Wakili wa shetani
JF-Expert Member
- Nov 22, 2022
- 2,159
- 4,078
KAMA UKITAKA KURINA ASALI USIPIGE TEKE MZINGA
Tarehe 7 mwezi wa tano mwaka 1931 kulikuwa na msako wa aina yake wa mhalifu ambao jiji la New York halijawahi kushuhudia. Baada ya msako wa wiki kadhaa, mhalifu aliyejulikana kama Crowley “Bunduki mbili”, muuaji na jambazi wa kutumia silaha ambaye hakutumia wala kuvuta kilevi chochote alikuwa amepatikana. Alikuwa amezingirwa katika makazi ya mpenzi wake katika mtaa wa West End.
Polisi mia moja na hamsini walizingira maficho yake yaliyokuwa kwenye ghorofa ya juu kabisa. Walikuwa wametoboa matundu kwenye paa. Walikuwa wanajaribu kumtoa Crowley “Muua polisi” kwa kutumia gesi ya kutoa machozi. Walitega bunduki katika majengo yanayozunguka. Kwa zaidi ya saa nzima, eneo tulivu la jiji la New York lilirindima kwa milio ya bastola na bunduki za rasharasha. Crowley alijificha nyuma ya sofa na kuwarushia polisi risasi mfululizo. Watu elfu kumi walikuwepo kushuhudia mapambano hayo. Kitu kama kile hakijawahi kutokea katika jiji la New York.
Crowley alipokamatwa, kamishna wa polisi, E. P. Mulrooney alikiri kuwa jambazi Crowley “Bunduki mbili’ ni moja ya wahalifu hatari zaidi kuwahi kutokea katika historia ya jiji la New York. “Huyu haoni taabu kuua,” alisema kamishna.
Lakini Crowley “Bunduki mbili” alikuwa na maoni gani kujihusu? Tunafahamu maoni yake kwa sababu wakati polisi wanarusha risasi kwenye makazi yake, yeye aliandika barua kwa “Yeyote atayejali.” Wakati anaandika barua hiyo, damu kutoka kwenye majeraha yake iliacha alama katika karatasi. Kwenye barua hiyo Crowley alisema: “Katika kifua changu mna moyo uliopondeka lakini wenye rehema, moyo usioweza kumdhuru yeyote.”
Kabla ya tukio hili Crowley alikuwa anafurahia maisha na mpenzi wake katika barabara moja huko Long Island. Ghafla polisi aliwafuata kwenye gari na kusema: “Naomba kuona leseni yako.” Bila kujibu kitu, Crowley alitoa bunduki na kummiminia mvua ya risasi. Polisi yule alipokuwa anakufa, Crowley alitoka ndani ya gari na kuchukua bastola ya polisi na kuumiminia risasi mwili uliokuwa umelala chini, huyo ndiye muuaji aliyesema: “Moyo wangu umepondeka lakini ni wenye rehema, hauwezi kumdhuru yeyote.”
Crowley alihukumiwa kifo kwa kiti cha umeme, alipokuwa anaingia kwenye gereza la wafungwa wanaosubiria kifo alisema, “Je hiki ndicho malipo ya kuua watu? Hapana, haya ni malipo ya mimi kujilinda.”
Lengo la hadithi hii ni kuonyesha kuwa: Crowley “Bunduki mbili” hakuona kama ana kosa lolote.
Je hilo ni jambo lisilo la kawaida kwa wahalifu? Kama unafikiri si la kawaida sikiliza haya:
“Nimetumia miaka yangu kuwapa watu furaha, na kuwasaidia kuwa na maisha mazuri na malipo niliyopata ni uonevu.Kuishi kama digididi.”
Hayo yalikuwa ni maneno ya Alcapone. Muhalifu hatari kabisa Marekani. Kiongozi wa genge la uhalifu hatari kabisa kuwahi kutokea katika jiji la Chicago. Capone hakujilaumu, badala yake alijiona ni mtu anayesaidia jamii. Msaidia jamii asiyeeleweka na asiyethaminiwa inavyostahili.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Dutch Schultz kabla ya kuuwawa na mwanachama wa genge la uhalifu huko Newark. Mtu mmoja alisema katika mahojiano kuwa Dutch Schultz alikuwa ni mtu anayesaidia jamii na aliamini hivyo.
Nimewahi kuzungumza kuhusiana na hili suala na Lewis Lawes ambaye alikuwa ni mkuu wa gereza maarufu huko New York la Sing Sing kwa miaka mingi, alikiri kuwa ni “Wahalifu wachache sana wanajiona kuwa ni watu wabaya. Wanajiona ni watu wa kawaida kama mimi na wewe tu. Wanajiona kuwa wana sababu za msingi za kufanya wanayoyafanya. Wanaweza wakakuambia ni kwanini wanavunja sanduku la pesa, au kwanini ni wepesi kufyatua risasi. Wengi wao hujitahidi kutafuta sababu za uwongo na kweli kutetea uovu wao. Hata wakijaribu kujiaminisha wao wenyewe kuwa hawana hatia. Hupaza sauti wakisema hawakustahili kufungwa.
Iwapo Al Capone, Crowley “Bunduki Mbili,” Dutch Schultz na wanaume na wanawake wengine waliojaa magerezani hawajilaumu kwa chochote, vipi kuhusu watu ambao mimi na wewe tunakutana nao?
Muanzilishi wa maduka ya Wanamaker, John Wanamaker aliwahi kiri hivi: “Nilijifunza miaka thelathini iliyopita kuwa ni ujinga kushutumu. Ninapata ugumu wa kutosha katika kukabiliana na mapungufu yangu, siwezi anza kuhangaika na ukweli kuwa Mungu aliamua kutogawa akili kwa usawa.”
Wanamaker alijifunza jambo hilo mapema sana, lakini mimi imenichukua kufanya makosa kwa theluthi ya karne kabla sijaanza kuelewa kuwa kati ya mia moja, mara tisini na tisa, watu huwa hawajishutumu kwa chochote. Haijalishi ni kibaya kiasi gani. Kushutumu hakusaidii lolote, na zaidi zaidi kunamfanya mtu ajitahidi kujitetea. Shutuma ni hatari kwa sababu zinaharibu heshima ya mtu, inampunguzia kujithamini na huleta chuki.
Mwanasaikolojia maarufu, B. F, Skinner alithibitisha kupitia majaribio aliyoyafanya kuwa, mnyama anayezawadiwa kwa kuwa na tabia njema hujifunza haraka, na hukumbuka vizuri kile alichojifunza kuliko mnyama anayeadhibiwa kwa kuwa na tabia mbaya. Tafiti zilizofuatia zilionyesha kuwa hata kwa binadamu iko hivyo. Kwa kushutumu hatuleti mabadiliko ya kudumu, na mara nyingi tunaishia tu kujenga chuki.
Mwanasaikolojia mwingine maarufu, Hans Selye alisema, “Kama ambavyo tunapenda kukubalika, ndivyo tunavyochukia kushutumiwa.”
Chuki inayoletwa na na shutuma, inaweza athiri ari ya wafanyakazi, washiriki wa familia na marafiki, na bado ikawa haijarekebisha jambo au hali ya mambo iliyosababisha shutuma.
George B Johnston kutoka Enid Oklahoma ni msimamizi wa masuala ya usalama katika kampuni ya uhandisi. Moja ya majukumu yake ni kuhakikisha wafanyakazi wanavaa kofia ngumu kila wanapokuwa kazini.Alisema kuwa, kila alipokuwa anakutana na mfanyakazi ambaye hajavaa kofia ngumu, alikuwa akimwambia kama mtu mwenye mamlaka kuhusu sheria ya kuvaa kofi na kuwa anapaswa aifuate. Matokeo yake ni kuwa walimkubalia kwa shingo upande, na mara tu alipotoka wafanyakazi walivua kofia zao.
Akaamua kutumia mbinu nyingine. Alipokutana tena na wafanyakazi ambao hawajavaa kofia zao, aliwauliza iwapo kofia zinawatinga au haziwatoshi vizuri. Kisha kwa kauli nzuri aliwakumbusha kuwa kofia zimetengenezwa kwa namna itakayowalinda na madhara, na kushauri kuwa zivaliwe mara zote wawapo kazini. Matokeo yake ni kuwa watu wakaongeza uvaaji wa kofia bila kinyongo wala kujihisi vibaya. Unaweza kukisoma chote ndani ya maktaba.co.tz
Itaendelea. . .