoja huku wakiinuka na kujitayarisha kuondoka.
HOFU
KABLA YA USIKU WA MANANE
II
Ilikuwa yapata muda wa saa tatu na nusu usiku, Willy na Nyaso walibisha hodi kwenye chumba cha Willy baada ya kujua kwamba wenzake walikuwa wanamsubiri ndani. Willy na Nyaso walikuwa wamefika pale chumbani kwa kupitia njia tofauti kama walikuwa hawafahamiani. Willy alikuwa amepanda kwa kutumia ngazi, wakati Nyaso alitumia lifti.
"Nani", Bon aliita kwa sauti.
"Willy".
Bon alifungua mlango huku akiwa na bastola mkononi. Alipomuona msichana Bon alirudisha mlango haraka haraka.
"Na wewe woga umezidi, karibu ndani Nyaso", Willy alimkaribisha huku akirudisha mlango baada ya Nyaso kuingia ndani.
"Maama", Mike alisema kwa mshangao.
"Nini?", Willy aliuliza kwa kebehi.
"Wewe huwa unawatoa wapi hawa?".
"Malaika huyu ama mwanadamu?", Mike aliendelea kushangaa.
"Wewe unafikiri vipi?", Willy alimuuliza.
"Malaika", Mike alijibu huku wote chumbani wakimwemwesa.
"Subiri sasa niwafahamishe kwa huyu 'malaika'. Mtoto huyu anaitwa Nyaso. Ni Nyaso tu. Msiulize zaidi. Nyaso hawa ndiyo rafiki zangu niliokuwa nikikueleza. Yule maneno mengi ni 'Kikuyu' toka Kenya. Huyu ni Bon toka Afrika Kusini na yule pale anayejifanya mkimya ni Rocky kutoka Zimbabwe", Willy alisema.
"Nashukuru kuwafahamu", Nyaso alijibu.
"Sisi ndiyo tunapaswa kushukuru kwani kumfahamu mtoto mzuri kama wewe ni fahari ati", Mike alisema.
"Willy kweli watanzania mnatoa watoto, mimi sina hata maneno. Hivi vijana wa hapa mtaweza kujenga?, Mtoto kama huyu akisema umpe mshahara wako wote wa mwezi unaweza kukataa? La hasha rocky alisema.
"Ahsante kwa sifa ulizonipa", Nyaso aliitika.
"Sikia sauti yake nyororo", Bon aliongeza.
"Wacha sauti na sura, Nyaso anayo mengi zaidi", Willy aliasa.
"Haya Willy, umemleta huyu mrembo ili tukusifu ama unayo mengine zaidi?". Mike aliuliza.
"Wacha maneno mengi, nyinyi wakenya mkijua kiswahili kadiri, sisi watanzania huwa watufui dafu", Willy alisema.
"Hayo ndio maendeleo", Mike aliongeza.
"Hebu jamani, nisikilize kwa makini. Sikuja na msichana huyu ili kuwakoga. Kusema kweli mambo yamepamba moto tayari na ni lazima na sisi tuwemo kazini", Willy alisema halafu aliwaeleza juu ya mazungumzo yake na Nyaso, juu ya F.K na mwisho jinsi walivyokwenda kwa Chris na kukuta ameuawa.
"Tunao uhakika kuwa F.K ndiye aliyefanya mauaji hayo. Mimi ninahisi amekuwa na wasiwasi baada ya kusikia kwamba mimi nimemhoji sana Chris. Kwa hiyo aliamua kutumia mbinu zile zile za siku zote: Yaani maiti hawana maneno. Hii ina maana kwamba fumbo limefumbuliwa tayari. Majasusi tunaowatafuta wamejificha kwa F,K. Kutokana na maelezo ya Nyaso kuhusu jumba la F.K. lilivyo ni dhahili kwamba majasusi hao wako mle ndani, hivyo kazi imebaki kwetu", Willy alisema.
"Sasa mipango iko vipi bosi?", Bon alimwuliza Willy.
"Kwanza kabisa mimi na Nyaso tutakwenda kufanya uchunguzi kwenye jumba la F.K. kama nilivyowaeleza, jumba hilo linazo njia za chini kwa chini. Na kama hivyo ndivyo, basi mle kuna sehemu nyingi ambazi ni za siri. Kwa sababu hiyo mimi naona ni bora niende na Nyaso ambaye atanionyesha mahali jumba hilo lilipo. Baada ya kufanya utafiti, nitarudi hapa ili tujadili jinsi gani ya kuwakabiri hao majasusi usiku huu, ama mnasemaje?", Willy aliuliza.
"Hisia zetu ni sahihi. Sasa kwa nini sisi sote tusivamie jumba hilo mara moja na kufunga kazi", Mike alipendekeza.
"Hapana Mike, huenda kazi yenyewe isiwe rahisi kama unavyofikiri. Haitakuwa vizuri sisi sote kujitumbukiza bila kufanya uchunguzi. Uwezekano wa kuangamia sisi sote upo, na hilo litakuwa pigo kubwa kwa Afrika huru na kwa wapigania uhuru wa Afrika Kusini. Hivyo utakuwa ushindi kwa makaburu. Amini usiamini, mapambano yanayoendelea huko Afrika Kusini, kwa kiwango kikubwa, yanategemea ushindi wetu", Willy alijibu.
"Mimi nakubaliana na wewe kabisa", Bon alisema halafu akaendelea, "Kusema kweli, vita kamili vimeanza ndani ya Afrika Kusini. Ushindi wetu hapa utawatia hamasa vijana wa kizalendo ambao wanapambana na askari wa makaburu. Nia ya makaburi ni kutuvuruga sisi huku na kufanya wana-ukombozi walio ndani na nje ya Afrika Kusini kuchanganyikiwa. Vita vya Ukombozi tayari vimevuka hatua ya kutumia mawe na marungu. Awamu hii ni ya kutumia silaha za moto. Hivyo, na sisi tuwe tayari kujitoa muhanga ili matunda ya uhuru yapatikane kwa watu wetu", Bon alisema.
Willy alikuwa karibu kuzungumza jambo fulani, mara simu ililia. Wote waliangaliana halafu Willy aliamua kusikiliza simu.
"Hallo", Willy aliitikia.
"Mimi ni mzee Hamisi, naomba kuzungumza na Willy", sauti ya mzee Hamisi ilisikika.
"Mwenyewe nazungumza, habari za saa hizi mzee", Willy alijibu.
"Habari ni nzuri, Willy nakuhitaji uje hapa nyumbani kwangu haraka kwani nina habari muhimu sana", Hamisi alisema, Willy alisita kidogo halafu akamjibu.
"Sawa, nakuja", halafu alikata simu bila kusema maneno zaidi.
"Huyo ni nani?", Mike aliuliza.
"Ni mzee Hamisi, anasema ni lazima niende nyumbani kwake kwani ana habari muhimu", Willy alibu.
"Hivi sasa itabidi mimi, Rocky na Nyaso tuandamane mpaka kwenye jumba la F.K. Sisi tutafanya utafiti halafu turudi hapa", Bon alishauri.
"Hiyo ni sawa, wewe Mike huna budi kubaki hapa. Kama kuna habari zozote, tutawasiliana. Bon na Rocky ni lazima kuchukua tahadhari kubwa kwani katika mazingira ya jumba kama lile, kunaweza kukatokea jambo lolote", Willy aliasa.
"Huyu Hamisi anakaa wapi?", Nyaso aliuliza.
"Anakaa kwenye nyumba za maafia huko Kijenge, karibu na barabara iendayo Themi Hill. Kwa hiyo tutaondoka wote halafu nyinyi mtaniacha barabarani. Baada ya kuzungumza na mzee Hamisi, mimi nitatafuta njia yangu mwenyewe ya kurudi ili tukutane hapa tena. Sasa Nyaso, wewe telemka chini na kutusubiri kwenye gari", Willy alielekeza.
Wote watatu walichukua silaha ambazo walifikiri wangezihitaji. Willy pia, ingawa alikuwa anakwenda kwa mzee Hamisi, alichukua silaha akiwa tayari kwa lolote. Wanaume walishajuwa kwamba walikuwa wanawinda na huku wakiwindwa. Mike ambaye alikuwa na jukumu la kubaki pale hotelini, naye alikaa tayari na silaha zake. Walipokuwa tayari, walielekea kwenye gari huku kila mmoja akitumia njia tofauti na wenzake.
HOFU
KABLA YA USIKU WA MANANE
III
"Ahsante". F.K. alimwambia mzee Hamisi baada ya kuzungumza na Willy.
"Hebu ondoa huo mtutu wa bunduki kwenye kichwa changu. Unajua mimi ni mzee sana na kuniweka katika hali hii kunaweza kunisababisha nipate ugonjwa wa moyo. Kazi uliyotaka nimekufanyia, zaidi unataka nini", mzee Hamisi aliuliza.
"Ha ha", F.K. aliangua kicheko kwa jeuri halafu akaendelea, "Mzee Hamisi sina budi nikushukuru kwa yote uliyonifanyia, maana bila kupata habari ulizonipa mipango yangu isingefikia hatua hii. Wewe ni mtu mwenye ujuzi na uzoefu katika shughuli za usalama. Sina shaka umeshahisi kitu gani kinatendeka baada ya kuona unavamiwa na kundi la Wazungu. Hawa ni askari kutoka Afrika Kusini. Ufahamu fika kwamba wewe ni msaliti wa nchi yako. Hii imetokana na nyinyi watu wenye vyeo Serikalini kupenda pesa. Pesa nilizokupa zilikufanya uisaliti nchi yako. Ha ha! Uchu wa pesa utaimaliza Afrika. Je, unajua adhabu ya usaliti ni nini", F.K. aliuliza kwa kebehi.
"Usiniue F.K. kwani hata ukiniua, Willy atakumaliza...", Hamisi alisema huku akipapatika.
"Stumke, fanya kazi yako", F.K. aliamrisha, mzee Hamisi aliinuka na kabla hajachukua bastola yake kutoka kwenye koti, alipigwa risisa ya paja na kichwani na kufa papo hapo.
"Sasa msubiri Willy. Nina imani kazi yenu itakuwa rahisi", F.K. alisema huku akimpa Stumke swichi ya gari lake. Stumke alikuwa kiongozi wa yale majasusi yaliyomvamia mzee Hamisi, na ambayo sasa yalikuwa yakimsubiri Willy. Baadaye F.K. alichukua funguo za marehemu Hamisi kutoka mezani kwake na kuaga.
"Stumke, tuonane nyumbani. Lakini nawashauri mkae macho sana. Ingawaje Willy atakuja bila tahadhari, ni mtu hodari kupindukia. Msimpe mwanya bali mtumie mbinu zote mnazozifahamu", F.K. alionya.
"Usiwe na wasiwas, F.K. mimi nilikwisha ongoza kundi hili hili na kuteketeza kikosi kizima huko Namibia. Itakuwaje tushindwe mtu mmoja?, Huyo mfute kutoka kwenye orodha ya adui walio hai. Labda asitokee!", Stumke alijigamba.
HOFU
KABLA YA USIKU WA MANANE
IV
Willy na wenzake walikuwa wanaingia kwenye barabara kuu iendayo Themi Hill. walipishana na F.K. ambaye alikuwa akiendesha gari la Hamisi na kuelekea mjini. Si F.K. wala Nyaso ambaye alimtambua mwenzake kwani wote walikuwa wanaendesha magari ambayo hayakuwa yao. Lakini Willy aligeuka na kuliangalia gari hilo ambalo lilikuwa linakwenda kasi na kupotea gizani.
Hilo ni kama gari la mzee Hamisi", Willy alisema baada ya kugutuka.
"Itakuwaje akuite halafu atoke", Bon aliuliza kwa mshangao.
"Hapo sasa", Willy aliitikia.
"Kama una hakika ni lenyewe, basi hilo siyo jambo la kawaida", Rocky alisema.
"Huenda ameona nimechelewa hivyo akaamua anifuate", Willy alijibu.
"Lakini hatujachelewa hata kidogo", Rocky alijibu.
Wakati huo walikuwa wamekaribia sehemu ya Kijenge ambako Hamisi alikuwa anakaa.
"Nyaso! Simama hapo pembeni", Willy alisema, Nyaso alijisikia raha kwani alijua yeye alikuwa msichana peke yake aliyepata fursa ya kuwaendesha wapelelezi mashuhuri wa Afrika, hasa wakiwa katika harakati za mapambano. Alisimamisha gari pembeni mwa barabara na Willy akatelemka.
"Haya nendeni lakini jihadharini sana. Huko mwendako panaweza kuwa moto. Nawatakia kila la kheri", Willy alisema.
"Ahsante", Bon na Rocky walijibu kwa pamoja.
Nyaso aliendesha kuelekea Themi Hill baada ya kumwacha Willy. Willy naye taratibu aliambaa kwa kufuata ua wa sehemu hii kuelekea nyumbani kwa Hamisi. Nyumbani kwa marehemu mzee Hamisi Stumke alikuwa amepanga watu wake tayari.
"Mtu huyu akiingia sharti auawe pale pale. Hakuna kusubiri. Yeyote atakayekuwa kwenye sehemu nzuri ya kumuua lazima afanye hivyo mara moja. Kama tulivyokwisha ambiwa, mtu huyu ni hatari sana. Kila mtu awe macho", Stumke aliwaonya wenzake.
Stumke alitokomea gizani. Aliambaa kwenye ua huku akielekeza macho na mawazo yake kwenye lango la nyumba. Majasusi wengine wawili walikuwa wamejibanza kwenye ua. Mmoja wao mwingine alikaa langoni kwani yeye ndiye ambaye angemfungulia Willy. Kila wakati waliposikia muungurumo wa gari, walijiweka tayari lakini hakuna gari lililojitokeza pale nyumbani. Gari la Nyaso liliposimama Stumke kutokana na uzoefu wa kazi yake, alihisi huenda mtu wao angeweza kuteremshwa njiani na kuingia pale kwa kutembea. Hivyo aliwashauri watu wake wawe macho kama mtu huyo angeingia kwa miguu.
Kengere ya ilani ilizidi kulia kichwani mwa Willy baada ya kila hatua aliyopiga kuelekea kwenye nyumba ya Hamisi. Ilikuwa kawaida yake kwamba kila hali hiyo ilipotokea, Willy alichukua tahadhari ya hali ya juu. Wakati huo huo Willy alimua kupita mlango wa nyuma badala ya mbele ya nyumba ile. Alizunguka ua wa nyumba huku akinyatia kama nyani. Aliruka ua huo wa michongoma na kutua ndani kwa kishindo kidogo.
Jasusi aliyekuwa upande wa kulia aligutuka kidogo halafu akaamua kuja kuangalia kuna nini. Alikuja kwa mwendo wa kunyatia kiasi kwamba hakutoa sauti yoyote. Lakini kwa kuwa masikio ya Willy yalikuwa na uzoefu kama wa mnyama awindwaye porini, aliweza kusikia mtu anajongea. Willy aliinuka mara moja na kujibanza kwenye pembe ya kulia ya nyumba. Aliangalia kwa chati na kuona yule kaburu anasogea huku bastola ikiwa mkononi. Macho ya Willy kama ya wale majasusi yalishazoea giza. Hivyo aliweza kuona vizuri.
Willy alikuwa na bastola mkononi, mara akaamua kuirejesha mahali pake, akajitayarisha kumkabiri jasusi yule kwa mikono. Pale pale akijuwa kuwa kuitwa kwake kulikiwa ni mtego na kwa hiyo ilibidi awe tayari kwa mapambano. Yule jasusi alisogea karibu kabisa na pale Willy alipokuwa amejibanza. Willy alimwacha afike kabisa kwenye usawa alipokuwa amesimama. Ndipo alipomrukia na kumkaba koo kiasi kwamba yule jasusi hakuwa na muda wa kuweza hata kukohoa. Willy alivunja shingo ya yule jasusi ambaye alikata roho bila kutoa sauti. Taratibu Willy aliilaza chini maiti yake.
Jasusi mwingine alipoona mwenzake anakawia kurudi, alitoa ishara kwa yule aliyekuwa kwenye lango. Alikuwa anamjulisha kuwa anaelekea nyuma ya nyumba. Wakati huo damu ya Willy ilikuwa tayari imechemka kwa hali ya vita. Mara alimwona jasusi mwingine anakuja mbio. Willy alimsubiri huku akimwemwesa kwani alikuwa anakwenda hovyo bila tahadhari yoyote. Lakini alipokaribia mahari Willy alipokuwa, yule jasusi alisimama kana kwamba alikuwa amegutushwa na jambo fulani. Willy alijua kuwa kama angesubiri, bila shaka angeonekana. Kama risasi, Willy alifyatuka na kumrukia yule jasusi pale alipokuwa amesimama. Alimkata mkono wa karate na kumpasua kichwa. Wote walianguka chini.
Walianguka kwa kishindo ambacho kilimshitua Stumke na yule jasusi aliyekuwa kwenye lango. Wakiwa kama watu waliotiwa ufunguo walikimbia kuelekea mahali alipokuwa, mmoja akipitia kushoto na mwingine akipita kulia. Hapo hapo Willy aligundua kuwa jasusi yule alikuwa kafa, hivyo aliinuka haraka. Aliruka kama nyani na kukamata sehemu ya juu ya ukuta. Alijipinda na kupanda juu ya paa akajibanza. Mara tu baada ya kupanda juu ya paa ya nyumba, Stumke na mwenzake walifika sehemu ambayo Willy alikuwa amesimama muda kitambo. Walikuta wenzao wawili wamekufa. Waliingiwa na woga sana.
"Grande, mtafute haraka tumuue, unasikia", Stumke alimwamrisha mtu wake wasiwasi mwingi.
"Willy, uko wapi? njoo tuonane uso kwa uso kama kweli wewe ni mwanaume", Grande alisema kwa sauti. Willy ambaye alikuwa amelala juu ya paa alijisikia raha alipoona majasusi yale yanapaparika kwa woga. Mara aliinuka na kwa spidi kubwa Willy alijirusha katikati yao. Lakini wakati akiwa bado yuko hewani aliipiga teke bastola ambayo Grande alikuwa nayo mkononi. Silaha hiyo ilianguka upande wa pili wa ua. Stumke ambaye alikuwa ameangalia upande mwingine aligeuka na kufyatua risasi. Wakati ule ule Willy alijiviringisha chini na risasi zile zikampata Grande.
"Stumke, umeniua! Aibu", Grande alilalamika halafu akakata roho pale pale. Willy aliamka na kumwahi Stumke. Aliipiga teke bastola yake ambayo iliruka na kutua juu ya paa ya nyumba. Mara mapambano makali yakaanza.
Stumke alimpiga Willy teke la tumbo ambalo lilimpata barabara na kumwangusha chini. Kabla hajaweza kusimama, Stumke alimwongeza teke jingine la ubavuni. Halafu aliamua kumrukia ili ammalize kabisa. Kumbe Stumke alikuwa amefanya makosa. Wakati huo huo Willy alijiviringisha kidogo na Stumke akamkosa. Willy alijipinda na kusimama. Alikuwa amejisikia damu yake imeanza kwenda mbio kutokana na kupigo. Hasira zilikuwa zimempanda. Angeweza kummaliza Stume pale pale, lakini Willy alimpa nafasi naye ainuke. Jambo hilo lilimshangaza sana Stumke.
"Simama kaburu mshenzi, wee! Ulichokuja kutafuta leo utakipata. Kama mlifikiri mkutano hautafanyika mlijidanganya. Wakati ukiwa jehanamu mkutano utakuwa unaendelea", Willy alisema kwa hasira.
Stumke alikuwa bingwa wa karate katika jeshi la KULFUT. Hivyo alimsikitikia Willy kwani alifikiri angeweza kumamliza mara moja. Aliamini kwamba hakukuwepo mtu yeyote kutoka katika nchi za Afrika ambaye angediriki kupigana naye. Stumke alikuwa mwoga kila mapambano yalipokuwa sura ya kutumia silaha kama vile bastola. Lakini kama mtu alipambana naye kwa kutumi mbinu za karate, basi Stumke alimhesabu mtu huyo kuwa ni marehemu.
"Utajijutia leo", Stumke alisema. Mara alimrukia Willy na kutoa mapigo matatu ya karate ambayo hata Willy hakutarajia kamwe. Stumke alishangaa kwani Willy aliyazuia yote. Ni mara chache ambazo Stumke alikuwa ametumia mapigo ya namna hiyo wakati wa mapambano. Na kila alipoyatumia ni watu wachache ambao waliweza kuyazuia. Jambo ambalo alikuwa hajui Willy alikuwa Ninja.
Stumke alibadili mbinu na kutumia zile za hali ya juu kabisa. alitoa pigo la kwanza ambalo Willy alilikwepa. Alitoa pigo na pili na Willy alilizuia. Alipotoa pigo la tatu Willy alimkamata mkono ghafla. Aliukata kwa kiganja chake nao ukavunjika. Hata hivyo Stumke alijirusha na kumpiga Willy teka farasi ambalo lilimwangusha chini. Wakati huo huo Stumke aliguna kutokana na maumivu ya mkono wake uliovunjika. Alimtupita teke la mauti Willy lakini alikuta patupu! Willy alikuwa amejipinda kama swala na kuushika mguu wa Stumke akiwa bado hewani. Aliupinda na kufyatua mfupa wa goti.
Willy alimsukumiza Stumke kwenye ukuta ambapo aligonga kichwa chake na kuona nyota. Fahamu zilimpotea. Willy alimfuata kasi na kumkata karate iliyoacha mkono wake wa pili bila kuwa na kazi. Alimtingisha huku akisubiri fahamu zimrudie. Stumke alipopata fahamu, alijuwa kuwa ameshindwa. Hivyo kama lile jasusi Paul lilivyokuwa limefanya, Stumke alitoa ulimi wake nje na kuukata haraka kwa meno. Kwa haraka, Willy alimtia ngumi moja Stumke halafu akamwacha akate roho kwa kutokwa na damu.
"Ama kweli majasusi hawa ni watu wa ajabu. Kujiua kwa kujikata ulimi ni jambo geni kabisa", Willy alijisemea huku akielekea ndani ya nyumba. Mle ndani alikuta maiti ya mzee Hamisi. Hapo hapo akagudua kuwa mzee hamisi alikuwa amelazimishwa kumwita ili aje auawa kama yeye. Vile vile Willy aligundua kuwa kama majasusi hawa waliweza kuutumia uhusiano wake na Hamisi, basi tayari walikuwa na habari nyingi juu yao. Willy alijipongeza, bahati yake nzuri kwani mtego waliokuwa wamemwekea ilikuwa bahati kuukwepa.
Mara wazo likamjia. Alifikiri jinsi F.K. alivyokuwa anaaminiwa hapo Arusha kuwa mtu mwaminifu kwa Serikali na Chama. Kama kweli anahusika, bila shaka ndiye anayetayarisha mpango mzima. Mzee Hamisi asingeweza kumhisi kitu F.K. Ndio sababu waliweza kumwingia kwa urahisi. Mzee Hamisi alikuwa anajulikana kama mtu matata. Isingekuwa rahisi kwake kuuawa 'kike' hivyo. Willy aliamua kurudi alipokuwa amelala Stumke. Alimkuta bado hajakata roho kabisa. Alimpapasa ili kuona kama angepata kielelezo chochote. Hakukuta kitu bali funguo za gari. Alizichukua na kuelekea sehemu ya mbele ya nyumba.
Alikuta gari aina ya Benz. Alichukua kalamu yake ambayo ilikuwa na tochi vile vile, na kumulika kwenye karatasi ya bima iliyokuwa imebandikwa katika kioo cha mbele cha gari. Bima hiyo ilikuwa imechukuliwa kwa jina la Feroz Kassam. Kwa kutumia funguo zile zile, Willy alifungua mlango wa gari na kuingia ndani. Aliwasha gari lile na kuondoka. Wakati akiendesha Willy alijikuta akisema.
"We gari, nipeleke nyumbani kwenu, na leo hii bwana yako atanitambua!".
HOFU
KABLA YA USIKU WA MANANE
V
"Jumba lenyewe ni lile pale", Nyaso aliwaonyesha mara walipofika kwa F.K.
"Seng'enge yote ile mnayoiona imezunguka eneo la jumba hilo", waliangalia eneo hilo kwa makini kwani kila sehemu ilikuwa inawaka taa.
"Hili ni jumba hasa", Rocky alisema.
"Wacha kulishangaa kwa nje. Ndani yake ni zaidi. Siku moja mimi nililala humo. Mara nilisikia mlio wa vitu fulani kutoka chini. Nilipomwuliza nini ilikuwa, F.K alijibu huku akiwa mwenye nusu usingizi.
"Hao ni watu wanafanyakazi huko chini, wewe lala usiwe na wasiwasi. Mambo haya hayakufai! Siku hiyo ndiyo nilijuwa jumba hilo lilikuwa na vyumba chini ya ardhi. Siku nyingine F.K alifurahi sana halafu akanieleza kwamba, kama lingetokea jambo la dharura, jumba lile lina njia mbili za kutokea nje kupitia chini kwa chini. Aliongeza kusema kwamba njia moja ilitokea Magharibi na nyingine ilitokea Kusini mashariki mwa jumba hilo. Alinieleza pia kwamba kwa nje mtu yeyote angefikiri labda sehemu ya nje ni mahali palipofunikwa tu. Aidha mfuniko wa njia ulionekana kama ule wa machafu", Nyaso alieleza huku akiendesha pole pole.
"Mimi naona usimame hapa. Sasa hivi ni saa nne kamili. Sijui utaegesha wapi halafu utasubiri, tusingependa waone gari lako", Bon alimwambia Nyaso.
"Itawachukua muda gani?", Nyaso aliuliza.
"Tupe nusu saa. Ukikuta hatujarudi, ujuwe mambo yameharibika. Hivyo utakwenda Hotelini na kumweleza Willy", Bon alijibu.
"Una maana gani?", Nyaso aliuliza.
"Usiniulize maswali, fanya kama nilivyokwambia kwani hiyo itakuwa rahisi kwako", Bon alijibu kwa sauti kali kidogo.
"Haya bwana, mimi nakwenda kwa rafiki yangu hapo juu kwenye nyumba za wasabato. Saa nne na nusu juu ya alama nitakuwa hapa", Nyaso alijibu.
"Sawa, tutakuwa tumejibanza kwenye mti ule pale", Bon alieleza na halafu wakatelemka. Nyaso aliondoka huku roho ikimdunda.
Kufuatana na maelezo ya Nyaso, jumba hili linazo njia mbili za kuingilia kwa chini. Moja iko magharibi na nyingine iko kusini mashariki, wewe utaingilia magharibi na mimi nitapita kusini mashariki. Kama hatukuonana ndani basi tukutane mahali petu kabla ya saa nne na nusu", Bon alimweleza Rocky.
Wote walitazamana kwa hisia zao zilizowajulisha kwamba walikuwa wanaingia mahali pa hatari. Huku wakiwa wamejidhatiti, walipeana mikono na kuingia kazini. Rocky alikuwa wa kwanza kuona mfuniko ulioziba mlango wa njia. Aliuinua taratibu na kuona ngazi za kutelemkia chini. Aliuweka kando mfuniko ule ili wakati wa kutoka nje usije ukampa tabu. Baada ya kufanya hivyo, alichukua tochi yake yenye saizi ya kalamu akamulika na kutelemka ngazi jambo ambalo Rocky hakufahamu ni kwamba wakati mfuniko ule ulipofunguliwa ulikuwa unapeleka miale ya ilani, ambayo ambayo ilionekana kwenye televisheni iliyokuwa chumbani, kwa ajili ya usalama.
Dave alikuwa ndani ya chumba cha kumi akiangalia helikopta ya namna yake ambayo ilikuwa chumbani tayari kwa ajili ya kuwachukua majasusi baada ya kufanya maovu yao. Mara alisikia jasusi mmoja kwa jina la Terre akimwita. Terre na wenzake wawili walikuwa wamejinyoosha kwa mapumziko. Aligutushwa na makelele kutoka kwenye televisheni pamoja na picha ya mtu aliyeonekana akiingia kwenye njia ya siri upande wa magharibi. Dave alipofika na kuona picha hiyo, aligundua mara moja kwamba yule alikuwa Rocky kutoka Zimbabwe. Dave aliweza kumtambua Rocky kwa sababu alikuwa ameonyeshwa picha za wapelelezi mashuhuri wa Afrika, majina yao na nchi walizotoka.
"Haya sasa, kazi imebaki kwenu. Huyu amejileta mwenyewe badala ya sisi kumtafuta. Terre na Gary nendeni kwenye mlango ule. Akifungua tu nataka mmalize mara moja. Sisi tunamwona lakini yeye hatuoni. Hivyo kazi yenu itakuwa rahisi. Hakuna haja yangu mimi kuhangaika. Nitakuwa nawaangalia kwenye televisheni. Sitaki mtumie bastola bali mikono yenu. Hapo ndipo watu hawa watatambua sisi ni nani", Dave aliamrisha huku furaha imemjaa. Dave na Howe walikaa tayari kushuhudia mapambano ambayo yangefuatia.
"Huyu ni chakula chetu", Terre alijibu huku akiondoka pamoja na Garry. Walikuwa wamepandwa na mori kwani walitaka kuonyesha uhodari wao, pia kuwa mtu wa kwanza kumuua mpelelezi mashuhuri wa Afrika. Bila kujua kuwa alikuwa anaonekana kwenye televisheni, Rocky aliendelea taratibu kwa tahadhari kubwa sana. Alipomaliza ngazi za kwanza, aliufikia mlango. Upande wa pili wa mlango, Terre na Garry alikuwa wakisubiri tayari.
Ili wamsaidie kuingia kwenye mtego, walikuwa wamefungua mlango na kuuacha umerudishiwa tu. Rocky alipojaribu kufungua mlango alikuta umerudishiwa. Kutokana na uzoefu wake wa kazi wa muda mrefu. Rocky alifungua mlango ghafla na kwa nguvu. Terre na Garry walitarajia Rocky angefungua taratibu na kuendelea kutembea. Badala yake alijirusha chini kwenye njia. Alifanya kitu ambacho hakikutarajia mpaka wakashindwa kufanya yale waliyokuwa wamepanga. Alijiviringisha chini na kujipinda huku akichukua bastola yake. Alifyatua risasi mfululizo ambazo zilimpata Terre na Garry. Wote wawili walikufa pale pale.
Dave na Howe ambao walikuwa wanafuatilia mapambano kwenye televisheni, walishangazwa na kitendo hicho cha Rocky chenye kuonyesha ujuzi wa hali ya juu.
Howe, twende tukamkabiri kwani naona mtu huyu ni hatari sana. Chukua bastola na mimi nipatie moja", Dave alimwagiza Howe.
"Wewi ni Ninja, huyu atakuwa nini kwako?", Howe alimpambisha Howe moto.
"Unasema kweli, kama hujaniona basi leo utaniona", Dave alijigamba huku wanaelekea kwenye mlango katika njia ambayo Rocky alikuwa akitokea.
"Dave, nafikiri tusisogee kwenye mlango kwani mtu huyu anaweza kutufanya kama Terre na Garry. Heri tumsubiri hapa. Kwa kuwa chumba hiki ni kipana kiasi cha kutosha, hata kama akijirusha bila shaka ataimba tu", Howe alisema huku akijitayarisha na kumwangalia Rocky kwenye televisheni kwa mara ya mwisho. Rocky aliendelea kunyata na kuusogelea mlango wa chumba kile cha mapumziko.
Mlango wa sita wa maarifa ulimjulisha Rocky kwamba chumba alichokuwa akisogelea kilikuwa cha hatari zaidi. Hivyo alichukua tahadhari zaidi. Alikuwa tayari amepandwa na mori wa kupigana. Kwa hiyo alijiona kuwa alikuwa na uwezo wa kupabana katika hali yoyote ile. Dave ambaye alikuwa amesimama pembeni karibu na mlango ule, alitarajia Rocky angejirusha chini baada ya kufungua. Badala yake Rocky aliruka hewani na kuufungua mlango kwa kuupiga teke akitumia miguu yake miwili. Wakati bado akiwa hewani, Rocky alijipinda na kutua njiani nyuma yake. Howe aliyekuwa anasubiri Rocky kwa hamu alifyatua risasi tatu ambazo zote zilikosa Rocky. Kitendo cha sasa cha Rocky kilikuwa hakikutarajiwa pia.
Dave alimtolea ishara Howe ili amfuate Rocky. Howe alijiviringisha chini kwenye njia huku akifyatua risasi ambayo ilimpata Rocky kwenye mkono wa kushoto karibu na bega. Wakati huo huo Rocky aliachia risasi ambayo ilimpata Howe kwenye paji la uso. Alikata roho pale pale. Akiwa anasikia maumivu makali. Rocky alikimbia mpaka nyuma ya mlango kulikokuwa na maiti ya Terre na Garry. Alirudisha mlango huo. Alichana shati lake mwenyewe na kujifunga mkono ili kuzuia damu isitoke kwa wingi. Dave alijuwa Rocky alikuwa ameumia hivyo alimfuata na kufungua mlango ule. Rocky alikuwa ameweka bastola yake chini. Dave aliruka na kumkumba Rocky na wote wakajiviringika chini.
"Rocky! Unakufa sasa", Dave alisema kwa sauti ya juu. Rocky alikuwa anasikia maumivu makali lakini hali halisi ilimfanya asahau maumivu hayo. Aliinuka haraka akiwa tayari kukabiliana na jasusi hilo. Hapo mapambano makali yalianza. Dave alimshambulia Rocky kwa mapigo safi yapatayo saba lakini yote yalizuiwa. Hapo ndipo Dave alipogundua kuwa alikuwa anapambana na mtu mwenye ujuzi zaidi ya vile alivyotarajia. Hivyo aliamua kutumia mafunzo ya U-Ninja. Vile vile Rocky aligundua kuwa Dave alikuwa na ujuzi wa hali ya juu. Hivyo ilimbidi atumie mbinu kali kuweza kumshinda adui.
Dave alitupa ngumi lakini Rocky aliikwepa nayo ikagonga ukuta na kulitoa tofari moja lililoangukia upande wa pili. Wakati huo huo Rocky alichukua nafasi hiyo kumtia mapigo makali Dave ambayo yalimfanya aanguke chini. Hapo aliamua kuchukua bastola yake kwani aliamini kuwa mtu huyu hakuwa saizi yake. Hivyo alijirusha lakini kabla hajawahi kuichukua bastola yake iliyokuwa chini, Dave naye aliruka na kumwahi Rocky hewani alipompiga teke la kichwa. Rocky alipoteza fahamu na kuanguka chini kwa kishindo.
Bon alikuwa amenyatia toka chumba hadi chumba wakati alipofika kwenye chumba cha televisheni alimwona Dave anampiga Rocky teke la kichwa. Bon aligundua kwamba Rocky alipigwa teke la ki-Ninja ambalo asingeweza kulistahamili.
Bon alikimbia haraka kuelekea kwenye njia ambayo aliamini ndiko walikuwa wakipigania huku hasira na chuki zimemjaa. Rocky alikuwa anapigana kishujaa. Bon alipofungua mlango na kuingia kwenye chumba walichokuwa wanapigania, kumbe alikuwa amechelewa. Dave alikuwa amemrukia Rocky na kumpiga teke la moyoni ambalo lilimuua pale pale Rocky.
"Kufa mbwa mweusi, we!" Dave alitukana. Mara aliona mlango unafunguliwa ghafla na Bon akiingia ndani.
"Mbwa we, umemuua Rocky, nawe utaambatana naye mpaka peponi", Bon alisema kwa uchungu huku machozi yakimtoka. Bon alikuwa na bastola mkononi. Angeweza kumpiga risasi Dave. Lakini badala yake aliitupa kando. Dave alishangazwa na kitendo cha Bon. Vile vile alimwonea huruma kwani aliamini hakuna mtu mweusi ambaye angepambana naye kwani yeye alikuwa ni Ninja.
"Pole sana mbwa mweusi! Na wewe umejileta kwenye kaburi lenu", Dave alijibu kwa dharau. Bila kuchelewa Bon alimrukia Dave na kumpiga vipigo, moja baada ya kingine mpaka akaanguka chini. Lakini alijiviringisha na kuinuka haraka tayari kumkabiri Bon. Bon hakumpa nafasi kwani kabla hajasimama sawa sawa Dave alipewa vipigo kadhaa ambavyo vilimtatanisha. Pale pale alijuwa kwamba alikuwa anapambana na Ninja kama yeye mwenyewe, Bon aliruka na kumtia Dave teke la ubavuni na kumzidishia hasira.
Bon alimwahi Dave na kumpiga teke moja la shingoni na jingine la kichwani kwa wakati ule ule, ambayo yalimfanya Dave achanganyikiwe. Bon alipima hali ya Dave na kuona mbaya. Hivyo alichukua nafasi hiyo na kumtia pigo takatifu la kifuani ambalo lilikibomoa na kufanya damu ifumke na kutapakaa kila mahali. Kabla dave hajaanguka chini, Bon alimwonyesha kiganja na kama kusema. 'pigo linalofuata ni kisasi cha Rocky! Alimzibua tumbo na kuyatoa matumbo ya Dave nje'.
"Kufa Kaburu mshenzi, we!" Bon alisema kwa hasira. Dave alianguka chini akiwa maiti. Bon aliangalia saa yake. Ilikuwa saa tano kasoro dakika tano.
HOFU
KABLA YA USIKU WA MANANE
VI
Ilikuwa yapata saa tano hivi wakati Willy alipokuwa anaegesha gari la F.K karibu na ofisi za mjini za mauzo ya General Tyre. Alikwenda haraka kwenye hoteli yake. Alibisha hodi kwenye chumba chake Mike akamfungulia.
"Vipi mwenzetu, mbona umenuna", Mike alimwuliza Willy.
"Hatari, akina Bon hawajarudi?", Willy aliuliza.
"Bado, mimi nina wasiwasi mkubwa", Mike alisema, "Je, umeonana na mzee Hamisi?".
"Mzee Hamisi ameuawa. Sasa hivi mtu wetu ni F.K. Hivi ninavyokueleza, nimeshaua makaburu wanne", Willy alisema na kisha alianza kumsimulia Mike yote yaliyotokea.
"Hivyo Mike, hapa mjini kuna kundi kubwa la makaburu wenye ujuzi mkubwa wa kupigana", Willy alimalizia.
"Kama ni hivyo, mimi napendekeza tulivamie jumba hilo kwani bila shaka majasusi wako humo. Nashauri kwamba kama ikibidi, tuombe msaada wa polisi ama jeshi", Mike alisema.
"Hapana Mike, kazi ya kupambana na majasusi haistahili kuhusisha polisi ama jeshi, kwani wao wanaweza kutumia mbinu za kijeshi tu na kusababisha maafa makubwa. Inatubidi sisi wenyewe tufunge vibwebwe na".... kabla hajamaliza sentensi, alisikia mtu anabisha hodi kwa kugonga mlango. Bastola za wanaume hawa zikawa tayari mikononi. Kwa tahadhari kubwa. Willy alifungua mlango huku bastola yake mkononi.
"Ni mimi....", Nyaso alisema kwa hofu alijikuta amekabiliana na mtutu wa bastola.
"Pole, usiwe na wasi wasi", Willy alisema huku akimvuta Nyaso ndani na kuurudisha mlango.
"Wenzako wako wapi?", Mike alimwuliza Nyaso huku akitweta.
"Waliniambia niwapitie saa nne na nusu. Nilipokwenda kwenye sehemu tuliyoagana, sikuwakuta. Hapo mwanzo walikuwa wamenieleza kwamba kama nisingewakuta basi ilibidi nije moja kwa moja huku ili niwaambie nyinyi", Nyaso alijibu huku machozi yakimlenga. Willy aliangalia saa yake na kuona kwamba ilikuwa saa tano na dakika kumi za usiku.
"Nyinyi subirini hapa. Mimi nitakwenda kuchunguza nini kimetokea, maana tukiondoka wote tunaweza kupishana nao, hivyo tutakuwa tumewachanganya. Nipeni mpaka saa sita na nusu, kama hamkuniona basi mjuwe mambo yameiva hivyo njooni", Willy aliwaambia.
"Hapana Willy, tuondoke wote. Nyaso atabaki hapa ili kama akina Bon wakirudi atawaambia watufuate", Mike alisisitiza.
"Hapana Mike, Willy halielewi sawa sawa lile jumba. Sharti nifuatane naye ili nimwelekeze", Nyaso alisema.
"Sawa Mike, utabaki hapa nami nitafuatana na Nyaso. Akisha nionyesha atarudi hapa. Kama ikifika saa sita na wewe hujaniona, basi nifuate", Willy alitamka.
"La hasha, mimi nitabaki huko na wewe....", Nyaso alisema na huku Willy akimkatisha.
"Nyamaza! Wewe unajuwa watu wale pamoja na bwana yako ni wauaji. Je, unataka kufa ama nini", Willy alisema kwa ukali.
"Hebu usiniambia kuwa bwana yangu ni muuaji! Kuna tofauti gani kati yake na wewe. Nyote wauaji tu. Kwani mimi nilifahamu kuwa yeye ni muuaji?", Nyaso alijibu kwa hasira. Willy alishikwa na hasira nusura ya kumnasa kibao Nyaso. Lakini Mike aliingilia kati.
"Basi basi, acheni hayo. Tunapoteza muda wetu. Wewe Nyaso usipende kugombana na wanaume. Utaumia. Mpeleke Willy kama alivyokwambia.
Nyaso alimtazama Willy kwa macho ya upendo. Alimkimbilia na kujilaza kifuani kwake huku akisema kwa sauti nyororo.
"Samahani Willy, sikuwa na maana hiyo. Nakupenda, tafadhali jihadhari", Willy alimvuta na wote wakatoka nje.
"Nawatakia kila la heri", Mike alisema.
"Ahsante!", Willy na Nyaso walijibu kwa pamoja wakati wakitoka nje.
HOFU
KABLA YA USIKU WA MANANE
VII
Mnamo muda wa saa tano na robo za usiku F.K, PG, George na vijana wao walikuwa wanarudi Themi Hill nyumbani kwa F.K. Hii ilikuwa baada ya kutega mabomu kwenye ukumbi wa mikutano wa AICC.
"Kesho Afrika itagwaya", P.G alisema.
"Kesho, watu hawa watatambua nguvu zetu. Tanzania imezidi kuzihamasisha nchi zilizo mstari wa mbele lakini baada ya kesho serikali itawafukuza wapigania uhuru wote kutoka nchini. Hiyo inatokana na kwamba baada ya pigo la kesho, tutatoa tangazo kuwa kama wataendelea kuwasitiri wapigania uhuru, tutaingia Ikulu na kutia kipigo", George alijigamba huku F.K akiegesha gari mbele ya nyumba yake. Walipotelemka walishangaa kuona kwamba gari la F.K lilikuwa bado halijawasili.
"Lo, hii ina maana kuwa Stumke na wenzake bado wanamsubiri Willy?", George aliuliza.
"Sidhani..." P.G alisema kwa sauti yenye kuonyesha wasiwasi kwamba kuna jambo ambalo halikwenda sawa. Waliingia ndani kwa kupitia mlango wa mbele. Walikwenda moja kwa moja mpaka kwenye chumba cha mapumziko walipokuwa wamemwacha Dave na wenzake. Walifungua mlango na kuingia ndani. Walipoangalia kwenye televisheni waliona maiti zimelala njiani.
"Mungu wangu", wote walisema kwa pamoja huku wakikimbilia yalipokuwa maiti.
"Mambo makubwa haya", F.K aligwaya.
"Sasa kazi imeanza", George alisema huku akiangalia maiti ya Dave na yale ya Rocky.
"Nakubali kwamba hawa watu siyo wa kawaida, njooni hapa niwaeleze", George aliwaita F.K na PG. waliokuwa wakiangalia maiti kwa mshangao. "Kazi hii ni ya Ninja", George alimaliza kusema na kwa mara ya kwanza alijisikia hofu.
"Dave, nitalipiza kisasi kwa ajili yako rafiki yangu", George alisema huku akichukuwa shuka na kuifunika maiti ya Dave. Mara wote walirudi chumbani na kukaa ili kupanga nini wafanye kwani mambo yalikuwa yamebadilika.
"Jamani, mmeona wenyewe jinsi mambo yalivyobadilika. Mimi nahisi Stumke na wenzake wameshauawa. Hata hivyo ni lazima tushinde vita hivi. Hatuwezi kushtushwa na haya yaliyotokea. Kulingana na habari tulizonazo ni kwamba Willy na Bon bado wangali hai. Kuanzia sasa ni wao wawili dhidi yetu watatu na vijana wetu wawili. Ninayo hakika watatufuata hapa kwani wameshajuwa siri yetu. Ni heri tuwasubiri hapa ili tuweze kuwamaliza watu hawa kwanza, tulijiamini kupita kiasi na kuwadharau wao. Lakini askari hawezi kufanya kosa lile lile mara mbili...", George alieleza.
"Maneno yako ni mazuri. Lakini mimi napendekeza tuwafuate kwa kuwa wanajuwa mahali tulipo. Kuna uwezekano wakatafuta msaada wa polisi na hata jeshi ili kutuvamia. Huo utakuwa mwisho wa kazi yetu ambayo bado haijamalizika na ushindi bado. Hatuwezi kuruhusu hali hiyo itokee kwani lazima kazi yetu ikamilike", P.G alishauri.
"Hapana P.G, tukifanya hivyo ujuwe tumekwisha. Kwanza tunajuwa watu hawa wako New Arusha Hoteli. Lakini baada ya mambo yaliyotokea ni vigumu kubashiri wao wako wapi. Hatimaye tutaanza kutafutana tusikutane hadi kesho asubuhi. Hiyo ina maana kazi yetu itakuwa haikumalizika usiku huu kama ilivyopangwa. Pili lazima tufahamu kwamba watu hawa ni wapelelezi wa muda mrefu. Wanaelewa sheria ya mchezo huu. Hivyo, amini usiamini, hawawezi kutumia polisi wala jeshi. Watatuwinda wao wenyewe. Muda siyo mrefu watakuja hapa maana mchezo umebadilika. Hivi sasa, sisi ndio wawindwa. Wao wanazo habari kamili kuhusu sisi kama sisi tulivyo na habari juu yao. Lililopo ni kujiweka tayari kupambana nao", George alisisitiza.
"Mimi nakubaliana na maneno yako George. Kama nilivyokueleza hapo mwanzoni, imetokea ghafla tu. Viongozi wa vyama vya ukombozi hawalali kwenye hoteli walizopangiwa. Tena hata polisi hawajui lolote kuhusu viongozi hao. Habari kuhusu viongozi hawa zimekuwa nyeti. Ni wapelelezi hawa tu ambao wanajuwa viongozi hawa wamepelekwa wapi. Nasi tutawaulia mbali washenzi hawa, wasije wakaharibu kazi yangu, ambayo imetokana na mpango wa muda mrefu wa kuleta hofu katika nchi hii. Lazima ushindi ni wetu", F.K aliwatia mori wenzake. Baada ya hapo George alianza kuwaeleza mpangilio wa kujiweka tayari wakati wakisubiri wapelelezi maarufu wa Afrika wakiongozwa na Willy Gamba.
HOFU
KABLA YA USIKU WA MANANE
VIII
Wakati George alipokuwa anawaelekeza wenzake. Willy alikuwa anaagana na Nyaso karibu na nyumba hii.
"Willy, tafadhali jihadhari sana. Nakupenda sana Willy. Tafadhali...", Nyaso alisema kwa sauti ya unyonge.
"Tulia mtoto, usinililie mimi kwani nakwenda kazini. Lakini nitachukua tahadhari na tutaonana baadaye", Willy alisema huku akimvuta Nyaso na kumbandika busu moto moto. Kisha Nyaso alianza kumpa maelezo kuhusu jumba la F.K.
"... Upande wa kushoto kuna madirisha mawili makubwa", Nyaso alimaliza kueleza.
"Unasema Bon na Rocky walipita kwenye njia za siri ulizowaeleza?", Willy aliuliza.
"Bila shaka maana baada ya kuwaelekeza, wote walitoa ishara ya kukubali kwa kutumia vichwa vyao", Nyaso alijibu.
"Oke, mpenzi! Kwa heri", Willy alisema huku akimvuta Nyaso na kumbusu tena.
"Willy tafadhali... tafadhali...", Nyaso alibembeleza huku machozi yakimlenga.
"Usinitilie uchuro, mtoto we!", Willy alisema huku akiyeyuka na kutokomea gizani.
Roho ya Nyaso ilikuwa nzito sana lakini aliwasha gari na kurudi hotelini.
Willy alipanda na kuruka seng'enge akaingia uani. Kwa kuwa taa zilikuwa zinawaka kuzunguka eneo hilo, ilimbidi aende huku ameinama. Kwa kujificha kwenye vivuli vya miti mingi mizuri iliyopandwa kuzunguka nyumba hiyo. Willy hakuonekana na mtu. Alifika kwenye ukuta wa kushoto wa jumba hilo. Alijibanza na kisha kutambaa ili aweze kuona upande wa mbele wa nyumba. Alipofika tu kwenye kona ya jumba hilo, aliliona gari la mzee Hamisi limeegeshwa mbele karibu na mlango. Mara Willy alihisi mambo mawili. Kwanza, Majasusi wa makaburu walikuwa ndani wakimsubiri. Pili, kwamba Bon na Rocky walikuwa wameuawa na ndio sababu walikuwa hawakurudi. Aligundua kwamba alikuwa katika hatari kubwa. Hivyo ilibidi achukue tahadhari zaidi.
Akiwa sasa amelala chini Willy alisikia kishindo. Aligeuka na kuangalia upande huo lakini hakuona kitu. Aliamua kusubiri. Alijua fika kwamba katika mchezo huo, subira ni jambo muhimu. Kumbe aligundua kuwa kile kishindo kilikuwa cha mmoja wa askari wawili waliobakia kwani alimwona anatokea kwenye mti. Alikuwa amepangiwa kukaa juu ya mti huo na kutoa ishara kama angekitilia kitu chochote mashaka. Ajabu ni kwamba askari huyo alikuwa hakumwona Willy wakati alipoingia. Hivyo alikuwa ameamua kutelemka na kupanda mti mwingine. Kutokana na woga baada ya kuona wenzake walivyokufa askari huyo alikuwa anatembelea kwa uangalifu mkubwa. Willy alimwona askari yule karibu naye huku akinyata.
Alimsuburi mpaka walipokuwa sambamba ndipo Willy alipomrukia kwa spidi ya umeme na kumbana mdomo. Alimkata mkono wa shingo na kumuua pale pale. Kisha alimburuza taratibu na kumlaza alipokuwa yeye. Willy aliamua kuingia ndani ya nyumba kwa kupitia dirisha la kushoto. Baada ya kuangaza huku na kule na kuona kwamba kila kitu kilikuwa shwari, alijongea mpaka kwenye dirisha mojawapo na kulikagua. Alikuta limefungwa. Willy alichukua kisu chake maalumu chenye ncha ya almasi na kukata kipande cha kioo kutoka kwenye dirisha. Alipitisha mkono wake kwenye tundu na kufungua dirisha. Kisha alikwea dirishani na kutumbukia ndani ya chumba kilichokuwa giza. Baada ya kusimama tu alisikia sauti inasema.
"Shenzi kabisa". Halafu alisikia kitu kinamgonga kichwani. Willy alidondoka chini na kupoteza fahamu pale pale.
ITAENDELEA