Ripoti ya TAKUKURU Mkoa wa Ilala: Mkandarasi akatwa zaidi ya milioni 327 kwa kuchelewa kukamilisha mradi wa vyoo vya umma Dar

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987
Sosthenes Kibwengo .jpg



View: https://www.youtube.com/watch?v=GsdrbCwShyU

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) – Mkoa wa Ilala, Sosthenes Kibwengo anatarajiwa kuzungumza na Wanahabari kwa ajili ya kutoa taarifa ya miezi mitatu, leo Januari 31, 2024.

Mkutano huo na Wanahabari unatararajiwa kufanyika kwenye Jengo la PCCB House, Upanga Jijini Dar es Salaam.

UPDATES

Anazungumza Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) – Mkoa wa Ilala, Sosthenes Kibwengo:

Ninawashirikisha taarifa ya utendaji wetu kwa kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2023 ili mtusaidie kuelimisha umma kwani vita dhidi ya rushwa ni jukumu la kila mmoja wetu.

UZUIAJI RUSHWA
Kwanza siku za nyuma tulitoa taarifa kuhusu ukaguzi tuliofanya wa mradi wa ujenzi wa vyoo vya umma Jijini Dar es salaam wenye thamani ya shilingi bilioni 3.27 unaosimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) na kubaini kasoro kadhaa ikiwemo kuchelewa kukamilika kwa mradi huo kinyume na mkataba.

Baada ya kufanya kikao kazi na DAWASA na kukubaliana maazimio ya utekelezaji, kasoro zilizothibitika zimeendelea kurekebishwa na Mkandarasi amekatwa kiasi cha shilingi 327,476,502.60 kama faini ya kuchelewesha kazi. Natoa wito kwa wakandarasi Mkoani kwetu kukamilisha miradi wanayopewa ndani ya wakati ili kupunguza gharama na kuwezesha nia njema ya Serikali ya ustawi wa Wananchi kutimia.

Pia tumefuatilia kwa lengo la kubaini iwapo thamani halisi ya fedha inafikiwa, miradi 9 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni kumi na tisa, milioni mia thelathini na sita, laki tisa tisini na tisa mia tatu themanini (19,136,999,380) katika sekta za Afya, Elimu na Ujenzi (barabara).

Tofauti na asilimia 78 ya miradi iliyokaguliwa na kukutwa na mapungufu katika kipindi kama hiki mwaka 2022 tumebaini miradi mitatu, sawa na asilimia 33 ya iliyokaguliwa robo hii, yenye thamani ya shilingi 1,350,000,000/= kuwa na mapungufu yafuatayo:

Ukiukwaji wa sheria na kanuni za manunuzi ya umma ikiwemo manunuzi ya vifaa vya ujenzi kwa mzabuni aliyepatikana bila ushindanishi.

• Kutofanyika kwa vipimo vya ubora wa vifaa vya ujenzi
• Usimamizi duni unaosababisha matumizi ya vifaa visivyokidhi ubora, na
• Ucheleweshaji wa miradi Tunaendelea kushirikiana na Taasisi zinazosimamia miradi hiyo ili kasoro bainishwa zirekebishwe.

Pili, tumeendelea kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam na kuwezesha shilingi 1,830,546,332/= zilizokusanywa kwa mashine za kieletroniki za POS kuwekwa katika akaunti ya Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam baada ya kutowasilishwa kwa muda mrefu.

Tatu, tumefanya chambuzi mbili za mifumo ya Usimamizi wa Ukusanyaji na Matumizi ya ada za huduma za usafi na ulinzi katika soko la Karume na Tathmini ya Utoaji huduma katika sekta ya ardhi. Katika uchambuzi wa soko la Karume tulibaini makusanyo pungufu kwa asilimia 47 ya makisio, kiasi cha shilingi 245,138,000/=, yalipotea kwa kipindi cha Januari hadi Septemba, 2023 mwanya ambao pamoja na mambo mengine, huchangiwa na kutokuwepo kwa taarifa za uhakika za idadi ya wafanyabiashara.

Katika uchambuzi wa huduma katika sekta ya ardhi tulibaini, pamoja na mambo mengine, kutozingatiwa kwa muda wa utoaji huduma kama maombi ya ardhi; vibali vya ujenzi; upimaji wa ramani; kuingiza viwanja vilivyopimwa kwenye mfumo; na utatuzi wa migogoro ya ardhi kinyume na muda uliowekwa kwenye miongozo iliyopo. Tutashirikiana na mamlaka husika kupitia vikao kazi kuweka maazimio ya namna ya kuziba mianya iliyobainishwa hapo juu.

Nne, kero zisipotatuliwa huzaa vitendo vya rushwa, hivyo kupitia Programu ya TAKUKURU Rafiki tulifanya vikao katika Kata tisa (9) za Kitunda, Mzinga, Segerea, Tabata, Kipunguni, Liwiti, Msongola, Zingiziwa na Bonyokwa ambapo wadau/wananchi waliibua kero 50 na kushauri namna ya kuzitatua ili kukuza utawala bora; kuboresha utoaji wa huduma; na kuzuia rushwa. Pamoja na vikao kukubaliana ufumbuzi wa baadhi ya kero, tunaendelea kushirikiana na watoa huduma husika ili kuhakikisha kero zinazowahusu katika sekta za maji, barabara, ilinzi, afya, ujenzi, umeme, masoko, mazingira na utawala zinapatiwa ufumbuzi na wananchi kupatiwa mrejesho.

Mfano wa kero zilizotatuliwa ni Kata ya Tabata ambapo takataka zilikuwa zinaachwa muda mrefu bila kuzolewa na baada ya kuwekwa Mkandarasi mpya sasa zinazolewa kwa wakati; na Kata ya Bonyokwa ambapo vifusi vilivyokuwa vimerundikwa kwenye Barabara ya Bonyokwa-Segerea vimesambazwa na Mkandarasi anaendelea na kazi. Ni vyema wote tushiriki programu hii katika Kata zetu ili tuwe sehemu ya ufumbuzi wa changamoto zetu za kijamii.

UELIMISHAJI UMMA
Vijana ni kundi kubwa zaidi katika jamii yetu. Ni chachu ya mabadiliko katika jamii na hivyo tumeweka nguvu kubwa katika kulifikia kundi hili ili kulibadili kifikra watambue wajibu wa kushiriki kivitendo kuzuia rushwa na kukuza Utawala Bora.

Kwanza, tulishirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuendesha mafunzo maalumu kwa walimu walezi 239 wa klabu za wapinga rushwa wa shule za Msingi na Sekondari za Jiji la Dar es Salaam ambao ni msingi wa kuimarisha klabu hizo.

Pili, tuliendesha shindano la ujumbe mfupi (video clip) kwa wanachama wa klabu za wapinga rushwa wa shule za sekondari Ilala kuhusu nafasi ya vijana kuzuia rushwa. Tumepokea jumbe fupi 96 na tayari washindi wamepatikana.

Tunawapongeza wote walioshiriki kwani tumepokea jumbe nzuri sana na tutazitumia kuwaelimisha vijana na jamii kwa ujumla.

Tatu, tumetembelea na kuimarisha klabu za wapinga rushwa mara 33 ambapo mkazo uliwekwa katika kuhamasisha wanachuo wapya kujiunga na klabu za wapinga rushwa. Pia, tumefanya mikutano 18 ya hadhara, semina 22, na vipindi 5 vya redio/televisheni.

Mbali na matumizi ya mbinu mpya za uelimishaji, kiwango cha uelimishaji kimeongezeka kwa zaidi ya asilimia 300 ukilinganisha na kile cha robo kama hii mwaka 2022 ambapo semina 17 zilifanyika; klabu 2 ziliimarishwa; na mikutano 2 ya hadhara ilifanyika.

UCHUNGUZI NA MASHTAKA
Tumepokea jumla ya malalamiko 88, yakiwa 20 pungufu ya tuliyopokea robo iliyopita na asilimia 5 pungufu ya yaliyopokelewa kwa kipindi kama hiki mwaka 2022. Kati ya hayo 54 yalihusu rushwa na 34, ambayo ni asilimia 39 ya taarifa zote, hayakuhusu rushwa ambapo wahusika walishauriwa au kupelekwa idara stahiki na hivyo taarifa hizo zikafungwa.

Taarifa zilizohusu rushwa zilishughulikiwa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa SURA ya 329 marejeo ya 2022 na zilihusu sekta zifuatazo: Elimu (12); Ardhi (11); Serikali za Mitaa (8); Afya (5); Binafsi (4); Fedha/benki (3); na zinginezo (11). Malalamiko mengi yasiyohusu rushwa yalihusu sekta Binafsi; Ardhi; na Benki.

Majalada 8 ya uchunguzi yalikamilika na kuwasilishwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, ukilinganisha na majalada 2 yaliyokamilika katika kipindi kama hicho mwaka 2022, na mashauri mapya 8, yakiwa na washtakiwa 24 na kuhusisha shilingi bilioni 8.7, yalifunguliwa mahakamani, ambapo mashauri 32 yanaendelea baada ya mashauri 3 yenye jumla ya washtakiwa watano kuhitimishwa kwa Jamhuri kushinda katika mashauri yote.

MIKAKATI YA ROBO YA JANUARI HADI MACHI 2024
TAKUKURU (M) Ilala itaendelea kuweka juhudi kwa vijana, ambao ni chachu ya mabadiliko, kwa kufanya bonanza la michezo ya soka na pete kwa wanafunzi na wanachama wa klabu za wapinga rushwa wa shule za Sekondari za Jiji la Dar es Salaam lililoahirishwa robo iliyopita.

Aidha, tutaendelea kwa kushirikisha wadau kuzuia rushwa kwa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo; kutekeleza programu ya TAKUKURU Rafiki; na kuelimisha jamii kwa kutumia mbinu tofauti kupitia mikusanyiko mbalimbali ya kijamii.

MWISHO, tunawakumbusha wananchi kuwa rushwa ina madhara makubwa na hivyo kuna thamani kubwa kushiriki kuizuia. RUSHWA HAILIPI.
 
Back
Top Bottom