SIMULIZI.. BALAA
MWANDISHI.. HALFANI SUDY
SEHEMU YA SABA
Dokta Yusha sasa alikumbuka hali atakayokuwa nayo mke wake kipenzi Nasra kwa tukio lile baya alilolifanya. Alikumbuka pia huzuni atakayokuwa kawaachia wazazi wake wapendwa kule ukumbini baada ya kuondoka bila kuaga. Alijiona kafanya kosa kubwa sana.
Ghafla, majimaji mepesi yalitiririka katika mashavu yake, Dokta Yusha alikuwa analia. Kwa kosa kubwa alilolifanya usiku ule.
Wakati Dokta Yusha akiwaza yale, na chozi la uchungu kumdondoka pale hospitali. Muuaji namba tano alikuwa hatua chache sana na pale alipokaa Dokta Yusha, akifikiria jinsi ya kumuua. Aliona kumuua kwa risasi itazua tafrani kubwa pale hosptali, alipanga kumuuwa Dokta Yusha kwa mikono yake ama kwa kisu. Alihisi njia hizo ni salama zaidi. Sasa alikuwa anasubiri Dokta Yusha afanye kosa lolote lile.
Kule Kilwa Masoko, hali ile ya taharuki na huzuni iliendelea mle ukumbini.
Baada ya saa moja watu wote waliamua kurudi majumbani kwao. Huku kila mmoja akiliongelea kwa aina yake tukio la kukimbia kwa bwana harusi katikati ya sherehe. Wapo waliolifanya kama hadithi nzuri ya kufurahisha, wapo waliolifanya kama hadithi mbaya ya kusikitisha na kuhuzunisha.
Watu wa mwisho kurudi nyumbani katika usiku ule wa sherehe ya harusi ni familia mbili zilizokumbwa na kisanga kile cha kuajabisha, familia ya Dokta Yusha na familia ya Nasra. Waliweka kikao kidogo mlemle ukumbini kulizungumzia tukio lile. Kikao kilichoisha bila maelewano yoyote. Walijaribu kumpigia Dokta Yusha, simu iliita tu bila kupokelewa. Sasa familia zile mbili wakiwa na Bi harusi walikuwa wanarudi nyumbani, katika gari mbili tofauti, wakiwa na huzuni na simanzi tele. Huku wanawake wachache ndani ya familia zile walikuwa wanalia, wakiongozwa vizuri na Bi harusi, Nasra.
Katika gari aliyopanda Nasra, kulikuwa na watu watano, Kulikuwemo na dereva, baba yake Nasra, mzee Mpaukha, mama yake Nasra, mama Mpaukha, na mpambe wa Bi harusi, rafiki yake kipenzi Nasra, Hasina Omary.
Dereva wa gari ile, alikuwa anaitwa Musa. Dereva wa siku nyingi sana wa familia ya mzee Mpaukha.
Musa alikuwa amelewa sana pombe, pombe ambayo aliinywa vilivyo na marafiki zake mle ukumbini. Pombe ilimfanya apoteze umakini pale katika sukani na kuleta balaa kubwa sana.
Walitoka vizuri pale ukumbini, lakini gari lilivyokamata lami mwendo ulibadirika. Musa akawa anaendesha gari bila umakini wowote, siku zote pombe haziongopi.
Hakukuwa na mtu aliyekuwa makini na mwendo ule, wakati Musa alikuwa amelewa pombe, watu wengine wote waliobaki walikuwa wamelewa na kitendo alichokifanya Dokta Yusha kule ukumbini. Gari zima walilewa kwa aina mbili tofauti. Kila mmoja alikuwa amekaa mkao wa kuchoka katika siti yake.
Gari wakati inakata kona ya kuelekea nyumbani kwa mzee Mpaukha, dereva ilimshinda. Ilikuwa kona kali sana, iliyomshinda kabisa Musa, gari liliacha njia na kujisweka kwenye kapori kadogo....ilikuwa balaa !
Gari ilijipiga kwa nguvu sana katika mti mkubwa kule kwenye kapori. Kishindo kikuu kilisikika......
ITAENDELEA MUNGU AKIPENDA
Maoni/ Ushauri 0757 633010