RIWAYA : Angamizo

RIWAYA : Angamizo

RIWAYA; ANGAMIZO
Imeandikwa na Halfani Sudy
Simu 0674 395733

Sehemu Ya Tatu

Nataka nikusaidie Abdul bila sharti lolote. Dhamira ya ndani ya moyo wangu nimeamua kukusaidia. Nimependa harakati zako za kuitafuta elimu. Unaonesha unapenda kusoma, na una akili sana."

"Nashukuru sana Mayasa. Wewe ni mwanamke mwenye moyo wa ajabu sana."
Walimaliza kuongea na Mayasa saa nne usiku. Walikodi gari iliyowarejesha Arusha mjini. Sasa Abdul alihamia himaya mpya. Himaya ya Mayasa, alimkabidhi kila kitu Mayasa kuhusu maisha yake, kasoro moyo tu. Alipunguza mawasiliano na Raiya na kuongeza mawasiliano na Mayasa.

***

Ilikuwa siku ya jumatano jioni ya wiki ya pili tangu waanze chuo. Abdul alikuwa na Mayasa wanajisomea darasani muda wa jioni.
Simu ya Abdul iliita.
Alikuwa Raiya anapiga.

" Wewe unajifanya kiburi sikuhizi eeh. Mimi nimekusomesha umefika Chuo unajifanya mjanja. Sasa kesho nakuja huko huko Arusha nione kinachokuzuzua. Ole wako nisikie una mwanamke" Bila salamu Raiya aliwaka kwenye simu. Abdul hakumjibu. Alikata simu na kuizima kabisa. Hamu ya kusoma ilimuisha. Mayasa alisikia kila kitu alichosema Raiya. Raiya alikuwa alimkaripia kama mtoto Abdul na kwa nguvu. Alimuonea sana huruma. Hamu ya kusoma ilimuisha. Alimuaga Mayasa na kurudi hosteli. Alifika kitandani na kulala chali. Alifikiria mustahabari wa maisha yake. Alijiona ni mtu mwenye mikosi. Aliulaumu umaskini wake. Aliulaumu umaskini wa wazazi wake. Machozi yalitoka yenyewe taratibu. Akauhisi mkono laini ukimfuta machozi. Alifumbua macho yake na kuangalia. Alikuwa Mayasa.

"Acha kulia Abdul. Nimejitoa kukusaidia kwa lolote kaka yangu. Naamini tutaushinda mtihani huu.Tutamshinda Raiya. Sitokubali ulie tena." Mayasa alimbembeleza sana Abdul. Mwishowe akamwelewa. Akanyamaza.

Ilipita wiki moja tangu Raiya ampe vitisho vyake Abdul. Hakutokea Arusha wala hakumpigia simu. Akajua labda amekata tamaa. Akawa anaishi maisha yake kama kawaida. Furaha ikarejea tena. Huku akimtegemea Mayasa kwa kila kitu. Naye hakuchoka. Alimsaidia Abdul.

Upande wa darasani alikuwa anafanya vizuri sana katika masomo. Alikuwa na uwelewa mkubwa sana. Mayasa hakuwa mzuri sana darasani. Alijitahidi kumsaidia kila alipopata nafasi. Alielewana sana na Mayasa. Walifatana muda wote. Walijisomea pamoja. Walikuwa mithili ya chanda na pete. Kila mwishoni mwa wiki walikuwa wanatoka nje ya jiji la Arusha kutembea na Mayasa.

Siku moja jumamosi Abdul na Mayasa iliwakuta Same. Sasa walikuwa marafiki walioshibana. Abdul alikuwa anafahamu sasa baadhi ya vitu vya Mayasa. Kumbe baba yake Mayasa alikuwa, Ally Hamisi. Makamu wa raisi wa Zanzibar. Baba yake alikuwa mtu mkubwa sana Serikalini lakini hakuna hata siku moja aliyemtamkia mdomoni Abdul. Alisikia tu kutoka kwa watu wa pembeni. Siku waliyoenda Same, walirudi chuoni saa kumi na mbili jioni kutoka. Same Ilikuwa mbali kidogo na Jiji la Arusha. Mayasa alimrudisha kwanza Abdul hosteli ili na yeye arudi kwao. Walienda Same na gari Mayasa. Walipofika karibu na chumba cha Abdul, nje walikutana na Justus. Kijana aliyekuwa wanakaa chumba kimoja pale hosteli.

"Daah afadhali umerudi Abdul, kuna mgeni wako ndani"

"Nani ?"

"Simfahamu, ila amefika zamani sana"

"Sawa kaka"

Waliingia ndani na Mayasa. Wakiwa hawana wasiwasi hata kidogo. Walipofungua mlango na kuingia ndani walimwona msichana amelala kitandani kwa Abdul. Wote walistuka sana! Walipomwangalia kwa makini, Abdul alimgundua msichana yule.
Alikuwa Raiya .

"Naitwa Raiya Mohamedi" Aliongea huku akimwangalia Mayasa usoni.

"Naitwa Mayasa Ally" Mayasa nae alijibu kwa kujiamini.

"Wewe ndiye unajifanya unajua kutembea na wanaume wa watu ?"

"Sema kilichokuleta "

"Kilichonileta ndio hiki ninachoongea "

"Usione vyaelea dada......"

"Sina muda wa kuongea na wewe"

"Abdul ?" Raiya aliita.
Hakuitika.

"Umenisaliti kwa sababu ya hiki kikaragosi ?" Abdul alikaa kimya anamwangalia tu.

"Kumbuka nilipokutoa Abdul, Kumbuka Siku ile pale Mwenge, ningekuacha ungekutana na hiki kikaragosi leo? " Raiya aliongea maneno yaliyomuingia kidogo Abdul.

Pamoja na madhaifu yake kadhaa lakini Raiya alikuwa na mchango mkubwa sana katika maisha ya Abdul hadi alipofikia sasa.

"Sasa chagua moja Abdul. Utakuwa na mimi au huyu?" Raiya aliongea kwa jazba.
Abdul alibaki njia panda.
Raiya na Mayasa wote walikuwa na mchango mkubwa katika maisha yake. Na wote walimwangalia yeye kusubiri jibu langu.

"Mayasa siyo mpenzi wangu" Alijua ametamka kwa sauti kumbe sauti haikutoka nje. Mdomo ulikuwa unatetemeka tu.

"Chagua Abdul"

"Achague nini, mimi Abdul siyo mpenzi wangu"

"Ni nani yako sasa ?"

"Rafiki yangu tu"

"Hahaha siku zote mapenzi yanaanzia kwenye urafiki, Ok marafiki. Basi mimi ni mke wa Abdul. Nasema naomba muvuunje kabisa huo urafiki wenu. Siutaki, siutaki, siutaki hata kuusikia. Mkewe nimesema!"

"Raiya wewe ni mke wa Abdul ?"

"Hilo jibu uliza swali "

"Una hakika Raiya ?"

"Ndio"

"Na Salehe je, unamwitaje Raiya ?" Swali hilo allouliza Mayasa lili mstua sana Raiya. Hali sasa ilibadilika mle ndani.

"Mimi ni Mayasa Ally Hamisi, unanikumbuka ?" Mumeo Salehe ni kaka yangu. Mtoto wa mama mdogo Fatma. Au nimpigie Salehe nimuulize kama kakuacha ?" Mayasa aliongea huku akitafuta namba za Salehe katika simu yake. Raiya sasa alikuwa amechoka hoi. Hajui lipi aseme, lipi aache. Alikosa kauli kabisa.
Ghafla alitoka nje ya hostel kwa ghadhabu mithili ya roketi, bila ya kuaga. Abdul aligundua kitu kimoja kuhusu Mayasa. Mayasa alikuwa msichana msiri sana. Alimficha cheo cha baba yake hadi sasa. Pia kumbe alikuwa anamficha kama Raiya ni wifi yake, hakumwambia kabla. Alianza kumwangalia Mayasa kwa jicho la kumuogopa sasa.

" Usijari Abdul. Raiya ni wifi yangu lakini yeye hakuwa ananijua. Tulionana na Raiya siku moja tu. Tena siku ya harusi yake na kaka Salehe. Hata wewe ulivyonisimulia historia ya maisha yako. Ulipotaja jina la Raiya sikujua kama Raiya wifi yangu, sikufikiria kabisa. Leo nilivyomwona hapa ndio nimemkumbuka ". Mayasa alinijibu kitu ambacho nilikuwa nakifikiria.

"Sawa Mayasa nimekuelewa"

Walitoka nje ili kumwangalia Raiya ameenda wapi? Hawakumuona.

Raiya kaenda wapi? Nini hatma ya uhusiano wake na Abdul? Swali la msingi ni kwanini Angamizo? Tuwe wote katika sehemu ijayo kujibu maswali hayo..Nina ombi moja leo, ninaomba like yako kama umeisoma..
 
RIWAYA; ANGAMIZO
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SIMU 0674 395733

Sehemu Ya Nne

Walitoka nje ili kumwangalia Raiya ameenda wapi? Hawakumuona.
Hawakujua ameelekea wapi? Aliyeyuka mithili ya upepo.

Baadae Mayasa aliaga na kuondoka kwao huku Abdul akibaki na wingi wa mawazo. Abdul alisinzia akiwa na mawazo mengi. Lakini kutokana na uchovu wa kutoka Same na ukijumlisha mawazo aliyomletea Raiya ndio yalimchosha kabisa, alilala fofofo.

Saa kumi usiku simu yake ilitoa mlio wa sauti alioutega Kwa ajili ya mwitikio wa ujumbe mfupi. Ikimaanisha kuna meseji mpya iliingia.

'Umeuchokoza moto. Niliacha zamani ukatili. Wewe unajitahidi kunirudisha huko. Nilikuwa katili sana zamani. Kama hupendi nirudie tabia zangu za zamani nakuomba achana na kikaragosi. Nitakuuwa, nitamuuwa pia. Nakupa siku tatu za kufikiria juu ya suala hili. Mimi bado nipo Arusha.
Namaanisha!" Abdul alikaa kitandani na kuurudia kuusoma ujumbe ule mara tano. Jasho lilikuwa linamtiririka kama maji. Akamtumia ule ujumbe na Mayasa.
Hakuujibu.
Na hajaujibu mpaka leo!

Asubuhi na mapema watu wanne walienda katika chumba cha Abdul. Walikuwa wamefuatana na kiongozi wa hosteli. Mshauri wa wanafunzi na Raisi wa Chuo. Walimuita pembeni na kumwambia.

"Sisi ni askari wa kituo kikuu cha Polisi Arusha. Unahitajika kituo cha Polisi kwa mahojiano kidogo"

"Nimefanya nini jamani ?"

"Utajua hukohuko kituoni" Askari mmoja alimnyanyua kwa nyuma suruali yake na kupelekwa kituoni. Alikuwa anatembelea vidole sasa. Wanafunzi wenzie walimuonea huruma pale chuoni.
Hakujua amefanya nini? Hawakujua amefanya nini?

Baada ya kufika kituoni ndipo alipoambiwa kosa lake. Eti alituhumiwa kwa kumuua Mayasa! Na ujumbe wake wa vitisho kutoka kwanye simu yake yake ulikutwa katika simu yake. Na ulitumika kama ushahidi. Alihemewa sana.
Alilia sana.
Aliuona mwisho wa ndoto zake umetimia. Akajua ataozea jela. Aliwekwa selo akisubiri ushahidi ukamilike. Akiwa ndani ya selo Abdul aliwaza mambo mengi sana. Moja kwa moja alijua kama kweli Mayasa ameuwawa basi Raiya ndiye mhusika mkuu wa kifo cha Mayasa. Lakini ujumbe ule aliomtumia Mayasa ulikuwa unamweka mashakani. Alikuwa analia mithili ya kichanga. Afande aliyekuwa anaitwa John ndiye alipewa jukumu la kupeleleza kesi ya kifo cha mtoto wa Makamu wa Raisi wa Zanzibar. Afande John alianza kumhoji Abdul kwanza. Mtuhumiwa wa kwanza wa mauaji yale.

" Unaitwa nani? "

"Abdul "

"Majina matatu !!"

"Abdul Ramadhani Washiro"

"Kabila? "

"Msukuma "

"Nambie uhusiano wako na Mayasa ?"

"Alikuwa mwanafunzi mwenzangu"

"Hamkuwa na uhusiano wa kimapenzi ?"

"Hapana, alikuwa ni rafiki yangu wa kawaida "

"Sasa kwanini uliamua kumuua rafiki yako?"

"Sijamuua mimi afande "

"Soma huu ujumbe "Askari ule ujumbe aliyomtumia Mayasa baada ya kutumiwa na Raiya. Ujumbe wa vitisho!

Ulisomeka' Umeuchokoza moto. Niliacha zamani ukatili. Wewe unajitahidi kunirudisha huko. Nilikuwa katili sana zamani. Kama hupendi nirudie tabia zangu za zamani nakuomba achana na kikaragosi. Nitakuuwa, nitamuuwa pia. Nakupa siku tatu za kufikiria juu ya suala hili. Mimi bado nipo Arusha.
Namaanisha'

"Alinitumia Raiya ujumbe huu, mimi nilimfowadia tu Mayasa."

"Raiya ndio nani ?"

Alimsimulia afande John kila kitu kuhusu ugomvi wao na Raiya. Alirudishwa selo na afande John alikwenda kwa kina Raiya kumhoji. Hakuwa anapajua , na wala Abdul alikuwa hapajui. Ila alisema atapajua tu. Afande john alifanikiwa kufika nyumbani kwa dada yake Raiya. Baada ya kumuonesha kitambulisho cha Polisi, Raiya alishangaa sana.

"Jamani, wewe ni askari wa tatu kuja kunihoji leo"

"Walikuja maaskari wengine hapa ?"

" Ndio na mmoja katoka nusu saa iliyopita"

"Walikuwa na vitambulisho ?"

"Ndio walinionesha"

"Unayakumbuka majina yao?"

"Nayakumbuka sana kwa kuwa majina yao wote yanafanana"

"Wanaitwaje?"

"Wote wanaitwa John"

Afande John alisikia kizunguzungu na mivumo isiyoeleweka masikioni mwake Ilikuwa taarifa ya kushangaza sana.

"Itabidi nikakuhoji kituoni " Afande John aliona pale siyo mahali salama pa kufanyia mahojiano. Walifuatana na Raiya kuelekea kituoni. Hapakuwa na umbali mkubwa sana toka nyumba aliyokuwa anakaa Raiya hadi kituo kikuu cha Polisi Arusha. Raiya alikuwa anakaa katika nyumba ya dada yake aliyokuja kukaa kwa muda mahsusi ili kutekeleza aliyoyakusudia, kutenganisha penzi la Abdul na Mayasa kama akivyoamini yeye kuwa walikuwa wapenzi.

"Raiya hebu nambie vizuri kuhusu hao askari waliokuja kukuhoji kwako."

" Ndiyo kama nilivyokwambia Afande. Walikuja askari wawili kunihoji. Mmoja alikuja asubuhi na mwingine alikuja muda mfupi kabla hujaja wewe. Na wote walitaka maelezo yangu kuhusu kifo cha Mayasa na uhusiano wangu na Mayasa na Abdul"

"Wewe uliwajibu nini?"

"Yule wa kwanza sikumjibu kitu. Maana aliniacha kwenye mstuko mkubwa sana baada ya kunambia Mayasa amefariki. Sikuamini kama Mayasa amefariki..nilikuwa nalia tu kila alichokuwa ananiuliza . Askari yule alifanya kazi ya kunibembeleza tu, akaondoka"

"Askari wa pili je ?"

"Yeye alinikuta nimetulia sasa. Nilimueleza kila kitu kuhusu ugomvi wetu mimi, Mayasa na Abdul."

"Alisemaje baada ya maelezo yako?"

"Aliandika kwenye kitabu chake na kuondoka" Afande John alishusha pumzi ndefu. Akajua ngoma sasa imekuwa nzito. Akamfungia Raiya selo na kutoka nje kwenda kutafakari. Alikaa chini ya mwembe mrefu uliokuwepo pale nje ya kituo. Akiwaza na kuwazua. Simu yake ikawa inaita. Namba ilikuwa ngeni. Zilitokea namba tu. Akaipokea na kuiweka sikioni.

"Hallo"

"Hallo nani mwenzangu ?"

"Huna haja ya kulijua jina langu. Cha muhimu acha kuifatilia hiyo kesi utauwawa bure. Au unahamu ya kumuweka eda mkeo?"

Mambo yameanza sasa! Nani kamuua Mayasa? Kwa lengo gani? Nini hatma ya Abdul na Raiya? Na huyu ampigiaye afande John ni nani? Tusome wote hadi mwisho katika Angamizo na Halfani Sudy.
 
Back
Top Bottom