The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,799
NDOA ZA KULAZIMISHWA Banner.jpg


Magonjwa ya zinaa, ukatili (wa kimwili na wa kingono), mateso ya kisaikolojia, kupoteza uhuru, na woga pamoja na athari nyingine nyingi mbaya ni baadhi tu ya madhara ya kudumu yanayowakumba waathiriwa wa ndoa za kulazimishwa.

Ukiukaji wa haki za kibinadamu kwa kuwalazimisha wasichana kuolewa ni tatizo ambalo limeenea katika tamaduni, makabila na dini mbalimbali duniani. Ukosefu wa usawa wa kijinsia duniani kote unapenyeza mila hatari, kunyamazisha wasichana wadogo na kuweka maisha yao katika hali mbaya.

Haki ya msingi ya elimu kwa watoto mara nyingi inahatarishwa na ndoa za kulazimishwa na za mapema.

Watoto wanaolazimishwa kuingia kwenye ndoa huacha shule katika kipindi cha matayarisho ya ndoa zao wakiwa na matumaini madogo ya kurejea kwenye mfumo wa elimu. Idadi kubwa ya wasichana hao hupewa mimba kabla ya kufikisha miaka 18 na kuzaa watoto ambao pia wananyimwa haki yao ya elimu na kuolewa mapema, wakiendelea na mzunguko wa unyanyasaji na umaskini.

Ndoa za kulazimishwa zinaeelezwa kuwa ni pale ambapo mhusika mmoja au wote wawili wanalazimishwa kufunga ndoa bila ridhaa. Mitazamo mibaya ya kijinsia na mila za kibaguzi husababisha wanawake kuwa wengi zaidi kuliko wanaume katika suala la ndoa za lazima.

Idadi ya wanaume, wanawake na watoto wanaoishi katika ndoa za lazima imeongezeka duniani kote. Kwa mujibu wa ripoti ya Makadirio ya Utumwa wa Kisasa Duniani mwaka 2022, inakadiriwa kuwa watu milioni 22 walikuwa katika mazingira ya ndoa za kulazimishwa mwaka 2021. Hili ni ongezeko la milioni 6.6 la idadi ya watu wanaoishi katika ndoa ya kulazimishwa kati ya 2016 na 2021, ambayo ina maana ya kuongezeka kutoka watu wawili hadi watu watatu kwa kila watu elfu moja.

Wanawake na wasichana milioni 14.9 wamelazimishwa kuingia kwenye ndoa. Wakati wanawake na wasichana wanachangia idadi kubwa ya watu wanaoishi katika ndoa za lazima, wanaume na wavulana pia wanakabiliwa na janga hili.

Pia, watu watatu kati ya watano walio kwenye ndoa ya kulazimishwa wako katika nchi za kipato cha chini cha kati. Hata hivyo, mataifa tajiri pia yanakumbana na janga hili.

Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa wanafamilia walihusika kwa kiasi kikubwa katika suala la ndoa za lazima. Watu wengi walioripoti hali ya ndoa za lazima walilazimishwa kuolewa na wazazi wao (73%) au jamaa wengine (16%). Ni 6% ambao wamelazimishwa na wasio ndugu kuolewa wakati 3% wakiwa wamemelazimishwa na madalali wa ndoa. Pia, ni 1% wamelazimishwa na mwenza/familia ya mwenza na wengine wanaeelezwa kulazimishwa na viongozi wa kijamii na kidini.

Nusu ya wale wanaoishi katika ndoa za kulazimishwa walilazimishwa kutumia vitisho vya kihisia au matusi. Kwa mfano, mzazi anaweza kumtisha mwanaye kuwa asipoolewa kwa wakati huo hatokaa akaolewa kwakuwa ni masikini au hana elimu.

Mbinu nyingine iliyotumiwa kuwalazimisha watu kuingia kwenye ndoa ni pamoja na matumizi ya ulaghai wa kihisia - kwa mfano, wazazi kutishia kujidhuru au kudai kuwa sifa ya familia itaharibiwa - au vitisho vya kutengwa na wanafamilia, n.k.

Kuna sababu nyingi kwa nini wasichana au wanamke wanalazimishwa kuolewa. Wazazi au wanafamilia wanaweza kuiona kama njia ya kurejesha heshima ya familia, kuboresha hadhi ya familia, au kupata manufaa ya kiuchumi. Familia zingine zinaweza kutaja mila za kitamaduni au imani za kidini.

Hata hivyo, kwa vyovyote vile, ni wazi kuwa ndoa za lazima ni ukiukaji wa haki za binadamu na ni suala ambalo linaathiri afya, ustawi na uhuru wa wahanga wake.
 
Ndoa za kulazimishwa ndio zinadumu muda mrefu kuliko ndoa za hiari mkichokana kila mmoja anafungasha virago kutafuta mtu mwingine anayempenda. Ndoa za zamani ukichumbiwa tu hakuna kukataa utaenda tu kwa lazima kuishi na bwana aliyekuoa hata kama havutii kisura na kiuchumi. Ndoa za siku zimeachwa watu wachumbiane kwa mvuto wa sura, umbo na hali nzuri ya uchumi, vikikosekana hivyo ndoa inakosa mvuto na inavunjika mapema tu. Ndoa za kibabe ndizo zinazodumu
 
Ndoa za kulazimishwa ndio zinadumu muda mrefu kuliko ndoa za hiari mkichokana kila mmoja anafungasha virago kutafuta mtu mwingine anayempenda. Ndoa za zamani ukichumbiwa tu hakuna kukataa utaenda tu kwa lazima kuishi na bwana aliyekuoa hata kama havutii kisura na kiuchumi. Ndoa za siku zimeachwa watu wachumbiane kwa mvuto wa sura, umbo na hali nzuri ya uchumi, vikikosekana hivyo ndoa inakosa mvuto na inavunjika mapema tu. Ndoa za kibabe ndizo zinazodumu
Zamani sio sasa hivi unakuta mtu ana jamaa yake halafu ww unalazimisha unaweka ndani utachapiwa mchana kweupe.
 
Back
Top Bottom