SEHEMU YA KUMI NA SABA
Kauli ya kwamba ukilijua jina la mbwa basi hakutishi
niliduwaa haikufanya kazi, niliita jina la Simba lakini mbwa
yule alionekana kuwa mwenye hasira kali zaidi,
aliunguruma kisha akaendelea kunisogelea. Mapigo ya moyo
yakazidi kwenda kasi na amani ikatoweka tena.
Mara akaanza kubweka, nikafanya kosa kutishia kuwa
naweza kupambana naye kwa kumtisha kama namfukuza.
Jibwa likatanua kinywa na bila shaka alitaka kufanya
shambulizi!!!
Nikaamini kuwa ngombe wa masikini hazai ni usemi sahihi
kabisa. Nikakiona kifo tena mbele yangu. Nguvu nazo
zilikuwa zimeniishia.
**UJUMBE! Kukata tamaa ndo asili ya mwanadamu,
hasahasa akishafanya jitihada zake binafsi pasi na
kumshirikisha mtu!! Lakini je? Kukata tamaa ni suluhu ya
kujikwamua kimaisha, ama kufanikiwa lolote lile?
Wanadamu wengi hushindwa kutimiza ndoto zao kwa
sababu ya pepo hili la kukata tamaa.
Ili ufanikiwe katika maisha ni lazima ulishinde pepo la
kukata tamaa lakini vinginevyo katika kila vita ulimwenguni
wewe utakuwa wa KUSHINDWA TU!!
Utaishindwa vita ya kuupinga umasikini, utashindwa vita ya
kudharauliwa na mwisho kabisa utashindwa vita kuu ya
KUSHINDWA KUIONGOZA AKILI YAKO!!!
TAFAKARI!!
ENDELEA
. . Acha simba!!! ikaamrisha sauti kali. Nikapepesa macho
ili nijionee ni nani huyo!!
Na hapo akatokea MAMA LAO akiwa na tabasamu usoni na
rungu kubwa mkononi!!
Alikuwa anatokwa damu mdomoni lakini hakuwa na kitu
kinachoitwa wasiwasi tena, akaanza kutembea zaidi.
Alikuwa anachechemea!!
. . Mama lao
nikajikuta natokwa na sauti yenye
kitetemeshi.
. . Tuondoke hapa Sam. Wajinga wana mtandao mpana
sana hawa. Simama Sam jikaze simama tupotee hapa.
Alinisihi Mama lao, lile jibwa lilibaki kutikisa mkia, bila
shaka lilimjua vyema Jojina na mbwa akojuaye
.
Hakuna kilichoharibika.
. . Nikajikaza nikasimama wima, mbwa huyu hakuwa na
madhara tena kwangu ilhali Jojina alikuwa amemkaripia
tayari.
. . Nikajikongoja huku nikiyasikia maumivu ya kiuno bado.
Lakini ilikuwa heri maumivu haya kuliko kuuwawa kabla
sijatimiza azma yangu.
. . Sikujua kama mwendo wangu ulikuwa mdogo kiasi cha
kumkwaza Jojina, hakusema na hata angesema isingesaidia
kuniongezea mwendo mgongo ulikuwa unauma sana, na si
hivyo tu hata nilipojaribu kukimbia yale maumivu ya kinywa
kilichopasuka yalisababisha kichwa kiwe katika maumivu
makali sana. Jojina alinitazama kwa huruma huku akizidi
kukaza mwendo.
. . Mara akasimama ghafla kisha akachuchumaa, nikamfikia
nikiwa nashangaa.
. . Panda mgongoni Sam
panda upesi aliniamuru, ni kitu
ambacho sikukitarajia hata kidogo lakini hakuwa na
masihara hata kidogo, akarudia kauli yake safari hii kwa
kuamrisha.
. . Nikajiweka mgongoni, Jojina akasimama kama kifaru
akaanza kutimua mbio mimi nikiwa mgongoni. Usiku wa
giza tukielekea anapopajua yeye. Niliyafumba macho yangu
kukabiliana na uchungu niliokuwa nikiusikia. Kichwa
kilikuwa kinauma haswa!! Lakini haukuwa wakati muafaka
wa kulalamika.
. . Mama lao akaendelea kutimua mbio.
. . Taksiii
.Taksiiii msaada tafadhali mgonjwaaa!! aliita
kwa nguvu baada ya kuziona taksi kadhaa zikiwa
zimeegeshwa.
. . Dereva moja akawahi upesi akaufungua mlango wa teksi
yake. Hapo sasa nilikuwa nimefumbua macho nikishuhudia
filamu hii ya aina yake.
. . Tupeleke Stendi ya mabasi
aliamuru Jojina na hapo
nilikuwa siti ya nyuma na yeye akiwa pembeni yangu.
Dereva alibaki kuduwaa ni kama hakuwa akiamini kama
tulikuwa na pesa ya kumlipa, Jojina akalingamua hilo, upesi
akajipekua na kutona na noti nyekundu akamlipa dereva.
Akatia gari moto tukatoweka
njia haikuwa mbaya sana
hivyo wakati huu nilipata fursa ya kutambua kuwa kinywa
kilipasuka japo si vibaya sana lakini shingo ilikuwa inauma
sana bila shaka yule bwana aliyenipiga mateke.
. . Stendi haikuwa mbali, tukapewa pesa yetu iliyosalia na
kutelemka, wakati huu nikijikongoja mwenyewe. Kila kitu
katika suala la maamuzi nikamuachia Jojina maana walau
yeye alikuwa na unafuu.
. . Sikujua alikuwa na maana gani usiku mnene kama ule
kuamua safari ya kuja stendi lakini hakuniacha niumie akili
kutafakari sana, mara akaita teksi nyingine.
. . Tupeleke Gangilonga akatajiwa bei akalipa.
Ukimya ukatawala kwa takribani dakika kumi na tano.
Tukatelemka mahali ambao Jojina aliamua yeye.
. . Teksi ilipoondoka tukatembea kwa mwendo wa miguu
hadi katika nyumba kubwa kiasi iliyozungukwa na majani
mengi, bila shaka ni kutokana na watu kutoishi eneo lile
kwa muda mrefu.
. . Jojina alivyofika pale geti lilikuwa limefungwa na
hakushtuka ni kama kitu alichokitarajia.
Akachumpa ukutani akatua upande wa pili. Kisha akafungua
geti dogo na kuniruhusu niingie ndani.
. . Miezi sita sijakanyaga hapa aisee. Alisema neno la
kwanza tangu tufike pale. Sikuchangia chochote.
Akaniongoza hadi ndani, uzuri wa Iringa hakuna vumbi kali
sana, badala yake vipindi vya baridi huchukua nafasi kubwa
zaidi hivyo hapakuwa na madhara ya vumbi.
. . Hapa hakuna umeme wala nini Sam. Alizungumza tena,
nikamuunga mkono kwa kumweleza kuwa hilo si tatizo cha
muhimu usalama wetu.
. . Akapapasa huku na kule akaibuka na mshumaa, kisha
akavuta kumbukumbu na kupapasa sehemu nyingine
akaibuka na kiberiti na kisha kutengeneza mwanga
hatimaye.
Nikaketi naye akaketi katika makochi chakavu yaliyokuwa
pale ndani.
. . Baba yangu alikufa maskini lakini walau alijenga kibanda
hiki kwa taabu. Akaanzia hapo, hili halikunigusa sana.
Nilitamani kusikia juu ya namna tulivyoweza kuokoka.
Nikaamua kumuuliza.
. . Akatabasamu kidogo kisha akaketi vyema!!
. . Sam, yaani japokuwa huwa siendi katika nyumba za
ibada hata miezi sita ama mwaka lakini nimeamini kuwa
Mungu huwa hamtupi mja wake
. Lakini najiuliza iwapo
nami ama sisi ni waja wake. Maana nikiwa katika kile
chumba changu nikaisikia sauti ya baba mwenye nyumba
ikilalamika, na kuna watu walikuwa wakitoa karipio.
Nikasitisha nilichokuwa nafanya, simu yangu nilikuwa
nimeweka katika chaji. Nikainyofoa kwanza nikaiweka katika
mkoba wangu. Nikatuliza akili, mara nikaona mwanga wa
gari. Mwenye nyumba wangu hana gari, nikajishtukia na
kuheshimu machale yangu kuwa hapa mambo yanaanza
kuharibika, nikapitia dirishani mbiombio nikakimbia hadi
nyuma ya nyumba ambapo sauti hizo zilikuwa zinatokea.
Nikasikia wakimuuliza juu yangu iwapo nimerudi, kisha
wakamuuliza iwapo amewahi kuniona na mgeni. Nikasikia
wakimuuliza iwapo anaifahamu sura fulani katika picha
ambayo najua tu ni yako hakuna mwingine. Mwenye
nyumba akakiri kuwa nilikuwa nimerejea tayari. Lakini
hakukubali kiwepesiwepesi badala yake walimpa kipigo
kwanza ndo akalainika.
. . Alipokubali kuwaongoza kuja upande wa kile chumba
changu na stoo pia ndipo nikashtuka na kuja mbiombio
upande ule, nikakuita hukuitika, nikawasha tochi ndo pale
ukanipa ile bahasha!!! Wajinga wakavamia pale mimi haraka
nikadidimia chini.
. . Sam niliumia sana nilipowashuhudia wakikupa kipigo
kiasi kile, bahati nzuri ndani ya chumba changu tofauti na
simu nilichukua pia kile kirungu changu cha mgambo si
nilikwambia nilipita huko, kiukweli hicho kirungu
niliwadhulumu.
. . Nikajiuliza sasa mimi na kirungu nitakusaidia kitu gani
mie. Wakakutukana matusi mazito, nikatamani kukimbia
lakini ningeweza vipi kukuacha ufe hivihivi.
. . Nikatamani kupiga kelele lalini mwenzangu we, sisi
wahehe ni waoga sio siri, yaani unaweza kupiga kelele
asitokee hata mtu mmoja sasa hapo ni kipi kama si
kujitafutia kufa burebure.
. . Nikataka kuwakabili kwa kirungu lakini kweli wanaume
wanne kwa kirungu kimoja, si matusi hayo!!
. . Nikajikuta naketi chini, na hapo nikakumbuka jambo la
muhimu kupita yote na siajui tu niliwaza vipi kuhusu mbwa
wa kufugwa wa baba mwenye nyumba. Yule mbwa huwa
hana masihara, baba mwenye nyumba alipewa na wazungu
fulani hivi rafiki zake. Nikavamia banda nikalifungua, uzuri
ananitambua yule mbwa!!
. . Nikamvuta hadi nyuma ya nyuma, ghafla nakutana na
wanaume wawili kati ya wanne nikatambua kuwa kazi sasa
imeanza.
. . Nikamwachia mbwa akala sahani moja na bwana mmoja
halafu mimi na kirungu dhidi ya mwanaume asiyekuwa na
silaha, Sam nilimrukia, akanipiga teke mbavuni yule -----,
nikajikaza nikafyatuka na rungu nikalituliza hapa (akagusa
utosi wake) jamaa akalainika bila kupiga kelele, chini!!. Ile
nageuka namkuta mwenzake akitapatapa pale chini damu
inamruka, nikammulika nikahisia kuwa uhai ulikuwa
unafanya urafiki naye. Nikamrukia kwa ghadhabu, kabla
sijamfikia nikajikwaa nikaanguka chini, nilipoamka hasira
zote kwa yule bwana, na yeye nikamtandika rungu kwenye
paji la uso. Bila shaka kajifia yule we tungoje taarifa ya
habari tu. Kuja kusimama wima tena simwoni mbwa.
Nikataka kumwita kwa sauti ya juu lakini nikahofia usalama
maana nilitambua fika kuwa wale wanaume wawili wapo
bado kule mbele. Nikaanza kunyata taratibu gizani ili
nitambua kulikoni, ndo hapo nikaisikia sauti ya baba
mwenye nyumba ikimwamrisha mbwa kushambulia!! Walau
amani ikarejea japo niliendelea kunyata, hadi wakati
nafanikiwa kufika ndipo namuona yule mbwa akitaka
kukushambulia nikamzuia
Sam Mungu ametupangia jambo
fulani amini!! Hili tukio halikuwa la kuokoka kirahisi namna
hiyo hata kidogo. Jojina alimaliza na kushusha pumzi kwa
nguvu, nami nikashusha pia kama tuliambizana kufanya vile
kwa pamoja.
. . Sam nadhani tunatakiwa kupumzika halafu kesho
twende Makanyagio. Lazima tuanzie huko.
. . Makanyagio? Ndo wapi huko??
. . Kweli wewe mgeni Iringa nimeamini. Huko ni sehemu
maarufu sana kuna makaburi kule, kama unakisikia chuo cha
Mkwawa basi ndo kuelekea hukohuko. Alimaliza kisha
akasimama, lakini mimi sikuwa na usingizi. Jojina akaleta
godoro la pamba ambalo lilikuwa linatoa harufu ya uvundo
akalitandika pale sebuleni.
. . Tutalala hapa maana huko chumbani hapalaliki kuna
harufu sana.
. . Popote tunalala Jojina. Nilimuunga mkono.
Akajitupa na baada ya muda alikuwa anakoroma, nilijaribu
kujilazimisha kulala lakini hata usingizi haukujileta jirani
nami.
Nikapata wazo la kujishughulisha na bahasha na yaliyomo.
Maana swali juu ya hawa watu walikuwa wanatafuta nini na
mbona wameacha ile bahasha lilikuwa linanisumbua.
Nikaichukua bahasha kutoka katika kiti alichokuwa ameketi
Jojina.
. . Nikashtuka na mapigo yangu ya moyo yakaongeza
mwendo kasi. Bahasha ilikuwa nyepesi sana tofauti na
ilivyokuwa awali wakati inabeba picha na makorokoro
mengineyo.
. . Nikaanza kutetemeka nikiamini kuwa ule ushahidi
nilioupigania kwa muda mrefu umetoweka, nikaingiza kwa
uoga mkono ndani ya ile bahasha. Hapakuwa na makaratasi
mengi sana.bali karatasi moja tu!!
. . Nikalichomoa upesi. Lilikuwa karatasi tofauti kabisa na
yale ambayo yalikuwa ndani ya bahasha ile awali.
Nilianza kumwamsha Jojina awe shahidi lakini bahati mbaya
hakunisikia hata kidogoa alikuwa amezama katika dimbwi la
usingizi.
. . Nilijaribu kuiweka akili sawa labda si bahasha
ninayoitazamia, lakini ilikuwa ni ile na sasa haikuwa na kitu
ndani yake.
. . Nikafungua ile karatasi kwa makini nitambue kama nayo
ni moja kati ya zile za awali lakini hapana hii ilikuwa
tofauti.
Nikajongea katika mshumaa, nikaanza kuisoma.
Hofu ikatanda maradufu, ulikuwa mwandiko wa kike.
. . Sam kama huu ujumbe utakufikia, fanya kila uwezalo
uniokoe Sam. Nimefanya kila jitihada nijitoe katika mikono
ya watu hawa lakini jitihada zimegonga mwamba.
Nakuandikia ujumbe huu nikiwa nimekata tamaa kabisa ya
maisha na sina uhakika kamaq utaupata ujumbe huu, Sam
yanayotokea huku hayasimuliki hata kidogo kwa maandishi,
ninayoyashuhudia huku nilipo ni mazito mimi na wewe
hatuyawezi bila msaada wa watu wengine, lakini hao watu
wengine ambao nawasema wote wapo katika upande wa
watu hawa. Sam kama ukiona ni ngumu sana kuniokoa,
amini kuwa nimeridhia kufa. Wewe funga safari ondoka
katika nchi hii, nenda mbali Sam maana ukiingia huku
hautatoka Sam. Jiondokee uende mbali labda utapata
msaada kutoka kwa watu wengine huko wasiokuwa wenyeji
wa ardhi hii.
Natamani sana walau ningejua huku nilipo ni wapi lakini
bahati mbaya sina hata kitu kimoja cha kufananisha eneo
hili. Na bora ningekuwa natulia sehemu moja, hawa jamaa
wananihamisha kila leo. Nimeuza utu wangu Sam na
nimeshiriki penzi na huyu bwana ambaye kama ni mkweli
atakufikishia ujumbe huu, ameshindwa kabisa kunivujishia
siri za humu lakini amesema kuwa hapendezwi na mambo
ya humo na atakushirikisha. Nimeamua kumwamini kwa
sababu sina namna na hata nisipomwamini mimi ni wa kufa
tu Sam wangu!!! Sama kama itakuwa sawa naomba
umsikilize huyu bwana, macho yake hayadanganyi hata
kidogo, na laiti kama pasingekuwa na vifaa vya kurekodia
humu ndani angeweza kunieleza jambo nami nikakuandikia.
. . Sina thamani yoyote zaidi ya uhai nilionao,
nimejirahisisha kimapenzi mara kadhaa ili niweze kuokoka
lakini haijasaidia. Nimejirahisisha kwa huyu bwana pia, sijui
kama nitafanikiwa ame nimeshindwa!!!
. . Samahani kwa mwandiko huu mbaya, nimeyaandika haya
nikiwa katika giza, narudia tena kama huyu bwana ni
mkweli basi alifanya hila ya kuzima taa na kuzuia kamera
kuweza kunirekodi, nikafanikiwa kukuandikia haya.
Sam, kama sitafanikiwa kupona nifikishie salamu hizi kwa
mama yangu mwambie nampenda sana, pia mwambie mzee
Matata katika maisha yake ajifunze kumsikiliza mtu kabla
hajaamua kumuhukumu. Hii itasaidia kuokoa wengi.
. . Akupendaye!!!
. . Anitha