Penzi la zamani

Mohamed Ismail

JF-Expert Member
Mar 16, 2014
214
229
Dunia inaenda kasi na maisha yanaenda kasi. Zamani upendo ulikuwa una thamani zaidi hata gharama iliyotumika ilikuwa ni ya thamani zaidi. Mahusiano yalighubikwa na maneno mazuri yenye kuvutia yakiwa yamejazwa na vionjo vyenye kusisimua nafsi.
Acha masikhara yale ndio yalikuwa mapenzi.

Hakukua na simu za mikononi bali posta ndio ilitumika kwa mawasiliano ya barua kwa watu ambao walikuwa mbali. Ilikuwa ukikutana na binti mnabadilishana anuani zenu hata shule tu ilitosha mtu kukupata. Somo la kiswahili katika uandishi wa barua kila mwanafunzi alikuwa makini nalo maana lilimgusa. Mapenzi yalihitaji usanii wa kupakwa rangi maneno na huku mwandiko unachongwa vizuri kwa ajili ya yule umlengaye.
Acha masikhara yale ndio yalikuwa mapenzi.

Mlimwengu mimi mapenzi niliyajua umdogo kutokana na kujua kuyachezea maneno na kisha kuyawasilisha kwenye karatasi. Niliyasimulia kabla sijayaishi. Walo na mwandiko wa kuku walinihonga visenti fundi niweze kuwaandikia. Maneno yale yalikuwa nta kila aliyepata ujumbe uliweza kumnasa. Nilipata shukrani za peke kwa wote walionitumia. Acha masikhara yale ndio yalikuwa mapenzi.

Tuliosoma boarding hakuna siku iliyokuwa ya thamani kama upokeayo barua kutoka kwa mpenzio. Ukiwa ndani ya uzio wa shule umeishashiba kande na ugali wa kutosha na mchuzi wa haragwe umepambwa na wadudu wanaoelea. Haikuwa jela bali sehemu ya kusaka maarifa na kutimiza ndoto zetu. Inapigwa kengele jioni halafu kiranja wa zamu anasoma barua zilizofika siku hiyo. Jina lako likiitwa ule mwendo unaoenda kuchukua barua thamani yake ni zaidi ya tuzo za BET. Acha masikhara yale ndio yalikuwa mapenzi.

Ukishapokea ile barua unaichukua huku wenzio wanakuzongazonga kutaka kujua nini kilichopo umbeya haujaanza leo. Unaiweka mfukoni kwanza unatuliza wenge. Kama ulikuwa hujala unaenda unachukua ugali wako unashiba kabisa. Mapenzi ni hisia tu ile barua ilikuwa inapewa heshima sana. Baada ya kumaliza kila kitu sasa ni muda wa kuifungua barua. Bahasha yenyewe inanukia utuli na kisha ndani ya bahasha kuna bahasha iliyopambwa na makopakopa kama yote. Acha masikhara yale ndio yalikuwa mapenzi.

Picha inaanza bahasha yenyewe ya ndani imepambwa wakati mwingine kuna na kadi ambayo ina muziki ndan yake. Unashindwa uanze na lipi huku kadi na huku barua acheni tu hawa mabinti walicheza na mioyo yetu. Unaanza kusoma barua isiyoisha utamu unairudia hata mara tatu utadhani unaenda kuijibia mtihani. Humo ndani kachora kopa lililopambwa na rangi nyekundu na kisha kwa umakini anachora kijimkuki kinaenda kulichoma kopa. Wahenga wanaita kunchoma kumoyo. Acha masikhara yale ndio yalikuwa mapenzi.

Barua ile ilisomwa kwa utulivu wa hali ya juu na milango yote ya fahamu ilijikuta yote iko pale. Dunia unaiona ya kwako. Walikuwa wana maneno matamu yamechanganywa na swaenglish. Unakuta na sentensi inasema without you i cant breath. Unajiuliza huyu Oksijeni anaijua kazi yake au ananipanga. Acha masikhara bana yale ndio yalikuwa mapenzi.

Enzi hizo walikuwa wana dedication nzuri za kukuhamasisha kusoma na hata kudevelop carrier zetu. Unakuta anakuita my Doctor au my Engineer ilikuwa inaleta nguvu ya kusoma unajikuta umefanikisha ndoto yake kumbe ndio ya kwako hivyo. Mwishoni unawekewa na dedication songs ambazo hizo ungezitafuta baadae. Acha masikhara yale ndio yalikuwa mapenzi.

Ngoja Mlimwengu mimi niishie hapa maana najua nimewatonesha vidonda wengine hadi leo zile barua bado mmezitunza. Maisha hayako fair kuna wengine nao ni wa zamani lakini hata haya ninayoyasimulia na kwao ni simulizi tu . Acha masihara yale ndio yalikuwa mapenzi.

#mlimwengumimi
#hubalazamani
Imesanifiwa na
Mohamed Ismail Rwabukoba
 
Umenena vema, enzi hizo barua unaiandikia kichwa cha habari kabisa "KUTOA NI MOYO SI UTAJIRI". Leo hii barua ni m-pesa yenye kichwa cha habari "HCA24673 IMETHIBITISHWA....
 
Umenena vema, enzi hizo barua unaiandikia kichwa cha habari kabisa "KUTOA NI MOYO SI UTAJIRI". Leo hii barua ni m-pesa yenye kichwa cha habari "HCA24673 IMETHIBITISHWA....
😂😂😂😂😂😂
 
Dunia inaenda kasi na maisha yanaenda kasi. Zamani upendo ulikuwa una thamani zaidi hata gharama iliyotumika ilikuwa ni ya thamani zaidi. Mahusiano yalighubikwa na maneno mazuri yenye kuvutia yakiwa yamejazwa na vionjo vyenye kusisimua nafsi.
Acha masikhara yale ndio yalikuwa mapenzi.
Daaaah, mkuu umenitonesha kidonda aiseeeee. Nimemkumbuka binti Magreth alivyoutesa moyo wangu enzi hizo. tulikuwa tunasoma shule moja lakini alikuwa anaenda mjini kupost barua alafu ije isomwe paredi.
 
Niliokotaga barua ya jamaa anamtongoza demu.Yule jamaa alikuwa mwamba sana basi ile barua nilikuwa naitumia kuwatongozea mademu mi nilikuwa naikopi tu. Hamna demu nilimtumia ile barua akanikataa.Basi wana wakawa wanakuja niwaandikie barua kali mi nkawa naingeza majanja kidogo. Kila likizo wana walikuwa wananiletea zawadi kibao kama shukrani.Hadi nikawa na comfidence wakati nlikuwa domo zege kinoma.
 
Dunia inaenda kasi na maisha yanaenda kasi. Zamani upendo ulikuwa una thamani zaidi hata gharama iliyotumika ilikuwa ni ya thamani zaidi. Mahusiano yalighubikwa na maneno mazuri yenye kuvutia yakiwa yamejazwa na vionjo vyenye kusisimua nafsi.
Acha masikhara yale ndio yalikuwa mapenzi.
Nakumbuka wakati nasoma barua zilikuwa zinagawiwa wakati wa luch time. Siku isiyo na jina nilipata barua toka kwa rafiki yangu wa kike, kwa papara zangu nikaifungua palepale mezani, podailiyokuwa ndani ya barua ikaangukia ktk mlo wangu, nikashinda njaa siku hiyo!
 
Nikisikiaga story za barua za mapenzi moyo unapata ganzi, niliwahi kuchezea stiki zisizo na idadi kisa barua, kile kichapo sijawahi kukisahau...boya kabisa huyu bro wangu sijui alinichapia nini 😏😏😏😏
 
Umenena vema, enzi hizo barua unaiandikia kichwa cha habari kabisa "KUTOA NI MOYO SI UTAJIRI". Leo hii barua ni m-pesa yenye kichwa cha habari "HCA24673 IMETHIBITISHWA....
Enzi hizo barua unaandika kichwa cha habari kabisa, "TENDO LA NDOA HADI TUKIFUNGA PINGU ZA MAISHA" , leo barua yenye kichwa cha habari "MPE BODA BODA SIMU NIMUELEKEZE AKULETE SEHEMU GANI."
 
Enzi hizo barua unaandika kichwa cha habari kabisa, "TENDO LA NDOA HADI TUKIFUNGA PINGU ZA MAISHA" , leo barua yenye kichwa cha habari "MPE BODA BODA SIMU NIMUELEKEZE AKULETE SEHEMU GANI."
Da, mapenzi yanapitia vita nyingi, lakini daima yanashinda...
 
Kuna jamaa wao walikua wanajiandikia barua wakati wa likizo; shule ikikaribia kufunguliwa wanaziposti then inawaijia shule...wanapata furahaa pale wanasomwa parede kuchukua barua.
Yote haya kisa domo zege.
 
Watu wa hivyo walikuwa wengi sana
 
Similar Discussions

Back
Top Bottom