*NYUMA YAKO (MSIMU WA PILI) --- 07*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Siku hiyo nilipoenda chumbani mwangu, sikuwasha runinga kabisa, nikakaa kuwaza sana juu ya Katie na hali aliyomo, alikuwa ananihitaji sana katika muda ule, lakini zaidi nikawazia kumhusu mwanangu endapo Katie atajifungua, masikini hatamwona baba yake. Niliumizwa sana.
Nilishindwa kulala siku hiyo.
Vipi kama kesho ikawa siku yangu ya kuuawa?
ENDELEA
Ili niupate usingizi, ilinibidi nijipe matumaini kuwa Katie atakuwa salama baada ya kuonana na Jack. Nilivuta pumzi ndefu na kujifunika shuka nikijaribu kulala lakini bado mawazo hayakunitoka.
Baada ya kama lisaa limoja baada ya kuamua kuwa Katie atakuwa vema, nikaanza kuuonja usingizi kwa kurembua, lakini napo usikae, nikasikia mtu akigonga mlango na kunisihi ninyanyuke. Alikuwa ni askari amekuja kutuhesabu.
Basi sikuwa na jinsi nikasimama na kumtazama askari huyo. Alinimulika usoni na kuniambia nitanue kinywa, nikatii. Kabla hajaondoka akaniuliza maswali mengine juu ya hali yangu. Aliponiuliza kama nimekula siku hiyo, nikiwa nimechoshwa na maswali yake yasiyokoma, nikalipuka na kumjibu aniache nilale!
Akatanua mdomo, “Ah!” kisha akaniuliza, “Unawezaje kunijibu hivyo wewe marehemu mtarajiwa?” aliniuliza akinimulika usoni, macho yakaniuma japokuwa nimeyafumba. Nikaweka kiganja changu kujiziba na mwanga huku nikikunja ndita.
“Nakuuliza wewe!” akafoka.
“Kuna haja gani ya kuzozana?” nikamuuliza kwa ustaarabu. “Mimi na wewe wote ni marehemu watarajiwa. Wadhani utaishi milele?”
Kauli hiyo ikamshangaza na kumuudhi bwana yule. Nilimsikia akinguruma kwa ubabe na akakandika lango langu la chuma akisema, “Kelele mbuzi wewe!”
Nami nikanyamaza. Nilikuwa naona ananichosha zaidi. Nilitamani kumwondoa pale alipo lakini sikuwa naweza. Alikuwa ni kero kupita kiasi.
“Heri ya mimi, wewe ni marehemu ambaye siku zake zipo wazi na zinahesabika. Hautapita juma hili utakuwa tayari ushakufa. Vipi utataka kifo cha aina gani? Sindano ya sumu? Kiti cha umeme, risasi ama chumba cha gesi?” kisha akacheka kinafki. “Msaliti wa taifa wewe!” akanitusi na kwenda zake.
Angalau akawa ameenda, lakini pia nikajikuta nikiwa nimefahamu hatma yangu; watanimaliza ndani ya juma hilo, basi ndiyo nikakosa usingizi kabisa mpaka jua linapambazuka.
Kesho yake nikaenda kwenye uwanja wa mazoezi na kuketi huko. Si kwamba nilitaka kufanya mazoezi, la hasha, nilikuwa nataka kubadilisha tu mazingira. Kukaa mule ndani kulikuwa kunachosha, na muda mwingine kulikuwa kunatisha.
Nikiwa nimekaa hapo, nikawatazama wenzangu waliokuwa wanaongoja hatma ya maisha yao kama mimi. Walikuwa ni watano kwa idadi. Mmojawao alikuwa mnene kupita wote na sura yake ilikuwa ya kipole kabisa, nilishangazwa ni nini kimemleta mule ndani ya gereza.
Akiwa amevalia miwani ya macho, alikuwa anachuchumaa na kusimama, zoezi alilokuwa analifanya taratibu taratibu. Alikuwa anatweta jasho jingi tofauti kabisa na zoezi alilokuwa analifanya.
Nikiwa namtazama, nikaanza kumhesabia zamu alizokuwa anaenda chini na kurudi juu. Akiwa amefikisha tatu tangu nianze kumpa jicho, akadondoka chini! Wenzake watatu waliokuwa mbali kidogo naye, wakaangua kicheko.
“Mtazame yule kiroba!” mmoja alidhihaki. Hakuna aliyeenda kumsaidia. Basi mimi nikanyanyuka na kupiga hatua kadhaa kumfuata. Nikamnyanyua na kumpa pole. Akaketi kitini na kunitazama kama mtu aliyejawa na woga. Hakusema neno akawa anapambana kutengeneza pumzi yake.
Kwa kumtazama tu nikafahamu hana miaka inayozidi ishirini na tatu. Alikuwa mdogo sana kuwamo eneo kama hilo.
“Naitwa Marshall,” nikajitambulisha nikimpa mkono. Hakuupokea, bado alikuwa anahema kwanza lakini pia akiwa na hofu usoni.
“Usijali, mimi si mtu mbaya,” nikamwambia nikimtazama.
“Usingekuwa mtu mbaya ungekuwa humu?” akaniuliza. Nikatabasamu na kuweka mkono wangu begani mwake. “Sikia, kid. Si kila unayemwona jela ana hatia. Maisha hayako sawa kama unavyoweza kudhani,” nilimwambia kwa sauti ya utaratibu kana kwamba mzazi akimwonya mwanae. Akanitazama na kuniuliza kwanini nipo mule, nikamjibu ni habari ndefu ambayo asingependa sana kuisikia kisha nikanyanyuka na kumwambia awe makini na afya yake.
“Kumbuka bado upo hai,” nikamwambia kisha nikachukua hatua kuondoka. Nilipopiga hatua nne, akapaza sauti yake akisema, “William, naitwa William Jones.”
Nikageuka na kumtazama. “Nashukuru Willy.” alafu nikaenda zangu.
Dakika kadhaa mbele, tukaja kutolewa kwenye uwanja wa mazoezi kurudishwa kwenye vyumba vyetu. Tulikuwa chini ya ulinzi pingu zikibana mikono.
Nilipofika nikaoga na kulala kitandani baada ya kuwasha runinga. Siku hiyo nikiwa natazama habari nikabahatika kumwona Makamu wa Raisi, ambaye kwa muda huo ndiye alikuwa akikaimu nafasi ya Raisi, akiwa anahojiwa na kituo kimoja cha matangazo.
Kusema ukweli kwa muda wote ule ambao sikuwa najifahamu, nimepoteza kumbukumbu zangu, nilikuwa nimepitwa na mengi sana ulimwenguni, haswa Marekani.
Sikuwa nafahamu kuwa Makamu wa Raisi alikuwa ndiye Raisi rasmi sasa baada ya yule wa awali kutoonekana, lakini pia kwa kupitia matangazo hayo nikapata kujua kuwa nchi ya Marekani ilikuwa kwenye mazungumzo na umoja wa nchi kubwa zinazozalisha mafuta duniani kwa minajili ya kibiashara.
Kiongozi huyo alipoulizwa kuhusu swala la kupotea kwa Raisi na namna gani linavyomuathiri, akapambanua kuwa jambo hilo ni jeraha kubwa sana kwake na kwa Marekani nzima, lakini akaenda mbele kwa kusema kuwa anaamini huo ni mchezo mchafu amba umefanywa na maadui wa Marekani kwa kutumia nyenzo waliyoiunda wao wenyewe.
“... adui anapokuwa nje, ni rahisi kupambana naye. Lakini anaposhirikiana na wa ndani, kunatengeneza nyufa. Ni rahisi kwa ukuta kubomoka,” alisema kwa hisia.
“Na vipi, unaona bado kuna matumaini ya kumpata mwenzako huyo wa karibu akiwa hai?” mtangazaji akauliza. Kidogo bwana kiongozi akatikisa kichwa akisema, “ Uwezekano ni mdogo mno, tunamini atakuwa ameuawa. Kama sivyo, basi itakuwa ni ajabu kubwa.”
Kauli hiyo ikagonga sana kichwa changu. SIKUAMINI KABISA KAMA RAISI AMEKUFA. Kama ni maadui zake wamemuua kama inavyoaminika, kwanini mwili wake usionekane? Kwanini ufichwe?
Bado niliamini Raisi yupo hai. Yupo mahali. Na watu wa kwanza kabisa wanaotakiwa kusema juu ya hilo, wakiwa ni wale wakina Ian Livermore. Niliumia sana kuhusishwa na lile jambo. Nikaumia zaidi kwani mwanangu atakuja kuishi akidhani baba yake alikuwa ni adui wa taifa.
Ni siku hiyo ndiyo nikaamua kufanya namna yoyote ilem nitoke humo ndani ya gereza. Nikitoka humo nikawasake wale wote ninaowatuhumu na mmoja baada ya mwingine atasema anachokifahamu.
Hata kama nikifa, basi nife nikiwa nasafisha jina langu.
Basi nikalala nikiapa endapo nitakuwa bado hai ndani ya juma moja tu la ziada, mipango yangu itakamilika bayana. Juma moja litatosha kabisa kwa mimi kutandaza mipango yangu ya kuaminika kabisa ya kutoroka mule ndani.
Ndani ya juma hilo nisome mianya yote. Kila mtu na kila zamu. Kila mlango na kila dirisha liwezekanalo na namna zake.
Lakini sasa nitapaje juma moja hilo moja la ziada? Hapo ndipo paliniumiza kichwa. Askari yule aliniambia halitapita juma hilo kabla ya pumzi yangu kung’olewa, ni nini sasa nifanye? Sikulala nikiwaza.
Kesho yake yalipofika majira ya mchana wa saa nane, nikapata ugeni, alikuwa ni Miss Danielle, ajenti wa FBI niliyekuwa nashirikiana naye kwenye kesi ya kupotea kwa Raisi.
Niliongea naye kwa uchache sana, akiwa amekuja kuhakikisha kama kweli nilichokisema mahakamni ni cha ukweli. Baada ya hapo nikamuuliza ni nini alipata kwenye chunguzi zake, lakini akaniambia hana muda wa kueleza hayo, na kesi hiyo ilikuwa tayari imeshafungwa.
“Kivipi?” nikashangaa. “kesi inafungwaje, ina maana nyote mnaamini Raisi amekufa?”
Danielle akatazama chini akitikisa kichwa. “Hata kama hatuamini, kuna nini cha ziada? Anyway, ilikuwa ni amri toka juu. Nilitakiwa kufunga kesi hiyo.” aliongea kama mtu aliyechoka. Niliona kwenye macho yake hakuwa na furaha juu ya hilo.
“Nikikuambia kitu utasadiki?” nikamuuliza nikimtazama machoni. Kabla hajanijibu, nikamwambia mimi sikuhusika na mauaji wala kupotea kwa Raisi, lakini najua wapi pa kuanzia kuutafuta ukweli.
Akaniuliza, “Utautafutaje ukweli na upo humu ndani, Marshall?”
“Ndio maana nataka kutoka,” nikamjibu na kumwambia, “Tafadhali nisaidie.”
“Nakusaidiaje Marshall?” akatumbua macho.
“Fanya namna univutie muda,” nikamwambia na kusisitizia, “Nahitaji juma moja tu.”
Punde askari akaja kunitoa. Kabla sijanyanyuka, nikamuuliza Danielle, “Promise?”
Hakunijibu. Alinitazama nikinyanyuka kisha akatikisa kichwa chake. Tukaachana.
**