*NYUMA YAKO (MSIMU WA PILI) -- 21*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
“Una uhakika kabisa?”
“Ndio, nina uhakika maafisa.”
“Sawa, tunashukuru,” mabwana hao wakasema na kunyanyuka.
“Vipi sasa kuhusu pesa yangu?” Sarah akawahi kuuliza.
“Usijali,” wakamtoa shaka, “utapata pesa pale ambapo taarifa zako zitazaa matunda.”
Baada ya kusema hayo, wanaume hao wakarudi kwenye gari lao na kuanza safari. Wakiwa njiani wakawataarifu na wenzao wengine juu ya tukio wanaloenda kufanya.
ENDELEA
Haikuchukua muda mrefu wakawasili na ndani ya muda mfupi wakawa wameshamwona Katie aliyekuwa ameketi kwenye mchanga akitazama maji ya bahari, Marshall haikuonekana yupo wapi.
Basi wakapashana habari, walikuwa ni watano kwa idadi, mawasiliano yao yalikuwa bora kabisa wakitumia vifaa binafsi.
“Kagua eneo zima,” agizo likatoka, “atakuwa ndani ya eneo hilihili!”
Ukaguzi ukafanyika kwa siri na kwa uadilifu kuangaza eneo zima la fukwe pamoja na viunga vyake vya karibu.
Wakiwa wanafanya msako huo, mmoja wao akamwona mtu ambaye alimtilia mashaka, mtu huyo alikuwa ni mwanaume aliyevalia bukta nyepesi na kofia ya kujikinga na jua, alikuwa anaingia kwenye kiunga kilichokuwa kinatumika kama sehemu ya kutolea haja.
Basi kufuatia shaka lake, mwanaume huyo akajongea, hakuona stara kuwataarifu wenzake maana bado hakuwa na uhakika. Akiwa ameshikilia silaha yake mfukoni akapiga hatua nzito kusonga.
Akazama kiungani, alipotazama akaona milango miwili, mmoja ukiwa umechorwa mtu wa jinsia ya kike na mwingine ukiwa kinyume. Hapo akangoja kumwona mwanaume yule aliyezama ndani.
Alipongoja kwa kama dakika mbili, akatoka huko mwanaume mzee mwenye mvi kichwani na miwani usoni. Mzee huyo alikuwa amevalia bukta tu na kandambili nyekundu, mahadhi ya fukweni, alikuwa ni tofauti kabisa na yule ambaye alionekana akizama ndani, hivyo bwana yule mpepelezi akastaajabu.
Kuhakiki akasonga na kuzama ndani choo, alipotazama hakuona mtu, lakini kabla hajajinasua kujitoa humo, akajikuta hawezi!
Hakukumbuka hata aliona nini, ni kufumba na kufumbua akawa yuko kizani. Kiza totoro.
**
“Hey Dennis! Upo sawa?” sauti ilitoka kwenye kifaa cha mawasiliano.
“Dennis! … Dennis!” sauti ikarudia tena kushika mawimbi, mara hii ikajibiwa, “Nipo sawa, nipo sawa mkuu!”
“Vipi haujafanikiwa kuona kitu?” sauti ikauliza tena.
“Hapana, sijafanikiwa, mkuu. Vipi wewe umeona jambo?”
“Hapana, bado tunatafuta. Hatujajua ameelekea wapi!”
“Vipi mwanamke?”
“Bado yuko mwenyewe. Sasa amesimama anachezeachezea maji!”
Baada ya mawasiliano hayo kukawa kimya, likapita kama lisaa limoja kabla ya mkuu wa oparasheni kurejea kwenye gari kwasababu ya kuteka hadubini, alikuwa anataka amwone Katie ameelekea wapi ndani ya maji, mwanamke huyo alikuwa amezamia asionakane kwa urahisi tena.
Akafungua mlango wa gari na kunyooshea mkono kwenye dashboard, akafungua na kutazama, akaiona hadubini, basi akaivuta kuijaza mkononi lakini kabla hajatoa kichwa chake garini akashtushwa kwa kuona miili kwenye viti vya nyuma! Ilikuwa miili miwili, tena ya wenzake aliokuja nao.
Basi akapandwa na hofu sana, akatazama kando na kando asione cha kutia shaka, akazama ndani ya gari kuwajulia hali wenzake na kheri akamkuta mmoja ambaye bado alikuwa anaweza kuzungumza, alikuwa hoi sana akipandisha macho juu na mdomo wake ameachama, anahema kama mtu aliyebanwa na mbavu!
“Vipi?” akauliza jamaa, “nini kimewatokea?”
Yule mmoja mwenye angalau akasema akiwa anajaribu kunyoosha kidole, ni kana kwamba mkono ulikuwa mzito sana kuunyanyua, akasema, “yupo … yupo ana ---” akakata pumzi!
Upesi bwana huyo akamtazama mwilini na kubaini alikuwa amevujia damu kooni na pia mbavu zake upande wa kushoto zilikuwa uji! Kidogo tu huyo mwanaume aliyekata pumzi akaanza kuchuruza damu mdomoni, damu ambazo zilikuwa zinaongezeka kwa wingi kadiri muda unavyoenda.
“Shit! Shit! Shit!” akalaani yule bwana akitoa kichwa chake garini, alikuwa amefura lakini pia amechanganyikiwa. Akawataarifu wenzake, wawili kwa idadi, juu ya yale yalitokea na kuwataka wamkamate Kate popote pale watakapomuona kwani mambo yalikuwa yanaelekea kuharibika.
Baada ya kusema hayo akaenda kusaka, alipofika majini akarusha macho yake kwa kupitia hadubi akikagua kila eneo la kwenye maji asimwone Kate kabisa. Ni kwamba amepotelea kwenye maji ama amepotelea nchi kavu?
Akakimbia fukweni akitupa macho yake lakini muda si mrefu akapata taarifa sikioni kuwa Kate ameonekana na tayari ameshakamatwa!
“Yuko wapi?” akauliza akiwa anahema kama mbwa, alipopewa maelekezo akaelekea huko upesi kutazama, ilikuwa ni garini. Alipofika akarusha macho yake na kuambulia kuona maiti nyingine ya tatu!
Mwenzake mwingine alikuwa ameuawa. Sasa walikuwa wamebaki wawili tu, wale wanaume pekee ambao walikuwa wameenda kuonana na Sarah kabla ya kuja huku fukweni.
“Tobias, mwingine ameuawa!” alisema kwenye kifaa cha mawasiliano. Uso wake sasa ulionyesha woga, macho yake yalibeba hofu.
“Serious?” sauti ikauliza kifaani.
“Ndio, serious! Sasa nimebaki na wewe tu.”
“Umemuona Katie?”
“Hapana, sijamwona. Vipi wewe?”
“Sijaona kitu! Sasa tunafanyaje?”
“Tuendelee kutafuta, yupo hapahapa anatutazama. Ukimpata Katie mshikilie, atatuletea Marshall mkononi!”
“Na vipi tusipompata?”
“Tumtafute Marshall.”
Kukawa kimya kidogo, kisha,
“Henry!”
“Toby!”
“Marshall huyu hapa.”
“Wapi?”
“Yupo hapa mbele yangu.”
“Toby kuwa serious!”
“I am serious! Marshall yupo hapa mbele yangu. Tumefeli.”
Baada ya hapo kukawa kimya. Bwana huyu akaitwa jina la mwenzake pasipo majibu. Akahofu sana na sasa akaafiki kwamba hana la kufanya. Ni kana kwamba Marshall amekaa pembeni akiwatazama wanahangaika, basi upesi akarudi kwenye gari na kuwasiliana na makao alipotoka kwamba misheni yao haijazaa matunda, mpaka muda huo ni mmoja tu ndiye amesalia kati ya watano.
Alikuwa anaongea kwa kuyumbisha sauti, macho yake yakiangazaangaza huku na kule huko nje, alikuwa anahofia usalama wake. Alipomaliza kutoa taarifa, akakata mawasiliano na kisha akawasha gari ili apate kuondoka.
Akatekenye funguo mara ya kwanza, hola! Akatekenya ufunguo mara ya pili, napo hola, gari haikuwaka. Akapiga usukani mara mbili akitusi, akachomoa ufunguo ili achomeke tena, ufunguo ukadondoka chini kwa papara! Mikono ilikuwa inamtetema.
Akainama kuuokota, na aliponyanyua kichwa , uso kwa uso akakutana na Marshall mbele ya gari! Akanyanyua kwapa ampate kumdungua na bunduki, hajafanya kitu, akasikia sauti ya kike ikimwamuru aweke silaha chini na kutulia kama maji mtungini!
Alipotazama kwenye kioo juu ya kichwa chake, akamwona Katie akiwa amemuelekea bunduki.
**
“Mkuu, inabidi uone hiki!” alisema kijakazi akiwa anamtazama bwana Ian Livermore. Bwana huyo alikuwa ameketi kwenye kiti kikubwa nyuma ya meza yake ya thamani. Juu ya meza hiyo kulikuwa na visosi vitatu vyenye kubebelea majivu ya sigara.
Basi akanyanyuka kuitikia wito wa kijakazi wake, akatoka nje ya jengo na kuona gari kwenye uwanja wa maegesho.
“Tumelikuta barabani hapo nje tukalisukuma kuingia ndani. Hamna aliyerudi salama,” akasema kijakazi akionyeshea mkono wake ndani ya gari, bwana Ian akatazama humo na kuona maiti za watu watano, wote wakiwa ni watumishi wake!
Basi akajikuta akicheka sana. Akashika kiuno chake na kutikisa kichwa.
“Nilijua … nilijua we fucked up!”
**
*NYUMA YAKO (MSIMU WA PILI) -- 22*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
“Tumelikuta barabani hapo nje tukalisukuma kuingia ndani. Hamna aliyerudi salama,” akasema kijakazi akionyeshea mkono wake ndani ya gari, bwana Ian akatazama humo na kuona maiti za watu watano, wote wakiwa ni watumishi wake!
Basi akajikuta akicheka sana. Akashika kiuno chake na kutikisa kichwa.
“Nilijua … nilijua we fucked up!”
ENDELEA
Akarudi ndani na kuwaza sana, alimaliza pakti mbili za sigaa akiwaza na kuwazua. Mwishowe akawaita watu wake, walikuwa takribani sitini na tano, akawaambia ni namnga gani anataka Marshall ashughulikiwe haraka na katika namna ipasayo.
Hakuwa na haja ya Marshall kukamatwa, alichokuwa anataka ni mwanaume huyo afe tu, afe tu basi!
“Nataka kichwa chake hapa!” alisema akibonyezea kidole chake mezani, “Nataka kusikia habari za kifo chake, mmenielewa!!” alipaza sauti kwa ukubwa kana kwamba anaongea na watu waliojiketia maili nane mbali na yeye, baada ya kusema hayo akatulia akiwa anafikiri, mdomo wake ulikuwa mkavu kwa kukaushwa na moshi wa sigara lakini pia ukiwa unanuka harudu ya pakti.
“Atakayefanya jitihada za kumuua Marshall, ama kuniletea hapa mwili wake nitamlipa dola milioni mia moja mkononi! Papo hapo!”
Alipotoa ahadi hiyo akawataka wote waondoke wamwache akiwa anawaza cha kufanya. Kuna muda akahisi kuna haja ya ‘wanaume’ wake wote wafike eneo lile kwa ajili ya kazi moja ya kumshughulikia Marshall.
Asingeweza kupumzika mpaka mwanaume huyo atakapofukiwa ardhini.
“Nataka wote mje Marekani!” aliteta na watu waliopo Ujerumani, kwa ufupi na wazi, kisha akaweka simu yake mezani na kudaka kichwa chake. Hakujua kama siku yake ingekuwa mbaya kiasi kile. Alipoambiwa kwamba taarifa ya kupatikana kwa Marshall imepatikana alikaa tenge kungoja mambo mazuri!
Baada ya kufikiri tena kwa muda kidogo akanyanyua simu yake na kumpigia kijakazi wake anayehusika na mawasiliano, huyo akamwambia achapishe matangazo mengine ya kuongeza donge nono kwa watakaotoa taarifa juu ya Marshall, pesa mara mbili ya awali!
Kijakazi huyo akapokea agizo na kuanza kulifanyia kazi. Alichokuwa anakifanya ni kuchapisha tena matangazo yaliyotolewa na polisi na kuyasambaza zaidi. Walikuwa wameshafanikiwa kudukua namba za kitengo hicho na basi kufanikiwa kupokea simu yoyote ile ya mwananchi atakayekuwa anatoa taarifa kuhusu upatikanaji wa Marshall.
Swala hilo halikuwa gumu sana kwa bwana Ian kwani vijakazi wake wengi walikuwa ni watu ambao wanafanya kazi kwenye taasisi za usalama, hususani FBI na CIA. Maajenti hao walikuwa wakimtumikia Bwana huyu kwasababu za kiusalama zaidi, kwani kwa mujibu wa bwana Ian alikuwa na taarifa na shahidi zao kedekede kuhusu uhalifu waliokuwa wakiufanya kwa kutumia migongo ya taaluma zao.
Kuepusha ubaya, watu hawa walikusudia kuungana na kufanya kazi yoyote alimradi itawapatia pesa ya maana, hata kama itakuwa ni kwa kuliumiza taifa lao!
**
“Hapa patakufaa!” alisema Marshall akitazama nyumba ndogo iliyokuwa imesimama mbele yao, yeye na Katie. Ilikuwa ni nyumba yenye ukubwa wa wastani ikiwa imefumwa vema na mbao.
“Yah! Patanifaa,” Katie akajibu na kisha akamgeukia Marshall, “Kwahiyo utakuja lini kuonana na mimi?” alimtazama Marshall kwa mapenzi huku akitabasamu.
“Usijali, nitakuja,” Marshall akamjibu akimwekea mkono begani. Wakazama ndani ya makazi hayo na Katie akapapekua na kuridhika napo, japo palikuwa padogo, vyumba viwilii tu, sebule na jiko, palikuwa pazuri panapovutia.
“Pazuri sana!” Katie alisema aking’aza macho.
“Nilipaona kupitia mtandaoni, nikaona patakufaa. Si nyumba ya kukufanya uhisi mpweke hata nisipokuwapo, ni padogo,” alisema Marshall akimtazama Katie anayekagua makazi yake mapya.
Katie akamtazama Marshal kisha akambusu na kumwambia kwa kumnong’oneza, “hata kama pangekuwa padogo kama stoo, bado nitahisi upweke usipokuwapo, Tarrus!”
“Ni Marshall.”
“Tarrus. Nakujua kwa jina la Tarrus na nitakuita vivyo peke yangu!”
Marshall akambusu Katie kisha akamwuaga aende zake. “Kwa leo acha niende, kuna baadhi ya kazi namalizia alafu tutakuwa pamoja, sawa?”
“Kazi gani hizo, Tarrus?” Katie akauliza kwa sauti ya puani. Alimtazama Marshall kwa macho ya huruma akiwa amemkumbatia kwanguvu asimwachie.
“Rafiki yangu yupo matatizoni, napaswa kumsaidia.”
“Nani? - yule Jack?”
“Yah! Kuna mambo hayapo sawa na maisha yake, siwezi kumwacha peke yake.”
Katie akamtazama Marshall kwa kitambo kidogo alafu akakubali japo kishingo upande. Marshall akambusu na kwenda zake.
**
Saa nne usiku …
“Ulitarajia nini, Tony?” aliuliza Jack akimtumbulia macho Marshall. “Amekwisha kufa!”
Marshall akanywa maji kwenye glasi yake na kuuliza, “Kwahiyo yupo wapi?”
“Yupo kule kule ulipomuweka!” akajibu Jack na kuweka kituo. Marshall akamalizia maji yake kwenye glasi kisha akajifuta mdomo kwa kutumia mgongo wa kiganja chake, akamtazama Jack kwa kitambo kidogo, hakuwa sawa, lakini hakutaka kuzua jambo muda huo, akanyanyuka akauone mwili wa yule mateka wake.
Ni kweli akaukuta ukiwa mfu, akauweka kwenye kiroba na kumtaka Jack wakautupie huko mbali. Wakaongozana naye kufanya vivyo.
“Tony, hii tabia ya kuua watu inabidi upunguze, imezidi sasa!” Jack alisema wakiwa njiani kurudi. Aliuwa anahofia mauaji, aliamini kama yamgeendelea basi mwisho wa siku yangewatia hatiani ingali mikono yao ni safi.
“Jack, huwezi kuelewa,” Marshall akadokeza, “Ulimwengu huu haupo sawa kama wewe udhaniavyo. Muda mwingine yakupasa kufanya vivyo kabla ya wewe kufanyiwa vivyo, lakini pia muda mwingine unafanya kwa ajili ya kutuma ujumbe. It is die-or-survive world!”
Wakafika nyumbani na kupumzika. Tangu Marshall alipoingia kwenye makazi hayo hakuona Vio akiongea na Jack. Walikuwa wakipishana kama magari moshi. Marshall aliona yote hayo lakini hakutia neno.
Usiku ukazidi kukua, na siku hiyo Marshall akiwa amelala akasikia tena mtu akifungua mlango na kutoka. Pasipo kujiuliza mara mbili alifahamu kuwa ni Vio.
Mwanamke huyo alitazama usalama na kujiona yu sawa, basi akanyata mpaka kuufuata mlango wa nyuma, akatoka na kisha akaurudishia mlango huo taratibu pasipo kelele. Alipofanikiwa akasonga mbali asisikike.
“Gotham, usinipigie kwa muda tafadhali, sipo kwenye hali nzuri na Jack,” alisema Vio kwa kunong’ona. “we ngoja mpaka pale nitakapokutaarifu, sawa?” akaendelea kuteta, “acha ubishi basi, ninavyokuambia hivyo nina maana yangu. Kuna mambo hayajakaa vizuri, ndio ni kuhusu ile ishu. Nakuomba uelewe hata mara moja, kwaheri!”
Akakata simu na kushusha pumzi kisha akatikisa kichwa chake kwa maulizo.
Alipogeuka, akashtuka kukutana uso kwa uso na Marshall!
“Mungu wangu!” moyo wake ulienda mbio na ghafla akahisi mwili unamtetemeka.
Marshall akamuuliza, “Ulikuwa unaongea na nani?”
Akabanwa na kigugumizi. Alitazama simu yake kisha akarudisha macho kwa Marshall, hakuwa na cha kusema. Marshall akarudia tena kuuliza, mara hii Vio akasema hakuwa anaongea na mtu, basi Marshall akamtaka ampatie simu aone.
“Siwezi kukupatia simu yangu, wewe kama nani?” Vio akamkazia macho Marshall. Marshall akamsogelea karibu zaidi na kumwambia, “Nadhani unajua mimi ni tofauti kabisa na Jack. Sina uvumilivu wala ujinga wake. Usinijaribu, sawa?”
Baada ya hapo Marshall akamwambia Vio kumhusu mwanaume wake, Gotham na amekuwa akimfuatilia kwa muda sasa.
“Huwezi kuniongopea kitu, Vio. Nataka tu nijue kwanini unamfanyia Jack hivi?”
**