KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amewekwa njia panda kutokana na matakwa ya wafuasi na mashabiki wa chama hicho kumtaka agombee ubunge katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, unaotarajiwa kufanyika Aprili mosi mwaka huu.
Hata hivyo, wakati shinikizo hilo likiwa hivyo, umeibuka mgongano wa mawazo miongoni mwa wanachama, wasomi na wadau kutokana na baadhi yao kupinga shinikizo hilo, wakidai kuwa kazi aliyonayo Dk. Slaa kwa sasa ya kukiimarisha chama akiwa nje ya Bunge ni kubwa na muhimu sana kuliko ubunge.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima kwa kufuatilia mijadala ya makundi hayo katika mitandao ya kijamii, umebaini kuwa wengi wanamtaka Dk. Slaa awanie kiti hicho, kwa matumaini kuwa CHADEMA watakinyakua kirahisi kutokana na umaarufu wake.
Katika maoni yao, wafuasi wa CHADEMA na wadau wengi walikwenda mbali zaidi wakisema kwamba kwa umaarufu aliojijengea Dk. Slaa tangu akiwa mbunge wa Karatu kwa vipindi vitatu na baadaye kugombea urais mwaka 2010 na kuteka nyoyo za wananchi, anaweza kugombea jimbo lolote nchini na kuibuka mshindi.
Walisema kuwa jambo hilo halitakuwa la kushangaza kwani linatokana na umaarufu wa kukubalika mahali popote nchini, huku wakitoa mfano wa Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, ambaye aligombea ubunge katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Temeke jijini Dar es Salaam mwaka 1996 na kuigaragaza CCM wakati huo akiwa NCCR-Mageuzi.
Hata hivyo uamuzi wa Dk. Slaa kushinikizwa agombee ubunge katika jimbo hilo umepingwa vikali na baadhi ya wasomi na wadau, wakidai huo ni mkakati unaochochewa na Chama cha Mapinduzi (CCM) ili kuhakikisha anarejea bungeni ambako atakuwa ametingwa zaidi na majukumu ya kibunge badala ya kukiimarisha chama.
"Unajua Dk. Slaa kama angekuwa ni mtu wa kutaka madaraka, tayari CCM wangekuwa wamekwisha kumshawishi Rais Jakaya Kikwete amteu mbunge katika vile viti vyake 10 ili arudi bungeni na kuacha kuwasumbua kama anavyofanya sasa. Akiwa mbunge hawezi kuzunguka kila sehemu kuimarisha CHADEMA kama sasa," alisema kigogo mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Dk. Slaa ambaye alishika nafasi ya pili katika kinyang'anyiro cha urais mwaka 2010 nyuma ya Kikwete, amejizolea uungwaji mkono miongoni mwa makundi hasa vijana, hatua iliyokifanya CHADEMA kunyakua majimbo mengi na viti vya udiwani kwenye uchaguzi huo.
Tayari mchakato wa kusaka wagombea katika jimbo hilo lililoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wake, Jeremiah Sumari (CCM), unaendelea ndani ya vyama kwa kutoa fomu kwa ajili ya kujiandaa na kampeni zitakazoanza Machi 9 hadi 29 mwaka huu.
Ushindani mkubwa unatarajiwa kuwa baina ya vyama vya CCM na CHADEMA, ambapo mtoto mkubwa wa marehemu Sumari, Sioi Sumari, amekuwa miongoni mwa wanachama wa kwanza wa CCM walioomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo, huku kada kijana aliyegombea kiti hicho mwaka 2010 kupitia CHADEMA, Joshua Nasari, akiwa ameomba kuteuliwa tena na chama chake.
"Dk. Slaa majukumu aliyonayo kwa sasa ni zaidi ya kuwa mbunge, kasi ya uwajibikaji na umahiri wa wabunge wa CHADEMA unayoiona ni kutokana na kazi nzuri ya kuwapika wabunge hao inayofanywa na yeye, kuna kazi kubwa zaidi ya hiyo?" alihoji mdau mmoja katika mtandao wa kijamii akiwapinga wanaokataa katibu mkuu huyo asigombee ubunge.
Maoni hayo yalipingwa na mchangiaji mwingine, akisema kama sheria inamruhusu Dk. Slaa, anaweza kugombea lakini ni bora awaachie vijana, awape mafunzo wawe tishio kama yeye.
"Mwacheni Dk. Slaa afanye kazi ya kuimarisha chama kwa mipango ya baadaye, tena azidi kuwapika wabunge vijana ili CHADEMA iwe na mvuto kwa sera zake. Maendeleo ya nchi hii yanahitaji mabadiliko makubwa, si bungeni peke yake, bali na kukijenga chama kujiandaa kwa uchaguzi ujao," alisema mchangiaji mwingine.
Mdau mwingie alisema kuwa mkakati wa kumtaka katibu huyo agombee, umeanzishwa na unashabikiwa na maadui wa CHADEMA, wakitaka aingie kwenye shindano la Arumeru ili wammalize kwa kutumia Tume ya Uchanguzi.
"Wanajua wakimmaliza Arumeru, hataweza kufurukuta tena mwaka 2015 kwenye urais au hata ubunge. Nadhani Dk. Slaa ajikite kwenye mambo ya Katiba Mpya zaidi. Kwa sasa, CHADEMA walio bungeni wanamwakilisha vya kutosha," alisema msomi mmoja.
Hata hivyo, Dk. Slaa alipotafutwa na gazeti hili aweze kuzungumzia juu ya hatua hiyo, alisema kwa kifupi: "Siwezi kulizungumzia jambo hilo, maana nilikwisha kusema muda mrefu kuwa sitaki tena ubunge na isitoshe mimi si mwenyeji wa Arumeru."
Alisisitiza kuwa kwa sasa ana kazi moja ya kukijenga chama chake cha CHADEMA ili kiweze kushika mizizi kwenye maeneo yote nchini.
Source: Tanzania Daima