Sehemu ya 48.
Hisia za mapenzi bado ziliendelea kumuumiza, kichwa chake kilikataa kabisa kumsahau Evelyne.
Muonekano wake mzuri uliendelea kuwatesa wasichana waliyokuwa katika kampuni yake hiyo, wote walimtetemekea.
Kama kulikuwa kuna uwezekano wa kutokea walau siku moja kila moyo wa msichana katika kampuni hiyo kusema chochote, hakika sauti za maombi ya kumuhitaji Richard ndiyo zingesikika ndani ya ofisi nzima, hakukuwa na msichana ambaye alipomuona Richard moyo wake haukuacha kushtuka, ulimuhitaji mno mwanaume huyo.
Kama kawaida maneno na mabifu ya chinichini hayakuacha kuwepo kwa wasichana hao, walijikuta wakiingia katika ugomvi na chuki kila wakati, sababu ikiwa ni Richard.
Msichana aliyepata bahati ya kutolewa lunch na Richard aliitumia nafasi hiyo katika kuwaumiza roho wafanyakazi wenzake, hilo lilizidi kutengeneza chuki kati yao.
Licha ya kuwepo na mambo yote hayo ofisini lakini hakukuwa na msichana aliyebahatika kuumiliki moyo wa Richard, kila siku waliishia kumpelekea zawadi na mialiko mingi ambayo haikuweza kuzaa matunda yoyote.
"Ni Mzuri ndiyo tena anavutia mno ila sijakuelewa kwani nini unachokitaka hasa kwa Boss?" Aliuliza msichana mmoja.
"Sijui niseme nini, sijui nianzie wapi kukuelezea ila kwa kifupi nampenda sana, natamani siku moja ajue ni jinsi gani moyo wangu unavyomuhitaji," alijibu msichana mwingine ambaye alizungumza kwa hisia.
Kitendo cha wasichana kuamini siku moja kufanikiwa kulimiliki penzi la Richard kilibaki kuwa ndoto, ulikuwa ni ukweli uliyowaumiza mno.
Maisha ya Richard yalikuwa mazuri kwa upande wake lakini upande mwingine alijiona kukosa bahati, licha ya kuwa alifanikiwa kununua nyumba maeneo ya Mbezi, kumiliki pesa, kutembelea gari la kifahari lakini tukio la kumpoteza Evelyne kilimuacha na pigo kubwa mno.