SoC03 Njia mbadala zinazoweza kusaidia tatizo la upungufu wa walimu mashuleni

Stories of Change - 2023 Competition

cilla

JF-Expert Member
Jul 15, 2011
369
296

NJIA MBADALA ZINAZOWEZA KUSAIDIA TATIZO LA UPUNGUFU WA WALIMU MASHULENI.


UTANGULIZI:

Nchi yetu bado inachangamoto kubwa ya uhaba wa walimu wa shule ya sekondari na msingi.Kwa mujibu wa taarifa ya mwezi wa pili ya wizara ya nchi ,Ofisi ya rais tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI), tulikuwa na upungufu wa walimu wa shule ya msingi wapatao 186325 sawa na asilimia 51.44 kulingana na uwiano unaohitajika wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45 huku sekondari ikiwa na upungufu wa walimu 89,932 sawa na asilimia 51.5.huku upungufu wa walimu wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu ukiwa ni 2,945 sawa na asilimia 66.

Kwa shule za sekondari tatizo la uhaba wa walimu lipo kwa sehemu kubwa katika baadhi ya masomo hasa ya sayansi. takwimu za mwaka 2021/22, shule za sekondari zilikuwa na upungufu wa walimu 12,577 wa somo la fizikia, walimu 13,686 wa somo la hisabati, walimu 12,027 wa somo la bailojia, na walimu 10,600 wa somo la kemia.

Kwa kuliona hili mwaka huu 2023 serikali iliamua kuajiri walimu wa sekondari na msingi wapatao 13,130 kipaombele ikiwa ni walimu wa sayansi kwa shule za sekondari.Tunaipongeza serikali kwa kazi hii nzuri ya kuongeza walimu.Lakini bado idadi hii ni ndogo sana ukilinganisha na uasilia wa mahitaji yenyewe.Hili linatusukuma kuona kuwa kuna haja ya kuongeza jitihada zingine kubwa ili kuweza kukabiliana na upungufu huu wa walimu.

Wakati huu ambao wizara ya elimu ipo katika mchakato wa mabadiliko ya sera ya elimu ni muhimu sana kuweka mikakati ya kufikisha ujuzi na umahiri unaokusudiwa kwa walengwa(wanafunzi).

Sera ya elimu na mitaala haiwezi kuzalisha ujuzi na maarifa yanayotarajiwa ikiwa huna walimu ambao ndio watekelezaji wa kubwa wa sera yenyewe .Katika elimu mwalimu ni nyenzo muhimu kuliko zote.Bila walimu itakuwa ni vigumu kutekeleza sera ya elimu nakupata matokeo tunayoyatarajia.hakuna elimu bila mwalimu.

Tunajua kabisa kwamba tatizo la upungufu wa walimu linaweza lisiishe kabisa lakini tunaweza kulipunguza kwa sehemu kubwa zaidi ya ilivyo sasa.

NAMNA TATU ZITAKAZOWEZA KUSAIDIA KUPUNGUZA UPUNGUFU WA WALIMU MASHULENI.

✔️ TUNAWEZA KUAZIMA WALIMU
Serikali kupitia Halmashauri zetu wanaweza kushirikiana na shule jirani na sekta binafsi katika kuangalia namna gani yakusaidiana kutoa elimu katika shule zetu.Shule za serikali zilizokaribu na shule za binafsi /umma wanaweza kutengeneza utaratibu wa walimu wa wa shule binafsi au za umma zilizokaribu kwenda kufundisha kwenye shule za umma kwa makubaliano fulani.

Serikali kushirikiana na halmashauri zetu zinaweza kutengeneza utaratibu wa kutoa posho ya nauli kwa baadhi ya walimu wa sayansi walio katika shule jirani kwaajili yakwenda kufundisha katika shule ambazo zina ukosefu wa walimu.shule yenye upungufu wa walimu pamoja na shule anayotoka mwalimu ,wanaweza kutengeneza ratiba maalumu kwaajili ya mwalimu mualikwa ambayo haita athiri ratiba pamoja na majukumu yake ya kila siku.Mfano mwalimu anaweza kutafutiwa siku maalumu kama jumamosi kwa ajili ya kufundisha. Au mwalimu anaweza kupatiwa muda wa vipindi katika ya wiki vyenye muda wakutosha ili aweze kukamilisha mada husika katika kipindi cha muda mfupi.

Mfano shule ya umma ya sekondari yenye upungufu wa mwalimu wa somo la fizikia wanaweza kuandaa orodha ya mada zinazotakiwa kufundishwa kwa darasa husika na kumuomba mwalimu wa shule nyingine binafsi au ya serikali afundishe angalau mada moja au zaidi kulingana na muda anaokuwa nao.serikali kupitia halmashauri wanaweza kuangalia namna yakutoa motisha kwa walimu hao ambao watakuwa wanafundisha kwakujitolea kusaidia shule zetu.Serikali inaweza kuandaa malipo au posho kwa kila mada moja itakayofundishwa.

Pia serikali inaweza kuangazia namna yakuwatumia walimu wastaafu ,wahitimu wa vyuo vya ualimu lakini hata mtu ambaye anauwezo wakufundisha hata kama si mwalimu kwa taaluma yake.Watu ambao kwa taalumu si walimu wanaweza kusimamiwa na wakafanya vizuri kama watapewa muongozo.Tuna walimu wengi sana mtaani tuwatumie watuletee faida.

✔️ TUNAWEZA KUTUMIA TEKNOLOJIA

Wakati shule zilipofungwa kutokana na kuenea kwa virusi vya korona, tulishuhudia matumizi makubwa ya teknolojia katika ujifunzaji.jambo hili hatuoni tena likiendelea kwa kasi ile ya kama ilivyokuwa wakati wa ugonjwa wa korona.

Serikali inaweza kuandaa walimu mahari wa chache ambao wangetengeneza mafundisho(tuitorial) ya picha mjongeo (video) za kutosha kwa kila somo na kuzitumia katika maeneo yenye upungufu wa walimu wa masomo hayo hasa kwa shule za sekondari.Faida ya matumizi haya ya teknolojia kwa njia ya picha mjongeo yanaweza kumraisishia mwalimu kuweka michoro, video au vigaragosi mjongeo na picha zinazoakisi kitu halisi na kumfanya mwanafunzi aweze kuelewa zaidi kile kinachofundwishwa.

Pamoja na kwamba njia hii inaweza kusaidia shule zenye upungufu wa walimu, pia inaweza kusaidia walimu wenye changamoto kwa baadhi ya mada(topic) ambazo zinawapa shida kuzifundisha au kujikumbusha baadhi ya sehemu ngumu kwake kuzifundisha.Kutumika kwa teknolojia hii ya video inaweza kuwa msaada kwa walimu na wanafunzi pia.

Faida ya teknolojia hii pia inaokoa muda wa kujifunza na ina rahisisha uwezekano wa kurudi rudi maeneo ambayo hajaeleweka kwa wanafunzi.

Kutokana na changamoto ya umeme kwa baadhi ya shule serikali inaweza kushughulikia changamoto hiyo kwa haraka na ikatumia teknolojia hii kwa ajili yakutimiza malengo ya kielimu kwa watoto wetu.

Kama tukitumia teknolojia vizuri inaweza kufikisha mbali sana kielimu.

✔️ TUNAWEZA KUIBUA VIJANA MASHULENI WANAOONYESHA MUELEKEO WAKUPENDA KUWAHUDUMIA WENYE UHITAJI MAALUMU.

Upungufu wa walimu wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu ni karibu asilimia 66 ambayo ni sawa na waalimu 2,945.Idadi hii ni kubwa sana ukizingatia wanafunzi hawa wanahitaji uangalizi na ufuatiliaji wa karibu wakati wakujifunza.

Katika shule za kawaida ambazo zina wanafunzi wenye mahitaji maalumu kule ndiko kunakozaliwa vijana wenye ujuzi wa lugha za alama na wenye moyo wakujitoa kuwasaidia wenye ulemavu.chakusikitisha sana ni kwamba vijana wenye ujuzi wa lugha ya alama na nukta nundu wanapotelea kwenye fani zingine kutokana na kutokuwa na utaratibu mzuri wakuwaendeleza vijana hawa na kuwatengenezea mazingira mazuri yakufikia kuwa walimu wa wanafunzi wenye uhitaji maalumu kwasababu wanaona kama wanachelewa kufikia malengo yao. wanaotoka katika shule hizi zenye walemavu.

Lugha ya alama ni msingi mkubwa sana kwa mwalimu wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu hasa wasiona na viziwi.Mwalimu asiye jua alama ni vigumu sana kuwa na ujasiri wakufundisha.Lugha ya alama ni kama lugha nyingine.Lugha ya alama ni rahisi kujifunza katika umri mdogo kama ilivyo lugha nyingine.Twendeni kwenye shule zenye walemavu na huko tutakutana na vijana wanaojitolea kuwasaidia wenye ulemavu, tuwachukue hao na kuwaendeleza na kuwajenga ili waje wawe walimu wa watu wenye mahitaji maalumu.

Serikali iangalie namna ya kuwapata vijana ambao tayari wanaujuzi wa lugha za alama iwahamasishe kwenda kusomea ualimu maalumu pasipokupita kwenye utaratibu wa kawaida ambao unachukua miaka 5 (miaka 2 ya chuo na uzoefu wa miaka 3) ndipo mtu awe na sifa kuingia chuo cha ualimu maalumu.

ELIMU NI WAALIMU,HAKUNA ELIMU BILA WAALIMU

 
Back
Top Bottom