UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail:
press@ikulu.go.tz
Fax: 255-22-2113425
PRESIDENTS OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Na Mwandishi Maalum, Micheweni, Pemba
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa hakuna Mtanzania yoyote atakayekufa kwa njaa kutokana na uhaba wa chakula unaotabiriwa kutokea nchini kutokana na uhaba wa mvua katika mikoa kadhaa nchini.
Amesema kuwa Serikali yake itachukua kila hatua inayostahili kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kupata chakula kama kawaida, hata kama ukitokea uhaba wa chakula kama inavyobashiriwa.
Rais Kikwete ametoa uhakikisho huo wa kupatikana kwa chakula leo, Januari 20, 2009, katika mikutano yake mitatu tofauti katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku sita kutembelea mikoa ya Tanzania Visiwani.
Rais Kikwete ameanzia ziara yake Kisiwani Pemba wakati alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Karume, Mkoa wa Kusini Pemba, na kupokelewa na mamia ya wananchi wakiwamo wana-CCM, wakiongozwa na Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Shamsi Vuai Nahodha.
Katika tukio la kwanza la ziara hiyo, ikiwa ni sehemu ya ziara zake katika mikoa yote ya Tanzania, Rais Kikwete ameweka jiwe la msingi la Nyumba ya Kufikia Wageni ya Serikali ya SMZ katika Wilaya ya Micheweni, zamani ikiitwa Wilaya ya Konde, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Akizungumza na wananchi baada ya kuwa ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Nyumba hiyo, Rais kikwete ameonya kuwa Tanzania inatabiriwa kuwa Tanzania itakabiliwa na uhaba wa chakuka kutokana na kushindwa kunyesha kwa mvua, kama ilivyo kawaida, katika mikoa mbali mbali.
Mikoa ya Tanzania Bara ya Pwani na Kaskazini Mashariki pamoja na ile ya Tanzania Visiwani haikupata mvua ya vuli mwishoni mwa mwaka uliopita. Mikoa ya Lindi na Mtwara ambayo hupata mvua ndefu nayo haipati mvua ya kutosha wakati kuna habari kuwa mvua katika baadhi ya mikoa ya kati ukiwamo Dodoma tayari imekatika.
Rais amesema kuwa hata kama Tanzania itakumbwa na uhaba wa chakula, bado hakuna mtu ambaye atakufa na njaa kwa sababu Serikali yake imejipanga vizuri kutimiza
wajibu wake kuhakikisha kuwa hakuna Mtanzania anayekufa kwa njaa.
Tutakuwa na upungufu wa chakula, lakini hakuna atakayekufa kwa njaa. Serikali zetu mbili zitashirikiana kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata chakula, amesema Rais kwenye mkutano huo.
Rais Kikwete pia amewaambia wananchi wa Micheweni kuwa kwa maana ya wananchi kupatiwa huduma za jamii, Pemba iko mbele sana ya maeneo yote ya Tanzania Bara ikiwa ni pamoja na huduma ya maji, huduma ya elimu, barabara, afya.
Rais Kikwete ameeleza ukweli huo baada ya Sheha wa eneo la Micheweni kuwa amethibitisha kuwa wananchi wa eneo hilo hawana tatizo kupata huduma hizo. Maji tunayo, barabara zipo, zahanati zipo, shule tunazo za kila rangi, tatizo letu ni kwamba hatuna fedha za matumizi, amesema Sheha wa eneo hilo.
Baada ya kuwa amesikia hayo, Rais amesema: Kule Bara ndio kwanza tunajaribu kufikisha huduma za afya karibu na wananchi, ndio tunajenga shule za sekondari, tunaendelea na ujenzi wa barabara za lami ambazo nyie mnazo
Kuhusu malaria, Rais Kikwete amesema kuwa wakati Tanzania Bara inaendelea kuhangaika kupunguza ugonjwa huo, upande wa Pemba dawa za malaria sasa hazina wagonjwa. Sisi Bara sasa tunajaribu kuiga hili kupitia ule mradi mkubwa wa afya wa miaka 10.
Rais Kikwete pia amekagua Bonde la Kilimo cha Umwagiliaji Maji katika Kijiji cha Saninga Tumbe, ambako amepata maelezo ya mradi. Kesho, Rais Kikwete anaendelea na ziara yake kwa kutembelea Mkoa wa Kusini Pemba.