SIMULIZI: BALAA
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU: 0757633010
SEHEMU YA MIA NA NNE
Hakukuwa na umbali mkubwa sana kati ya chumba namba nane alichokuwemo Dokta Kilumba na chumba namba kumi na tatu walipokuwepo watu hawa wawili, Mwanasheria mlevi na Dokta Yusha. Kulikuwa na tofauti ya vyumba kama vinne hivi ili kufika katika chumba alichokuwa amepanga Dokta Kilumba.
"Tutaingiaje sasa chumbani kwake?" Dokta Yusha aliuliza huku akimwangalia Mwanasheria mlevi usoni.
"Tutagonga tu mlango" Mwanasheria mlevi alimjibu Dokta Yusha kwa kifupi.
"Je akiuliza nani anagonga akiwa bado hajafungua mlango?" Dokta Yusha aliuliza tena.
"Tutasema Mhudumu" Mwanasheria mlevi alikuwa anajibu majibu mafupi huku akiwa na uhakika tele.
"Ahaaa..poa twende tukajaribu" Dokta Yusha alikubaliana na Mwanasheria mlevi, bila ya kudadisi sana.
Usiku uleule wa maneno Dokta Yusha na Mwanasheria mlevi walitoka katika, chumba namba kumi na tatu, walichopanga na kwenda chumba namba nane, chumba alichokuwa amepanga hasimu wao, adui yao, Dokta Kilumba.
Kule ndani Dokta Kilumba baada ya kwenda kujimwagia maji, sasa alikuwa amekaa katika shuka nyeupe iliyokuwa imetandikwa juu ya kitanda kikubwa, ndani ya nyumba ile ya kulala wageni ya Mjaka. Dokta Kilumba alikuwa akisubiri ujio wa mgeni, mwanamke baamedi aliyekubaliana kwenda kustarehe nae alivyokuwa kule baa.
Dokta Kilumba akiwa kule baa, alipatana kwa siri, kuja kufanya mambo ya siri. Alikuwa Baamedi wa Masoko by night, aitwaye Alice na alikuwa amemuelekeza namba ya chumba alichofikia, pia alikuwa ameshampa hela ya usafiri wa kumfikisha pale, na sasa alikuwa anamsubiri tu ili aje kupewa huduma ya siri atakayoilipia.
Dokta Kilumba hakutaka kufatana nae wala kukaa nae karibu Alice baamedi, alikuwa anaogopa kuchafua taswira yake ya heshima mbele jamii. Ingawa Alice alikuwa mwanamke mrembo sana, lakini kutokana na kazi aliyokuwa anaifanya (Ya ubaamedi) Dokta Kilumba aliiona kama kazi ya dharau, kazi ambayo yeye kama Dokta anayeheshiwa hakustahili kuambatana na mwanamke wa aina hiyo. Tena akielekea nae katika nyumba ya kulala wageni.
"Ngongongo"
Mara mlango wa chumba alichokuwa Dokta Kilumba uligongwa, na Dokta Kilumba bila kufikiria alinyanyuka pale kitandani kwa mbwembwe bila tahadhari yoyote na kwenda kuufungua ule mlango....
Je nani atakuwa kagonga mlango...Alice au kina Dokta Yusha.. Nini kitatokea...
ITAENDELEA KESHO MUNGU AKIPENDA