SEHEMU YA 164
“Unamaanisha unachokisema?” aliuliza Nikola, Buffet akayatoa macho yake upajani mwa Nikola na kumwangalia usoni.
“Ndiyo! Ila naomba unipe nafasi moja tu, kisha baada ya hapo, tutaelekea Munich kuanza maisha yetu,” alisema Buffet.
“Nafasi gani?”
“Nataka nirudi hospitalini nikamuage Tatiana, japo kwa kumbusu tu,” alisema Buffet.
“Nikupe dakika ngapi mpaka kurudi?” aliuliza Nikola.
“Saa moja.”
“Sawa. Unaweza kwenda, ukipitiliza, tusijuane,” alisema Nikola.
“Hakuna tatizo.”
Hilo ndilo aliloliomba na kuruhusiwa, alichokifanya ni kuondoka hotelini hapo na kurudi hospitalini. Japokuwa alikuwa ameumia sana lakini hakuwa na la kufanya, ili kuwa na msichana Nikola ilitakiwa amuache Tatiana.
Alijua fika kwamba Tatiana alikuwa msichana mrembo hasa zaidi ya Nikola lakini hakujua kwa nini alimpenda sana Nikola, hakuwa na jinsi, kila kitu alichokuwa akikfanya mahali hapo ni kumfurahisha Nikola na mwisho wa siku kuwa naye tu.
Hakuangalia dunia ingesema nini, hakuangalia watu wangemuonaje, kitu pekee alichokuwa akikihitaji mahali hapo ni kuwa na Nikola tu, hivyo alitakiwa kufanya kile alichokuwa akikihitaji msichana huyo wa Kijerumani.
Hospitalini kulikuwa na idadi kubwa ya watu, wote hao walifika hospitalini hapo kwa ajili ya kumuona mwanamuziki huyo. Kulikuwa na usumbufu mkubwa kwani kila mtu aliyeambiwa aondoke, hakuondoka, alitaka kumuona Tatiana tu.
Kama ni fujo, zilikwishatokea mahali hapo, watu waligoma kabisa, ila kwa kuwa ilikuwa ni hospitalini, polisi hawakufanya kitu zaidi ya kukubaliana na watu hao tu, kusimama nje ya hospitali hiyo, ila kuingia ndani, hakuna aliyeruhisiwa.
Mara baada ya kufika hapo, Buffet akaanza kuufuata mlango, polisi wote walimfahamu, hawakumzuia, wakampa ruhusa ya kuingia ndani ya jengo hilo. Wakati akipiga hatua kuelekea katika chumba alicholazwa Tatiana, machozi yalikuwa yakimbubujika tu, hakuamini kama hiyo ndiyo ingekuwa siku ya mwisho kumuona msichana huyo.