RIWAYA : Angamizo

RIWAYA : Angamizo

RIWAYA: ANGAMIZO
MWANDISHI:HALFANI SUDY
SIMU 0674395733
WHATSAPP 0757633010

Sehemu ya Tatu

ILIPOISHIA JANA

" Sasa Abdul mimi nitakupa hela"
"Nitashukuru sana yaani dada yangu"
"Lakini kwa sharti moja tu"
"Nipo tayari kufuata sharti lolote Raiya"
"Kweli ?"
"Kweli nakwambia"
SONGA NAYO SASA..
..
"Nitakupa shilingi laki tano leo. Na nitakuwa nakutumia matumizi kila utakapohitaji. Lakini naomba twende chumbani ukaniridhishe Abdul. Ukaupe nafuu moyo wangu. Ukanipe vile nilivyovikosa tangu niolewe na mume wangu na tutakuwa tunafanya hivyo kila nitakapokuwa nahitaji"
Abdul alipigwa na butwaa. Kwanza hakutegemea kupata msaada mkubwa kama ule kutoka kwa Raiya. Ulikuwa msaada mkubwa uliokuja wakati akiouhitaji sana. Kwa Abdul, laki tano Ilikuwa ni zaidi ya msaada. Tatizo lilikuja katika sharti lake. Raiya alikuwa anataka kufanya mapenzi na Abdul. Lilikuwa sharti gumu sana kwa Abdul. Pesa alikuwa anazitaka sana lakini kufanya mapenzi Na Raiya tena mke wa mtu alikuwa hataki kabisa.
"Umenielewa Abdul ? "
" Nimekuelewa Raiya, lakini wewe mke wa mtu"
"Kwahiyo ? "
"Utakuwa humtendei haki mumeo"
"Hizi laki tano ninazotaka kukupa wewe nimemuibia yeye. Je kumuibia hela zake ni kumtendea haki ?" Raiya aliongea huku akimuonesha burungutu kubwa la pesa.
"Kama hutaki pesa nenda kwa miguu Mtwara"
Abdul alikuwa katika wakati mgumu sana wa kufanya maamuzi katika maisha yake. Alijikuta anakubali kufanya mapenzi na Raiya, siyo kwa kumpenda ila kwa kupenda kusoma. Aliamua kuutumia mwili wake kwa manufaa ya maisha yake ya baadae. Walivunja amri ya sita ndani ya Kebby hoteli !
***
Abdul alistuka na kuangalia saa yake ya mkononi. Akakumbuka alikuwa na ahadi na Mayasa saa mbili usiku Tengeru. Na sasa Ilikuwa saa moja kamili. Alijiandaa kwa ajiri ya kwenda kutekeleza ahadi hiyo. Alioga. Akavaa suruali yake nzuri ya jeans pamoja na T-shirt nyeupe iliyoandikwa maneno kwa rangi nyeupe
'Napenda Riwaya".
Chini alivaa raba nyeupe, zenye nembo ya Ocafona. Alijupulizia pafyumu. alikuwa ananukia vizuri sana. Akaenda Tengeru hoteli. Alifika hotelini saa mbili na dakika mbili usiku. Alimkuta Mayasa ameshawasili tayari. Mayasa alimlaki kwa furaha kubwa sana. Walikaa na Mayasa na kuongea mambo mbalimbali hadi saa nne usiku. Ndipo Mayasa alipotaka kujua sababu ya Abdul kuwa na mawazo na kuongea peke yake.
"Abdul"
"Naam"
"Kwanini unaonekana mtu mwenye mawazo sana ?"
"Niko sawa Mayasa"
"Hauko sawa Abdul,unafikia hatua ya kuongea peke yako Abdul "
"Kweli nina matatizo Mayasa, ila tutafute sehemu iliyotulia zaidi ya hapa nitakueleza. Wewe ushakuwa rafiki yangu sasa sina budi kukwambia kila kitu kinachonisibu "
"Nitafurahi sana, sehemu gani unadhani itakuwa nzuri kwako "
"Popote patakapokuwa pametulia zaidi ya hapa"
"Sawa kesho jioni nitakupigia. Tutaenda Moshi. Kule kuna bustani moja nzuri sana kwa maongezi"
"Sawa Mayasa"
Walikodi teksi pale Tengeru liyowarudisha hadi Arusha mjini. Mayasa alimuacha Abdul hosteli za Chuo, na yeye kuelekea nyumbani kwao.
Kesho yake jioni, Abdul na Mayasa walienda Moshi, Paradise garden ndipo alipompeleka. Ilikuwa sehemu tulivu. Yenye maua mazuri na majani machache yaliyopandwa kwa ustadi mkubwa. Kulikuwa na meza zilizokaa mbali mbali. Walichagua meza moja . Walikaa na Mayasa na alianza kumsimulia historia ya maisha yake. Alimsimulia Mayasa historia yake kuanzia Bagamoyo. Magumu yote aliyopitia katika kusoma. Alimsimulia jinsi alivyokutana na Raiya. Na mkataba wa ngono alioingia na Raiya. Sasa alikuwa mtumwa wa ngono wa Raiya. Kumpa penzi Raiya kila atakapojisikia, naye kumhudumia katika matatizo yake yote.
"Ukweli sikuwa nampenda Raiya. Sikuwa napenda mkataba ule wa ngono. Niliuchukia sana. Lakini sikuwa na jinsi Mayasa. Nilikuwa napenda kusoma. Ilibidi nifanye akivyotaka Raiya. Naamini Raiya nae hakuwa ananipenda. Alinipenda mimi kwa ajili ya ngono tu, alinifanya 'sex toy. Nilimaliza kidato cha sita kwa kusomeshwa na Raiya chini ya mkataba ule wa ngono. Matokeo ya kidato cha sita yalipotoka nilifaulu vizuri . A ya baiolojia B ya fizikia na B ya Kemia. Nilichaguliwa kusomea udaktari. Katika Chuo cha udaktari hapa Arusha. Ambapo ndipo jana nilikutana na wewe."
"Daah pole sana Abdul. Hakika umepitia makuu. Umekuwa mtumwa wa mapenzi. Sasa una mpango gani Abdul ?"
"Natamani kujitoa katika utumwa huo. Lakini sina jinsi Mayasa. Elimu yangu inamtegemea Raiya. Maisha yangu yanamtegemea Raiya. Nitakapomaliza Chuo na kupata kazi hapo ndipo nitakuwa nimejivua utumwa. Utumwa wa mapenzi kama ulivyouita ".
" Nataka nikusaidie Abdul bila sharti lolote. Dhamira yangu ya ndani nimeamua kukusaidia. Nimependa harakati zako za kuitafuta elimu. Unaonesha unapenda kusoma, na una akili sana."
"Nashukuru sana Mayasa. Wewe ni mwanamke mwenye moyo wa ajabu sana."
Walimaliza kuongea na Mayasa saa nne usiku. Walikodi gari iliyowarejesha Arusha mjini. Sasa Abdul alihamia himaya mpya. Himaya ya Mayasa, alimkabidhi kila kitu Mayasa kuhusu maisha yake, kasoro moyo tu. Alipunguza mawasiliano na Raiya na kuongeza mawasiliano na Mayasa...

HAYA SASA ABDUL KAHAMIA KATIKA HIMAYA YA MAYASA, JE NDIPO ANGAMIZO LITAKAPOTOKEA? AU KWANINI RIWAYA HII YAITWA ANGAMIZO? USISAHAU LIKE KURASA YA Napenda Riwaya KWA HADITHI KALI ZA HALFANI SUDY...
 
RIWAYA: ANGAMIZO
MTUNZI: HALFANI SUDY
SIMU: 0674 395733
WHATSAPP: 0757 633010

SEHEMU YA TANO

ILIPOISHIA JANA.....

Walimaliza kuongea na Mayasa saa nne usiku. Walikodi gari iliyowarejesha Arusha mjini. Sasa Abdul alihamia himaya mpya. Himaya ya Mayasa, alimkabidhi kila kitu Mayasa kuhusu maisha yake, kasoro moyo tu. Alipunguza mawasiliano na Raiya na kuongeza mawasiliano na Mayasa.

SASA ENDELEA.....
Ilikuwa siku ya jumatano jioni ya wiki ya pili tangu waanze chuo. Abdul alikuwa na Mayasa wanajisomea darasani muda wa jioni. Simu ya Abdul iliita. Alikuwa Raiya anapiga.
"Wewe unajifanya kiburi. Mimi nimekusomesha umefika Chuo unajifanya mjanja. Sasa kesho nakuja huko huko Arusha nione kinachokuzuzua. Ole wako nisikie una mwanamke. Ole wako!"
Bila salamu Raiya aliwaka kwenye simu. Abdul hakumjibu. Alikata simu na kuizima kabisa. Hamu ya kusoma ilimuisha. Mayasa alisikia kila kitu alichosema Raiya. Raiya alimkaripia kama mtoto Abdul na kwa nguvu.Halafu walikuwa karibu na Mayasa. Alimuonea sana huruma. Hamu ya kusoma ilimuisha. Alimuaga Mayasa na kurudi hosteli. Alifika kitandani na kulala chali. Alifikiria mustakabari wa maisha yake. Alijiona ni mtu mwenye mikosi. Aliulaumu umaskini wake. Aliulaumu umaskini wa wazazi wake. Machozi yalitoka yenyewe taratibu.
Akauhisi mkono laini ukimfuta machozi. Alifumbua macho yake na kuangalia. Alikuwa Mayasa..
"Acha kulia Abdul. Nimejitoa kukusaidia kwa lolote kaka yangu. Naamini tutaushinda mtihani huu.Tutamshinda Raiya. Sitokubali ulie tena."
Mayasa alimbembeleza sana Abdul. Mwishowe akamwelewa. Akanyamaza.
Ilipita wiki moja tangu Raiya ampe vitisho vyake Abdul. Hakutokea Arusha wala hakumpigia simu. Akajua labda amekata tamaa. Akawa anaishi maisha yake kama kawaida. Furaha ikarejea tena.Huku akimtegemea Mayasa kwa kila kitu. Naye hakuchoka. Alimsaidia Abdul.
Upande wa darasani alikuwa anafanya vizuri sana katika masomo. Alikuwa na uwelewa mkubwa sana. Mayasa hakuwa VIzuri sana darasani. Alijitahidi kumsaidia kila alipopata nafasi. Alielewana sana na Mayasa. Walifatana muda wote. Walijisomea pamoja. Walikuwa mithili ya chanda na pete. Kila mwishoni mwa wiki walikuwa wanatoka nje ya jiji la Arusha kutembea na Mayasa.
Siku moja jumamosi Abdul na Mayasa iliwakuta Same. Sasa walikuwa marafiki walioshibana. Abdul alikuwa anafahamu sasa baadhi ya vitu vya Mayasa. Kumbe baba yake Mayasa alikuwa, Ally Hamisi. Makamu wa raisi wa Zanzibar. Baba yake alikuwa mtu mkubwa sana Serikalini lakini hakuna hata siku moja aliyemtamkia mdomoni Abdul. Alisikia tu kutoka kwa watu wa pembeni.
Siku waliyoenda Same, walirudi chuoni saa kumi na mbili jioni kutoka. Same Ilikuwa mbali kidogo na Jiji la Arusha. Mayasa alimrudisha kwanza Abdul hosteli ili na yeye arudi kwao. Walienda Same na gari Mayasa. Walipofika karibu na chumba cha Abdul, nje walikutana na Justus. Kijana aliyekuwa wanakaa chumba kimoja pale hosteli.
"Daah afadhali umerudi Abdul, kuna mgeni wako ndani"
"Nani ?" "Simfahamu, ila amefika zamani sana"
"Sawa kaka" Waliingia ndani na Mayasa. Wakiwa hawana wasiwasi hata kidogo. Walipofungua mlango na kuingia ndani walimwona msichana amelala kitandani kwa Abdul. Wote walistuka sana! Walipomwangalia kwa makini, Abdul alimgundua msichana yule. Alikuwa Raiya .
"Naitwa Raiya Mohamedi" Aliongea huku akimwangalia Mayasa usoni.
"Naitwa Mayasa Ally" Mayasa nae alijibu kwa kujiamini.
"Wewe ndiye unajifanya unajua kutembea na wanaume wa watu ?"
"Sema kilichokuleta "
"Kilichonileta ndio hiki ninachoongea "
"Usione vyaelea dada......"
"Sina muda wa kuongea na wewe"
"Abdul ?" Raiya aliita.
Hakuitika.
"Umenisaliti kwa sababu ya hiki kikaragosi ?" Abdul alikaa kimya anamwangalia tu.
" Kumbuka nilipokutoa Abdul, Kumbuka Siku ile pale Mwenge, ningekuacha ungekutana na hiki kikaragosi leo ? " Raiya aliongea maneno yaliyomuingia kidogo Abdul. Pamoja na madhaifu yake kadhaa lakini Raiya alikuwa na mchango mkubwa sana katika maisha ya Abdul hadi alipofikia sasa.
"Sasa chagua moja Abdul. Utakuwa na mimi au huyu ?" Raiya aliongea kwa jazba. Abdul alibaki njia panda. Raiya na Mayasa wote walikuwa na mchango mkubwa katika maisha yake. Na wote walimwangalia yeye kusubiri jibu langu.
" Mayasa siyo mpenzi wangu" Alijua ametamka kwa sauti kumbe sauti haikutoka nje. Mdomo ulikuwa unatetemeka tu.
"Chagua Abdul"
"Achague nini, mimi Abdul siyo mpenzi wangu "
"Ni nani yako sasa ?"
"Rafiki yangu tu "
"Hahaha siku zote mapenzi yanaanzia kwenye urafiki, "OK marafiki. Basi mimi ni mke wa Abdul. Nasema naomba muvuunje kabisa huo urafiki wenu. Siutaki, siutaki, siutaki hata kuusikia. Mkewe nimesema !"
"Raiya wewe ni mke wa Abdul ?"
"Hilo jibu uliza swali "
"Una hakika Raiya ?"
"Ndio"
"Na Salehe je, unamwitaje Raiya ?" Swali hilo allouliza Mayasa lili mstua sana Raiya. Hali sasa ilibadilika mle ndani!
"Mimi ni Mayasa Ally Hamisi, unanikumbuka ?" Mumeo Salehe ni kaka yangu. Mtoto wa mama mdogo Fatma. Au nimpigie Salehe nimuulize kama kakuacha ?" Mayasa aliongea huku akitafuta namba za Salehe katika simu yake.
Raiya sasa alikuwa amechoka hoi. Hajui lipi aseme, lipi aache. Alikosa kauli kabisa. Ghafla alitoka nje ya hostel kwa ghadhabu mithili ya roketi, bila ya kuaga.
Abdul aligundua kitu kimoja kuhusu Mayasa. Mayasa alikuwa msichana msiri sana. Alimficha cheo cha baba yake hadi sasa. Pia kumbe alikuwa anamficha kama Raiya ni wifi yake, hakumwambia kabla. Alianza kumwangalia Mayasa kwa jicho la kumuogopa sasa.
"Usijari Abdul. Raiya ni wifi yangu lakini yeye hakuwa ananijua. Tulionana na Raiya siku moja tu. Tena siku ya harusi yake na kaka Salehe. Hata wewe ulivyonisimulia historia ya maisha yako. Ulipotaja jina la Raiya sikujua kama Raiya wifi yangu, sikufikiria kabisa. Leo nilivyomwona hapa ndio nimemkumbuka ". Mayasa alimjibu kitu ambacho alikuwa akifikiria.
"Sawa Mayasa nimekuelewa" Walitoka nje ili kumwangalia Raiya ameenda wapi ?
Hawakumuona.
Hawakujua ameelekea wapi? Aliyeyuka mithili ya upepo. Baadae Mayasa aliaga na kuondoka kwao huku Abdul akibaki na wingi wa mawazo. Abdul alisinzia akiwa na mawazo mengi. Lakini kutokana na uchovu wa kutoka Same na ukijumlisha mawazo aliyomletea Raiya ndio yalimchosha kabisa, alilala fofofo.
Saa kumi usiku simu yake ilitoa mlio wa sauti alioutega Kwa ajiri ya mwitikio wa ujumbe mfupi. Ikimaanisha kuna meseji mpya iliingia.
'Umeuchokoza moto. Niliacha zamani ukatili. Wewe unajitahidi kunirudisha huko. Nilikuwa katili sana zamani. Kama hupendi nirudie tabia zangu za zamani nakuomba achana na kikaragosi. Nitakuuwa, nitamuuwa pia!.Nakupa siku tatu za kufikiria juu ya suala hili. Mimi bado nipo Arusha. Namaanisha!"
Abdul alikaa kitandani na kuurudia kuusoma ujumbe ule mara tano. Jasho lilikuwa linamtiririka kama maji. Akamtumia ule ujumbe na Mayasa.
Hakuujibu.
Hajaujibu mpaka leo!
Asubuhi na mapema watu wanne walienda katika chumba cha Abdul. Walikuwa wamefuatana na kiongozi wa hosteli, Mshauri wa wanafunzi, na Raisi wa Chuo. Walimuita pembeni na kumwambia.
"Sisi ni askari wa kituo kikuu cha Polisi Arusha. Unahitajika kituo cha Polisi kwa mahojiano kidogo "
"Nimefanya nini jamani ?"
"Utajua hukohuko kituoni!
Askari mmoja alimnyanyua kwa nyuma suruali yake na kupelekwa kituoni. Alikuwa anatembelea vidole sasa. Wanafunzi wenzie walimuonea huruma pale chuoni .
Hakujua amefanya nini ?
Hawakujua amefanya nini?
Baada ya kufika kituoni ndipo alipoambiwa kosa lake. Eti alituhumiwa kwa kumuua Mayasa! Na ujumbe wake wa vitisho kutoka kwanye simu yake yake ulikutwa katika simu yake.
Na ulitumika kama ushahidi
.
INAITWA ANGAMIZO...LIKE, SHARE NA TOA USHAURI WAKO KUHUSU RIWAYA HII....ILA NAKUSHAURI USITHUBUTU KUIKOSA SEHEMU YA SITA...
 
RIWAYA: ANGAMIZO
MTUNZI: HALFANI SUDY
SIMU: 0674 395733

SEHEMU YA SITA

Mpende sana mama yako. Tuwaheshimu mama zetu. Tuwajari sana. Usimdharau hata siku moja mama yako. Mama ni kila kitu katika maisha. Ukimdharau mama basi ni sawa na kuitafuta laana kwa nguvu. Tuwaombee sana mama zetu kwa Mungu kwa wale wote mama zao waliotangulia mbele za haki. Wapate makazi bora huko mbinguni.Hakuna kama mama katika dunia. Hakuna katu..NA HII NI SEHEMU YA SITA...

*****
Baada ya kufika kituoni ndipo alipoambiwa kosa lake. Eti alituhumiwa kwa kumuua Mayasa ! Na ujumbe wake wa vitisho kutoka kwanye simu yake yake ulikutwa katika simu yake. Na ulitumika kama ushahidi.
Alihemewa sana.
Alilia sana.
Aliuona mwisho wa ndoto zake umetimia. Akajua ataozea jela. Aliwekwa selo akisubiri ushahidi ukamilike. Akiwa ndani ya selo Abdul aliwaza mambo mengi sana. Moja kwa moja alijua kama kweli Mayasa ameuwawa basi Raiya ndiye mhusika mkuu wa kifo cha Mayasa. Lakini ujumbe ule aliomtumia Mayasa ulikuwa unamweka mashakani. Alikuwa analia mithili ya kichanga. Afande aliyekuwa anaitwa John ndiye alipewa jukumu la kupeleleza kesi ya kifo cha mtoto wa Makamu wa Raisi wa Zanzibar, Mayasa. Huku wapelelezi mahiri Tanzania wakiletwa Arusha kufumbua chanzo cha kifo hiki kisichoeleweka. Afande John alianza kumhoji Abdul kwanza. Mtuhumiwa wa kwanza wa mauaji yale.
" Unaitwa nani ? "
"Abdul " "Majina matatu !!"
"Abdul Ramadhani Washiro"
"Kabila
" "Msukuma "
"Nambie uhusiano wako na Mayasa ?"
"Alikuwa mwanafunzi mwenzangu"
"Hamkuwa na uhusiano wa kimapenzi ?"
"Hapana,alikuwa ni rafiki yangu wa kawaida "
"Sasa kwanini uliamua kumuua rafiki yako ?"
"Sijamuua mimi afande "
"Soma huu ujumbe "
"Alinitumia Raiya, mimi nilimfowadia tu Mayasa."
"Raiya ndio nani ?"
Alimsimulia afande John kila kitu kuhusu ugomvi wao na Raiya. Alirudishwa selo na afande John alikwenda kwa kina Raiya kumhoji. Hakuwa anapajua , na wala Abdul alikuwa hapajui. Ila alisema atapajua tu!
Afande john alifanikiwa kufika nyumbani kwa dada yake Raiya. Baada ya kumuonesha kitambulisho cha Polisi, Raiya alishangaa sana.
"Jamani, wewe ni askari wa tatu kuja kunihoji leo !"
"Walikuja maaskari wengine hapa ?!"
" Ndio na mmoja katoka nusu saa iliyopita"
"Walikuwa na vitambulisho ?"
"Ndio walinionesha"
"Unayakumbuka majina yao"
"Nayakumbuka sana kwa kuwa majina yao wote yanafanana"
"Wanaitwaje?"
"Wote wanaitwa John" Afande John alisikia kizunguzungu na mivumo isiyoeleweka masikioni mwake Ilikuwa taarifa ya kushangaza sana !
"Itabidi nikakuhoji kituoni " Afande John aliona pale siyo mahali salama pa kufanyia mahojiano.
Walifuatana na Raiya kuelekea kituoni. Hapakuwa na umbali mkubwa sana toka nyumba aliyokuwa anakaa Raiya hadi kituo kikuu cha Polisi Arusha. Raiya alikuwa anakaa katika nyumba ya dada yake aliyokuja kukaa kwa muda mahsusi ili kutekeleza aliyoyakusudia, kutenganisha penzi la Abdul na Mayasa kama akivyoamini yeye kuwa walikuwa wapenzi.
"Raiya hebu nambie vizuri kuhusu hao askari waliokuja kukuhoji kwako."
" Ndiyo kama nilivyokwambia Afande. Walikuja askari wawili kunihoji. Mmoja alikuja asubuhi na mwingine alikuja muda mfupi kabla hujaja wewe. Na wote walitaka maelezo yangu kuhusu kifo cha Mayasa na uhusiano wangu na Mayasa na Abdul ."
"Wewe uliwajibu nini?" "Yule wa kwanza sikumjibu kitu. Maana aliniacha kwenye mstuko mkubwa sana baada ya kunambia Mayasa amefariki. Sikuamini kama Mayasa amefariki..nilikuwa nalia tu kila alichokuwa ananiuliza . Askari yule alifanya kazi ya kunibembeleza tu, akaondoka"
"Askari wa pili je ?" "Yule alinikuta nimetulia sasa. Nilimueleza kila kitu kuhusu ugomvi wetu mimi, Mayasa na Abdul."
"Alisemaje baada ya maelezo yako ?"
"Aliandika kwenye kitabu chake na kuondoka"
Afande John alishusha pumzi ndefu .Akajua ngoma sasa imekuwa nzito ! Akamfungia Raiya selo na kutoka nje kwenda kutafakari. Alikaa chini ya mwembe mrefu uliokuwepo pale nje ya kituo. Akiwaza na kuwazua.
Simu yake ikawa inaita.
Namba ilikuwa ngeni. Zilitokea namba tu. Akaipokea na kuiweka sikioni.
"Hallo"
"Hallo nani mwenzangu ?"
"Huna haja ya kulijua jina langu. Cha muhimu acha kuifatilia hiyo kesi utauwawa bure. Au unahamu ya kumuweka eda mkeo ?"
"Usinitishe kijana "
"Nitakuuwa !"
"Huna jeuri hiyo"
"Unajifanya kiburi"
"Nitawakamata wote wauaji waoga!'
" utaenda kutukamata kuzimu.."
Afande John alihisi amerukiwa na kitu kama maji maji utosini. Aligusa kwa mkono wake wa kulia. Aligusa yale maji. Sauti ya kwenye simu ilianza kucheka.
Ghafla ngozi ya afande John ilianza kuvuka. Afande John alitupa simu chini, alisikia maumivu makali sana. Alikufa taratibu kwa maumivu makali sana! Alikufa aina ya kifo sawa na alichokufa Mayasa!
Sasa ilikuwa mshikemshike. Mauaji ya Polisi kuuwawa nje ya kituo. Ilizua mambo mengi. Mauaji haya ya pili yaliwafanya Polisi wafikirie nje ya boksi. Watuhumiwa wawili wapo ndani, lakini Afande John kauwawa akiwa nje. Bila shaka na wauaji walewale waliomuuwa Mayasa.
Mauaji ya hayo yalilitikisa Jiji la Arusha. Arusha iligeuzwa nje ndani kumtafuta muuaji au wauaji. Hawakupata fununu zozote. Polisi walibaki gizani. Giza totoro!
Mayasa alikuwa Mtoto wa mkubwa Serikalini. Serikali ilituma wapelelezi mahiri watatu. Kwenda Arusha kumsaka muuaji! Walienda wapelelezi watatu. Lakini kila mmoja alivuliwa ngozi kwa siku yake. Waliuwawa kwa maji yaleyale yaliyomuua Mayasa. Maji yaleyale yaliyomuuwa afande John!
Mmoja alikutwa amekufa hotelini kwake, akiwa amelala.Ngozi ikiwa imejitenga na mwili wake.... Wapili alikutwa amekufa akiwa kwenye gari lake. Aina ileile ya kifo alichouwawa mwenzake. Wa mwisho aliuwawa mgahawani. Akiwa anakula chakula cha usiku.

Hali sasa ilitisha!

MAMBO YAMEKUWA MAMBO, SASA VIFO VIMEHAMIA KWA POLISI NA WAPELELEZI, JE NINI SABABU YA VIFO HIVI? JE KUNA MKONO WA RAIYA KWELI...NJOO TENA HAPA Napenda Riwaya KESHO MWANDISHI HALFANI SUDI AENDELEE KUTUSIMULIA MAMBO HAYA YA KUSHANGAZA YALIYPOTOKEA JIJINI ARUSHA
 
RIWAYA: ANGAMIZO
MWANDISHI: HALFANI SUDY
SIMU 0674 395733
WHATSAPP 0757 633010

CHUKI ni kitu kibaya sana. Siku zote chuki ina matokeo mabaya kwa wote, anayechukia na anayechukiwa. Tuache kuikumbatia chuki moyoni mwetu, kuikumbatia chuki moyoni ni sawa na kulikumbatia kaa la moto katikati ya kiganja chako. Bila shaka utaumia mwenyewe mshikaji, na pengine utamuumiza unayemchukia. Utajitesa mwenywe bure, pengine usimtese unayemchukia. Tuache kuibeba dhambi ya chuki moyoni mwetu, Namaanisha tupendane.
NA HII NI SEHEMU YA SABA....
***
Mayasa alikuwa Mtoto wa mkubwa Serikalini. Serikali ilituma wapelelezi mahiri watatu. Kwenda Arusha kumsaka muuaji ! Walienda wapelelezi watatu. Lakini kila mmoja alivuliwa ngozi kwa siku yake. Waliuwawa kwa maji yaleyale yaliyomuua Mayasa. Maji yaleyale yaliyomuuwa afande John ! Mmoja alikutwa amekufa hotelini kwake, akiwa amelala.Ngozi ikiwa imejitenga na mwili wake ! Wapili alikutwa amekufa akiwa kwenye gari lake. Aina ileile ya kifo alichouwawa mwenzake. Wa mwisho aliuwawa mgahawani. Akiwa anakula chakula cha usiku.
Hali sasa ilitisha !
Ndani ya selo hali Abdul Ilikuwa mbaya sana. Polisi hawakuwa wamempiga hata kidogo . Lakini alikuwa amechoka taabani. Alichoka kimwili. Alichoka kimawazo. Kifo cha Mayasa kilimuumiza sana kichwa. Akilini mwake alijua Raiya anahusika kwa asilimia zote. Aliukumbuka sana wema wa Mayasa. Mayasa alikuwa kama malaika kwa Abdul. Mayasa alikuwa mwanamke mwenye roho ya kipekee sana. Alimsaidia bila ya sharti lolote. Alimkumbuka kila dakika mle selo. Sasa alimchukia sana Raiya. Chuki kwa Raiya ilianza taratibu. Lakini sasa ilikuwa imeota mizizi. Alimwona ni adui yake namba moja duniani. Adui kwa kumuua Mayasa. Rafiki mwenye upendo wa kweli kwake.
Wazazi wake hawakuwa wanajua kama yuko jela. Na wala hakutaka kuwaambia, maana hata angewaambia isingesaidia lolote, maana hakuna atakayeenda Arusha. Wasingekuwa na nauli ya kwenda Arusha. Alikuwa anaijua hali ya uchumi ya nyumbani kwao. Aliacha kuwaambia akihofia kuwapa presha za bure. Wakati akiwa anawaza hayo, mlango wa selo ulifunguliwa. Aliingia askari mmoja wa kike. Alikuwa na sura ya huzuni. Alikuja kumpa taarifa mbaya ya kifo. Taarifa ya kifo cha Afande John !
"Inamaana Raiya kamuua na Afande John ?"
" Sidhani kama Raiya anahusika. Afande John amefariki wakati Raiya yuko selo"
"Unasema !"
"Ndio hivyo Abdul, hebu tuambie mtu mwengine unayehisi anaweza kuwa nyuma ya mauaji haya Abdul ?"
"Hakuna nilijualo Afande kweli sijui kitu afande" Alisema huku machozi yanamtoka .
Alirudishwa selo baada ya mahojiano mafupi na askari yule wa kike. Sasa akaona uzito na ugumu wa kesi hii iliyokuwa inamkabili. Akaamua kuwaeleza wazazi wake Bagamoyo kwa simu. Hakuwa na jinsi sasa. Alikuwa anahitaji hekima za wakubwa. Alikuwa anahitaji sana majaliwa ya Mungu. Kutoka katika mkasa huu mzito...!
Aliwaomba askari wampe simu ili awapigie wazazi wake. Awataarifu juu ya kukamatwa kwake.
Walimruhusu.
Alimueleza baba yake mzazi, Mzee Washiro juu ya kukamatwa kwake na Polisi na tuhuma za mauaji zinazomkabiri. Alisikitika sana baba yake. Kwa mara ya kwanza alimsikia baba yake akilia kwenye simu. Alipatwa na uchungu sana. Abdul alikuwa mtoto wake wa kwanza kati ya watoto saba. Alikuwa ndiye tumaini hai la familia yake. Mtoto aliyesoma zaidi ya wote katika familia yake. Habari ya kutuhumiwa kwake kwa kesi ya mauaji, kwa baba yake ilikuwa mithili ya kuzimika ghafla kwa mshumaa pekee akioutegemea gizani. Pamoja na yote alimuahidi kitu. Alim-ahidi lazima aende Arusha punde atakapopata pesa. Abdul alijua baba yake hatokukwenda Arusha karibuni. Na pengine hatokwenda kabisa. Na anaweza kuozea jela Arusha bila kumuona ndugu yake yeyote. Walikuwa mafukara sana nyumbani kwao. Lakini kidogo alipata imani. Kwakuwa nyumbani kwao walikuwa wanafahamu sasa kuwa mtoto wao yupo katika matatizo makubwa ugenini.
Kwa upande wa Polisi wa Arusha Ilikuwa hekaheka ndani ya Jiji. Walitafuta wachuna ngozi wale wasio na huruma bila mafanikio. Walimkamata kila waliyemuhisi, lakini hawakufanikiwa kumkamata muuaji halisi. Ilikuwa kama ametoweka ghafla Arusha. Jiji lilibaki likisubiri Muuaji yule katili ataibukia wapi?
Baada ya wiki mbili yalitokea mauaji!. Safari hii katika Jiji la Mwanza . Mauaji ya aina ileile kama yaliyotokea Arusha. Katika Chuo kikuu cha St Augustine cha huko jijini Mwanza kuna mwanafunzi aliuwawa kikatili. Alikuwa anatoka kujisomea usiku akielelekea Hosteli. Alinyang'anywa njiani roho yake!
Maiti yake iliokotwa asubuhi katika uwanja wa mpira wa chuo ikiwa haitamaniki! Ngozi iliokotwa upande wa goli la kaskazini. Kiwiliwili kisicho na ngozi kiliokotwa karibu na goli la kusini. Yalikuwa mauaji ya kinyama sana! Yaliowaacha na uwoga mkubwa sana wanafunzi wa Chuo hiko kikubwa jijini Mwanza. Mwanafunzi huyo alikuwa ni mtoto wa waziri wa ujenzi, Mheshimiwa Karimu Nduguga.

TUKUTANE TENA KESHO KUENDELEA NA MAMBO HAYA YA AJABU...JE KWELI KUNA MKONO WA RAIYA KATIKA MAUAJI HAYA?
 
RIWAYA: ANGAMIZO
MTUNZI: HALFANI SUDY
SIMU 0674 395733

SEHEMU YA NANE

ILIPOISHIA JANA...
Maiti yake iliokotwa asubuhi katika uwanja wa mpira wa chuo ikiwa haitamaniki! Ngozi iliokotwa upande wa goli la kaskazini. Kiwiliwili kisicho na ngozi kiliokotwa karibu na goli la kusini. Yalikuwa mauaji ya kinyama sana! Yaliowaacha na uwoga mkubwa sana wanafunzi wa Chuo hiko kikubwa jijini Mwanza. Mwanafunzi huyo alikuwa ni mtoto wa waziri wa ujenzi, Mheshimiwa Karimu Nduguga.
SASA ENDELEA...
Polisi wa Mwanza nao wakalipata hekaheka kama ilivyokuwa kwa wenzao wa Arusha, wa kumsaka muuaji huyo asiye na huruma! Lakini hawakumpata na wala hawakukaribia kumpata! Ndipo hali ya hatari ikatangazwa nchi nzima, na Waziri wa wa mambo ya Ndani ya nchi, Mheshimiwa Frank Chali. Ilitolewa tahadhari hasa kwa watoto wa viongozi wakuu wa chama na Serikali. Watoto wa vigogo wakawa wanalindwa hasa. Huku doria za Polisi zikishamiri Tanzania mzima.
Abdul na Raiya waliendelea kusota selo. Sasa walihamishiwa Gereza kuu Arusha.Ilikuwa kwa usalama wao kama Polisi walivyosema.
Wiki mbili zilipita maisha yao yakiwa selo.
Ilikuwa siku ya jumatatu asubuhi. Ya wiki ya tatu tangu wahamishiwe Magereza. Abdul alitolewa selo na kupelekwa katika chumba cha mahojiano cha Gereza lile. Siku hii alihojiwa na mtu mpya. Hakuwa wa gereza la Arusha. Maana wengi ailikuwa anawafahamu sasa.
"Unaitwa nani ?"
"Naitwa Abdul Ramadhani "
"Niambie kwa kifupi unavyolielewa sakata hili ?"
Alimsimulia kila kitu tangu safari yangu ya kutoka Bagamoyo hadi nilivyofika Arusha.
"Unajua Kwa nini umewekwa ndani ? "
"Ndio"
"Kwanini ?"
"Kwa ajiri ya usalama wangu."
"Sasa mimi nataka nikutoe nje Abdul "
"Ati !"
"Ndio nataka uisaidie Polisi ukiwa nje"
"Nahofia usalama wangu, wataniua vibaya "
"Usiwe na shaka. Utakuwa na mimi kila hatua utakayopiga, mimi naitwa Daniel Mwaseba!!"
Alistuka sana kusikia jina hilo. Hakuna Mtanzania ambaye alikuwa halijui jina la Daniel Mwaseba . Alikuwa mpelelezi namba moja Tanzania. Alikuwa mtu hatari kuliko hatari yenyewe. Alishawahi kuliokoa Taifa hili katika matatizo makubwa sana. Aliliokoa kutoka katika hila mbaya za maadui zetu. Alikuwa kijana makini, mpiganaji, mzalendo wa kweli kwa nchi yake. Kuja kwa Daniel Mwaseba kwenye kesi hii Abdul akajua mambo yamefikia pagumu. Mbele ya Daniel alikuwa radhi atolewe. Aliamini atakuwa salama.
Alikubali.
Walitoka Gerezani wakiwa wamefuatana na Daniel Mwaseba. Alijisikia fahari kufuatana na Daniel. Njiani alikuwa anamuuliza hili na lile. Yeye alikuwa anajibu kwa mkato tu. Daniel alikuwa anampekeka Kijenge juu. Kwenye nyumba aliyopangiwa na jeshi la Polisi kuishi kwa muda. Hosteli haikuwa sehemu salama kwake tena. Walishuka kwenye gari ya Daniel wakiwa sambamba. Walikuwa wanakatisha barabara ili waingie katika nyumba aliyopangiwa. Wakati wakiwa katikati ya barabara gari dogo aina ya Noah nyeusi ilikuja kwa kasi kwa lengo la kutaka kuwagonga. Abdul aliliona lakini hakuwa na jinsi ya kufanya.
Liliwakaribia sana.
Kwa kasi ile Abdul alijua lazima wagongwe. Lazima wafe yeye na Daniel Mwaseba. Kilikuwa kifo dhahiri usoni mwao!
Ghafla Abdul alijikuta amerudi nyuma kwa haraka sana!
Gari lilipita sentimita chache sana na pale waliposimama na Daniel. Kilikuwa ni kitendo cha haraka sana. Abdul hakuelewa amerudi vipi nyuma kwa kasi ile. Akamwangalia Daniel Mwaseba alikuwa anatabasamu, hana wasiwasi wowote. Huwezi jua kama kiliwakosa kifo sikunde chache zilizopita .
"Mwanzo mzuri" Abdul alimsikia Daniel akinong'ona mwenyewe.
"Hivi limetukosaje lile Gari? Halafu alidhamiria kutugonga kwa makusudi !."
"Nilikuvuta mkono" Daniel alijibu jibu fupi na kumshika mkono Abdul, wakarejea kwenye gari yake.Kwa hakika Daniel Mwaseba Alikuwa mtu wa ajabu sana. Kwenye gari hakuongea neno. Alikuwa kimya, makini na usukani huku akipiga mluzi. Akiimba wimbo usioeleweka. Lakini akiangalia kwenye vioo vya pembeni vya gari kila mara.
"Hivi kitu gani cha siri alichowahi kukwambia Mayasa?" Ghafla Daniel alimuuliza swali Abdul huku akiwa anaangalia mbele.
"Hakuna kitu cha siri alichowahi nambia Mayasa"
"Una uhakika Abdul ? Nakuuliza hili kwa ajiri ya maisha yako. Kuficha hakukusaidii kitu"
"Kweli kaka Daniel. Hakuna siri yoyote aliyowahi nambia Mayasa."
Safari yao ilishia kituo kikuu cha Polisi Arusha. Walikaa kaunta pamoja na Daniel na askari mwengine. Mara simu ya mezani ya pale kaunta ikaita.
"Hallo "
"Napiga toka Magereza Arusha"
"Ehh nambie Afande"
"Kuna tatizo hapa Magereza"
"Tatizo gani Afande ?"
"Yule mwanamke aliyewekwa mahabusu kwa ajiri ya usalama wake amefariki!!!"
"Nani ?" "Raiya"
"Unasemaa !"
"Ameuwawa Afande"
"Natuma askari sasa hivi"
"Sawa"
Yule askari aliwaambia taarifa ya kifo aliyoipokea. Ilikuwa ni taarifa ya kifo cha Raiya, iliwastua sana. Lilikuwa pigo la ghafla na la kushangaza sana. Mtu kufariki akiwa mikononi mwa askari siyo tatizo sana. Lakini mtu kuuwawa mikononi wa askari ilikuwa ni tatizo kubwa sana. Tena ndani ya Gereza lenye ulinzi mkali kama la Arusha. Yalikuwa maajabu!
Walifuatana Abdul na Daniel kuelekea Magereza. Daniel hakutaka kumuacha Abdul hata sekunde moja. Alijua lazima wauaji watataka kumuua. Kwa vyovyote walikuwa wanataka kupoteza ushahidi kwa kuuwa. Daniel aliamini kwa kumtumia Abdul ndipo atakapowatia mkononi kwa urahisi wauaji. Alimtumia kama chambo. Alijua kwa vyovyote atakuwa anawindwa auwawe.
Waliwasili magereza majira ya saa nne asubuhi. Walikuta hali ya gereza ikiwa shwari na vikundi vidogovidogo vya askari wakijadiliana. Walienda moja kwa moja kwa mkuu wa Gereza. Baada ya salamu walianza kuongea.
"Ilikuwaje mkuu?"
"Mnamo mida ya saa tatu asubuhi alikuja mtu. Alidai yeye ni ndugu na Raiya. Baada ya kumkagua askari walimruhusu aingie. Hakuwa na kitu chochote cha hatari. Baada ya kama dakika nne aliaga anaondoka, na marehemu alirudi selo. Lakini baadae askari walipoenda kwenye selo yake walimkuta ameuwawa kikatili sana!."
"Marehemu alipomuona huyo mtu alionesha dalili yoyote ya kumtambua?"
"Siwezi kujibia hilo ngoja tumwite askari aliyekuwa zamu" Mkuu wa Gereza alimpigia Simu huyo askari. Baada ya kumaliza wakaendelea na maongezi yao
"Kwanini mnahisi huyo mgeni ndiye anahusika Katika mauaji ?"
"Marehemu hakuongea na mtu mwengine yeyote baada ya yule mgeni kuondoka"
Baada ya maelezo hayo yule askari aliyepigiwa simu na mkuu wa Gereza alikuwa ameshafika. Yeye alisema hakuwa makini kuchunguza kama mgeni na marehemu walikuwa wanajuana ama lah. Yeye aliwakutanisha tu na kuondoka. Bila kutafiti chochote. Waliongazana na mkuu wa magereza pamoja na Daniel kwenda kuuangalia mwili wa marehemu Raiya. Ilikuwa ni picha mbaya sana ambayo haitafutika kichwani kwa Abdul hadi leo. Picha mbaya ilioje kumkuta binadamu unayemfahamu kachunwa ngozi mithili ya Ng'ombe! Abdul alikuwa anamchukia sana Raiya lakini siku ile alitoa machozi kwa ajili ya yake. Alimuonea huruma sana. Alijua kapitia maumivu makali sana akiwa anaipigania roho yake. Mwili usio na ngozi uliwekwa hapa. Na ngozi iliyokusanywa iliwekwa pale...! Hali ilikuwa ya kutisha sana. Hakuna aliyeongea kwa zile dakika tano walizokaa katika chumba. Abdul alimwangalia Daniel usoni. Alikuwa anatabasamu bila wasiwasi wowote. Walirudi ofisini kwa mkuu wa Gereza. Sasa Abdul aligundua tabia moja ya Daniel. Huwa anatabasamu kila mambo yanapokuwa magumu. Alimwona Daniel anatabasamu mbele ya maiti ya Raiya iliyouwawa kinyama.
"Nimemuona mkuu. Ni aina ya mauaji sawa na ya Mayasa. Sawa na ya mtoto wa waziri wa ujenzi aliyeuwawa kule Mwanza. Itakuwa ni kundi moja kama siyo muuaji mmoja. Lakini awe mtu kiwe kikundi nitahakikisha hafanyi mauaji mengine ya raia wema !" Alisema kwa uchungu mkubwa Daniel.
Waliondoka pale Magereza wakiacha mwili wa marehemu Raiya ukipakiwa kwenye gari kupelekwa hospitali. Abdul alikuwa mwenye majonzi sana. Watu wawili waliojitolea kumsaidia kwa hali na mali walikuwa wamefariki kwa tofauti ya masaa machache sana. Ni mkosi gani huu.
Njiani alimuona Daniel Mwaseba akitabasamu. Akajua kuna kitu kakiona. Tena bila shaka cha hatari!
"Tunafuatwa" Alimsikia akisema kwa sauti ndogo.
"Ama zetu, ama zao! Akamaliza huku akitabasamu.

NJOO TENA KESHO TUUSOME UHONDO HUU..
 
Back
Top Bottom