MAKACHERO wa Marekani wamesema walivamia nyumbani kwa Osama bin Laden na kumuua baada ya kunasa mawasiliano ya simu yaliyokuwa yakifanywa baina ya mmoja wa wafanyakazi wa kiongozi huyo wa kundi la Al Qaeda na jamaa zake wa karibu.Makachero hao walifichua siri hiyo Jumatatu na kueleza jinsi mawasiliano hayo yalivyowawezesha kumfuata mfanyakazi huyo hadi alikokuwa amejificha Osama.Kwa mujibu wa makachero hao, Osama hakumwamini mtu yeyote kwenye jengo hilo. Awe kamanda wa ngazi za juu au walinzi wake, lakini aliwaamini wafanyakazi wake wawili tu ambao aliwatumia kupeleka ujumbe nje ya makazi hayo.
"Kwenye jela ya kisiri ya CIA Ulaya Mashariki, kiongozi namba tatu wa Al Qaeda, Khalid Sheikh Mohammed, aliwataja wafanyakazi hao wa karibu wa bin Laden," mmoja wa makachero wanne wa zamani wa Marekani alisema.
Kwa mujibu wa kachero huyo, mtuhumiwa huyo wa ugaidi aliwaambia makachero hao kuwa iwapo wangempata mfanyakazi mmoja wa Osama, angewawezesha kumkamata Osama Bin Laden.
Mchakato wa kumpata Osama
Kwa mujibu wa kachero huyo wa zamani wa Marekani, iliwachukua makachero wa nchi hiyo miaka kadhaa kutambua jina la mfanyakazi huyo, ambalo hata baada ya mauaji ya Osama bado halijajulikana.
Alisema ilikuwa ni amri ya bin Laden kuwataka wafanyakazi wake hao kutotumia simu au kompyuta wakiwa karibu naye.
"Lakini katikati ya mwaka jana, mfanyakazi huyo alikuwa na mazungumzo ya simu na mtu ambaye alikuwa akifuatiliwa kwa karibu na majasusi wa Marekani," alisema ofisa mwingine wa makachero wa Marekani ambaye hakutaka kutajwa.
Alisema makachero hao walianza kumfuatilia mfanyakazi huyo hadi maficho ya Osama.
Agosti mwaka jana 2010, mfanyakazi huyo bila kujua alielekeza makachero hadi makazi katika jiji la Abbotabad, Kaskazini Mashariki mwa Pakistan na ambapo walibaini kuwa nyumba ya Osama ilikuwa imezungukwa ukuta wenye urefu wa futi 18 na kuwekwa seng'enge juu yake.
Kwa mujibu wa habari hizo, tangu wakati huo makachero wa Marekani waliogopa kuvamia jumba hilo kwa hisia kwamba, Osama angekuwa amelindwa na walinzi wenye silaha kali. Katika uchunguzi wao walibaini kuwa hakukuwa na mtu aliyekuwa akiingia wala kutoka ndani na kwamba hakukuwa na nyaya za simu wala intaneti zilizoonekana kutoka nje ya makazi hayo.
Habari hizo zinaendelea kudai kuwa CIA baadaye iliamini Osama aliishi katika makazi wazi, kwenye jengo lililojengwa kwa namna ambayo ni vigumu kumtambua kwa kuwa hakuna yeyote anaweza kuingia ndani bila kupitia lango kuu lenye ulinzi mkali.
Makazi ya Osama
Ilipofika katikati ya Februari mwaka huu, makachero hao wa Marekani walijiridhisha kwamba Osama yumo ndani ya jengo hilo na hivyo kumjulisha Rais Barack Obama ili aweze kuchukua hatua zaidi.
Kwa mujibu wa sheria za Marekani, ni rais pekee anayeweza kuidhinisha majeshi ya nchi hiyo kufanya uvamizi katika eneo lolote baada ya kushaurina na wakuu wa masuala ya usalama.
Lakini kutokana na nyumba hiyo kuwa kwenye makazi ya watu Obama alisita kutoa amri ya kuvamia haraka kwani aliamini kuwa kufanya hivyo halafu usimkute Osama, kungeibua mzozo wa kidiplomasia.
Hata hivyo, Jumapili wiki hii baada ya kujiridhisha kwamba wanaweza kufanya uvamizi huo bila athari kwa raia, Rais Obama aliamuru helikopta mbili zitoke Jalalabad, Mashariki mwa Afghanistan na kuingia kwenye anga la Pakistan kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili Pakistan isizitambue.Helikopta hizo ziliwaingiza makachero hao kwenye makazi hayo ya Osama, lakini moja ikaanguka.
Mtandao wa WikiLeaks
Mtandao huo nao umeeleza kuwa aliyewezesha Marekani kujua alikojificha Osama, ni mmoja wa wahudumu wake ambaye alipata mafunzo ya kigaidi ili kutekeleza tukio la mashambulizi ya Septemba 11, 2001 nchini Marekani.
Abu Faraji al Libi ambaye aliwahi kufanya kazi karibu na Osama, anadaiwa kutoa taarifa muhimu kwa Shirika la Kijasusi la Kimataifa la Marekani (CIA) zinazomhusu mtuhumiwa huyo wa kigaidi duniani ambaye aliisumbua Marekani kwa zaidi ya miaka 10.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, CIA iliweza kumfahamu Abu baada ya kupata taarifa zake kupitia mtuhumiwa mwingine wa kigaidi ambaye alikuwa katika gereza la Guatanamo, Khalid Sheikh Mohammed.
Mahabusu mwingine wa Guantanamo, Muhammad Mani al-Qahtani aliiambia CIA kuwa Abu ndiye aliyempa mafunzo ya kompyuta katika mpango wa kutekeleza shambulio la kigaidi la Septemba 11, 2001.
Baada ya upelelezi huo, inadaiwa kuwa Abu aliorodheshwa kwenye kundi la watu muhimu mwenye kujua mambo yahusuyo matukio ya kigaidi ya kulipua ili kusababisha mauaji.
Mtanzania mpishi wa Osama
Mtanzania Ahmed Khalfan Ghailan mwenye asili ya Zanzibar, ndiye aliyekuwa mpishi wa aliyekuwa kiongozi kundi la Al-Qaeda, Osama Bin Laden.Ghailan ambaye sasa anatumikia kifungo cha maisha katika gereza la Marekani la Guantanamo lililopo nchini Cuba, kutokana na kuhusika katika kulipua ubalozi wa Marekani nchini Kenya na Tanzania na kusababisha vifo vya watu 257 na kuacha majeruhi 4000, alizaliwa mwaka 1974 visiwani Zanzibar.
Ghailan alikatisha masomo yake mwaka 1996 na kwenda jijini Dar es Salaam kuuza mitumba kabla ya kuanza kujihusisha na masuala ya ugaidi. Alikuwa akisafirisha foronya za magodoro kutoka Dar es Salaam kwenda Mombasa, nchini Kenya.
Alikuwa akifanya biashara na mwezake aliyefahamika kwa jina la Suleimani Abdallah ambaye alikuwa rafiki yake wa karibu. Baadaye aliamua kusafiri kwenda nchini Somalia, Dubai na Uarabuni kufanya biashara ya kuuza samaki.
Lakini baada ya biashara hiyo kuwa ngumu kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha, marafiki hao waliamua kurudi Mombasa, Kenya ambapo mwaka 1997 na mwanzoni mwa 1998 marafiki hao waliachana ambapo Ghailani alianza kufanya biashara ya sabuni akitokea Arusha na kuzipeleka Dar es Salaam.
Siku moja akiwa Arusha akipakiza sabuni kutoka kwenye duka la Hussein Abbe, uligundulika kuwa mzigo aliopakia haukuwa wa kawaida. Alikuwa anafanya safari zake mara kwa mara, lakini, siku hiyo aligundua kuwa alichokuwa amebeba siku ile haikuwa sabuni, bali ni malighafi yaliyotumika katika ulipuaji wa mabomu, katika balozi za Marekani.
1998 alielekea nchini Kenya na baadaye kwenda Pakistan na Afghanistan ambako alifanya mazoezi ya ugaidi aliyoyatumia kuulipua ubalozi wa Marekani mjini Nairobi, Kenya na Dar es Salaam.
Mwaka 1998 na 1999 Ghailani alifundishwa kwa miezi mitano masuala ya ugaidi na mwalimu wake Abdi Al Hakam Al Yamani. Pia alifundishwa lugha ya Kiarabu na akakijua vizuri kwani awali alikuwa akifahamu kuzungumza Kiingereza.
Baada ya kumaliza mafunzo hayo, Ghailan alienda Kandahar kati ya mwaka 1999 na 2001 baada ya kughushi hati ya kusafiria akionyesha kuwa ni Mujahideen na familia yake wanarudi nyumbani kwao Kandahar na baadaye alirudi tena nchini Kenya.
Taaluma ya kughushi
Baada ya kufanikisha azma yake ya ulipuaji wa bomu alitoka Kenya kuelekea nchini Afghaniastan kwa ajili ya mafunzo katika kambi ya Al Faruq. Kati ya 1999 na 2001 alikuwa mpishi wa kundi la Osama Bin Laden na baadaye alighushi vyeti na barua akawa anafanya kazi na Khalid Bin Attash na Ammar Al Baluchi.
Ahmed Abdul Aziz alimtambulisha kama mlinzi wake, alikuwa anawahudumia wenzake akiwa kama mwanafunzi, lakini baadaye alikataa kufanya kazi ya ulinzi kwa sababu walinzi walitumia muda wao mwingi kufanya kazi, huku wakikosa uhuru wa kufanya mambo mengine.
Wakati akiendelea na kazi yake hiyo ya upishi wa chakula katikati ya mwaka 2001 na wakati huo huo akitambulika kama mlinzi alipata mafunzo ya kughushi nyaraka.Alijifunza kughushi nyaraka kuanzia mwaka 2001 kutoka kwa mwalimu wake aliyefahamika kwa jina la Abu Yahya wa Afghanistan. Ujuzi huo aliutumia kughusshi nyaraka ambazo alizitumia kusafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine akiutumikia mtandao wa Al Qaeda.
Anasema alifundishwa na mwalimu wake huyo namna ya kupiga picha na kuweka katika hati ya kusafiria, stempu, namna ya kutengeneza kitambulisho, leseni ya udereva, na namna ya kutumia Adobe Photoshop.
Ghailan aliendelea kuwa mwanachama wa Al Qaeda kwa sababu alikuwa yeye ndiye mtu aliyetumika kufoji nyaraka mbalimbali za kundi hilo.
Wakati bado yupo nchini Pakistani aliweza kuwasaidia wanachama wa kundi la Al Qaeda kuwagushia vyeti vya kuzaliwa na hati za kusafiria ambao wengi walikuwa wakisafiri na familia zao bila ya wasiwasi.
Osama alivyoishi na majirani
Katika hatua nyingine wakazi wa mji mdogo wa Abbottabad wanaoishi jirani na nyumba alimokuwa akiishi Osama bin Laden, wamesema katika nyumba hiyo kulikuwa na watu wazima 30 na watoto kadhaa.
Walisema watu hao walionyesha ustarabu mkubwa kwa majirani, lakini hawakupenda kuzoeleka.Miongoni mwa matendo waliyoonyesha kuwa ya kistaarabu yaliyofanywa na familia hiyo ya Osama ni kushiriki katika mazishi na kutoa msaada wa lifti kwa majirani waliokuwa wanaenda mjini kupata mahitaji.
Mmoja wa majirani aliyesema ana ufahamu mdogo kuhusu watu waliokuwa wakiishi kwenye nyumba hiyo, ingawa walikuwa majirani. Alisema ni wanaume wawili tu waliokuwa wanatoka kwenye nyumba hiyo na kuwakaribisha majirani.
Wanaume hao walijitambulisha kwao kuwa ni Tariq na Arshad Khan na walijieleza kuwa ni wenyeji wa eneo la Kaskazini Mashariki mwa Pakistani.Arshad alijitambulisha kuwa ndiye mwenye umri mkubwa kwenye familia hizo na alikuwa akizungumza lugha mchanganyiko zikiwapo za Kipashto na Kiurdu, ambazo zimezoeleka kwenye eneo hilo la Kaskazini Magharibi mwa Pakistani.
Khurshid Bibi (70), ambaye ni mkazi wa muda mrefu katika eneo hilo alisema kuwa ni nadra kuwaona wakazi wa nyumba hiyo mitaani.Lakini alisema anakumbuka kuwa mmoja wa wanaume waliokuwa wanaishi kwenye nyumba hiyo, aliwahi kumpa lifti wakati anaenda sokoni wakati mvua ikiwa inanyesha.
Jirani mwingine alieleza kwamba aliwahi kuona wanaume wawili kutoka nyumba alimoishi Osama wakishiriki kwenye msiba uliotokea eneo hilo.Walibaini pia kuwa kwenye nyumba hiyo ziliishi familia nyingi na hata wakati maofisa wa afya walipokuwa wanatoa chanjo ya polio kwa watoto, walishiriki.
Walisema siku hiyo ya chanjo ya polio ndiyo mtu nje ya familia hizo, aliruhusiwa kuingia kwenye jengo hilo.
Inaelezwa kuwa ofisa afya alipofika katika eneo hilo akitoa chanjo nyumba kwa nyumba, aliruhusiwa kuingia na kutoa huduma kwa watoto kwenye nyumba hiyo baada ya kueleza umuhimu wa huduma hiyo.
Inaelezwa kuwa wanaume waliokuwa ndani ya wigo walimruhusu ofisa huyo na alipoingia alitoa chanjo kwa watoto 23.