RIWAYA; DUKA LA ROHO
SEHEMU YA MWISHO
Upande wa Gunner na Lobo, hali yao ilikuwa ni imara kimawazo na kimwili. Walikuwa hawana wasiwasi hata kidogo kuhusu maisha yao. Kila muda walitazama saa zao na kuangalia kama muda umefika.
"Masaa ishirini na mbili yamebaki." Gunner aliongea huku akienda huku na huko ndani ya nyumba ya Salome.
"Muda wa kushinda vita unawadia." Lobo akajibu mapigo huku tabasamu la kikatili likichanua katika uso wake.
"Kila kitu kipo tayari. Tutahakikisha mbwa wote wanakufa wale." Gunner akajitapa.
"Nakuamini kamanda. Ungekuwa hivi tangu mwanzo, maboya wangekuwa kaburini."
"Muda wao ndio huu sasa." Maongezi hayo yalichukua nafasi mida ya saa sita usiku wakati huo Masai na wenzake tayari walikwishafika jijini Dar es Salaam na kwenda katika nyumba ya Lisa tayari kwa mtanange wao na kundi la Gunner.
"Kesho ni siku ambayo itakuwa tofauti sana kwetu. Ni kati ya kifo na kuishi, damu na machozi, kilio na maumivu, na zaidi ni siku ya uhuru wangu na wenu. Hii ni siku ambayo hatutakiwi kuikosa katika maisha yetu kwani MUNGU pamoja na SHETANI, wanaingia vitani kugombea kondoo wema. Ni kazi kwetu, eidha kwenda kuwa kondoo wema au kuwa kondoo wa SHETANI. Naamini sote ni binadamu ambao miili yetu inaendeshwa na damu pamoja na moyo. Tunahisi na kuyapokea maumivu sawa na mnyama yeyote anayejeruhiwa. Hakuna cha kupoteza kama maumivu hayo utayapokea kwenye kuutafuta uhuru wako." Maneno ya Masai katika kuwahamasisha kundi lake kwenda kupambana na kundi la Gunner wajiitao Duka La Roho.
"Mimi napenda kuita siku hii kuwa ni SIKU YA MPAMBANO KWA TUWAPENDAO. Tunapigana kwa sababu tunapendana na tunapenda kile tukifanyacho. Tunawapenda Watanzania na hatupendi kuwaona wakiingia kwenye migogoro na nchi nyingine. Tunampenda Lisa na Martina, tunampenda Mubah na Ndita, Masai na Yogo na ndio maana tunaingia na mioyo ya kupambana. Tupambane kwa umoja na tufe kwa pamoja kama wenzetu wanavyofanya. Tupambane kwa kile tunachokipenda. Nani yupo pamoja katika hili?" Malocha aliongea huku akinyoosha mkono wake mbele ya duara waliweka katikati ya sebule lao.
"Kwa Watanzania." Yogo, mmoja wa wataalamu wa kompyuta aliunga mkono wake kwa Malocha na kuwa kama anatoa tano.
"Kwa Martina." Mubah aliongeza naye mkono wake.
"Kwa familia ya Mubah na Baba yangu. Na wote waliotutoka sababu ya mapambano haya." Lisa aliunga.
"Kwa FISSA." Ndita, au rafiki wa Martina, hakuwa nyuma. Macho yakabaki kwa Frank Masai. Jamaa akatabasamu kisha akasogea mbele ya wenzake na kuunga ngumi.
"Kwa Manchester United." Watu wote wakamshangaa Masai. "Nini sasa." Masai aliwauliza huku anatabasamu.
"Hao Manchester, wanahusika nini hapa." Lisa akauliza kwa hasira.
"Basi wife kha! Hutaniwi?" Masai aliongea huku akishika kidevu cha Lisa. "Kwa Martina, nakuja kukuchukua muda si mrefu." Masai akaongea huku uso wake ukipotea lile tabasamu alilokuwa nalo kabla.
"Kwa upendo." Malocha akafunga kazi.
****
Ilikuwa ni saa tatu usiku katika ghorofa moja refu na ambalo liliandaliwa mahususi kwa ajili ya kazi ya makundi mawili mahasimu katika mapambano.
Masai akiwa na kundi lake zima waliobeba mfuko wenye silaha, walienda hadi ghorofa ya kumi na kumkuta John Lobo akiwa kamkamata Martina aliyevaa begi dogo kama la shule.
"Mama." Martina aliita na kutaka kumkimbilia mama yake lakini Lobo alimzuia na kumfanya Martina aanze kujipapatua kutoka. Kwa ghadhabu, Lobo alimtandika kofi yule mtoto na kuweka kidole cha shahada mdomoni kwa akimaanisha Martina atulie.
"Unarisasi yangu moja kwa sababu ya hilo kofi." Masai akamwambia Lobo huku macho yake yakiwa mekundu kama nyanya sababu ya hasira.
"Ooooh. Masai the Soldier. Karibu Bro." Sauti ya Gunner ilitoka huku akitoka katika chumba kimoja kilichokuwa kama ofisi.
"Mmekuja kabla ya muda. Yaonekana mna usongo sana." Gunner alizidi kuzogoa huku nyuma akiwa kafuatana na wale wataalamu wake wenye miili.
"Nilimuahidi Lobo kuwa saa la arobaini, moja kutoka sasa, atakuwa hana uhai wake." Masai akajibu kwa kujiamini.
"Kwa hiyo umekuja na hawa wote wa nini?" Gunner akauliza.
"Kwa sababu ya upendo. Tunapigana kwa upendo." Malocha akasogea mbele na kujibu.
"Oooh! Kwa hiyo upendo umewavuta hapa. Haya bwana. Karibuni wazee wa upendo." Gunner akajibu huku akisogea hadi kwa Lobo na kumkamata Martina.
"Mbona unalia." Gunner akamuuliza.
"Anko huyu kanipiga." Mtoto akajibu.
"Usimsumbue tena. Atakuumiza kabla ya muda." Gunner akamuonya huku akionesha kutokujali hali ya Martina.
"Tubadilishe sheria." Lobo alifungua mdomo wake na kuongea jambo hilo.
"Unatakaje Kamanda." Gunner akataka kumsikiliza mshirika wake.
"Masai apambane na mimi. Ndani ya saa limoja ambalo limebaki. Akifanikiwa kunizimisha, tunampa kimdoli chao. Asipofanikiwa, utamuua huyu mdoli mbele ya macho yake." Lobo alitoa pendekezo.
"Masai unaafiki hili swala." Gunner akamuuliza Masai.
"Nipo kupambana. Na lazima afe bwege huyu. Am in." Masai akaongea huku akivua koti lake la jeshi na kulitupia pembeni.
"Sheria imepita." Gunner akawa kama refa.
"Sitaki kupigana mbele ya Martina." Masai akapendekeza.
"Oooh! Hiyo hamna. Ataona yote unayofanya na kufanywa. Hamna kumtoa." Gunner aliongea na kumfanya Masai ajute kukubali ule mpambano.
"Anko usipigane." Martina aliongea wakati Lobo anamkabidhisha kwa Gunner.
"Hee! Anakuita Anko? Mi nilidhani kishakujua. Kumbe huna tofauti na Lobo. Mi ndiye Baba hapa." Gunner alijitapa baada ya Martina kumuita Masai, Anko. Masai akazidi kunyong'onyea kwa maneno ya Martina kumkataza asipigane lakini alishaamua, na kama walivyo Makamanda wengi, wakiamua kufanya jambo, hufanya hata kama yanawagalimu damu na maisha yao.
Masai na Lobo wakaingia katikati na kwa kasi ya ajabu, Lobo aliruka teke na kulituliza kifuani kwa Masai na kumrusha mbali.
"Anko John muache Ankoo." Martina alilia kwa uchungu kwa lile tendo lakini Lobo hakusikia, akaruka sarakasi haraka na kutua karibu na Masai aliyekuwa anagalagala chini na kumpa teke aina ya dochi kwenye tumbo.
Maumivu yakamzidi Masai kwa kile kitendo lakini alikuwa hana jinsi kwa sababu mwanaye alikuwa anaona na yeye alikuwa hataki Martina aone kitu chochote cha kikatili atakachokifanya. Uwanja ukawa wa John Lobo. Masai alikuwa anachambuliwa kama karanga mbele ya Lobo.
"Mmeona? Hamna kitu hapa." Lobo aliongea huku kamkanyaga Masai aliyeelemewa kwa kipigo kikali ndani ya dakika kumi tu.
"Safi sana kamanda." Gunner akamsifu Lobo. Hapo hapo Lobo akamtandika teke lingine zito Masai lililotua kidevuni na kufanya damu zilizochanganyikana na mate kuruka kama bata kachinjwa.
"Sema Loboo." John Lobo aliwaambia wenzake na wote wakaitikia kama sauti za jeshini.
"Loboo." Akatupa teke lingine la tumbo. Baada ya hapo akamkalia Masai kifuani na kuanza kumchapa ngumi za uso. Masai akawa kachanika katika paji la uso na juu ya jicho. Kipigo kikaendelea kwa dakika ishirini huku Lisa, Martina wakiwa wanalia kwa.kuomba msaada.
"Baba mpige huyo." Martina akatamka hasira baada ya kuona baba yake kaelemewa.
"Umeniitaje Martina." Masai akawa kama haamini anachokisikia toka kwa Martina.
"Mpige baba. Mpige na muue." Martina akajibu swali la baba yake wakati huo Lobo alikuwa kifuani kwake.
"Zamu yangu." Masai akamwambia Lobo na kisha akambetua haraka na kumbwaga chini. Yeye akawa juu sasa. Ngumi zisizo na idadi zikaanza kushuka usoni kwa Lobo. Zikamchana na kumfumua yule jamaa aliyekuwa kamiliki mchezo muda mchache uliyopita.
Masai akakamata kichwa cha Lobo na kuanza kukibamiza kwenye sakafu nzito ya pale ndani. Lobo akawa hoi, ndipo Masai akashuka toka juu yake.
"Unakufa kilaini sana Lobo. Sababu ya ujinga wako. Ulimpiga kofi moja mwanangu, nikakuahidi ni sawa na risasi moja." Masai alimwambia Lobo ambaye alijiinua na kupiga magoti mbele ya Masai. Masai akamuonesha ishara Mubah ampe kitu. Mubah akachomoa bastola yake iliyofungwa kiwambo cha kuzuia sauti toka kiunoni kwake na kumrushia Masai.
"Kwa ajili ya kofi." Masai akafyatua risasi iliyomkuta begani Lobo.
"Na pia nilikwambia roho yako namnunulia Mubah. Natimiza ahadi." Masai akatembea hadi kwa Mubah na kumpa bastola yake. "Kazi kwako." Masai akamwambia.
Mubah akamsogelea Lobo na mara akaanza kuvuta picha ya familia yake. Akavuta picha ya mjomba wake ambaye alikuwa anapenda sana kucheka akiwa na Mubah. Hasira zikampanda na kujikuta machozi yakimtoka bila kupenda.
"Kuniua si suluhisho. Huwezi kuwarudisha mbwa zako bwege wewe." Lobo aliongea kwa kejeli. Mubah akampiga risasi kwenye bega lilelile alilompiga Masai.
"Hiyo kwa kuwaita niwapendao mbwa." Mubah akaongea baada ya ile risasi.
"Kwa mama." Akafyatua nyingine na kutua kwenye bega lingine
"Na hii ni kwa mama pia." Akampiga kwenye paja la kulia. Akaelekeza kwenye paja la kushoto na kufyatua risasi nyingine.
"Kwa dada." Akadedicate risasi nyingine.
"Na hii ni kwa mjomba wangu." Chozi likamtoka Mubah baada ya maneno hayo na bastola yake kailekezea kichwani kwa Lobo. Akafyatua lakini risasi zikawa zimekwisha.
"Hahahaa. Mjomba wako hataki nife." Lobo aliongea huku akilazimisha cheko palipo na maumivu.
"Hapana. Hataki ufe na bastola hii, bali hii." Malocha aliongea na kumrushia Mubah bunduki aina ya SMG. Mubah akampiga risasi za magotini yule bwana na kumfanya alie huku katanua mdomo, akaingiza ncha ya bunduki kwenye kinywa kile kilichowazi na kumimina risasi zisizo na idadi. Hadi anamaliza, kichwa cha Lobo kilikuwa kimepukutika.
"Kwa mjomba." Mubah akaongea kupeleka salamu za risasi zile lakini ghafla ukasikika mlio wa risasi na wakati huohuo Mubah akarushwa mbali.
"Safi Salome." Gunner alionga na simu ya sauti ya upepo kumpongeza Salome aliyefyatua risasi iliyomkuta Mubah upande wa kulia wa kifua chake. Mubah akawa kama amekufa, na kuacha macho ya wenzake yameshikwa na butwaa. Ndipo kwa ghafla, wakavamiana na kila mtu akagawana wake.
Malocha akapambana na Gunner, wale wataalamu wa kompyuta, wakapambana wao kwa wao na wakati huo Lisa na Masai wakaenda kumuangalia Mubah.
Lisa akakimbia kwenye begi lao la silaha na kutoa bunduki ya udunguliaji (sniper rifle) na kwenda hadi sehemu ambapo risasi ile ilipita. Akaweka lensi yenye uwezo wa kuona usiku na kuanza kumtafuta Salome. Akamuaona mwanamke yule akivuta sigara wala hana mpango na kazi yake.
Akamlenga kichwani na kufyatua bunduki yake. Mlio mkali ukasikika na kuwashtua wengi mle ndani.
"Nimemuondoa Salome." Lisa akaongea huku katabasamu. Wakati Martina alikuwa kajibanza kwenye pembe ya chumba kile na kuziba masikio yake asisikie kitu.
Gunner aliposikia kuwa Lisa kaumuua Salome, akapata hasira na kumuacha Malocha aliyekuwa kalegea kwa kipigo na kwenda kwa kasi mbele ya Lisa. Lakini akakutana na upinzani mzito kwa teke la Masai. Gunner hakujilaza chini muda mrefu, akajibetua haraka na kumpiga teke la kuzunguka Masai.
Hajakaa sawa Masai, akapokea teke lingine lililompeleka hadi chini. Lisa akajitoma kwenye mpambano lakini kofi alilokutana nalo, hakuwa na budi kujitupa pembeni.
Malocha kuona hivyo, naye akajiachia na kuruka teke la kutanguliza mguu, lakini Gunner akajizungusha kwa nguvu na kumzuia Malocha akiwa angani kwa teke la korodani. Malocha akatua chini na kuanza kugalagala.
Masai akanyanyuka na wakati huo wale wataalamu wao nao walikuwa wanazidiwa ufundi wa ngumi za kundi la Gunner.
Masai akamfuata Gunner na kuanza kurusha ngumi ambazo Gunner alikuwa anazipangua kwa ustadi na pale aliporusha yake, ikatua puani kwa Masai. Masai akarudi nyuma kidogo lakini akarudishwa nyuma zaidi kwa teke lililotua usoni.
Lisa haraka naye akanyanyuka na kwenda kumdandia Gunner mgongoni na kumkaba kwa nguvu, lakini bahati.mbaya alikutana na mtu makini aliyeinama kidogo kisha akamtupia mwanamke yule kwa mbele. Akamuongezea na dochi zito la tumbo lililomsogeza hadi kwa Masai. Mpambano akawa kaumiliki Gunner.
"Hamna kitu nyie. Napiga wote." Gunner akajitapa. "Na bado dakika ishirini masaa arobaini na nane yatimie. Kwenye begi la Martina kuna zawadi ya bomu kama masaa arobaini na nane yatatimia. Sheria ilibadilika lakini bomu hatukubadili sheria zake, bado dakika ishirini. Na rimoti hii hapa, nikishinda tu! Nakibomoa kijitu chenu." Gunner alimaliza na kunyoosha rimoti ya kulipulia bomu kisha akaiweka mfukoni.
Lisa na Masai wakaangaliana, kisha wakakumbuka kipindi cha nyuma walivyowahi kupambana katika umoja. Hapo wakapata nguvu mpya na kuanza kunyanyuka.
Lisa alikuwa wa kwanza kumvamia Gunner kwa kuruka teke la mguu mmoja, Gunner akamkwepa na Lisa akapitiliza lakini bahati mbaya Gunner alikuwa kampa mgongo Masai baada ya kumkwepa Lisa. Masai akatumia fursa hiyo kwa kumpiga teke la kisogo jamaa yule. Gunner alipojaribu kugeuka apambane na Masai, Lisa akajitupa naye kumpiga teke la mgongo lililomsukuma Gunner hadi kwa Masai ambaye naye akarusha ngumi kali na kutua kifuani kwa Gunner.
Malocha alinyanyuka na kwenda kuongeza nguvu kwa wale wataalamu ambao baada ya hapo, wakaanza kuumiliki mchezo kama Masai na Lisa kwa Gunner.
Gunner akawa kalegea na wenzake pia baada ya dakika kumi. Kwa mbali Gunner akamuona Mubah akihangaika kumvua begi Martina.
"Muache huyo we bwege." Gunner alifoka huku kalala chini baada ya kipigo kikali toka kwa Masai na Lisa. "Navunja sheria tuliyoweka." Gunner akaanza kujipapasa atoe rimoti yake.
Hadi anaipata, Mubah alishavua begi lenye bomu na kwa kujitutumua, akanyanyuka na kukimbia kwa kasi kwenda kwenye dirisha la kioo cha ghorofa lile la kumi, akapita na kujitupa nje na wakati huo Gunner akabonyeza kitufe cha kutegulia bomu. Mlipuko mkubwa na mwanga mkali wa bomu lile aliloruka nalo Mubah ukatokea nje. Macho yakawatoka Lisa na wenzake kwa kitendo kile. Masai aakashindwa kuvumilia na kujikuta akipiga kelele za uchungu.
Kelele hizo zilikuwa za hasira kali zilizomkumba moyoni mwake kwa kile kilichotokea kwa Mubah. Alipomtazama Gunner, alishuhudia tabasamu la kero usoni pake.
Masai akanyanyuka na kumfuata kwa kasi pale alipo yule mtu. Alipofika karibu yake, Gunner akataka kumkata mtama lakini kijana yule ni kama alikuwa kauona, akaruka juu kidogo na kumtandika ngumi ya utosi adui yake. Maumivu yakakikumba kichwa cha Gunner, lakini haikutosha kumnyamazisha Masai asiendelee kutupa makonde yake ya nguvu kwenda kwenye uso wa wake.
Gunner akawa kahelemewa na mapigo mazito ya Masai. Makonde aliyokuwa anayatupa kijana ni kama ya Tyson au Frank Bruno. Hadi anamaliza kumtupia zile ngumi, Gunner alikuwa kachakaa kwa vidonda na damu hasa upande wa usoni.
Akadondoka chini yule mwanaume na kuwa kama mwenye kupiga magoti.
"Lisa. Huyu ni wako." Masai akasogea pembeni na kwenda alipo Martina ili amfiche asione ambacho mama yake anakifanya.
"Ulifanya kosa kubwa sana kuniambia kuwa ulimuua baba yangu. Lakini nilikusamehe kwa sababu nilijua ni kosa letu. Ukamteka mwanangu na kabla ya hapo ukataka kumfundisha ugaidi, ukaona haitoshi ukamfunga bomu ili umuue. Bahati mbaya, kaenda mwenye roho nzuri. Siwezi kukusamehe mume wangu wa zamani." Lisa akachomoa bastola yake na kumpiga risasi moja ya kichwa iliyoacha tobo katika paji la uso wa Gunner.
Mwanaume Gunner akaiacha dunia kwa mtindo wa kipekee. Lisa akapiga magoti na kulia hasa kwa sababu yule alikwishakuwa ubavu wake, alijaribu kumpenda kwa moyo wake lakini mwanaume huyu hakuona thamani ya upendo wake na kuamua kubadilisha moyo wake kuwa wa kishetani. Mwisho wa yote, Lisa anamuua mumewe kama mumewe alivyomuua mkwewe.
"Kwa nini Gunner, kwa nini." Lisa alilia kwa uchungu na kwa sauti kuu.
"Oya kama mmemmaliza huyo boya njooni mnivute bwana. Mi' naning'inia tu huku." Sauti ilisikika toka katika dirisha ambalo Mubah alipita na kujitupa pamoja na bomu. Malocha na Masai wakajikuta wakikimbilia kule inapotokea sauti. Wakati huo wale jamaa wa Malocha walikuwa wamewaweka chini ya ulinzi washirika wa Gunner na John Lobo.
Lisa naye akanyanyuka haraka na kwenda katika dirisha lile kubwa lililokuwa wazi. Wakachungulia kwenda chini na kumkuta Mubah kanasa shati lake kwenye bomba dogo la chuma linalotumiaka kupitishia maji ya mvua pale itakaponyesha.
"Mnaangalia nini badala ya kunivuta, nyie wajinga nini?" Mubah akalalamika na kuwafanya washirika wake watabasamu na kuanza kuhangaika kumrudisha juu. Wakafanikiwa na kumwingiza ndani.
"Imekuaje wewe? Si' umepigwa risasi wewe?" Malocha alimuuliza Mubah. Mubah kwa mbwembwe akafungua vishikizo vya shati lake na wote wakashuhudia vazi la kuzuia risasi likiwa mwilini kwa Mubah.
"Mlidhani siogopi kufa? Nani afe kibwege. Mngekufa nyie mi' mngeniacha."
"Kumbe boya ulivaa bullet proof." Malocha aliongea huku akianza kumsogelea tayari kwa kumuadhibu kijana wake.
"Na hii ndio imenisaidia asee. Ningelipuka mimi leo hii. Mwee. Yaani nilivyojitupa tu, shati likaingia kwenye lile bomba. Lakini shati pekee halikutosha kunishikilia hadi mwisho, hii nayo ilinisaidia sana. Wakati huo namsikia huyu boya anawaambia anabonyeza kidude, nikalitupa lile begi likalipukia huko chini. Na bahati nzuri hakuna watu usiku huu." Mubah aliongea na kuwaacha wenzake wakiwa katika taharuki wakati huo Malocha akawa kasimama tu, hajui amfanye nini Mubah.
"Una MUNGU mkubwa Mubah. Karibu tena." Masai aliongea na kwenda kumpa mkono Mubah pale alipokuwa kakaa. Mubah akampa mkono, Masai akamvuta juu na kumsimamisha kisha akamkumbatia kijana yule. Lisa na Malocha nao wakajiunga katika upendo ule.
"Martina njoo." Martina kusikia anaitwa na Mama yake, naye akanyanyuka haraka na kukimbia hadi pale walipofamilia yake inayompenda. Wakacheka na kufurahi hasa baada ya Martina kumkubali Masai kama baba yake.
Wataalamu wa Gunner wakapigwa pingu na baada ya hapo, wakaanza kushuka ghorofa lile taratibu ikiwa tayari ni saa kumi alfajiri.
Baada ya kufika chini, wakaenda hadi kwenye mlango wa kutokea. Wakafungua na wote kwa pamoja wakatoka nje.
"Mpo chini ya ulinzi." Sauti kali kutoka kwenye kipaza sauti ilisikika ikiwaamrisha Malocha na kundi lake.
Mbele yao kulikuwa na magari ya polisi karibu ishirini na taa zake za bluu na nyekundu zikilanda juu ya magari hayo. Polisi wapatao thelathini wakiwa wakamata bastola na mitutu, walielekeza dhana zote hizo katika mlango wa kutokea.
"Tayari hapa. Hamna ujanja tena." Masai aliongea huku akimshusha Martina na kunyoosha mikono yake juu sambamba na wenzake.
Askari kadhaa wakafika eneo lile na kuwapora silaha zao kisha wakawafunga pingu kasoro Martina. Baada ya tendo hilo, wakawachukua na kuwapeleka kwenye magari yao tayari kwa safari kuwafikisha kituoni.
Asubuhi ya saa moja, vituo mbalimbali duniani vilikuwa vinatangaza habari za vifo vya Gunner na Lobo pamoja na kukamatwa kwa watu wanaotafutwa kwa muda mrefu na mashirika mbalimbali ya kipelelezi. Picha za wakina Malocha zilionyeshwa kwenye vituo vingi vya runinga na kuwafanya watu wale kuonekana katika vituo vingi vya runinga kuliko mtu mwingine yeyote duniani.
Rais wa Tanzania akatoa tamko lake rasmi kuhusu watu wale. Japo hapo mwanzo walishukiwa kuwa ni magaidi, lakini Rais aliwatunuku cheo cha mashujaa. Na kwa furaha, akawarudisha Malocha na kundi lake FISSA. Akatimua wale waliokuwepo kwenye viti vya watu hawa.
Kwa Frank Masai, alikuwa kapata ugumu sana kutoka katika msala wake hasa kwa sababu alikuwa anakesi nzito ya mauaji aliyoyafanya huko nyuma (SIMULIZI NYINGINE HII. UTAPATA MKASA HUU KWA UNDANI).
Rais alionesha ukali wake kwa alichokifanya Masai huko nyuma na hakuthubutu kutoa maneno ya kumtetea kwa sababu karibu mataifa makubwa yote yalikuwa yanamshutumu kijana huyu kwa mambo aliyokuwa kayafanya.
"Kwa Masai. Naiachia mahakama ya makosa ya jinai imuhukumu, sina mamlaka naye hata chembe. Na siwezi kumtetea hata kidogo sababu ya ushenzi ambao kaufanya." Sauti ya Rais ilitangaza baada ya kuwarudisha wakina Malocha ndani ya FISSA. Watu walilalamika na kuishutumu serikali kwa kushindwa kutetea mashujaa wake lakini maneno hayo hayakumaanisha kauli ya Rais itenguke japo moyoni alikuwa anajiona kama mwenye kusaliti wananchi wake.
Hatimaye ikafika siku ambayo Masai alipaswa kupewa hukumu yake na mahakama ya makosa ya jinai kutokana na kosa la mauaji alilolifanya miaka kadhaa iliyopita. Waaandishi wa habari waliruhusiwa kutangaza kesi ile mwanzo hadi mwisho. Hivyo hukumu yake ilipatwa kuhudhuriwa na watu wengi na pia kusikilizwa na kutazamwa kwa wingi uleule.
"Frank Brown Masai. Hutakiwi kujibu chochote katika hukumu hii. Vithibitisho vyote vipo kwa uliyoyafanya. Maneno na matendo yako yapo yote, hamna haja kujibu kesi hii." Ni hakimu wa kesi ya Masai akiwa katika ubora wake.
Wanasheria mbalimbali walijaribu kumtetea Masai lakini hawakufanikiwa kupunguza ukali wa kesi ile na mwisho wake ulikuwa ni hukumu nzito kwenda kwa Masai.
"Kwa makosa aliyoyafanya Frank Masai, anahukumiwa kifungo cha maisha katika jela ya L.O.R.D. Atafanya kazi ngumu na kukutana na vikwazo vingi sana. Hiyo ndio hukumu yake." Watu wote waliokuwa wanafuatilia ile kesi wakashikwa na butwaa na macho yakawatoka baada ya hukumu ambayo kwao waliona ni nzito kuliko hukumu zote. Waliona ni kheri kuhukumiwa kinyongo kuliko kupelekwa ile jela ambayo hakuna anayejua ipo sehemu gani katika nchi ile ya Cambodia.
Hakimu wa mahakama ile ya juu duniani, akagonga nyundo yake kumaliza kesi ile. Masai akawa kahukumiwa na kuwaacha Lisa na Martina katika simanzi, lakini alipewa ruhusa ya kuwaaga na kuwaahidi ataishi licha ya vikwazo vitakavyomkuta.
MWISHO