Sehemu ya 34.
Happy alijitahidi kadri ya uwezo wake katika kumshawishi rafiki yake akubali kumsamehe Richard lakini jambo hilo lilikuwa ni gumu mno kutokea, kila mbinu aliyokuwa akiitumia iligonga mwamba.
Ilibidi afanye mawasiliano na Richard kisha wakapanga sehemu ya kukutana kwa ajili ya mazungumzo yao, walipanga kukutana Mlimani City, Samaki Samaki na sehemu hiyo ndipo walipopanga kufanya mazungumzo yao. “Rich, Evelyne anakuchukia sana yani hataki kulisikia jina lako hata mara moja,” alisema Happy.
“Nalijua hilo lakini amesemaje?”
“Amekataa kabisa kukusamehe.”
“Umekumbuka kumueleza kuwa ninampenda?”
“Ndiyo ila kwa kifupi hataki kusikia habari zako,”alisema Happy kisha Richard akaonekana kuwa mwenye mawazo.
“Rich naweza kukuuliza kitu?”
“Ndiyo niulize.”
“Kwani bado unaendelea kuwa na mahusiano na Monalisa?” aliuliza Happy swali ambalo lilimchukua muda Richard kuweza kulijibu.
“Hapana sipo naye,” alijibu Richard baada ya kumaliza kutafakar.
Richard hakuona sababu ya kumueleza ukweli Happy, aliamua kumficha lakini moyo wake bado ulizidi kuumia, alimpenda sana Evelyne, hakuwa tayari kumpoteza. ****
Wakati wa mawazo bado uliendelea kumtawala, alipokuwa nyumbani kwao usiku aliuona kuwa mrefu, kichwa chake kiliendelea kimfikiria mpenzi wake ambaye mpaka kufikia muda huo alikataa kumsamehe.
Aliwaza kumnunulia zawadi kama gari, kumpangishia nyumba kama ishara ya kumuomba msamaha lakini alipokumbuka uzito wa kosa alilokuwa amelifanya aliona zawadi hizo zisingeweza kufidia maumivu ambayo alikuwa amempa mpenzi wake.
Wakati akiendelea kuwaza hayo aliamua kuichukua simu yake kisha akaamua kumtumia ujumbe Evelyne, ujumbe huo uliweza kujibiwa kwa haraka sana.
“Mambo mpenzi.”
“Sorry nachat na nani?”
“Ina maana namba yangu umeifuta?”
“Hujajibu swali, nimekuuliza nachat na nani?”
“Mimi Richard.”
“Nikusaidie nini?”
*
*
Je, nini kitaendelea?