SEHEMU YA ISHIRINI NA SABA
Hatimaye simu yangu ikanirejeshea fikra za msaada.
Kutazama ilikuwa ikilalamika kuwa betri imeishiwa chaji.
Nikafanya upesi kumpigia Jojina lakini hata simu haikuita
ikawa imezima.
Sikuwa na muda wa kupoteza. Nikaruka matuta kadha wa
kadha na hatimaye nikaupata uelekeo sahihi wa kuelekea
Michigani kwa Masawe! Sikuliacha faili langu na sasa likiwa
katika mfuko. Nilihitaji kujua nini chanzo cha haya yote.
Siku hii dukani pale umati ulijaa, nikastaajabu nini
kinaendelea. Nikaomba kupita lakini watu walikuwa wabishi
sana, nikajitahidi kupenya hivyohivyo. Nilijihisi moyo
ukisaidiana na kiherehere ukinisukua kusonga mbele,
nilitaka kila mtu ajue kitu asichokijua nilitamani kila mmoja
awe shahidi. Ile dunia iliyokuwa imenitenga nilitaka iungane
nami huku ikiona aibu.
Nilijibana kinguvunguvu Hadi nikaufikia ukuta wa polisi
ambao haukuruhusu mtu yeyote kupenya pale, mimi nikiwa na
kihoro nikapenya huku nikiwa nusu nakimbia nusu natembe,
risasi ikafyatuka na kuchimba pembeni ya mguu wangu, mara
nikasikia napaishwa hewani. Sasa nikayasikia maumivu!!
Risasi ilikuwa imenichuna!!
Mimi raia mwema jamani, mimi raia mwema!! nikapiga
kelele sana. Askari wakanisogelea wakiwa na hasira kali,
wakataka kuchukua kilicho mikononi mwangu nikawa mbishi
sana sikuwa nawaamini hata kidogo. Niliamini kabisa kwa
jinsi sura yangu ilivyokwanguka kwanguka hakuna ambaye
angeweza kunijua.
Kipigo kikazidi wakinisihi niachie faili na hapo nikamkumbuka
mtu wa kunisaidia. Lakini kipigo kikaniweka gizani, huku faili
likinitoka mkononi.
Umuhimu wa faili lile ukanipa nguvu tena, nikazivuta pumzi
zangu ndani na nilipotoa nje niliuita msaada!!
Mama laooooo!! nikaita kwa nguvu zote nikiuona mgongo
wake.
Sauti yangu niliyoipaza kwa nguvu zote, labda nguvu za
mwisho kabisa za kunikomboa ilimfikia.
Jojina akageuka ghafla! Macho yetu yakagongana na hapo
nikaanguka chini kinywa changu kikiyauma majani machache
yaliyokuwa katika ardhi ile huku macho yangu yakimtazama
mwanamama yule akinijia kwa kasi ya ajabu. Jojina alikuwa
mwepesi sana, akatimua mbio na kunifikia pale nilipokuwa
akawasukuma askari wale huku na huko.
Wakamtisha na bunduki zao lakini hakutishika, hakuzitazama
zile bunduki bali alichokitazama ni mimi, mimi pekee!!
Mwacheni mwachee!! alikaripia huku akitapatapa, askari
wakastaajabu sana wakabaki wameduwaa wasijue la
kufanya.
Wakati wakiendelea kupigwa na bumbuwazi, macho yangu
yakaona kiatu ninachokifahamu, kiatu ambacho hakikuwa
kigeni hata kidogo machoni mwangu!!
Nikajitutumua na kutazama ni kiatu chake ama nilikuwa
nimemfananisha!!
Huku nikiyasikia maumivu makali nilifanikiwa kugonganisha
macho yangu na mtu aliyekuwa amevaa kiatu hicho.
Naam!! Hakuwa mwingine, alikuwa ni yule bosi aliyenisalitiu
na baada ya kashkash mtoto wake akaamua kuungana nami
lakini hakudumu sana akatoweka kimaajabu.
Mzee Matata alikuwa amesimama mbele yangu.
Hakika alikuwa amekongoroka kama Jojina alivyonieleza kwa
njia ya simu, tukatazamana akawa anaona haya!
Nikamsalimia kwa shida. Shkamoo bosi. Akanijibu kiaibu
aibu. Wakati huo Jojina alikuwa akiwaeleza jambo askari
ambao walikuwa wananishushia kipigo.
Huduma ya kwanza waliokuja na polisi wakafika pale
nilipokuwa wakitaka kunichukua, nikawasihi wangoje kidogo
nimalize kazi. Maana huo haukuwa muda muafaka wqa
kutulia kitandani nikipata huduma.
Wahudumu walilazimika kunielewa hasahasa baada ya
kuwaeleza kuwa eneo lile si salama sana. Kuna jambo lazima
liwekwe sawa. Nikaeleweka!!
Na hapo nikasimama tete japo nikiwa nayumbayumba,
wakaniwekea dawa mguuni nilipokuwa natokwa damu.
Nikawauliza akina Jojina nini kinaendelea hapo.
Wakadai kuwa mlango ule haufunguki hata kwa kuvunjwa na
inaonekana ni miaka mingi tangu ufunguliwe hivyo kuna
uwezekano mkubwa kuwa hapana lolote hapo.
Nikatabasamu kidogo na kisha nikawaeleza kuwa ule mlango
unafunguka tena mara kwa mara tu! Na iwapo wanadhani
hakuna lolote linalofanyika pale wanakosea sana.
Wakati huo faili lilikuwa limerejeshwa mikononi mwangu,
wale askari wasijue kuna nini ndani ya nyaraka ile muhimu!!
Sam, hapana si kweli mpenzi wangu hakuna haufunguki
maana kila jitihada imefanyika huenda ulikuwa unaota siku
hiyo!! alinijibu Jojina.
Tukiwa katika maongezi, akatokea ofisa wa polisi kanda ya
Dar es salaam ambaye aliongozana na msafara huo,
nilimuuliza Jojina kwa kunongona iwapo anamuamini huyo
ofisa, akadai wanamuamini sana. Na hapo akanieleza kuwa
baada ya mambo kuwaendea mlama na mzee Matata
kufukuzwa kazi basi huyu ndiye alikuwa kimbilio la mwisho na
ni huyu aliyewawezesha kufika Iringa na kama hiyo haitoshi
aliwawezesha kuwakamata baadhi ya wahusika ambao
waliwatia mashaka. Hawa walikuwa ni wale wanaume wawili
ambao nami niliwahi kuwaona hapo kabla.
Sam, kama hiki kilichotuleta huku hakipo basi utawajibika.
Alinikaripia yule bwana, nikayatazama macho yake na kuona
hatia ikimtawala.
Walewale!! Nilijisemea.
Nikapiga hatua mbili mbele na kufanikiwa kuwaona wale watu
wawili waliomkamata Shanta siku kadhaa nyuma, wote
walikuwa wameunganishwa mikono yao kwa pingu!! Na askari
wababe walikuwa wamewazunguka na bunduki zao.
Sam kama hauna uhakika, tusifike mbali na mambo haya!!
Jojina akanieleza wakati najongea taratibu huku umati
ukisubiri kujua kuna nini hapo.
Jojina, si wewe uliyenisihi nisiwe nakata tamaa, si wewe!!
Ama umekuwa pamoja nao. Nikamkaripia. Akajirudi.
Nikaufikia ule mlango wa siri. Nikazuga kuuvuta kwa nguvu.
Tumetumia nguvu nyingi zaidi ya hiyo uliyojaribu
kutumia!! alinipa angalizo askari mmoja, huku akionekana
kama anayekejeli!!
Na ndo maana haukufunguka maana mlitumia nguvu bila
akili!! nikawajibu kimoyomoyo.
Nikawatazama wale waliopigwa pingu na wao walikuwa
wakicheka kwa dharau. Bila shaka waliamini kuwa sitaweza
kufanya lolote lile, na waliamini kuwa siri ambayo
hakuitambua Masawe basin a mimi ni mbumbumbu vilevile.
Nikajipekua mifukoni na kutoka na funguo! Kabla ya
kufungua nikawaonyesha wale wanaharamu waliobadili
historia ya maisha yangu kuwa mbaya nay a mashaka.
Hukumu yenu imewadia!! nikawaambia kwa lugha ya
kiingereza.
Macho yakawatoka pima!
Sikuwajali, nikaingiza ule funguo na kuufungua mlango!!
Kila mtu akaduwaa!! Kama nilivyoingia awali bado palikuwa
na mwanga!!
Wale askari waliokuwa wameduwaa wakaamrishwa kuingia
ndani na mbwa wao, mbwa wa kwanza tu alipoingia ndani ya
sekunde kadhaa yakasikika mayowe.
Angalia asijekuwa yeye
tafadhali..
Hatujaziruhusu kuuma
usijali. Wakanieleza.
Yule ofisa niliyemuhisi kuwa ana hatia ina mkabili
akanifuata na kunivuta kando, alibaki kutikisa kichwa
asiseme neno na kisha akasema.
Jeshi letu linahitaji roho za paka kama wewe. Kuanzia
ulipokuwa mwandishi hadi harakati hizi nakupa heshima
yako!!
Nikajikuta natabasamu! Aliyeniona wa nini sasa
ananithamini!!!
Zile hekaheka zikanichangamsha mwili, nikayasahau maumivu
na mimi nikaingia katika mtafutano huu wa aina yake.
*****
MTU wa kwanza kutolewa mle ndani alikuwa ni swahiba wangu
Masawe, alikuwa amejikojolea tayari huku akiwa haelewi
kama analia ama anajaribu kulia. Askari walikuwa
wanamgombania huyu akivuta huku huyu anavuta kule
ilimradi kumtia wazimu Masawe!!
Jamani mi sijui kitu mnanionea bure asee kwa lafudhi ya
kichaga Masawe alilalamika. Nilitamani kucheka lakini
haikuwepo sababu ya kunifanya nicheke mambo yalikuwa bado
sana.
Masawe akarushwa katika karandinga na kupigwa pingu!!
Nikamfuata yule afsa ambaye sasa alikuwa rafiki
nikamweleza juu ya Masawe nikamsihi kuwa simfundishi kazi
lakini yule bwana hajui lolote na ametumiwa tu! Akanielewa
na kwenda kusema naye.
Baada ya nusu saa akanieleza alichosema Masawe. Ni kwamba
alipigiwa tu simu ya ghafla na kusisitizwa achukue funguo
mahali na kufungua kile kitasa na kuingia ndani kisha afunge
kabisa. Masawe akadai kuwa ilikuwa mara yake ya kwanza
kuingia na kukijua chumba hicho.
Nikamweleza afisa pia juu ya Masawe. Akaahidi kumsaidia!!
Mzee Matata alikuwa mstari wa mbele kuhangaika huku na
kule, mimi walinisihi nipumzike lakini niliamini bila nguvu
yangu wasingefanikisha lolote, nikaamua kuungana nao.
Vioo vikavunjwa pale pasipoweza kufunguka, watoto zaidi ya
themanini wakatoka wakiwa uchi. Hii ilistaajabisha sana,
hakuna aliyejua maana ya watoto hawa kuhifadhiwa katika
maficho ya namna ile.
Vyumba vyote vikafunguliwa, wakatoka watu wazima wakiwa
hoi kwa vipigo, wengine walikuwa maiti tayari.
Shanta alitoka akiwa hai!! Kumbe naye walimuingiza humo?
Nilistaajabu!!
Hatimaye akatoka yule mwanamke nimpendaye kupita wote
Mama Eva, alikuwa na majeraha makubwa sana mwilini
mwake, macho yake yalikuwa wazi lakini ni kama hakuwa
anaona lolote mbele yake. Nilimuita lakini hakuitika, nguo
zake zililowa damu na uso wake ulikuwa umevimba
hovyohovyo!!
Niliuma meno yangu kwa uchungu mkubwa, nikajenga hasira
maradufu kwa yeyote yule ambaye amehusika na mpango huu
hadi kumuingiza mke wangu katika mateso asiyohusiana nayo
hata kidogo. Nilitamani kufuata msafara wa wauguzi
waliombeba mke wangu, lakini nikajionya kuwa uwepo wangu
hautamsaidioa lolote lile, nikaamua kuwaachia jukumu lile
wanaohusika.
Nikiwa nataka kurejea shimo mara macho yangu yakawa
kama yananidanganya, ama la yalikuwa yanasema ukweli.
Nikayapikicha vyema, huku miguu ikigoma kupiga walau hatua
moja mbele. Nikataka kuita lakini koo nalo lilikuwa
limekauka.
Macho yangu yalikuwa yanatazamana na kiumbe cha ajabu
sana, kiumbe ambacho labda ni mimi mwenyewe kiliniogofyua
maana waliokibeba hawakuwa na hofu hata kidogo, kasoro
mimi t undo mapigo ya moyo yalikuwa yakiongeza kasi yake.
Nilikuwa natazamana na mzimu wa ajabu sana!!!
Mzimu ulioniingiza katika maswaibu haya, mzimu uliotoweka
kishja ukaonekana, ukatoweka tena na sasa nauona tena
mzimu wa Anti Ezekiel wa Temeke!!
Nikiwa napitiwa na mambo lukuki kichwani mara mzimu ule
ukajitutumua na kuyafumbua macho yake wakati huo ukiwa
katika machela ya kubebea wagonjwa!!
Mzimu ukatabasamu. Maajabu!! Si alikufa na akazikwa huyu,
na niliyaona maiti yake kitandani
. Sio Ezekiel huyu?
Wakati najiuliza hayo, Anti Ezekiel alinyanyua mkono wake
na kunifanyia ishara ya dole gumba. Bado alikuwa
anatabasamu
Ezekiel hakufa?
Sasa ile maiti ndani ya chumba chake alikuwa nani yule?
Au ushirikina? Nilijiuliza wakati huo Ezekiel akizidi
kutokomea katika machela aliyokuwa amepakizwa!!