Penzi bila maumivu

Penzi bila maumivu

SEHEMU YA 170

Siku hiyo walizungumza mengi na kisha kulala. Siku iliyofuata, wakafuatwa na gari kutoka ubalozini ambapo wakachukuliwa na kupelekwa katika hospitali hiyo ambapo baada ya kufika, moja kwa moja wakapelekwa katika chumba alicholazwa Tatiana.

Japokuwa kulikuwa na watu wengi waliotaka kumuona msichana huyo lakini wao waliruhiswa kutokana na kibali maalumu walichokuwa nacho. Walipofika chumbani humo, macho yao yakatua kwa wazazi wa Tatiana na balozi aliyekuwa na familia yake.

Wakasalimiana. Peter akaanza kupiga hatua kukifuata kitanda alicholazwa Tatiana. Alipofika, akaanza kumwangalia msichana huyo, hapohapo kumbukumbu za maisha yake ya nyuma aliyopitia na msichana huyo yakaanza kujirudia kama mkanda wa filamu, ghafla machozi yakaanza kujikusanya mashavuni mwake.
“Tatiana....amka,” alisema Peter huku akimwangalia. Watu wote walikuwa kimya.
“Peter,” aliita mzee Sangiwa.
“Ndiyo!”

“Hii ni laana Peter, yote yametokea baada ya kukuacha wewe,” alisema mzee Sangiwa.
“Hakuna, nahisi Mungu anataka kuzungumza nami kuhusu yeye. Hebu subiri,” alisema Peter.

Akayarudisha macho yake kwa Tatiana, akamshika mkono na kuyafumba macho yake. Wote wakabaki kimya, walimwangalia Peter, hawakujua alifanya nini, ila alibaki kimya kabisa. Ghafla, machozi yakaanza kububujika mashavuni mwake, moyo wake ukaumizwa mno.

Akamwachia mkono Tatiana na kisha kuelekea pembeni, aliisikia sauti ikimwambia kitu, ilimhuzunisha sana, alibaki akilia peke yake kiasi kwamba watu wengine wakaanza kuogopa.
“Mchungaji, tuambie kuna nini,” alisema mzee Sangiwa.

“Tatiana atapona,” alisema Peter.
“Asante Mungu!”
“Ila...”
“Kuna kuna nini?”
“Hatoweza kuona tena,” alisema Peter huku akiyafuta machozi yake, mama Tatiana, bi Frida akaanza kulia kwa sauti kubwa, kile alichoambiwa kwamba binti yake asingeweza kuona tena, kiliuchoma moyo wake.
 
SEHEMU YA -171

Ilikuwa ni taarifa mbaya lakini walitakiwa kukubaliana nayo, mtu ambaye walimuamini sana, Peter aliwaambia kwamba msichana Tatiana hatoweza kuona tena katika maisha yake yote, ila pale kitandani, angepona kama kawaida.
Machozi hayakukauka machoni mwa bi Frida, kila alipokuwa akiyakumbuka maneno ya Peter, yaliuumiza mno moyo wake, akawa hana la kufanya. Kila mmoja ndani ya chumba kile alibaki akimwangalia Tatiana aliyekuwa akiteseka kitandani, mioyo yao iliumia sana lakini hawakuwa na jinsi.

Baada ya kuwa kipofu tangu alipozaliwa, akafanikiwa kupata umaarufu, fedha lakini mwisho wa siku, ajali aliyoipata ilibadilisha maisha yake yote. Kila walipokuwa wakifikiria hilo, mioyo yao ilizidi kuhuzunika.
“Tatiana....” alisema Peter, kila mmoja akatega sikio kusikia alitaka kuzungumza nini.
“Amefanyaje?”

“Hii si laana yangu,”alisema Peter.
“Kama si laana ni nini?” aliuliza mzee Sangiwa.
Peter akabaki kimya, akatoka kule pembeni alipokuwa amesimama na kumsogelea Tatiana kitandani pale, tayari machozi yaliyokuwa yakimtoka yalilowanisha shati lake, alipofika karibu na kitanda cha Tatiana, akasimama na kumwangalia msichana huyo usoni.
“Mungu anataka tujifunze kuhusu Tatiana,” alisema Petr huku akimwangalia msichana huyo.
“Tujifunze nini?”

“Tatiana alikuwa mnyenyekevu, Mungu alimpa sauti nzuri, alikuwa na lengo la kuisikia sauti ya msichana huyu ikimuimbia kila siku. Alipopata umaarufu, akajisahau, akajitoa katika suala la kumtumia Mungu na kuanza kumtumikia shetani kwa nyimbo zile za kidunia.
“Mungu amefanya haya ili tujifunze kwamba unapopata nafasi, Mungu anapoacha neema yake juu yako, kamwe usiichezee. Tatiana alipewa nafasi, akaichezea na ndiyo maana Mungu amemrudisha kule alipokuwa,” alisema Peter huku machozi yaliendelea kumbubujika.

Vilio vikazidi kusikika ndani ya chumba kile, maneno aliyoongea Peter yalimuumiza kila mmoja, hawakuamini kama kila kitu kilichokuwa kimetokea kilikuwa ni mipango ya Mungu kumrudisha kule alipokuwa kutokana na kuiacha njia yake na kwenda njia nyingine.
 
SEHEMU YA 172

Hali yake iliendelea kuwa mbaya kitandani pale, mpenzi wake, Buffet alikuwa amemtoroka na hakukuwa na mtu yeyote aliyejua mahali alipokuwa. Mateso yote hayo aliyapitia peke yake kitandani.
Siku ziliendelea kukatika, Peter na mkewe wakarudi nchini Tanzania ambapo mara kwa mara walifanya maombezi kwa ajili ya Tatiana, Mungu amponye na kuwa kama zamani. “Koh koh koh!” kilisikika kikohozi kutoka kwa Tatiana.

Wazazi wake ambao walikuwa pembeni, wakasogea kule alipokuwa, hawakuamini kama binti yao alikuwa amerudiwa na fahamu baada ya kipindi kirefu kupita. Wakamsogelea pale alipokuwa na kisha kumshika mkono.

“Who are you?” (Wewe ni nani?) aliuliza Tatiana kwa sauti ya chini, alihisi mbele yake kulikuwa na watu.
“Tatiana binti yangu!”
“Mama!”
“Nipo hapa binti yangu,” alisema mama yake huku sauti yake ikisikika kama mtu aliyekuwa na majonzi mno.

“Nini kimetokea mama! Mbona sioni chochote, madaktari wamenifumba macho?’ aliuliza Tatiana, hakuwa akiona kitu chochote kile zaidi ya giza.

Bi Frida hakujibu kitu chochote kile, alibaki akilia tu kwani swali alilouliza binti yake lilimhuzunisha mno. Akashindwa kuvumilia kubaki chumbani mule, akatoka na kuelekea nje. Mzee Sangiwa akabaki chumbani mule, alikuwa akibubujikwa na machozi lakini hakutoa sauti yoyote ya kilio kwa kuhofia kwamba angemfanya Tatiana kuwa kwenye wakati mgumu.
“Tatiana binti yangu!” aliita mzee Sangiwa huku akimshika mkono binti yake.

“Baba! Kumbe upo hapa! Naomba uniambie, mbona sioni,” aliuliza Tatiana.
“Sikiliza mwanangu!”
“Baba niambie kuna nini,” alisema Tatiana lakini hata kabla hajapewa jibu, ghafla mlango ukafunguliwa na daktari mmoja aliyeongozana na nesi kuingia ndani.

Kitu cha kwanza kabisa wakamtaka mzee Sangiwa atoke chumbani mule kwani walitaka kumfanyia vipimo Tatiana huku nao wenyewe wakimshukuru Mungu kwa muujiza alioufanya kwamba mara baada ya kupita kipindi kirefu, hatimaye msichana huyo alikuwa amefumbua macho.
 
SEHEMU YA 173

Walichokifanya ni kumchoma Tatiana sindano ya usingizi, walitaka wachukue kila kipo wakati yupo usingizini, hawakutaka afahamu kitu chochote kile. Baada ya kumfanyia vipimo hasa kumpeleka katika chumba maalumu, wakampa muda wa kupumzika kisha kuwaita wazazi wake kwa ajili ya kuzungumza nao huku wakiwa na mkalimani ambaye aliifahamu vilivyo lugha ya Kiswahili.

“Kuna kitu tunataka kuwaambia,” alisema Dk. Berg.
“Kitu gani?”
“Kuhusu binti yenu.”
“Tunajua, ni kwamba hatoona tena.”
“Mmejuaje?”
“Tuliambiwa. Ila mnaweza kutuambia tatizo limekuwaje kiutaalamu.”

“Kuna msuli mmoja mkubwa ambao huwa unawezesha kuyafanya macho haya yawe na nguvu ya kuona, msuli ule unaonyesha kwamba ulirekebishwa baada ya kulegea kwa kipindi kirefu, alipopata ajali, msuli ule umelegea sana kiasi kwamba sisi kama madaktari, kuurudisha kwenye hali yake ya kawaida ni ngumu sana, na kama tukiulazimisha, unaweza kukatika kitu kinachopweza kupelekea kifo chake kwani damu zitatoka na kuelekea ubongoni,” alisema Dk. Berg huku akiwapa karatasi gumu (X-ray) kwa ajili ya kuangalia kile kilichokuwa kimetokea baada ya kupiga picha.

Taarifa za kuzinduka kwa Tatiana kukaanza kutangazwa kila kona, wazazi wake hawakujua taarifa hizo ziliwafikiaje watu wengine lakini ndani ya masaa matano tu, tayari dunia nzima ilijua kile kilichokuwa kimetokea.

Watu walitangaza kupitia katika mitandao ya kijamii kama Facebook, Twitter, Instagram na mingine mingi huku vituo vya televisheni na redio vikitumia nafasi hiyohiyo kuwapa watu taarifa juu ya kile kilichokuwa kimetokea likiwemo suala la kutoweza kuona tena.
“Mungu wangu! Hatoweza kuona tena?” aliuliza mwanamke mmoja, alikuwa ameshika simu na alikuwa akisoma habari mbalimbali kwenye Mtandao wa Kituo cha Televisheni cha BBC.
“Nani?”
“Tatiana!”
“Nani kakudanganya?”

“Wameandika hapa. Angalia mwenyewe.”
Zilikuwa taarifa zilizomhuzunisha kila mtu aliyeziona, msichana mrembo ambaye alivuma kwa kipindi kichache na kupata mafanikio makubwa, hatimaye hakuwa na uwezo wa kuona tena, kila aliyezisoma taarifa zile alihuzunika na hata wengine kulia kabisa.
 
SEHEMU YA 174

Tatiana alipopewa taarifa kwamba asingeweza kuona tena, akabaki akilia tu, hakuamini kile alichokuwa ameambiwa lakini kila alipojaribu kufumbua macho yake, yalifumbuka lakini hakukuwa na kitu chochote alichokiona mbele yake zaidi ya giza tu.

“Mama! Sitoona tena?” alimuuliza mama yake huku machozi yakimbubujika mashavuni.
“Tatiana....”
“Mamama niambie...sitoona tena?’ aliuliza tena huku machozi yakiendelea kububujika mashavuni mwake, kile kilichoendelea, hakikumuumiza yeye tu bali hata wazazi wake na watu wengine.
 
SEHEMU YA 175

Makachero wa CIA wakishirikiana na wale wa Ujerumani wakaanza kazi ya kumtafuta Buffet na Nikola ambao waliamini kwamba walikuwa jijini Berlin kama ambavyo mawasiliano yao ya mwisho yalivyoonyesha.

Kazi haikuwa ndogo hata mara moja, ilikuwa kubwa na nzito, walijitahidi kuwatafuta jijini hapo tena kwa kugawanyika kimakundi lakini hawakufanikiwa kuwaona kitu kilichowafanya kuhisi kwamba inawezekana watu hao wakawa wameondoka zao nchini humo.

Hawakukata tamaa, waliamini kwamba kuna siku wangeweza kuwaona watu hao hivyo wakaendelea zaidi kuwatafuta katika kila kona lakini matokeo yakaendelea kuwa yaleyale kwamba watu hao hawakupatikana kabisa.

“Lakini huyu msichana si anajulikana?”
“Ndiyo! Tena hiyo ndiyo njia nyepesi, cha msingi tuwasiliane na wazazi wake.”
Hicho ndicho kilichofanyika, kwa haraka sana wakaanza kuwasiliana na wazazi wa Nikola walioishi ndani ya Jiji la Munich, walitaka kufahamu mahali alipokuwa msichana huyo kwa kipindi hicho.

Walichokifanya ni kuanza kufuatilia vitu vyake vingi vilivyokuwa vikiendelea. Walichogundua ni kwamba msichana huyo alikuwa akisubiri majibu yake kutoka katika Chuo cha Ludwin Maximilians kilichokuwa hapohapo jijini Munich ili aweze kujiunga nacho kwa masomo ya biashara.

Mtu ambaye alikwenda nyumbani kwao alikuwa mpelelezi lakini yule aliyejifanya raia wa kawaida, alikwenda kama mhudumu wa posta, kazi yake ilikuwa ni kupeleka vifurushi katika makazi ya watu.

“Nimekuja kumuona Nikola,” alisema jamaa huyo, alionekana kijana mpole mno, kwa kumwangalia, usingedhani kwamba alikuwa mpelelezi.
“Hayupo! Alitoka.”
“Sawa. Kulikuwa na mzigo wake hapa!”
“Kutoka wapi?”
“Chuo cha Ludwig Maximilians.”
“Hebu tuuone.”

“Hapana! Mpaka awepo ndipo atakabidhiwa kwani anahitajika kusaini pia, akifika, mwambie atupigie simu,” alisema jamaa huyo, hakutaka kuendelea kusubiri, alichokifanya ni kuondoka nyumbani hapo.

Nikola alipopewa taarifa kuhusu mtu aliyeleta mzigo wake nyumbani kwao, alishtuka sana, alikuwa na hamu kubwa ya kujiunga na chuo hicho kikubwa jijini Munich, alichokifanya ni kutoka hotelini alipokuwa akiponda starehe na Buffet na kisha kuelekea nyumbani haraka sana.
 
SEHEMU YA 176

Simu ikapigwa na hivyo mtu huyohuyo kufika nyumbani hapo huku akiwa na mwenzake, walipomuona msichana Nikola, hawakutaka kufanya kitu chochote kile zaidi ya kumuweka chini ya ulinzi hali iliyomchanganya sana msichana huyo kwani hakujua kosa lake hasa lilikuwa nini.

“Kuna nini jamani?” aliuliza Nikola huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Wewe twende! Utayajua yote tukifika kituoni.”
“Naomba niwasiliane na mwanasheria wangu!”
“Hii si sehemu yake, utawasiliana naye ukiwa kituoni.

Wakamchukua na kuondoka naye nyumbani hapo. Wazazi wake walishangaa, hawakujua ni kitu gani kilichokuwa kimetokea mpaka binti yao kuchukuliwa na watu waliojitambulisha kwamba ni wapelelezi kutoka CIA.

Kulionekana kuwa na tatizo kubwa, mpaka mtu kukamatwa na CIA kutoka nchini Marekani, halikuonekana kuwa jambo dogo. Wazazi hao hawakutaka kubaki mahali hapo, walichokifanya nao kuingia ndani ya gari na kuanza kuwafuatilia ili kuona kama kweli walitoka polisi au la.
“Buffet yupo wapi?”

“Ninataka kuzungumza na mwanasheria wangu kwanza,” alisema Nikola huku macho yake yakianza kukusanya machozi.
“Utazungumza naye tu. Tunamtaka Buffet.”
“Sijui yupo wapi.”
“Sawa.”

Walichokifanya ni kuchukua simu yake na kisha kuangalia majina, hasa kwa simu zilizoingia na kutoka, wala hawakuchukua muda wakaliona jina la Buffet ambapo wakaichukua ile namba na kuanza kuangalia kwenye kompyuta yao kwa staili ya kuitraki ili wafahamu mahali alipokuwa mwanaume huyo.

Simu ikaanza kuonekana, ikaanza kusoma mahali alipokuwa, alikuwa katika Hoteli ya Lion King iliyokuwa pembezoni mwa Jiji la Munich, wakaanza kuelekea huko. Walitaka kuwa na watu hao wote ili watakapokwenda kituoni kusiwe na tatizo lolote lile, au kumtafuta mtu mwingine.
Walipofika hotelini hapo, wakateremka na kisha kuelekea mapokezini, baada ya kuonyesha vitambulisho vyao,

wakaambiwa chumba alichokuwa Buffet na kuelekea huko. Hawakuwa na kazi kubwa, walifanikiwa kazi kwa asilimia mia moja, wakamchukua Buffet ambaye alikuwa akishangaa tu, wakampeleka mpaka garini ambapo huko akakutana na mpenzi wake ambaye alikuwa akilia tu.
“Nikola! Kuna nini?”
“Sijui! Wamenichukua tu na kuniambia niwaambie ulipo.”
 
SEHEMU YA 177
“Kwa hiyo ukawaambia?”
“Hapana! Wamechukua simu yangu na kuanza kutraki namba yako,” alisema Nikola huku akiyafuta machozi yake.
Safari hiyo iliishia kituo cha polisi ambapo wakawekwa ndani na kuambiwa wasubiri. Wote kwa pamoja walikuwa wakishangaa, watu wakiowafuata na kuwakamata hawakuwa polisi wa
Ujerumani, walikuwa ni Wamarekani ambapo baadae wakavaa makoti yao makubwa yaliyosomeka CIA mgongoni.
“Kuna nini? Mbona mmetuleta hapa?” aliuliza Buffet huku akionekana kuwa na hasira, alikuwa ameshasahau kuhusu Tatiana.

“Mnamfahamu huyu?” aliuliza jamaa mmoja miongoni mwa watu wanne waliokuwepo ndani ya chumba kile, alikuwa ameitoa picha ya Tatiana na kuiweka mezani. Buffet alipoiona sura ile, moyo wake ukapiga paaaa.
“Mnamfahamu?”
“Ndiyo! Ni Tatiana!”

Hicho ndicho walichotaka kukijua kwanza kama watu wale walikuwa wakimfahamu msichana huyo au la. Hapo ndipo walipoanza kuwaambia kile kilichokuwa kimetokea, ilikuwa ni stori ndefu iliyohusu ufuatiliaji wao mpaka mwisho wa siku kuwadaka.

Waliwaambia kuhusu mawasiliano yao kwa njia ya meseji na sauti ambapo mpango mzima wa kummaliza Tatiana ulikuwa umepangwa, waliposikia hivyo na meseji hizo na sauti zao kuonyeshwa, kila mmoja akainamisha kichwa chake na kuanza kulia kwani tayari waliona kwamba walikuwa hatarini.

Hawakuchukuliwa na kuhukumiwa nchini Ujerumani, wakapelekwa nchini Marekani ambapo huko kesi ikaanza kuunguruma. Kila mtu aliyesikia juu ya kile kilichoendelea alisikitika, utetezi mkubwa wa Buffet ni kwamba alishawishika kiurahisi kwa kuwa alimpenda kweli Nikola na alikwenda kwa Tatiana kwa sababu alihitaji kuwa maarufu kupitia msichana huyo tu.

Kesi hiyo iliunguruma kwa muda wa miezi sita, kipindi chote hicho, ilikuwa ikiahirishwaahirishwa mara kwa mara lakini mwisho wa siku, hukumu ikatolewa na wote kwa pamoja kufungwa kifungo cha miaka kumi jela kwani kile kilichotokea lilikuwa moja ya tukio lililopewa jina la kukusudia kuua.

“Nisamehe Tatiana! “ alijisemea Buffet wakati akichukuliwa na kupelekwa katika gari la magereza, uso wake aliuinamisha, waandishi wa habari walikuwa wakipiga picha tu kwa ajili ya magazeti yao ya siku inayofautia.
 
Santeee,leo nilipamiss humu kila dakika nilikuwa naingia kuchungulia
 
SEHEMU YA 178

Kwa mara ya pili, Tatiana alikuwa kipofu, hata alipopona kabisa, hakutaka kukaa nchini Marekani, alichokifanya ni kurudi nchini Tanzania tena kijijini Chibe, kule alipozaliwa ili kama kufa, basi alitaka kufa ndani ya nchi yake, tena katika kijiji alichozaliwa.

Kila Mtanzania alihuzunika, wengi walikuwa wakimlaumu Buffet na msichana wake Nikola kwa kile walichokifanya kwa msichana yule.Nyota kali ya mafanikio iliyokuwa ikiwaka, ilizimika ghafla.
Kila siku Tatiana alikuwa mtu wa kulia tu, aliyakumbuka maisha yake ya zamani, alitamani kurudi kule alipokuwa, aombe msamaha kwa kila kitu kilichotokea ili arekebishe maisha yake lakini hilo halikuweza kujirudia tena.

Mapenzi yalimchanganya, mapenzi hayohayo yalimfanya kuwa kipofu kwa mara nyingine tena. Peter hakutaka kumtenga Tatiana, akaamua kurudi kijijini kule kama ilivyokuwa zamani. Kipindi kile, alirudi akiwa na mapenzi ya dhati, alilia sana lakini katika kipindi hiki alirudia akiwa mtu tofauti kabisa, alimchukulia Tatiana kama msichana wa kawaida, kila kitu kilichopita kama mapenzi na ubaya aliotendewa, akaamua kuusahau, hakutaka kuupa tena nafasi.
Kila Tatiana alipokuwa akiisikia sauti ya Peter, alibaki akilia tu. Katika maisha yake yote hakuwahi kumuona mwanaume huyo, hakujua alifananaje, alipotabasamu uso wake ulikuwaje. Alikuwa kipofu ambaye mara kwa mara alikuwa akishinda chumbani kwake.

Kupitia fedha zake, akafungua biashara nyingi, akaendelea kuingiza fedha na kuwa mwanamke tajiri kuliko wote Afrika Mashariki. Alichokifanya ni kugawa asilimia ishirini ya utajiri wake kwa Peter kama msamaha kwa kila kitu kibaya alichomfanyia kwani aliamini kwamba mwanaume huyo alikuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati.

“Naomba unisamehe kwa kila kitu Peter, ni shetani tu aliyenifanya nikuumize,” alisema Tatiana huku akilia, machozi yalimbubujika mashavuni mwake.
“Usijali Tatiana! Mungu ni mwema, labda kutokuwa nawe kulikuwa na sababu, labda ningekuwa nawe hata hatua hii niliyofikia ya kumtumikia yeye nisingeifikia,” alisema Peter kwa sauti ya chini.
 
SEHEMU YA 179

“Peter! Moyo wangu unakupenda mno, nahisi mapenzi mazito kwangu juu yako, ninakupenda, una mke, ila kamwe sitoweza kuwa nawe tena, japokuwa ninakupenda, kamwe moyo wangu hautokuwa na maumivu juu ya upendo wako kwa mke wako,” alisema Tatiana kwa sauti ya chini iliyoonyesha kuwa alikuwa na maumivu makali ya moyo.

Baada ya safari ndefu katika maisha yake, Tatiana hakuwa na jinsi, alitakiwa kukubaliana na ukweli uliokuwepo kwamba kila kitu kilibadilika na hatimaye akawa kipofu kama alivyokuwa kipindi cha nyuma.

Japokuwa alikuwa na utajiri mkubwa maishani mwake lakini hakuweza kubadilisha kitu chochote kile. Kila mwaka, masupastaa wengi walikuwa wakifika kijijini hapo kumjulia hali, walimfariji na kumtia nguvu ili kuendelea kupambana katika maisha yake.

Baada ya miaka miwili, akaamua kuandika kitabu cha maisha yake, alielezea kila kitu, tangu siku ya kwanza alipopata ufahamu mpaka siku ile ambayo maisha yalibadilika na kuwa kipofu tena. Hakuficha kitu, alieleza mapenzi mazito aliyokuwa nayo kwa Peter mpaka siku aliyokuja kumsaliti na kuwa kipofu kwa mara nyingine tena.

Kilikuwa moja ya vitabu vilivyohuzunisha mno, kila aliyekisoma, alibubujikwa na machozi na kumuonea huruma Tatiana. Kitabu hicho kiliandikwa kwa lugha saba na kulisambazwa duniani kote. Kiliteka hisia za watu wengi, kilinunulika mno, aliuza zaidi ya kopi milioni ishirini, utajiri wake ukaongezeka, ila kwake, utajiri mkubwa bila kuona chochote kile, ilikuwa kama mateso mazito yasiyoweza kubebeka.

MWISHO

Nashukuru sana kwa kuifuatilia simulizi hii tangu siku ya kwanza mpaka leo hii. Lengo la simulizi hii ni kujifunza na kuburudisha. Kuna mengi sana ya kujifunza lakini kuna mengi ya kukupoteza. Kwa yale mazuri, yachukue na kwa yale mabaya achana naye na nina uhakika kuna siku kwa yale mazuri yatakusaidia.

AHSANTENI.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom